Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Stanslaus Haroon Nyongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Maswa Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa nakushukuru sana wewe na nikupongeze kwa kazi yako nzuri ya kutuongoza, wewe pamoja na Mheshimiwa Spika. Nichukue fursa hii kuendelea kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan Mheshimiwa Rais wetu kwa kazi nzuri anayoifanya. Vile vile nawapongeza sana Mawaziri hawa wawili ambao leo wameweza kuwasilisha mpango na masuala yote na mikakati ya utekelezaji wa mpango. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kusisitiza na niendelee kupongeza kwamba Mheshimiwa Rais wetu amekuwa na maono makubwa sana kwa maana ya kujenga miundombinu kwa ajili ya kuimarisha uchumi wa nchi yetu. Miundombinu inayojengwa, kwa mfano SGR, tunatambua kabisa ndio msingi wa kwenda kuinua uchumi wa nchi yetu; na vile vile ujenzi wa barabara pamoja na miundombinu mingine kwa mfano uboreshaji wa ujenzi wa bandari na mambo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimwambie Mheshimiwa Waziri wa Mpango, Mheshimiwa Waziri kama utafikiria SGR na ambao utekelezaji unaendelea, tusipofikiria kujenga barabara na kuimarisha barabara kubwa, kwa mfano, barabara kutoka Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma kwenda Kanda ya Ziwa Pamoja na kwamba kuna SGR tunajenga mfikirie kujenga hizi barabara na kuzitanua. Haiwezekani leo tupo karne ya 21 tunapishana barabara moja, malori makubwa, mabasi, magari madogo tunapishana kwenye barabara moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kwa sababu tukipata breakdown kidogo barabara hizi inakuwa ni chaos, watu wanasimama wanashindwa kutembea, barabara zetu zaina hali mbaya. Tusije tukaegemea kwenye SGR tukasahau barabara. Fikiria kujenga barabara nne Dar es Salaam - Morogoro, Morogoro – Dodoma, Dodoma – Singida kwenda Mwanza na upande wa Magharibi. Jengeni barabara hizi highway ziwe nne watu waweze kutembea, ndiyo uchumi wenyewe, siyo starehe. Barabara siyo starehe, barabara ni uchumi. Jengeni barabara watu waweze ku-move usiku na mchana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona uchumi wetu unavyokua, trend ya ukuaji ni mdogo. Ukiangalia mwaka 2022 ukuaji wa uchumi wetu ulikuwa ni asilimia 4.7, mwaka 2021 asilimia 4.9, ina maana kuna difference ya asilimia 0.2. Mwaka 2023 asilimia 5.2 na tunategemea kuwa na asilimia 6.1 mwaka 2024. Ni lazima tuangalie uchumi wetu umekaa vipi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukitazama uchumi wetu, amezungumza Mheshimiwa Prof. Kitila Mkumbo kwenye hotuba yake kwamba sekta ya kilimo ndiyo inayoongoza kwa ukuaji kwa asilimia 15.9, ikifuatiwa na sekta ya ujenzi pamoja na uzalishaji kwa maana ya viwanda. Ukiangalia ukuaji huu wa sekta ya kilimo ni nani anayeukuza huu uchumi? Nani yupo kwenye sekta ya kilimo? Ukitazama aliyeko kwenye sekta ya kilimo ni Watanzania wa kawaida. Asilimia 80 ndio wanaolima kilimo cha kawaida. Sasa kama wewe unategemea uchumi wako kukua na unayemtegemea ni mkulima, unamfanyia nini mkulima huyu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Bashe, amekuja na BBT na mambo mengine, lakini tuna hii document ambayo ameizungumza hata Mheshimiwa Mkumbo ya ASDP (Agriculture Sector Development Program). Hii program itekelezwe kwa asilimia 100. Kwa sababu gani? Katika SDP 2 tumeona mipango mizuri ya uzalishaji kwenye sekta ya kilimo, tumeona mipango mizuri ya uchakataji wa bidhaa za kilimo, tumeona mipango mizuri ya packaging kwa maana kutengeneza na kuweza kuongeza thamani ya bidhaa za kilimo ikiwa ni pamoja na kufanyiwa promotion na masuala ya ulinzi wa mazingira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu mpango wa SDP ushughulikiwe, utekelezwe ndiyo mkombozi mkubwa wa uchumi wa nchi yetu. Kwa mfano, zao la pamba. Nazungumzia pamba kwa sababu natoka kwenye kilimo cha pamba. Tunalima pamba miaka yote toka tumepata uhuru mwaka 1961, tuna-process asilimia 25 tu. Tunachukua pamba tunai-gin kwa ginners asilimia 75 tunaipeleka nje ya nchi. Kupeleka nje ya nchi asilimia 75 ni kupeleka ajira nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba value chain; uchakataji wa zao la pamba uongezeke. Ule Mkoa wa Simiyu mtusaidie. Serikali lazima mwekeze kwenye ku-add value zao la pamba. Badala ya ku-export pamba lint, kwa maana ya nyuzi, tu-export majora ya nguo, tu-export nguo. Bila kufanya hivyo na Serikali ku-intervene hatuwezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukimtegemea mfanyabiashara mmoja awekeze kwenye ku-gin pamba, atengeneze kiwanda cha kufanya spinning, kiwanda cha kutengeneza nguo, mfanyabiashara mmoja hawezi. Hili tunalizungumza kila siku. Katika Mpango huu tunaomba mje na mkakati na mtenge fedha tutengeneze textile industry kwa maana ya kuhakikisha kwamba ule mpango wa cotton to cloth uweze kutekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesikia cotton to cloth toka enzi zile Mzee Mwijage, mzee wa vyerehani anaongelea cotton to cloth. Hivi mpaka leo cotton to cloth iko wapi? Miaka saba sasa tunaongelea cotton to cloth. Bila intervention ya Serikali kuwekeza kwenye textile kuhakikisha kwamba value chain ya zao la pamba ina-take place, bila kufanya hivyo, zao la pamba litaendelea kubaki vile vile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkulima wa pamba mwaka jana 2022 tuliuza pamba kwa shilingi 2,000/=. Mwaka huu 2023 tumeuza pamba kwa shilingi 1,160/=, hii inakwenda wapi? Mwakani inawezekana tukauza kwa 1,000/= au chini ya shilingi 1,000/=. Huyu mkulima wa pamba mnampeleka wapi? Mkulima wa pamba analima kwa gharama kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwenye ule mpango wa ASDP imeeleza namna ya ku-increase productivity kwenye zao la pamba mwongeze productivity kwa maana ya ku-improve mbegu za pamba; kwenye heka moja ya mtu anayelima pamba, basi mfanye namna ya kuongeza uzalishaji kwa sababu sasa hivi mtu anazalisha kwenye heka moja kilo 200 mpaka 300., wakati nchi nyingine wanazalisha mpaka kilo 1,000. Ukishaongeza productivity maana yake ni kwamba tayari hawa watu umeshawaongezea ajira. Ukiweka vile viwanda vya ku-process zao la pamba tuta-add value zao la pamba na tutauza nguo badala ya kuuza lint kama tunavyofanya sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, Mheshimiwa Rais wetu ni mtu msikivu, ni mtu ambaye ana upendo, tunakuomba sana Mheshimiwa Dkt. Mwigulu na Mheshimiwa Prof. Kitila Mkumbo tunaomba mfanye jambo kwenye zao la pamba. Bila hivyo hatutakuwa na maendeleo yoyote katika mikoa ya Kanda ya Ziwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, kengele imegonga, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii.