Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Florent Laurent Kyombo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkenge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi hii ya kuchangia katika taarifa ambayo imewasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Utawala, Katiba na Sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nashukuru na kuipongeza Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Wizara zote ambazo zinasimamiwa na Kamati. Tumeona kazi kubwa ambayo inafanyika katika kipindi cha mwaka mmoja na hizo ni Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na utawala bora; Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji; Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano; Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu na Wizara ya Katiba na Sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuangalia nia ya dhati ya Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, tunaona jinsi alivyodhamiria kuishi kwa misingi ya Utawala Bora, misingi ya haki na misingi ya utii wa sheria. Katika kipindi cha mwaka mmoja, Kamati yetu imepitia Miswada 12. Ndani ya Miswada hiyo 12, kuna sheria zaidi ya 74. Kwa kuangalia hivyo, inatuambia nini? Ni kwamba Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amedhamiria kusimamia nchi yake katika mfumo wa Utawala Bora, katika mfumo wa utii wa sheria na katika mfumo wa haki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuishi katika haki hizo maana yake Mheshimiwa Rais anaishi katika Falsafa yake ya 4Rs ya kuhakikisha kwamba maridhiano yamekuwepo, uvumilivu umekuwepo na ustahilivu, lakini pia reforms na rebuilding zinakuwepo katika nchi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona, tumekagua miradi mbalimbali, lakini mahususi nitaongelea miradi miwili, na miradi hiyo yote inalenga kupeleka huduma karibu na wananchi, na pia inalenga kutekeleza haki. Tumeona miradi ya ujenzi wa jengo la Kituo Jumuishi cha Kutoa Hati. Katika eneo hili tunaona katika jengo moja Mahakama ya Mwanzo mpaka Mahakama ya Rufani mwananchi akiingia pale maana yake anapata huduma zake zote. Pia na Watendaji wetu wa Mahakama, maana yake akihitaji faili kama ni rufani, ahitaji kuandika kesi ambayo imeenda katika Wilaya nyingine au kitongoji kingine, zote ziko ndani ya jengo moja. Hiyo imerahisisha utoaji wa haki za kisheria. Kwa hiyo, tunayo kila sababu ya kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali yake na wasaidizi wake wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tumeona ujenzi wa Kituo Jumuishi kwa Taasisi za Kisheria. Ukiingia ndani ya jengo moja unamkuta Wakili Mkuu wa Serikali yuko pale, unamkuta Waendesha Mashtaka wako pale, Jeshi la Polisi wako pale, Taasisi zote zinazosimamia sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi siwezi kusema maneno mengine zaidi ya kusema nia ya dhati ya Mheshimiwa Rais ya Utawala Bora, nia ya dhati ya Mheshimiwa Rais ya utii wa sheria, nia ya dhati ya Mheshimiwa Rais ya haki kwa wananchi wake, tunaiona kwa matendo. Tuna kila sababu pia ya kumpongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati yetu ya Utawala, Katiba na Sheria inasimamia Wizara tano kama nilivyotaja, na leo nitajikita katika maeneo makubwa ambayo ni Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu na nitaongelea kwa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano kama muda utaruhusu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya kwanza, katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Uratibu na Bunge nitajikita katika Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Madawa ya Kulevya. Ni lazima nimpongeze Mheshimiwa Rais na wasaidizi wake katika Wizara hiyo ambao ni Mheshimiwa Jenista Mhagama, msaidizi wake Mheshimiwa Ummy Nderiananga, Katibu Mkuu Jimmy na mahususi, Kamishna Jenerali Ndugu yangu Aletas Lyimo, Makamishna Wasaidizi na Watendaji wote wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Madawa ya Kulevya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa imesomwa hapa tumesikia, ongezeko la matumizi ya Madawa ya Kulevya Duniani ni zaidi ya milioni 200 ambayo ni sawasawa na asilimia nne ya watu wote duniani. Tanzania siyo kichaka, tunaendelea pia, suala hili tunaliona ndani ya nchi yetu, lakini tumekuwa na watumishi ambao chini ya Wizara ya Sera, Bunge na Uratibu chini ya Mamlaka ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya wakijituma usiku na mchana, tumeona wanakagua, tunagundua viwanda vya kutengeneza biscuit za madawa ya kulevya, sehemu mbalimbali wanagundua haya mambo yanaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaona katika uchukuaji wa sheria katika eneo hili kuna upungufu mkubwa sana. Katika eneo hili tunazo kesi 9,538. Kwa masikitiko makubwa nasema, kesi 16 tu ndiyo zimechukuliwa hatua, na hizo kesi siyo kwamba zimemaliza, yaani nne tu ndiyo zimemalizika kwa Serikali kushinda, nne tu walipata haki yao wakaruhusiwa lakini nne ziko katika hatua za usikilizwaji, tatu ziko katika hatua za kutajwa na moja iko katika hatua ya kusubiri hukumu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini cha kusikitisha kesi 1,158 ni za mwaka ulioisha 2023. Sasa tunaenda wapi? Tunawekeza fedha nyingi kwa kuhakikisha tunaandaa utaratibu wa Serikali kuchukua hatua dhidi ya madawa ya kulevya lakini sasa pale wanapogundulika waliofanya hivyo hawapewi haki yao au sheria hazichukuliwi. Kwa kweli ukiangalia kesi 938 na 16 tu ndio zimechukuliwa hatua. Tuna jambo la kujiuliza kama Serikali, tuna jambo la kujiuliza kama Bunge. Tuna jambo la kuhakikisha kwamba tunaisimamia Serikali inahakikisha kwamba wenzetu ambao wanasimamia kesi hizi, haya mashauri; tushauri kitu ambacho kitaisaidia Serikali kuchukua hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nakuja na ushauri, maana yake ukiziacha kesi hizi, kwanza zinapunguza imani katika mfumo wa haki; lakini pili, ukiangalia kesi hizi kukaa namna hii maana yake tunaendeleza biashara haramu ya madawa ya kulevya. Pia, ukiangalia katika kesi hizi kukaa hivi maana yake jitihada za kupambana na dawa za kulevya zote kwa kweli zinakatishwa tamaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa hiyo hata watumishi wetu …

