Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Cecil David Mwambe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ndanda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nikushukuru pia kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia kwenye Mapendekezo ya Mpango, 2024/2025.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejipa nafasi ya kusoma hotuba zote mbili za Waheshimiwa Mawaziri ambazo wamewasilisha hapa leo na mimi nikasema basi nijipe nafasi niweze kuchangia kwa maana ya kulishauri Taifa letu. Nilipata nafasi ya kuchangia mwaka 2016 na wakati nachangia nilionesha umuhimu wa chuma kilichopo Mchuchuma ikiunganishwa na bandari yetu ya Mtwara, nashukuru Serikali imefanya maendeleo na sasa hivi tunaambiwa kwamba kule Mchuchuma pamoja na Liganga wameanza kulipa fidia ili wale wananchi waweze kuondoka eneo lile kwa ajili ya kuendeleza huu mradi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nishauri kwenye jambo hili kwamba mpango wa sasa wa Serikali ni kuona kwanza tunachimba makaa kadri ya taarifa ambayo iko mbele yetu, wakati ule nachangia mwaka 2016 nakumbuka, nilisema nchi yetu imekuwa inapoteza pesa nyingi sana za kigeni kwa ajili ya ku-export chuma ili kije kuweza kujenga na kufanya matumizi mbalimbali kwa sababu nchi yetu inakuwa kwa kasi, kwa hiyo shughuli nyingi za ujenzi zinafanyika. Kwa hiyo, tuna import nondo nyingi sana lakini pia karibia asilimia 90 au 85 ya chuma chote ambacho kimetumika kwenye ujenzi wa SGR kimekuwa imported.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hii tafsiri yake tumeiondoa forex nyingi sana kupeleka nje. Wakati kimsingi nchi ambazo zinaendelea au zilizoendelea, kabla ya kutekeleza miradi mikubwa ambayo kwa vyovyote vile itapoteza pesa nyingi sana za kigeni wanaanza kuangalia kwanza resources walizonazo wao ndani. Kwa hiyo, kwa ushauri wangu kama nchi tungeanza kwanza ku-extract Chuma cha Liganga ili kiweze kutusaidia kwenye kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo reli hii ya SGR ambayo tunaisema sasa hivi lakini pamoja na ujenzi katika maeneo mbalimbali yanayoendelea ikiwa ni pamoja na majengo ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo bado nasisitiza kwamba tunayo makaa ya mawe maeneo ya Ngapa kule Mbinga na maeneo mengine ambayo kwa sasa hivi yanachimbwa na hatujaweza kufikia hata asilimia kubwa kama ambavyo yanahitakija. Nashangaa kuona sasa Serikali inataka tena kuchimba makaa ya mawe Liganga badala ya kutafuta kwanza mwekezaji wa chuma ambae hatuna kabisa huo mradi hapa Tanzania ili mwisho wa siku chuma hiki ki-support pamoja na kupunguza export ya kwetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine sijaona msisitizo mkubwa sana kwenye suala la LNG. Natambua kwamba Lindi tuna mradi ambao unakwenda kutekelezwa karibuni lakini ili kutekeleza huu Mradi wa LNG ambao na wenyewe utakwenda kutusaidia kupunguza matumizi makubwa ya forex kwa ajili ya kuagiza mafuta kutoka nje lakini pia sasa hivi gesi kubwa tunayotumia Tanzania tunaagiza nayo kutoka nje, wakati kimsingi bomba letu la gesi linalotokea Lindi kwa maana ya Mkoa wa Mtwara na Lindi linatumika siyo zaidi ya asilimia 10, tena kwa kuzalisha tu umeme kwenye eneo la Kinyerezi I