Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Liwale
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi na nianze mchango wangu jioni hii kwa kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyopambana kuhakikisha wananchi wa nchi hii wanaishi maisha yaliyo bora. Nimshukuru Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, Manaibu Waziri wote wawili, Katibu Mkuu na Makatibu Wakuu kwa namna wanavyoonyesha ushirikiano mkubwa na Kamati yetu ya TAMISEMI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kusahau kumshukuru sana Mheshimiwa Mwenyekiti wetu wa Kamati na Makamu wake pamoja na Sekretarieti ya Kamati, kwa weledi mkubwa uliowezesha ripoti hii kukamilika na kuileta hapa Bungeni leo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niaze na jamaa wa TARURA, kama mnavyofahamu, mfano mmojawapo wapo, Wilaya yetu ya Liwale, sisi kwetu lami ni msamiati mgumu, ni msamiati ambao haueleweki. Sasa, najaribu kuangalia, hebu Serikali iangalie picha hiyo, kama lami yenyewe tu kuiona ni mtihani mkubwa. Barabara zetu nyingi za udongo na hali hii tuliyonayo leo, kukoje Liwale? Hiyo ichukuliwe kama mfano muone namna gani tunapozungumzia TARURA, TARURA, TARURA tunamaanisha nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwenye Kamati tumezungumza hapa kwamba bajeti ya TARURA iongezwe, lakini naenda mbali zaidi, siyo tu iongezwe bajeti, na fedha hizi ambazo zimewekwa kwenye bajeti basi nazo ziende. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, imeonekana hapa shida kubwa ni rasilimali fedha. Wiki nzima hii kila Mwenyekiti kwenye hotuba yake akija hapa anawaambia ongeza watumishi, inataka rasilimali fedha, kila taasisi tunaomba iongezewe bajeti zote unakuta rasilimali fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ombi langu kwa Serikali, kama ambavyo sisi tunasisitiza halmashauri ziongeze wigo wa kukusanya mapato Serikali nao walione hili, kwamba rasilimali fedha sasa hivi hapa nchini kwetu ndilo jambo kubwa tunalopambana nalo. Kwa hiyo ndugu zetu hawa tuliowakasimu Madaraka, kwa maana ya Wizara ya Fedha, waone ni namna gani wanakwenda kuongeza fedha hizi ili rasilimali fedha hii isiwe bidhaa adimu kama ilivyo sasa hivi leo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine limegusiwa hapa kwa upande wa afya ni suala la maboma ya zahanati na vituo vya afya; hapa napo mimi nina mchango mdogo. Mimi nafikiri Serikali ije na utaratibu sasa wa kuratibu haya maboma kwamba yanajengwa kwa mtindo gani; kwa sababu tumeshawahamasisha wananchi wamejenga haya maboma mengi mno. Kinachoonekana sasa kwamba mipango ya Serikali iko nyuma ya mipango ya wananchi. Wananchi wanajenga maboma mengi lakini Serikali uwezo wa kuyahudumia unakuwa ni mdogo. Sasa umefika wakati Serikali wafanye uratibu, labda wapewe wakurugenzi, kwamba kila Mkurugenzi alijenga maboma mangapi kwa mwaka kulingana na uwezo wa Serikali. Lakini kama tukiacha hivi maboma haya yaendelee kujengwa bado tunaendelea kupata lawama kwa wananchi kwa sababu wanajenga maboma mengi lakini uwezo wa kuyahudumia unakuwa ni mdogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu elimu. Tunashukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ameleta fedha nyingi sana kwenda kuboresha miundombinu ya elimu, na hili jambo hakuna mtu anaweza akapinga ni jambo jema sana lakini bado kuna tatizo la vyoo kwa upande wa elimu. Shule nyingi hata shule za msingi zina matatizo makubwa sana ya vyoo na hapa naomba nitoe ushauri kwamba Serikali kupitia TAMISEMI, ione namna ya