Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa na Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha uliuoishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Seriakli za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishi tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezajiwa wa Mitaji ya Umma kuhusu uwekezaji wa mitaji ya umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Dr. Charles Stephen Kimei

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vunjo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa na Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha uliuoishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Seriakli za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishi tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezajiwa wa Mitaji ya Umma kuhusu uwekezaji wa mitaji ya umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa fursa hii. Mimi naanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais na Amiri Jeshi wetu Mkuu kwa mambo mengi anayofanya. Pamoja na kumwaga fedha nyingi kwenye Jimbo langu la Vunjo; papo tu na mimi inabidi nimpe maua ya Vunjo. Lakini zaidi kwa namna ambavyo alichukua hoja zilizoletwa kwake na CAG na akaweza kuzifanyia kazi. Kwa wale wanaofuatilia watajua kwamba Mheshimiwa Rais ameshafanyia kazi hoja nyingi, ikiwemo kubadilisha watendaji kwenye taasisi fulani fulani ambazo zilionekana kwamba zina udhaifu. Pamoja na miongozo mingine ya kutekeleza zile hoja, nampongeza sana kusema kweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza CAG mwenyewe kwa namna ambavyo ameweza kutuletea hoja nzuri na amechambua vizuri hesabu hizi na akatoa ushauri ambao kweli umeweza kuongoza mjadala kwenye Bunge hili kuhusiana na utendaji wa Serikali katika kusimamia fedha za umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nawapongeza wanakamati wa PAC, PIC na LAAC kwa kazi nzuri na maazimo mazuri ambayo wameyaleta, na ninasema kwamba mimi nayaunga mkono kwa asilimia 100. Kuna moja tu ambalo sitaliunga mkono sana, kwa sababu lile la taasisi za umma au mashirika ya umma kupeleka asilimia 15 ya mapato yao ghafi Serikalini kabla ya kufanya hesabu kwamba wanapata hasara au faida, hilo mimi nafikiri kwamba linapunguza sana uwezo wa mashirika ya umma yaweze kuendelea kufanya kazi kibiashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba niwasilishe hoja moja, na nitajikita zaidi kwenye mashirika ya umma. Endapo mashirika ya umma yataendelea kufanya kazi kwa namna tulivyoona kwenye hoja zilizoibuliwa na Mheshimiwa CAG ninaamini kwamba hatutaweza kuwa na uhakika wa prudence of fiscal stability; yaani utulivu wa fedha za kibajeti kwa miaka inayokuja. Kwa sababu issue ni hii; kwenye sheria ya bajeti tunaambiwa kwamba msingi ni mmoja; ni kwamba Serikali ijiendeshe na ijiendeshe kwa fiscal policy yake kwa kuhakikisha kwamba kuna utulivu endelevu kwa vizazi vijavyo; kusije kukawa na madeni yameji-accumulate kila mahali halafu wewe huyajui, huyatambui, halafu yakiibuka hapa unaambiwa ulipe. Kwa sababu hii unakuwa unaingiza bajeti kwenye stress kubwa na hii inakuwa ni fiscal risk kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nasema kwamba, kwanza cha msingi ni lazima tuchukue hatua za kuhakikisha kwamba mashirika ya umma yanabadilika kwa namna yanavyojiendesha. Tumeambiwa kwamba mashirika ya umma yanajiendesha kwa hasara. Hasara iliyofanywa na mashirika 14 yaliyo kwenye ripoti ya CAG kwa mwaka 2020/2021 na 2021/2022 ni shilingi bilioni 217. Hasara ya mashirika 14 tu. Hatujayaweka mashirika mengine yote kwa sababu na yeye ametupa sample tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kitu cha ajabu. Utaona kwamba kwa mfano, Shirika la ATCL, limefanya hasara ya shilingi bilioni 105, ukijumuisha fedha ya ruzuku ambayo walipewa. Kama wasingalipewa ruzuku ya shilingi bilioni 30.6 wangefanya hasara ya jumla ya bilioni 105 kwa hiyo miaka hiyo miwili, ni fedha nyingi. Ukiangalia Shirika la TRC limefanya hasara ya shilingi bilioni 54, NDC imefanya hasara bilioni 38, ukiangalia Mkulazi Holding imefanya hasara ya bilioni 20, Kilimanjaro Lather bilioni saba. Vyote hivi vinakula ndani either ni ruzuku au wamechukua mkopo au sijui wame-finance namna gani hiyo hasara, lakini ni kwamba inaingiza bajeti yetu kwenye kutokuwa na sustainability ya uhimilivu wake kwa miaka ile inayokuja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachosikitisha ni kwamba mashirika haya yanayofanya hasara hamna mkakati ambao wamejijengea ya kuweza kujinasua kwenye kufanya hasara hizi, na hawalazimishwi kutengeneza hizo business plan za kuhakikisha kwamba baada ya miaka miwili au mitatu wanajiondoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nafurahi kwamba TTCL walikuja kwetu kwenye Kamati ya Bajeti; wakaonyesha kwamba wamefanya hasara kubwa lakini ndani ya mwaka huu na mwaka ujao watakuwa wamekuwa sustainable. Kule tunaona kwamba Mkurugenzi Mtendaji naye alibadilishwa na Mheshimiwa Rais. Lakini kwa kweli ni tatizo kubwa kwa sababu hatuwezi kujua mbeleni ni wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Shirika la ATCL, Mkaguzi Mkuu anasema kwamba ilipata hasara kwa sababu ndege zilikuwa grounded. Mimi Nakasema niseme kwamba kama ndege zisingekuwa grounded basi hasara ya ATCL ingekuwa kubwa zaidi; kwa sababu mashirika mengi ya ndege duniani yamepata hasara kubwa tu. Kwa hiyo, ni kwamba pengine lingepata hasara kubwa zaidi kwa sababu haya mashirika hayako proactive katika ku-adjust to market changes.