Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Stanslaus Shing'oma Mabula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyamagana

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na mimi walau kwa dakika chache niweze kuchangia mambo machache, hasa kwenye sekta hii ya barabara upande wa TARURA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niungane na Wajumbe wote waliopita waliozungumza habari ya barabara, lakini niwapongeze sana Wajumbe wa Kamati wakiongozwa na Mwenyekiti, Mheshimiwa Londo, kwa kazi nzuri waliyoifanya, hasa kwenye kuichambua na kuieleza vizuri issue ya barabara upande wa TARURA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa najaribu kutazama; Bunge hili limepitisha bajeti siyo mara moja siyo mara mbili namna ambavyo linatamani kuona TARURA ikifanya kazi. Kwa bahati mbaya sana hatujafikia malengo wakati wote tuliokubaliana na kupanga hapa ya kuwahudumia wananchi kwenye barabara zao. Kwa mfano tunapozungumza tumepanga bajeti kwa TARURA kwa mfano shilingi bilioni 710 ukijumlisha na zile bilioni 107 za wadau lakini nimejaribu kuangalia mtandao wa barabara; TARURA peke yake inahudumia barabara za wilayani, mijini na vijijini zaidi ya kilomita 144,000. Nikajaribu kutafuta uwiano TARURA na TANROADS ukoje? TANROADS wanahudumia barabara zipatazo kilomita 91,532 nchi nzima na katika barabara hizo kilomita 12,197 ni barabara kuu na 21,298 ni barabara za mikoa lakini kilomita 58,037 ni barabara zinazohudumiwa na TANROADS wilayani na vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema nini? TARURA hii leo tunaipa nusu ya bajeti sawa na bajeti inayopewa TANROADS. Sasa Bunge hili ndilo limeifanya TANROADS ikafikia bajeti ya zaidi ya trilioni moja milioni mia nne. Bunge hili ndilo linashindwa kuifanya TARURA ifikie kiwango angalau cha trilioni moja na milioni mia sita inayosemwa hapa. Nafahamu tulikotoka kwenye shilingi bilioni 400 mpaka leo tuko shilingi bilioni 700, lakini masikitiko yangu makubwa ni kwamba hata fedha zile ambazo Bunge liliahidiwa zaidi ya shilingi bilioni 350 kupelekwa TARURA kwa ajili ya kuimarisha mtandao wa barabara hazijakwenda mpaka leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sio hilo tu, ripoti ya Kamati hapa inasema ni asilimia 12 ya fedha peke yake ndizo zimepokelewa kule TARURA kwa ajili ya utekelezaji wa kazi ambayo ni chini ya asilimia 39. Mheshimiwa Rais kafanya kazi kubwa sana, kawekeza sana kwenye sekta ya afya, kawekeza sana kwenye sekta ya elimu. Bahati mbaya sana maeneo yote yaliyoboreshwa kwa ajili ya huduma za kijamii hayawezi kufikika kiurahisi kwa sababu barabara hazipitiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nikupe mfano, ukichukua Jiji la Mwanza peke yake lina mtandao wa barabara kilometa elfu mia mbili na sabini na kitu. Barabara zilizojengwa zinazoweza kupitika vizuri kwa kiwango cha lami, kiwango cha mawe na kiwango cha changarawe hazizidi kilomita 90 kati ya hizo. Kwa namna yoyote ile bado tunayo kazi kubwa sana Waheshimiwa Wabunge. Ndiyo maana asubuhi nikasema hili jambo sio la Dar es Salaam peke yake hili jambo tulitazame kama jambo la nchi nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge kazi yetu hapa tumesema mara kadhaa tusipopata fedha za kutosha kwenye upande wa barabara na kuiwezesha TARURA ifanye kazi yake vizuri; leo uki-post kitu kizuri na cha thamani umejenga kituo cha afya kizuri, umejenga shule nzuri ukaki-post kwenye page yako wanaweza kuja watu 10 mpaka 15 wanakueleza habari ya barabara na hawazungumzi kile ulichokiweka pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inaonesha ni namna gani wananchi wetu wanatamani maendeleo makubwa tunayoyafanya kwenye sekta za afya, elimu, maji na maeneo mengine tuwekeze hivyo hivyo kwenye Barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani unatoka mjini kilomita mbili ni barabara ya lami halafu unakwenda kilomita 11 barabara ya tope na siyo changarawe na kule unakokwenda umejenga kituo cha afya kizuri, wananchi wanaweza kwenda kupata huduma lakini hawapati. Kwa hiyo mimi nachotaka kusema, na Serikali itusaidie sana, tunakwenda kwenye Bunge la Bajeti sasa hivi. Haiwezekani asilimia 12 peke yake ndiyo fedha iliyotolewa kwa ajili ya kujenga barabara. Leo kazi zimetangazwa asilimia 60 wakandarasi wako site hawana hela, asilimia 40 zilikuwa zitangazwe haziwezi kutangazwa kwa sababu fedha hakuna. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe sana na Bunge lako hili kule kwetu tunapotoka sisi kuna maeneo; na nishukuru sana Serikali kwa kutumia miradi ya TSCP toka mwaka 2010 mpaka 2014; lakini sasa tuko kwenye miradi ya TACTIC, Serikali iwekeze zaidi kwenye kutafuta miradi ya washirika ya namna hii itakayosaidia sana miji yetu kupendeza na kuwa na barabara nyingi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mifano mingi ipo, leo hata ukiongea na Mheshimiwa Spika, yuko mbele yangu hapa; Jiji la Mbeya leo ukichukua Mradi wa TSCP, ukachukua Mradi wa TACTIC ukienda Mwanza uchukue Mradi wa TACTIC, Mradi wa TSCP ndiyo maeneo ambayo yamesaidia zaidi kwenye uwekezaji wa barabara. Tufanye hivyo tupate fedha ziweze kujenga barabara. Bila hivyo tunapiga mark time na thamani ya miradi yetu haitaonekana kwa sababu hatujaitendea haki kwa kuitengenezea miundombinu mizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua umenipa dakika tano nikushukuru sana lakini nisisitize Waheshimiwa Wabunge, tunakokwenda bila kuwa na barabara nyingi nzuri tutaadhibiwa kwa sababu ya kukosa barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)