Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Eng. Ezra John Chiwelesa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Biharamulo Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niwe miongoni mwa wachangiaji katika taarifa zetu hizi mbili ambazo zimewasilishwa na Kamati. Kipekee niwapongeze sana Wenyeviti wetu wote wawili kwa uwasilishaji mzuri kwa niaba ya Kamati zao lakini pia nipongeze Mawaziri na Watendaji wote kwa kazi nzuri ambazo wanaendelea kuzifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee mimi nitajikita kwenye upande wa Wizara ya TAMISEMI na kwa sababu ya muda, nitaenda moja kwa moja kwenye sehemu ya TARURA. Tukiangalia ukurasa wa 37 wa taarifa ya Kamati, imejaribu kutupa kwa kina mchanganuo wa barabara ambazo zinahudumiwa katika nchi hii; barabara za lami, barabara za changarawe na barabara za udongo. Sasa tunaona asilimia zaidi ya 69 ya barabara katika nchi hii zinazohudumiwa na TARURA bado ni barabara za udongo, lami ni asilimia 2.23; na changarawe ni asilimia 28.46.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukijaribu kuangalia hali zetu mnazijua, tunaposema udongo, udongo hata ukimwaga maji tu ya kawaida ule udongo unaondoka. Sasa unaweza uka-imagine hali ya mvua kama hii ambayo tumekuwepo nayo katika kipindi hiki na ni mateso kiasi gani wananchi wa nchi hii wanapata shida. Kama barabara za lami zinaharibika udongo ukoje? Kwa hiyo picha tunayoondoka nayo hapa, kwa sababu mvua inanyesha nchi nzima maana yake ni kwamba zaidi ya asilimia 70 ya miundombinu ya nchi hii ipo taabani na iko katika hali mbaya, kwa sababu taarifa yenyewe inasema zaidi ya asilimia 69 ni udongo. Maana yake maeneo yote yenye barabara za udongo leo hayaingiliki wala hayafikiki na nyote ni mashahidi tuko hapa wananchi wetu tunajua yanayoendelea majimboni huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kidogo nilitaka tujikite hapa tujaribu kuchambua na kuona ni jinsi gani tunaweza tukawatoa wananchi hawa wa Tanzania katika lindi hili kubwa ambalo limewakwamisha na zaidi linawarudisha nyuma. Linawarudisha nyuma kwa sababu bila miundombinu mizuri no matter what you are doing, mimi kama siwezi kutoka nyumbani leo, umejenga kituo cha afya lakini mvua imenyesha hamna daraja, nafia ndani kwa sababu sintoweza kuvuka kwenda kwenye kituo cha afya. Umejenga shule watoto hawawezi kwenda shule kwa sababu ya miundombinu mibovu. Umejenga masoko na vitu vingine vyote vizuri watashindwa kusafirisha mazao toka mashambani wayafikishe kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo unapokuwa huna miundombinu maana yake unakwama completely na unabaki kule chini. Kwa hiyo cha kwanza focus yetu kubwa kupitia Wizara hii ya TAMISEMI ni lazima tuangalie jinsi tunaweza tukawasaidia TARURA wafanye kazi zao na kazi hazifanyiki bila pesa, maana kazi hizi za ujenzi ni pesa, mafuta yanahitajika kwenye mashine ni pesa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikiliza ripoti hapa tunasema wakandarasi wanasuasua wengine hawana mitambo, wengine hawana nini; akini nikwambie wakandarasi wa nchi hii ni wazalendo na Wabunge ingebidi tuwapigie makofi kuwapongeza. Kwa sababu wanafanya kazi kubwa na wanamadeni mengi sana ambayo hawajalipwa ni lazima tusema tu, tusipowasemea sisi nani atawasemea? Kwa sababu kama leo ndani ya Bunge ripoti inasema zaidi ya kazi ambazo zimefanyika ni zaidi ya bilioni 339 exchequer imekuja zaidi ya bilioni 339 lakini barabara tunachojua kwa TARURA walishatangaza mpaka asilimia 80 ya barabara zote walikuwa wametangaza ilibaki asilimia 20.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nina uhakika asilimia 80 ya zile barabara zilizotangazwa wakandarasi wako site na wanaendelea na kazi lakini kama watu wamefanya kazi kwa asilimia 80 au hawajafikisha bado wanaendelea, wewe pesa uliyoleta ikawafikia na asilimia 12, leo huyo mkandarasi huyo unamlaumu na nini? Wakandarasi wamekopa kwenye mabenki, ni benki gani itakupa pesa kama hurejeshi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, pamoja na mpango mzuri wa kuja na hiyo Samia Infrastructure Bond lakini kama hatutapanga mpango mzuri wa kuwalipa wakandarasi, mimi nakwambia ukweli watashika hizo barabara lakini barabara zitaishia njiani. Sasa tuombe, tuiombe Serikali hasa Wizara ya Fedha yaani leo unapofanya prioritization yako wewe ukifanya vipaumbele vyako wewe, huwezi kufanya vipaumbele ukasahau miundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Wabunge tunaondoka hapa tunarudi majimboni, inabidi turudi tukafanye ziara tuwaambie wananchi ni vitu gani tunarudi navyo, tukakusanye mawazo yao kwa ajili ya Bunge la Bajeti. Unafikaje huko? Kila mwananchi anakwambia barabara haifikiki, ukirudi leo jimboni unaenda kuongea nini? Ukirudi jimboni unaitisha mkutano watu hawawezi kufika, madaraja hamna barabara zote zimeharibika unawaambia nini? Na ukifika hapo, wakandarasi tena wanaodai huwezi kuwaita kwa sababu wao bado wanakudai pesa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tulikuwa tunaomba Wizara ya Fedha, katika maazimio ambayo tunayo kabla ya Ijumaa tunapoondoka hapa, hili jambo siyo la kusubiria tuje tupewe taarifa mwakani, kwa sababu ni jambo la kibajeti, tulipitisha hapa tukaongezewa milioni 350. Tukaondoka tukaenda majimboni tukawaambia wananchi, Mheshimiwa Rais kaongeza pesa bilioni 350 kwa kila jimbo tulikuwa tunategemea tupate milioni mia tano, mia tano. Tukachagua na barabara za kwenda kujengwa tukasema kwenye mikutano tukimtaja Rais kwa maendeleo haya na pesa aliyoiongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo pesa hiyo bilioni 350 haijaja hata moja, Wabunge hatujaulizwa barabara, tumejaribu kukaa na mameneja wetu tukapanga zikija tutafanya hivi. Tumeenda tumefanya mikutano tukawaambia wananchi, tukachagua na barabara tulizotaka zikajengwe kwa hiyo milioni 500, unarudije leo ukiwa imebaki miezi minne kwa wananchi kuwaambia ile nilikuambia habari njema ya bilioni 350 haipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachonganishwa na Mheshimiwa Rais anachonganishwa kama tunafanya hivi, if that money wasn’t there ingebidi watuambie haipo lakini hatuwezi kuondoka hapa katika Bunge, tumekaa hapa tumepitisha bajeti tunaenda tunawaambia wananchi kuna pesa imeongezeka yet mpaka leo hatuambiwi ni barabara gani zinajengwa, hatuambiwi pesa inakuja lini? This is not fair, siyo fair kwa Mheshimiwa Rais lakini si fair kwa wananchi ambao tunawawakilisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikua naomba hili tulione…