na II pamoja na kwamba hata sisi Watu wa Mtwara tunashida kubwa sana ya umeme, kwa hiyo tunategemea tuone Serikali inaacha kuagiza sasa gesi pamoja na mafuta kutoka nje na kuweka nguvu kubwa kwenye kuimarisha huu Mradi wa LNG Lindi kupitia Wizara ya Nishati. Kazi ambayo inaendelea sasa hivi lakini utekelezaji wake basi uharakishwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kuhusu suala la Liganga na Mchuchuma linakwenda sambamba na kuikumbusha Serikali, kwamba Serikali hii iko kwenye movement, iko kwenye mwendelezo unaoendelea, sasa hivi tuko kwenye Awamu ya Sita ambayo tuko nayo sasa hivi, lakini mtakumbuka mradi mkubwa wa Mtwara Corridor ulipigiwa sana chepua na Mheshimiwa Hayati Mkapa wakati huo kwenye Serikali ya Awamu ya Tatu nakumbuka lakini ukija kuangalia yanayotokea sasa hivi kama Mtwara Corridor imekuwa abandoned, yaani utekelezaji wa miradi ile ambayo ilikuwa inakwneda sambamba na maboresho ya Bandari ya Mtwara, maboresho ya Uwanja wa Ndege Mtwara hayawi serious namna hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naishauri Serikali na siku moja hapa Mheshimiwa Bishop Gwajima alishauri kwamba tunapokuwa na nchi kama nchi yetu Tanzania, nchi inayokua lazima tuhakikishe tunapoleta hii mipango inakuwa ni ya muda mrefu, tuseme tunajadili mipango ya miaka 50, kwa hiyo, kila Rais atakayeingia kwenye uongozi wake ahakikishe kwanza anatekeleza yale tuliyokubaliana katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa, badala ya kuwa na mpango wa miaka mitano mitano ama mpango wa miaka sita sita kiasi kwamba kila Rais anapokuja basi anakuwa na vipaumbele vya kwake anavyofikiri kwamba ndiyo mambo ya msingi ya kuyafanya.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hali ya kawaida, Bandari ya Mtwara kwa mfano sasa hivi, Serikali imewekeza pale pesa nyingi sana kwa ajili ya kuona ile bandari inakua lakini matumizi makubwa ni kusafirisha makaa ya mawe kwa kiasi kidogo, makaa ya mawe haya yanaletwa na malori yanaleta athari za kuharibu barabara zetu ambapo Serikali hivi karibuni itaingia gharama kubwa ya kufanya marekebisho ya barabara kutoka Songea mpaka Mtwara pia kutoka Mtwara mpaka Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, lazima tukumbuke kwenye huu Mpango wa Mtwara Corridor kulikuwa kunatajwa habari ya reli ya kusini. Sasa Mheshimiwa wakati unakuja kuhitimisha kwenye jambo hili utueleze, mkakati wa kuwa na reli ya kusini bado upo ama Serikali wameamua kuuacha na unafanya mikakati mingine. Kwa sababu kuna watu wengi ambao ukitokea ukanda wa Mtwara mpaka kufika Songea eneo lile ambako inasemwa reli ya kusini itapita watu waliwekewa “X” mpaka Peramiho nakumbushwa hapa na Mheshimiwa Jenista. Watu waliwekewa “X” kwenye majumba yao, kwa maana ya kwamba nyumba hizi zitavunjwa kwa ajili ya kupitisha reli, ni zaidi ya miaka kumi, zaidi ya miaka 20 sasa hivi mradi huu hautekelezwi tena. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunataka tuone Serikali itueleze kwamba mkakati ule wa kuwa na reli ya kusini inayoanzia Mchuchuma na Liganga mpaka Bandari ya Mtwara bado upo au Serikali imeuacha? Kama bado upo basi tuuone kwenye vitabu kwa sababu kimsingi tunataka tuone watu wetu ili waweze kuendeleza maeneo yao.