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi niseme hiki, hata nasikitika kwamba kuna kiongozi mmoja alisema kwamba anasikitika kwamba alibinafsishwa. Lakini kama asingebinafsisha tungekuwa wapi kama mashirika ndiyo yanajiendesha hivi? TANOIL tumesikia imefanya hasara ya bilioni saba. Kwa hiyo, takribani kila shirika ambalo linajiendesha kwa kusimamiwa na Serikali linamatatizo. Kwa nini Serikali isiingie ubia ikawezesha private sector kwa management contract kuendesha mashirika haya na wakaachana na haya mambo ya kufanya hasara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo linasumbua kwenye mashirika ya umma ni madeni. Mashirika ya umma yana madeni ya ajabu. Nilishangaa mimi, kwanza nilisoma nikasema ni bilioni au trilioni. Mashirika 11 ya umma ukichanganya yana madeni yanafikia jumla ya trilioni 27.5. Ni trilioni 27 siyo bilioni. Na haya ni yale mashirika yanayosemekana ni ya kibiashara. Sasa ukiongeza taasisi za Serikali ambazo hazitakiwi kufanya biashara na kupata faida, jumla ya madeni ni trilioni 5.2. Ukijumuisha inakuwa ni trilioni 32 kwenye mashirika ya umma, imekaa kwenye vitabu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo tunalojiuliza ni hivi, ukichanganya hilo kwa sababu hata extended public sector debt unajumuisha ile ya Serikali ya about 8 trillion inakuwa ni 112 trillion. Sasa hilo ni deni kubwa sana kwa sababu huwezi kusema kwamba madeni ya mashirika ya umma hayatalipwa unless kuna namna nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninachoshauri na ninaomba Bunge likubaliane ni kwamba, haya madeni ya mashirika ya umma yafanyiwe uchambuzi, tujue yametoka wapi na nani Aliya-finance. Je, kuna transactions au miamala ambayo imefanyika na Serikali Kuu? Kama ipo, je, kuna uwezekano gani wa kugeuza madeni haya kuwa ni mtaji wa hisa? Halafu vile vitabu vya mashirika haya vikawa angalau a little bit clean, na vikiwa vimesafishwa, hiyo balance sheet ikiwa imesafishwa ina maana kwamba mashirika haya kama yatakuwa yamegeuka kuwa mashirika ambayo siyo mabaya, basi pengine hata yanaweza kukopa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kimoja ambacho naomba tu-encourage mashirika ya umma yaweze kuchukua mikopo ya biashara, overdraft ili kuendesha biashara zao kwa gharama nafuu.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi naomba hiyo ifanyiwe kazi, na kama isipofanyiwa kazi tujue kwamba tunaweka mrundiko wa matatizo kwenye bajeti ya Serikali kwenye miaka hiyo inayokuja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili la Mkulazi ni tatizo sana. Mkulazi imefanya accumulative growth kati ya 2020/2021 na 2021/2022 ya bilioni 20. Astaghafiru-llah, sasa inakuwaje? wenzake wamekuja nyuma, Bagamoyo Sugar imekuja wanaanza kufanya faida, hawa wanaendelea kupata hasara, hawajaanza hata biashara wanafanya mahasara. Mimi ninaomba Serikali iangalie namna gani ifanyike. Kama ambavyo nimeshauri, kwamba tuendelee sasa kuona namna. Kwa mfano, kampuni kama hiyo immideately ipewe private sector aiendeshe ili tuweze kuepukana na matatizo. (Makofi/Vicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti,…

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa kengele imelia ya pili. (Makofi)

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, haya kumbe imelia ya pili. Naomba tu nitoe kahoja kamoja, yaani one minute.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mambo ya mifuko ya pension. Mifuko ya pension return investment yake iliyofanya ya 604 billion kwa miaka hii miwili inayozungumzwa, imekuwa ni 0.4 percent. Sasa 0.4 percent ni kidogo sana ukilinganisha na average return kwa mifuko hiyo ambayo inatakiwa iwe 5 percent. Kwa hiyo iko 4 percent ten times. Sasa kama wangefanya biashara yao ya uwekezaji sawa sawa hata wasingelia kwamba sasa ukwasi umepungua kwa sababu Serikali haitoi michango yake na kadharika; wangepata fedha za kutosha kwenye uwekezaji. Kwa hiyo, mimi nasema kweli, nawaomba wale wanaosimamia mifuko hii wajiangalie upya kwa sababu 0.5 percent kwenye return on asset ni haiwezekani (Makofi/Vicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, basi naunga mkono tena na Mungu atujalie wote tuishi na mashirika haya. (Makofi)