Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Salome Wycliffe Makamba

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kunipa nafasi. Mimi niseme mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya TAMISEMI na ningependa kuchangia pale alipoishia Mheshimiwa Mwenyekiti wetu wakati anawasilisha taarifa yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama nchi tuna changamoto kubwa sasa hivi tunayoipitia. Tuna janga na si changamoto, ni janga kubwa sana la uharibifu mkubwa wa miundombinu. Hapa hatupepesi macho, changamoto ni kwamba watu wanaohusika na kutengeneza barabara hawajapelekewa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sisi tuko hapa Wabunge tunashauri, kwenye Kamati tulimwita Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI kwa nini barabara hazitengenezwi? Changamoto ni fedha, wenyewe wameshafanya tathmini wanataka shilingi bilioni 131 kuweza kukabiliana na changamoto ya barabara zilizoharibika na miundombinu yote ya barabara nchi nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, anayetoa fedha ni Hazina, hapa hayupo Waziri wa Fedha, hakuna Naibu Waziri wa Fedha tutapata wapi haya majibu?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa hivi wametoa shilingi bilioni 21 tu…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mbunge, Serikali ipo Bungeni kwa hiyo usiwe na wasiwasi endelea kuchangia. (Makofi)

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilishauri kwenye Kamati aitwe Waziri wa Fedha atuambie tunapata wapi shilingi bilioni 131 kwa ajili ya kutengeneza barabara za nchi hii? Hakuja kwenye Kamati. Nikawa namsubiri nije nimwambie Bungeni, hayupo; sasa nitaenda kumwambia wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka kitokee nini ili tujue kwamba kuna dharura? Madaraja yameshakatika, barabara zina mashimo, ajali zimetokea. Juzi Shinyanga pale kwangu Mto Mumbu, mtu amesombwa na maji na mafuriko, amekufa. Tunataka kitokee nini ili tujue kwamba jamani tuko kwenye hali ya dharura? Mheshimiwa Aida anasema kwake Nkasi watu wameshakufa kule, Dar es Salaam watu wanakufa; tunataka kitokee nini? Kazi ya Serikali ni kuwahudumia wananchi na kuhakikisha wako salama. Nchi ipo kwenye janga, iko kwenye changamoto, shilingi bilioni 131 zinatakiwa… (Makofi)

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MHE. SALOME W. MAKAMBA: …mpaka sasa hivi wamepeleka shilingi bilioni 21 tu kwa ajili ya kwenda kutatua hali ya dharura.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Salome, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Naibu Waziri, Mheshimiwa Dkt. Festo Dugange.

TAARIFA

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na ninatambua mchango mzuri wa Mheshimiwa Salome Makamba. Naomba tu nimpe taarifa kwamba kazi ya utengenezaji wa barabara zilizoharibika katika maeneo mbalimbali kutokana na mvua zinaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kasi yake kwa mfano Dar es Salaam; Kibamba wamepata, Kawe wamepata na maeneo mbalimbali wamepata. Kwa hiyo nimhakikishie tu kwamba pamoja na kwamba kuna uharibifu mkubwa lakini Serikali haijalala inaendelea kufanya matengenezo ya barabara hizo na hali itakwenda vizuri, ahsante. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana; Mheshimiwa Salome taarifa hiyo unaipokea?

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri, mimi naomba utulie tu nikusaidie kwa sababu tuna changamoto. Nina ripoti ya Mheshimiwa Waziri hapa kuja kwenye Kamati anasema, tathmini imefanyika nchi nzima, halmashauri 184 hali ya uharibifu ili tuweze kurekebisha hiyo hali inatakiwa shilingi bilioni 131. Mpaka sasa hivi Serikali imepeleka shilingi bilioni 21 out of 131 unasema nchi kazi inaendelea au ndio hao wakandarasi wazawa mnawakopa hela wanafanya kazi wanaendelea kufilisika? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, we have a serious problem sisi kama nchi na tukifanya maigizo well and good, lakini kama jambo limeshatishia uhai wa wananchi, kama jambo limeshatishia usalama wa nchi, kama jambo linatingisha uchumi wa nchi hakuna muujiza. Yaani ni kwamba tukirudi hapa bajeti ijayo mtakusanyaje hizo fedha kwa ajili ya kutengeneza bajeti? (Makofi)

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Salome, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Patrobass Katambi.