kuwawajibisha wakurugenzi wetu iwe ni mojawapo ya vipimo vya Mkurugenzi ni kuona kwamba kwenye halmashauri yake hakuna tatizo la hivi vyoo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tukiweka kipimo kama task, kwamba Mkurugenzi tutampima kwa namna anavyoweza kukabiliana na vyoo shuleni iwe ni mojawapo ya kipimo. Kwa sababu gani nasema hivyo? Kwa sababu sasa hivi kinachoonekana halmashauri nyingi baada ya Mheshimiwa Rais kuwapelekea fedha nyingi za miundombinu ya elimu wako likizo. Kwa hiyo wao wanasubiri wapelekewe bajeti kwamba wewe kwenye halmashauri yako unahitaji vyoo vingapi, unahitaji madarasa mangapi, unahitaji maboma mangapi na vitu kama hivyo. Lakini wapewe task sasa kwamba kwenye halmashauri yako nikisikia malalamiko ya vyoo, nikisikia malalamiko ya madawati kuwe na jambo la kujibu kwa hawa watendaji wetu kule kwenye halmashauri zetu, hapo ndipo tunaweza tukakabiliana na tatizo hili la vyoo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri mwingine kwa upande wa TARURA, mimi nafikiri imefika wakati sasa kufikiria Meneja wa Wilaya wa TARURA awe na vitendea kazi kama vile ma-bulldozer yale au hizi excavator zile, kwa sababu gani; kwa mfano mimi kwangu kule kuna Barabara ya udongo unakuta dimbwi lipo katikati ya Barabara kinachohitajika pale ni kijiko tu kuja kuweka mfereji pale maji yale yaondoke yarudishie udongo Barabara ipitike. Sasa Meneja wa TARURA anakuambia kumpata mkandarasi kwa kazi ile hakuna mkandarasi ambaye yuko tayari atoke Masasi na bulldozer kuja kufukia mashimo mawili, matatu yenye thamani labda mradi tu wa shilingi milioni 50. Kwa hiyo Meneja wa TARURA anachofanya ni kusubiri mashimo yawe mengi zaidi angalau apate mradi kuanzia milioni 500 ndipo amwite mkanadarasi aje kufanya kazi kwa sababu kulitoa bulldozer kutoka Masasi au kutoka Mtwara kulifikisha Liwale si jambo jepesi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa hiyo mimi nafikiri hivi vifaa kama tulivyofanya kwenye idara ya maji, kwamba kila mkoa kuna lori la maji, basi tuone namna ya kuwawezesha hawa TARURA. Hii mitambo midogo midogo ya kufukia mashimo kuanzia zile Barabara za udongo ziwepo kule kwenye halmashauri zetu, kwa sababu miradi hii ni midogo midogo. Kwa mfano mimi nilikuwa mradi wa shilingi milioni 200, yule meneja ametafuta mkandarasi amekosa mwaka mzima, kwa sababu hakuna mkandarasi ambaye yuko tayari atoke umbali mrefu kufata shilingi milioni 200 au 300, minimum watakwambia shilingi milioni 500. Kwa hiyo kuwe na mradi zaidi ya shilingi milioni 500, 600 ndipo anaweza kuja kufanya kazi. Kwa hiyo hawa mimi napendekeza wapewe ile mitambo midogo midogo ya kuweza kufukia mashimo kwenye zile Barabara za udongo itakuwa imetusaidia zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, narejea tena kwenye upande wa afya. nashukuru Mheshimiwa Rais amejenga vituo vingi vya afya na hospitali zetu za wilaya mpaka mikoa; na vifaa tiba sasa hivi ni vingi. Lakini tatizo lililozuka kule sasa ni wataalam wa kuhudumia na kutumia vile vifaa lakini sio wataalam peke yake hata kuvifunga. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa, malizia.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: … vipo vituo vya afya vingine vyenye vifaatiba zaidi ya miezi sita havijafungwa viko ofisini. Mimi nashauri kwamba tuletewe wataalam vifaa vile vifungwe ili wananchi waendelee kupata huduma nzuri. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja ya Kamati yetu, maazimio yote, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)