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, katika maazimio ambayo tunataka tuondoke nayo…

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina wazo, nina wazo la kusaidia TARURA. Ukijaribu kuangalia barabara nyingi za vijijini zinajengwa kwa upana.

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Engineer Ezra, kuna taarifa.

Waheshimiwa Wabunge niwakumbushe taarifa ni sehemu ya mchangiaji lakini pia inatolewa kwa idhini ya kiti, kwa hiyo Mheshimiwa Tarimba taarifa kuwa ufupi.

TAARIFA

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ufupi sana, nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa mchango wake mzuri sana. Nilitaka nimuongezee tu katika mchango wake kwamba kuomba barabara siyo hisani, barabara ina mkono wa moja kwa moja na uchumi wa Nchi hii. Siyo tu kwamba inakwenda kutusaidia sisi majimboni lakini inasaidia uchumi wa Tanzania ilivyo hivyo Serikali haina hiari kusema ipeleke fedha ama isipeleke mathalan Bunge hili lilitangaza na kutoa maamuzi kwamba fedha ziende basi Serikali ipeleke, ahsante sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa, taarifa ilitakiwa iwe fupi; Mheshimiwa Engineer Ezra taarifa unaipokea?

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeipokea hiyo ni nyama kabisa nyongeza nzuri nimeipokea. Sasa nataka nitoe ushauri wa kitaalamu. Barabara zote za nchi hii especially upande wa TARURA zinajengwa kwa upana wa mita 6.5 hadi mita saba lakini standard ya magari katika dunia na utengenezaji; gari dogo kabisa lina upana wa mita 1.8, zile gari kubwa semi zina 2.4 meters.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unajiuliza huko kijijini unajenga barabara ya mita saba, barabara ya mita sita matokeo yake tairi zinakuwa zinapita tu pale katikati ya barabara huku pembeni majani yameota na huku pembeni majani yameota. Umejenga daraja la upana wa mita saba huko kijijini ni la nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka TARURA waende kwenye standard zinazoendana na mahitaji ya wananchi kule vijijini. Waweke upana wa barabara 4.5 meters au five meters na daraja likiwa vile tutajenga madaraja mengi na barabara zitakuwa ndefu zaidi. Ina maana hii plan ya kwenda kufika mbele zaidi itaweza kufikiwa kwa haraka zaidi, kuliko leo unajenga barabara pana baada ya muda majani yameota huku, yameota huku wakati eneo lote lile lililipiwa. Hiyo nayo bado ni hasara ambayo tunaipata. Kwa hiyo wa-review ili waweze kuona kwamba twende kwa barabara finyu lakini zinazoweza kwenda mbele zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimeomba kwenye hili. Tunachoomba wakati tunamalizia hapa Ijumaa kwenye maazimio ambayo Bunge linaleta hapa tupate majibu ya shilingi bilioni 350 za nyongeza na tupate majibu ya fedha yetu ya bajeti hii ambayo imeenda asilimia 12. Hizi fedha zinatolewa lini na hiyo iwe ndani ya maazimio ya Bunge Serikali itujibu hapa siku ya Ijumaa wakati Bunge linahitimishwa ili tunaporudi majimboni tukawaambie wananchi nini kinafanyika kwa habari ya barabara kabla ya mwezi wa saba.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru ahsante sana kwa nafasi na ninaunga mkono hoja. (Makofi)