Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Margaret Simwanza Sitta

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Urambo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami nichangie hoja iliyoko Mezani. Kwanza kabisa, naunga mkono taarifa nzima ya Kamati hii na niseme wazi kwamba nami pia ni Mjumbe wa Kamati ya TAMISEMI. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa aliyofanya hasa kwa upande wa elimu, afya, barabara na mengi ambayo ameyafanya kwa ajili ya maendeleo ya nchi hii, hongera sana Dkt. Samia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naishukuru Serikali anayoiongoza kwa kumpongeza Mheshimiwa Mchengerwa, Manaibu Waziri, Makatibu Wakuu, Wakuu wa Idara mbalimbali na vitengo, hongereni kwa kazi kubwa sana mnayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono kipengele kimojawapo ambacho wenzangu waliotangulia wamekiongea kwa uchungu na kuonyesha ukweli kwamba kinahitaji kufanyiwa kazi, suala la barabara vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, TARURA ina umuhimu sana kufanya kazi kwa bidi. Naipongeza pia TARURA kwamba inafanya kazi kubwa na ni kutokana na uwezo wanaopewa na Serikali. Kipindi hiki cha mvua, barabara nyingi za vijijini zimeharibika. Kwa msingi huo naunga mkono Maazimio yaliyotolewa na Kamati yangu kwamba Serikali itoe fedha ili barabara zilizoharibika zitengenezwe haraka iwezekanavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiomba Serikali yetu sikivu kweli itenge fedha haraka sana ili TARURA iweze kutengeneza barabara ambazo sisi wote ni mashahidi kwamba mvua aliyotupa Mwenyezi Mungu mwaka huu zimeharibika. Kwa hiyo, zinahitaji kurudishiwa madaraja na kadhalika ili wananchi wa vijijini na hata na mjini pia waweze kufanya kazi zao kikamilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikirudi kwa upande wa elimu, unapozungumzia shule, ni walimu na wanafunzi, yale mengine yote yanayoongezeka; madarasa na nini ni kusaidia ili elimu itolewe vizuri, lakini unapozungumzia elimu ni walimu na wanafunzi. Ukiangalia kazi kubwa aliyoifanya Mheshimiwa Dkt. Samia ya kujenga madarasa, kwa kweli ni kazi kubwa sana lakini inahitaji walimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa msingi huo, naomba kuchukua nafasi hii pia kuunga mkono Maazimio yaliyotolewa na Kamati kwamba Serikali ifanye iwezavyo, walimu wapatikane ili miundombinu iliyojengwa na Mheshimiwa Dkt. Samia ya madarasa na kadhalika iweze kutumika iwezekanavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia walimu hasa vijijini, wanakaa mbali sana na ndiyo maana neno linalotumika mara nyingi, ni shule shikizi. Zile shule shikizi ni mahali ambapo ni katikati ambako hakuna shule, hakuna vijiji, wanafunzi wanatembea mwendo mrefu na kwa msingi huo wananchi wanakuja na wazo kwamba hapa tunaanzisha shule shikizi na Serikali au halmashauri inaunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nasema kwamba, madarasa ya wanafunzi yanapatikana, tatizo linakuja nyumba za walimu, wapange wapi? Ninyi wenyewe mnafahamu maeneo ya vijijini, wapange nyumba wapi? Kwa kipindi kama hiki cha mvua kilichopita, walimu wamepata tabu sana kwenda mwendo wa mbali, apigwe na mvua ili afike kwa wakati afundishe. Kwa hiyo, naunga mkono Azimio lililozungumziwa hapa la kuwa Serikali itenge fedha maalum kwa ajili ya nyumba za walimu ili wakae karibu na shule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza lile wazo la two in one or three in one hii ambayo itawezesha nyumba kupatikana nyingi iwezekanavyo ili walimu waweze kufika sehemu za kazi kwa urahisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kuna jambo ambalo linazungumziwa sana hapa kwamba walimu wengi wamejazana hapa, walimu wengi wamejazana hapa. Siyo kosa lao, ombi langu mimi kwa kuunga mkono Kamati yetu, ni kwamba zitengwe hela za kusawazisha au wanaita msawazo ili walimu walioko sehemu ambayo wako wengi basi wasogezwe sehemu zingine ambazo kuna uhaba, huwezi kumuhamisha Mwalimu bila kumtengea fedha za uhamisho. Tunaomba Serikali itenge fedha maalum kwa ajili ya kuleta msawazo mzuri Walimu waweze kusambaa kwenye maeneo yenye mahitaji (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo ni la muhimu sana, ni suala la vyoo. Tuna tatizo kubwa sana la vyoo, kwa mfano kama vile sisi Urambo, kuna uhaba wa vyoo, matundu ya vyoo zaidi ya 1411 na mimi naona wananchi wana haki yao kabisa, mahali ambako walianzisha kwa mfano shule shikizi, ni kwamba wanafunzi wanatembea mwendo mrefu. La kwao, kubwa kabisa ni kwamba kuwe na darasa la kuanzia, sawa, lakini wakichanga fedha wananchi kama tunavyojua uwezo wao, darasa likiisha kunakuwa hakuna hela tena za vyoo. Kwa hiyo, nilikuwa naomba tuangalie utaratibu gani ambao tunaweza kuuweka shule zinapojengwa, waanze kwanza na vyoo kwa sababu tunaanza madarasa, yakiisha kunakuwa hakuna vyoo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, si vizuri wanafunzi wakaenda shuleni kwenye madarasa lakini hakuna vyoo. Kwa hiyo,naomba tuweke Mkakati Maalum wa kuwa na vyoo wakati shule mpya zinapojengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nisingependa nimalize bila kulizungumzia, ni suala la taulo za kike, tumekuja kugundua kwamba, Halmashauri zenye nia nzuri zimetenga fedha kwa ajili ya taulo za kike tukijua kwamba familia nyingi hazina uwezo na hili ni tatizo ambalo linawakwaza wanafunzi wa kike kutokuhudhuria shuleni wakati fulani Fulani, ombi langu ni kwamba, taulo za kike zitengewe bajeti ili Watoto wetu wa kike waweze kusoma vizuri na waendelee na masomo kadri iwezekanavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeweza kusema maneno mengi lakini Kamati yetu imeleta Taarifa nzuri na tutashukuru kwamba tuone utekelezaji wake. Wajumbe wa Kamati wameshasema kabisa hapana, safari ijayo hatuandiki tena Maazimio kama yale ya kwanza kutengenezwa, yaani hayakufanyiwa kazi. Tunaiomba kabisa Serikali ichukue yale Maazimio, yafanyiwe kazi ili mwakani basi mambo yaendelee vizuri kutokana na jitihada kubwa aliyofanya Mheshimiwa Dkt. Samia ya kuleta maendeleo. Hatua zichukuliwe ili yale mama aliyoamua kuyatendea haki ya kuleta maendeleo ya haraka, basi yaweze kutekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hivyo, naunga mkono Hoja. Ahsanteni sana. (Makofi)