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tupate matumizi makubwa ya Bandari yetu ya Mtwara kwa sababu sasa hivi…

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwambe kuna taarifa.



TAARIFA

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka tu nimpige taarifa rafiki yangu na Mbunge makini, katika suala la kuleta mapinduzi huko kusini na kwa Taifa, ujenzi wa barabara ya kiwango cha zege inayotoka Lusitu Kwenda Mawengi ambayo ilikuwa inalenga kwenda Nkomang’ombe kuliko na madini ya makaa ya mawe inaendelea kuhitaji kujengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo imepangiwa bajeti ya Itoni kuja Lusitu lakini kutoka Nkomang’ombe kuja Liganga kwenda Madaba kwenda Songea ambayo ingetakiwa ijengwe kwa kiwango cha zege kama ilivyoaanza kile kipande cha kwanza, kilometa zilizojengwa ni 50 tu, hatuwezi kwenda kwa kutarajia kufanya mapinduzi kwa kutumia Chuma cha Liganga kwa kwenda kwa kasi ndogo kiasi hicho, vinginevyo mradi huu utaendelea kubaki miaka mingine 20 hadi 30 ijayo.

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Mwambe taarifa unaipokea?

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Senior hapa Mzee wangu kwa taarifa hii nzuri, nami niungane na wewe kwamba hicho unachokisema pia kiwe kama sehemu ya mchango wangu kwa maana ya kutaka kuboresha mchango wangu, taarifa yako nimeipokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, bado nizidi kusisitiza, kwa mfano sasa hivi sisi Wabunge wa Mtwara tunakuwa tunabishana kila mara, kuhusu matumizi sahihi ya Bandari ya Mtwara, badala ya kufikiri kuhusiana na huu mradi wa Mtwara Corridor ambalo ni jambo ambalo lingeweza kuongezea mapato nchi yetu, sisi tumeng’ng’ana na kufikiri kwamba kusafirisha korosho, korosho inayotoka huko Tandahimba, Masasi na maeneo mengine ili kuweza kuboresha bandari yetu kitu ambacho kinafanyika katika msimu wa miezi mitatu mpaka minne tu ambayo haiwezi kusaidia na uwekezaji mkubwa uliofanyika pale na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona hapa katika mpango wanasema wanataka sasa kuweka taa kwenye Uwanja wa Ndege wa Mtwara, niendelee kumsisitiza Mheshimiwa Waziri hapa kwamba umuhimu wa Uwanja wa Ndege wa Mtwara utaonekana wakati wa utekelezaji wa Mradi wa LNG. Pia, tuangalie na umuhimu wa Bandari ya Mtwara kwa sababu kimsingi barabara ya kutoka Dar es Salaam, Lindi mpaka Mtwara literally imekufa, inahitaji matengenezo makubwa sana. Kwa hiyo, wawekezaji wengi kwa vyovyote watatumia uwanja wa ndege lakini pia watatumia Bandari ya Mtwara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hizi zinakufa kwa sababu ya matumizi makubwa ya barabara kwa sababu tunakosa njia nyingine za usafarishaji. Kwa hiyo, tulikuwa tunatumia barabara muda wote kiasi kwamba barabara zetu sasa zimekufa, zinahitaji matengenezo makubwa kwa sababu ya kupitisha malori makubwa ya sementi yaliyokuwa yanatoka Kiwanda cha Dangote na sasa hivi tunashuhudia barabara ya kutoka Songea kupitia Madaba – Tunduru – Masasi - Ndada kuelekea Mtwara na yenyewe imekufa almost, kwa sababu ya kupitisha magari makubwa yanayobeba mkaa kutokea Ngapa, Peramiho na maeneo mengine ambako wanachimba madini haya ya makaa ya mawe. Hii ni pamoja na uchafuzi wa mazingira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kwa vyovyote kama tutakuwa tume-concentrate kwenye ujenzi wa reli ya kusini inayoanzia hayo maeneo niliyoyataja kufika Mtwara bandarani, kwanza tutajitahidi kulinda mazingira yetu kwa sababu reli itakuja moja kwa moja mpaka bandari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mchango wangu nitaleta mchango mwingine wa maandishi ambao uko more detailed lakini ninaomba haya ya sasa myachukue na kuona namna ya kuboresha kwenye taarifa yako. Ahsante sana.