TAARIFA

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mchango mzuri wa Mheshimiwa Mbunge; ni kweli kwamba Watanzania wanapata changamoto kutokana na majanga ambayo yanaendelea. Uhalisia ni kwamba TMA (Tanzania Meteorological Agency) ilitangaza uwepo wa mvua za El Nino, na uwepo wa mvua hizi umesababisha majanga makubwa karibia nchi nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata katika fedha iliyokuwa imetengwa ya bajeti ambayo ilikuwa ni kwa ajili ya dharura tume-burst, kufikia hatua kwamba fedha zile hazitoshi tena kulingana na uharibifu mkubwa ambao umetokea. Kwa hiyo taarifa yangu ni kwamba Mheshimiwa Mbunge ajue kwenye mazingira ya dharura kuna vitu vinaitwa natural catastrophes ambazo ni majanga asilia ambayo hakuna mtu yeyote alipanga mvua za El Nino zitokee. Ikitokea majanga kama hayo nchi yoyote inaweka utaratibu wa kuhakikisha inakabiliana nayo. Kwa hiyo ni majanga wala siyo kwamba ni Mpango wa Serikali inapanga hivyo. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana; Mheshimiwa Salome taarifa hiyo unaipokea?

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi hiyo taarifa siipokei, nataka tu nimsaidie kaka yangu pale, Mheshimiwa Katambi. Bajeti iliyopita kwenye TARURA waliomba wapewe 1.6 trillion, wakapewa shilingi bilioni 800 na ushee tukatenga. Akaja Waziri wa Fedha akatulaghai kwamba anaiongezea TARURA shilingi bilioni 350. As I speak right now wakili msomi wamepewa shilingi bilioni 89 tu. Ile 800 hawajapewa, tuliyodanganywa hapa wameongezewa 350 hawajapewa, hiyo hela unayosema inaenda kufanya mambo ya natural catastrophes haifiki hata asilimia 10 ya target ambayo tunayo. Sasa si tunafanya mzaha? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tuchukulie jambo la miundombinu ya barabara kwa udharura wake. Kamati ya Miundombinu, Kamati ya TAMISEMI, Kamati ya Bajeti na Kamati ya Fedha ni lazima tukae tuje na msimamo wa Bunge. Nini kifanyike kutatua changamoto ya barabara kwenye hii Nchi? Watu wameshakufa, ajali zimeshatokea, uchumi umeshatetereka inatosha kulifanya jambo hili kuwa ni jambo la dharura na kuchukuliwa kwa uzito wake. Sisi kama Bunge tuishauri Serikali juu ya jambo hili, unless otherwise sisi tutaonekana tumeshindwa kuishauri Serikali katika jambo hili la dharura, tutaonekana tumeshindwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwa wakandarasi wazawa. Mheshimiwa Waziri amekuja na wazo zuri sana la TARURA Samia Bond, lakini nikwambie tu changamoto siyo bond, changamoto ni sheria mbovu ambazo zinawabana wakandarasi wetu wanashindwa kufanya kazi za Serikali. Leo mkandarasi atapata kazi ya kujenga barabara anaambiwa nenda kalete bank guarantee, anaambiwa nenda kalete sijui nini ya benki. Yaani kabla hajaanza kujenga Barabara asilimia 80 ya fedha zake ameenda kuziweka kama bond benki ili aweze kupata guarantee akafanye hiyo kazi; atafanyaje kazi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naelewa miradi mingi hasa inayotekelezwa kwa fedha za wahisani inakuja na masharti magumu lakini you scratch my back I scratch yours. Kama wanataka kutupa misaada watupe misaada ambayo inatufaa na inayowanufaisha wakandarasi wetu wazawa. Ni lazima tufanye mapitio ya sheria kuhakikisha Watanzania wananufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachi zote zinazoendelea duniani mtaji wao namba moja ni population yao. Population ya Watanzania tumefika milioni 60 na kitu. Tukiwawezesha wakandarasi wazawa angalau watano tu (makampuni matano kwenye kila mkoa) lazima tutoboe, yaani lazima tufanikiwe. Hakuna muujiza kwenye hilo. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Salome, muda wako umekwisha.

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.