Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kishapu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili mradi nami niweze kutoa mchango wangu. Kwanza naomba kuwapongeza sana Waheshimiwa Mawaziri wa Wizara tano ambazo Kamati yetu ya Utawala, Katiba na Sheria zimekuwa zikitoa taarifa ama tumekuwa tukifanya nazo kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kati ya mambo makubwa ambayo wamekuwa wakifanya na katika kipindi hiki wamefanya mambo makubwa sana ni kutoa taarifa njema na hasa katika utekelezaji wa maagizo mbalimbali ambayo katika kipindi cha mwaka mzima uliopita kwa sehemu kubwa sana yameweza kutekelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma ni moja kati ya Wizara ambazo ziko chini ya Kamati yetu ya kudumu chini ya Dkt. Mhagama. Vile vile Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji; Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira na pia Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Mipango, na hii chini ya Mheshimiwa Jenista Mhagama pamoja na Mheshimiwa Nderiananga wamekuwa wakifanya kazi kubwa sana katika kusimamia mambo mbalimbali katika Wizara yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuna Wizara ile ya Katiba na Sheria, unaweza ukaona ni majukumu makubwa ambayo Kamati imekuwa ikifanya wakati wote, lakini tunashukuru kwamba uwezeshwaji wa Bunge kwa maana ya Mheshimiwa Spika, Kamati imekuwa ikitekeleza majukumu yake sawa sawa, na mambo mbalimbali, hata ya Miswada mmekuwa mkishuhudia kwamba Kamati imekuwa ikitekeleza wajibu wake vizuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuanza na upande wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, yako majukumu makubwa ambayo yamekuwa yanafanyika na hasa suala zima la miradi ya kimaendeleo. Ipo miradi ya kimaendeleo ambayo katika hali ya mapambano ya tabianchi, tuna miradi mikubwa ambayo imekuwa ikisimamiwa kupitia mradi wa EBA na Wizara hii imekuwa ikisimamia pakubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hiyo ni pamoja na baadhi ya halmashauri hapa nchini ambazo zimekuwa zikihudumiwa. Halmashauri hizi ni pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu. Miradi mizuri, mikubwa na fedha nyingi zimekuwa zikitolewa katika halmashauri hizi kwa ajili ya mapambano ya hali ya tabianchi. Unaweza ukaona katika Wilaya ya Kishapu tumepokea shilingi bilioni 1.7 katika kipindi cha miaka mitatu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi ni fedha nyingi sana na moja kati ya mambo makubwa ambayo yamekuwa yakifanyika ni pamoja na kujenga mabwawa makubwa, viwanda vidogo vidogo vya kuchakata ngozi na madume bora ya kisasa ya aina ya borani. Masuala ya uwezeshaji wananchi, ziko mashine zimeanzishwa za kuchakata mafuta na mashine za kuchakata nafaka mbalimbali. Pia wamekuwa wakienda mbali zaidi ikiwa ni pamoja na kuwawezesha wananchi kupata eneo kwa ajili ya ufugaji wa kisasa na uwekezaji mwingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, yanafanyika mambo makubwa na unaweza kuona kwamba Wizara hii chini ya Mheshimiwa Jafo na ndugu yangu Chilo wamekuwa wakifanya kazi kubwa sana kusimamia shughuli za miradi hii na imekuwa ni miradi inayowanufaisha sana wananchi na kuwakwamua kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuzungumzia masuala mengine ambayo yanasimamiwa na Wizara hii chini ya Makamu wa Rais, ni pamoja na kushughulikia masuala mazima ya utatuzi wa kero mbalimbali ambazo zimekuwa zikiwepo pande mbili za Muungano. Tangu kuanzishwa kwa utaratibu huu wa kutatua changamoto hizi za Muungano, sote tunafahamu, kati ya changamoto ambazo zilikuwepo 25 mpaka sasa 22 zimeshatatuliwa. Unaweza ukaona tumebakiza mambo makubwa matatu tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jitihada kubwa sana inayofanywa na Mawaziri hawa na timu ya wataalam ambao kwa kweli na sisi tunaendelea kuomba Mwenyezi Mungu awasaidie, tuna uhakika baada ya muda mfupi historia kubwa iliyokuwepo kati ya pande mbili kutokana na hizi changamoto zilizokuwepo, sasa kero hizi za muungano itakuwa ni historia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Rais kwa sababu ukweli ni kwamba amekuwa akiwezesha, kwanza, kuhakikisha kwamba timu hizi za pande zote mbili zinakutana kila wakati na wanapokutana wanatoka na suluhu kila wakati. Kwa hiyo, ni jitihada kubwa sana na hivyo tunauona Muungano wetu unaendelea kustawi na tuna uhakika kwamba baada ya kipindi kifupi sasa tutakuwa tunazungumza kama historia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya taasisi 36, taasisi 33 tayari ufumbuzi umeshapatikana. Kuna taasisi tatu tu ambazo zimebaki, lakini unaweza ukaona ni jitihada kubwa sana ambayo imefanywa chini ya usimamizi wa Wizara hii. Pia, yako mambo mengine mengi ambayo ni ya kiutawala wanayokwenda nayo vizuri, nawapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka nizungumzie upande wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge, Sera na Uratibu, jitihada hizi zinafanyika vizuri sana. Naomba kumpongeza sana Mheshimiwa Jenista na Naibu Waziri Nderiananga, kazi wanayofanya ni kubwa. Sisi sote ni mashahidi, moja kati ya matukio makubwa ambayo yalipatikana hii juzi na hasa kule Hanang, jitihada kubwa iliyofanyika ya hawa Mawaziri, Katibu Mkuu na viongozi wengine na Wizara nyingine walioshirikiana kwa pamoja, jitihada kubwa ya uokozi imefanyika ikiwa ni pamoja na kurudishia miundombinu katika mji wetu wa Hanang. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, unaweza ukaona Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania naye pia ameweza kufika akazungumza na wahanga. Rais wetu kwa moyo wa upole, kwa moyo wa huruma, kwa kweli ameonyesha jitihada kubwa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba miundombinu ya kijiji kile ambacho kimekwanguliwa kabisa na maji hayo sasa unarudishwa. Kwa hiyo, kijiji kile na maeneo hayo ambayo nyumba zake zimeharibiwa, Serikali ya CCM chini ya Rais wetu mpendwa Mama Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuhakikisha kwamba maeneo yale yanarudishwa kama kawaida. Sasa hivi jitihada zimeshaanza kwa ajili ya kuhakikisha maeneo hayo yanarudishiwa ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba za makazi ya watu hao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hili tunawapongeza sana kwa kweli kwa jitihada hizo nzuri zinazofanyika. Tunaomba katika maeneo mengine, kwa sababu mvua hizi zinaendelea kunyesha na matukio ya maafa yamekuwa yakijitokeza maeneo mengine, tunaomba wafanye jitihada kubwa za kuhakikisha kwamba uratibu na ufuatiliaji ili mradi Watanzania wajisikie na waone matunda ya Serikali ya CCM wakihudumiwa vizuri, waendelee nayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna eneo lingine ambalo ni la madawa ya kulevya. Eneo hili mapambano yake ni makubwa, sisi sote Watanzania tumekuwa mashuhuda. Jitihada za kupambana na madawa ya kulevya zinafanyika kubwa. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni kama Mungu kamjaalia kwa sababu ameteua Kamishna Jenerali ambaye anashughulika na masuala haya ya madawa, ndugu yetu Lyimo, anafanya kazi kubwa sana na Mwenyezi Mungu kwa kweli amlinde ampe afya njema. Nami naomba kumtia moyo kwa moyo wake wa kizalendo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu yale yanayofanyika ikiwa ni pamoja na kwenda kuyabaini mashamba ya bangi, kukamata madawa ya kulevya ikiwepo unga, heroine na mambo mengine mengi ikiwa ni pamoja na mirungi. Sote tunaona kwa macho yakikamatwa madawa, wakikata mazao ya bangi, jitihada hizi ziko wazi na taarifa zimeonekana ziko wazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru sana kwa sababu tunauona uzalendo wake na sisi tunamwombea kwa Mwenyezi Mungu, nami namtia moyo Mheshimiwa Rais kwa kweli kwamba aendelee kuwezesha Idara hii inavyotakiwa, nasi kama Wabunge kwa kweli tuna-support sana jitihada kubwa inayofanyika kwa ajili ya kuwakomboa Watanzania na hasa wanaoathirika na madawa ya kulevya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mengine ambayo nataka nizungumzie kwa kweli, nataka nigusie kwa upande wa TAMISEMI. Eneo hili la TAMISEMI na hasa upande wa TARURA kuna kila sababu ya kuhakikisha suala la fedha tunazokuwa tunatenga ama tunazopitisha kama bajeti kama Bunge ni lazima zipelekwe katika maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeweka zaidi ya shilingi bilioni 880, lakini mpaka sasa fedha zilizokwenda kwa kweli ni aibu. Nataka niseme, kazi ya Bunge ni pamoja na kuishauri Serikali na kuielekeza juu ya mambo ya msingi yanayotakiwa kufanyika. Sisi tunasisitiza fedha zitolewe ziende kule zikasaidie halmashauri. Leo ninavyozungumza, Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, kata sita kati ya kata 29 hazipitiki, lakini ni kwa sababu, kwanza, ni ucheleweshaji wa fedha zile ambazo ni za kibajeti zilizokuwa zinatakiwa zipelekwe, hazijapelekwa kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata sasa hivi pamoja na uharibifu wa mvua kubwa zinazoendelea kunyesha, jitihada yoyote haipo. Sasa kama lipo tatizo tunashauri kama Bunge, ni lazima tuwasaidie wananchi. Watanzania wanalia, wanakosa barabara za kusafirisha wagonjwa, wanakosa barabara za kusafiri wao wenyewe, wanakosa barabara za kusafirishia mazao na vitu vingine. Lazima Serikali katika hili isikie na ione umuhimu wa kuhakikisha barabara zinafunguliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna zile shilingi bilioni 305 zilizoongezwa ambazo kimsingi sisi Wabunge huwa tunashauriana na mameneja wetu wa wilaya kuona ni namna gani tushughulike na matatizo ya barabara. Tunaomba sana fedha hizi na zenyewe zitolewe. Zimesaidia sana katika kipindi kilichopita, tumefungua madaraja, nyingine tumepeleka kwenye lami, miji midogo. Fedha hizi zinapochelewa, zinachelewesha sana jitihada za maendeleo na hasa ufunguzi wa barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nilitaka kuzungumzia upande wa TAMISEMI ni upande wa Waheshimiwa Madiwani. Mimi ni Diwani kwa mujibu wa taratibu, lakini kinachofanyika siyo. Tangu tumeanza Bunge hili katika kipindi hiki cha mwaka 2020, kila mwaka tumekuwa tukizungumza juu ya jambo hili. Tatizo liko wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kusema, tusifike mahali tukaonekana tunavutana. Nashauri sana jambo hili katika kipindi cha mwaka huu wa bajeti tutakaoanza kufanya…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli ni kwamba fedha hizi kwa ajili ya kuwasaidia Madiwani ziweze kutengwa na tuwaongezee kiasi cha posho ili mradi na wao weweze kujisikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)