Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilolo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote na mimi nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia Hoja ya Kamati na nitajielekeza zaidi kwenye Kamati ya Bunge ya Kudumu ya TAMISEMI. Ninamshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya hasa kwa uwekezaji wa fedha nyingi sana kwenye miradi ya maendeleo katika halmashauri za nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mifano ipo mingi, shule za sekondari za mikoa, kila mkoa fedha zimepelekwa na ujenzi unaendelea lakini kupitia SEQUIP kila halmashauri inaendelea kupokea fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule; lakini wote tunaona miundombinu ya afya pamoja na vituo vya afya pamoja na hospitali na vifaatiba vimepelekwa kwa wingi. Kwa kweli kazi inafanyika na naamini kabisa mwenye macho haambiwi tazama, tunaona mambo megi ambayo yanafanyika, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nichukue nafasi hii pia kumshukuru na kumpongeza Waziri wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI pamoja na Manaibu Mawaziri na Makatibu Wakuu kwa ushirikiano mkubwa wanaoendelea kuonyesha katika utekelezaji wa kazi hizo kwenye maeneo mbalimbali tunapoendelea kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijielekeze kwenye maoni na mapendekezo mbalimbali ambayo yamefanywa na Kamati ya TAMISEMI hasa kwenye upande wa eneo la TARURA. Barabara ni siasa kubwa kwenye nchi yetu hasa maeneo ya vijijini na hali tuliyonayo kwa sasa ni mbaya hasa baada ya kipindi hiki cha mvua. TARURA ilitengewe shilingi bilioni 818, hivi tunavyozungumza zilizoenda ni bilioni 82 tu ambayo ni sawa na asilimia 12, ndiyo fedha zilizopokelewa. Maana yake ni kwamba kuna fedha zaidi ya asilimia 80 ambazo hazijapelekwa na sasa tuko kwenye kipindi ambacho tunaelekea kumalizia mwaka wa fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kabla hatujazungumzia ongezeko la bajeti kutoka hii milioni 800 kwenda trilioni 1.6, hizi fedha ambazo mwaka huu zilitengwa, tunaiomba Serikali na tumeiweka kwenye maazimio ipeleke fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara, fedha ambazo zilikuwepo kwenye bajeti iliyopita; na kwenye azimio hili tumesisitiza sana Wizara ya Fedha kuweka vipaumbele vyake sawa sawa kwa sababu hatuoni kipaumbele kikubwa kwa sasa hivi cha dharura zaidi ya miundombinu ya barabara. Kwenye maeneo mbalimbali ya vijijini, akina mama wanakufa kutokana na kushindwa kusafirisha wagonjwa kwenye maeneo hayo. Mazao yanaoza kwa sababu hatuwezi kusafirisha mazao katika kipindi hiki ambacho barabara zimekatika na kuharibika na changamoto mbalimbali zinazotokana na miundombinu ya barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hatujajua Wizara ya Fedha ina kipaumbele gani kingine kikubwa zaidi ya miundombinu ya barabara kwa sasa, hadi kusababisha fedha asilimia 12 tu ya bajeti ipelekwe hadi kufikia Desemba, ambapo ni nusu ya mwaka, ambapo tulitarajia fedha ambayo imepelekwa ingekuwa angalau zaidi ya asilima 50. Kwenye azimio letu hili lipo na naomba Bunge likubali kuazimia jambo hili lakini baada ya kuazimiwa jambo hili litekelezwe na Wizara ya Fedha mara moja kwa kuipa TARURA fedha ili iweze kutekeleza majukumu yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la elimu yako mambo mawili ya muhimu pamoja na ujenzi wa miundombinu mizuri, halmashauri zimepokea fedha nyingi sana kutoka Serikali Kuu na kwa sababu zimepokea fedha nyingi sana kutoka Serikali Kuu na ujenzi wa madarasa umefanyika vizuri kuna changamoto mbili. Kwanza ni madawati lakini pili ni miundombinu ya vyoo kwenye shule za msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa halmashauri zimekwisha kusaidiwa ni muhimu sasa TAMISEMI kuangalia halmashauri zote kuja na mkakati wa kumaliza tatizo la madawati kwa kupitia mapato ya ndani kwa sababu tayari wameshasaidiwa madawati; kwa sababu tayari wameshasaidiwa miundombinu ya madarasa. Kwa hiyo katika eneo hili, katika bajeti