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, … ambao wanatakiwa kufanya kazi vizuri maana yake watashindwa kufanya kazi kwa wakati…

TAARIFA

MWENYEKITI: Mheshimiwa Florent kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Ester Bulaya.

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpa taarifa mchangiaji mzuri kwa mchango wake na mbali tu hizo jitihada za upambanaji wa dawa za kulevya kushindwa kuungwa mkono kwa watuhumiwa kuchukuliwa hatua stahiki, sasa hivi wamebuni mbinu mpya ya kwenda kuwauzia kemikali bashirifu kwenye zile center za wale warahibu wa drugs. Mwisho wa siku wanatoka kunywa dawa anarudi tena kutumia kemikali bashirifu ambazo ndio mbaya zaidi, nilikuwa naomba nimpe taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Florent, taarifa unaipokea?

MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa naipokea, ina msingi wa kujenga na kuonyesha lazima tuongeze mbinu za mapambano ili kukabiliana na madawa ya kulevya. Mimi naomba kama ambavyo Kamati tumeshauri, tunaomba Bunge liazimie kuanzisha division maalum ya kushughulikia mashauri ya madawa ya kulevya. Tumeona katika maeneo ambapo division hizi zimeanzishwa kazi kubwa imeendelea kufanyika kupunguza haya mashauri ambayo yako pembeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona division maalum ya ardhi ambayo iliundwa kwa ajili ya kupambana na mrundikano wa kesi za ardhi inaendelea kufanya kazi vizuri lakini tunaona division ya kazi na yenyewe inaendelea kufanya tu vizuri. Kwa hiyo, niombe Bunge lako Tukufu tuanzishe division maalum ya kushughulikia mashauri ya dawa za kulevya kusaidia Taifa letu, kusaidia Mheshimiwa Rais wetu ambaye anataka utawala bora, anataka haki na nchi yetu iweze kusonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho katika eneo hili naomba nichangie katika Ofisi ya Makamu wa Rais, eneo la muungano na eneo hili naomba nitoe pongezi za dhati kwa Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na wasaidizi wake, Mheshimiwa Selemani Jafo, Naibu Waziri wake, Katibu Mkuu. Pia, katika eneo hilo tulikuwa na Hoja za Kamati ambayo ilitakiwa hoja za Muungano 25 ambazo zilikuwepo lakini tunaona asilimia 88 za hoja hizo zote zimejibiwa. Maana yake hoja 22 zote zimejibiwa, tuna kila sababu ya kumpongeza Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia azimio la pili ilikuwa ni kuhakikisha kwamba taasisi zote za kimuungano zinakuwa na ofisi katika pande zote mbili na tunaona utekelezaji wake hapa ni asilimia 97. Maana yake taasisi 33 zote zina ofisi katika maeneo yote mawili ya muungano na taasisi chache zilizobaki tatu ambazo ni TIC, NBS na TEA na zenyewe ziko katika hatua za mwisho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna kila sababu ya kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia kwa utayari wake wa utawala bora, kwa uongozi wake wa kufuati haki lakini na utii wa sheria; na tunaamini tukiendelea kumuunga mkono na haya yote basi yatatimizwa. Basi tunaiona Tanzania njema ya kesho na leo; na watu wote wataendelea kuishi kwa ustawi wa utii wa sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nikushukuru kwa muda wako na naunga mkono hoja ya Kamati na naomba Wabunge wote tuungane kwa ajili ya kuunga mkono hoja za Kamati ya Utawala, Katiba na Sheria, ahsante sana. (Makofi)