ijayo miundombinu ya vyoo pamoja na madawati iwe ni kipaumbele kwenye sekta ya elimu kwa sababu kama madarasa ni mazuri basi na miundombinu ya vyoo iwe mizuri na madawati yawepo ili watoto wetu waendelee kuwa kwenye mazingira mazuri ya elimu na waweze kuendelea na masomo vizuri. Hili pia tumeliweka kwenye maazimio na nina hakika Bunge litaazimia na kupitisha ili liweze kutekelezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mwenyekiti wa Kamati ya TAMISEMI anawasilisha aliataja suala la halmashauri mbalimbali kujifunza kuhusu kutunza misitu ya asili kwa ajili ya uvunaji wa hewa ya ukaa. Ningependa kutoa mfano mmoja wa Halmashauri ya Kilolo, Hifadhi tu za misitu ya Kijiji, Halmashauri ya Kilolo ni hekta 50,531 lakini hapo nimeacha kutaja hekta za TFS ambazo ni 198.599. Ninaamini hii ni moja kati ya halmashauri zenye eneo kubwa sana la hifadhi ya misitu ya asili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale TAMISEMI kuna kitengo nafikiria au idara kuna mtu anashughulika na kuanzisha hii miradi ya uvunaji ya hewa ya ukaa na kuna halmashauri nyingi ambazo zingeweza kukusanya mapato zaidi ya mapato yake ya ndani kwa kupata fedha kutokana na uvunaji wa hewa ya ukaa na tayari kuna halmashauri chache zimeshaanza kunufaika. Tunachojiuliza ni nini kinachelewesha TAMISEMI pamoja na Ofisi ya Makamu wa Rais, Wizara ya Mazingira kuwekeza katika kuhakikisha kwamba halmashauri zote zenye misitu ya asili zinaingia kwenye uvunaji wa hewa ya ukaa ili kujiongezea mapato, kwa sababu jambo hili lingeweza kupunguza sana gharama za unedeshaji wa halmashauri kwa kutoa fedha kwenye Serikali Kuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hii jambo limetajwa pale kwenye taarifa yetu na tunasisitiza na kuiomba TAMISEMI pamoja na Wizara ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na Muungano kuliangalia na kuangalia ni mkakati upi unaweza ukafanywa ili halmashauri zote zenye misitu ya asili na imezitunza kuweza kuingia kwenye uvunaji wa hewa ya ukaa kwa kufuata miongozo ilipo. Ni kwa nini halmashauri chache zipate mabilioni ya pesa na halmashauri zenye misitu mikubwa kuliko hata hizo zinazopata zenyewe hazijaanza. Ni nini kipo hapo? Na kwa nini hakiwezi kutatuliwa? hilo tungeomba liweze kufanyiwa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapoelekea kumalizia nitaje mambo mawili ya muhimu. La kwanza ni suala zima la kuwa na mwongozo mzuri wa posho za viongozi katika ngazi za vijiji na ngazi ya kata, hasa kwa sababu kwa sasa kuna halmashauri nyingi viongozi hao hawapati posho zozote. Kwa hiyo ni lazima tuwe na mwongozo …
MHE. ROSE V. BUSIGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: …ili viongozi hao waweze kupata posho katika…
MHE. ROSE V. BUSIGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: …kwa kufuata mwongozo uliotolewa na TAMISEMI. Kwa sasa inakua ni changamoto kubwa kwa sababu…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Lazaro…
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: …hakuna mwongozo wowote…
TAARIFA
MWENYEKITI: Kuna taarifa kwa Jirani yako.
MHE. ROSE V. BUSIGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa Kaka yangu mchangiaji, kwanza Serikali yetu ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan iliridhia kabisa Watendaji wa Kata waweze kupewa posho za madaraka, lakini pamoja na hiyo sambamba na hivyo halmashauri nyingi hawawapi posho za madaraka kwa wakati.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Justin Lazaro, taarifa unaipokea? Malizia mchango wako.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea na kuongezea tu pamoja na hilo kwa sababu ni muda mrefu umepita, madiwani pia posho zao hazijafanyiwa mapatio. Kwa hiyo tunatarajia kwenye bajeti ijayo Serikali italeta mapendekezo ya nyongeza ya posho za madiwani lakini na mwongozo mzuri wa ulipaji wa posho kwa viongozi wa ngazi za vijiji na viongozi wa ngazi za vitongoji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja zote mbili, ahsante sana. (Makofi)