Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Godwin Emmanuel Kunambi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlimba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, mimi nianze na shukrani. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa sababu nimeagizwa na wananchi pia wa Mlimba kumshukuru Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Mlimba wameniagiza nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa barabara ya lami kutoka Ifakara kwenda Mbingu - kilomita 62.5. Wananchi wa Mlimba wameniagiza nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa gari ya wagonjwa, wananchi wa Mlimba wameniagiza nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa sekta ya elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naanza kuchangia. Mimi naanza na mapato ya ndani na matumizi yake ya Halmashauri zetu zote nchini na hapa nitatoa mifano ya Halmashauri mbili Mrimba DC na Dodoma CC; nianze na Mlimba DC, Halmashauri ambayo mimi ndiye Mbunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazo changamoto kubwa kwenye Serikali za Mitaa, mimi niliwahi kuwa Mkurugenzi nina-declare interest lakini naomba Wakurugenzi wenzangu wanisamehe nchini. Halmashauri nyingi Wakurugenzi wamegeuza kama comfort zone. Mkurugenzi anafika ofisini tangu ateuliwe hawezi kuwa hata mbunifu kwenye vyanzo vipya vya mapato ya ndani, Mkurugenzi wa Halmashauri hawezi hata kubadilisha mkao wa kiti. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema haya? Halmashauri zetu nchini zimekuwa tegemezi kwa asilimia zaidi ya sabini wanategemea Serikali Kuu, asilimia sabini Majiji mengine tutoe mfano Kenya, Rwanda nchi zinazotuzunguka majirani hawa. Majiji yote yanajitegemea kwa mapato ya ndani. Manispaa zote zinajitegemea kwa mapato ya ndani lakini why not Tanzania? Kwa nini Tanzania hatuwezi kujitegemea kwenye majiji?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimetoa mifano miwili nianze na Mlimba DC; kwa miaka mitatu mfululizo nitatoa mapato yetu. Tulianza na bilioni 3.2. Sasa hivi mwaka huu wa fedha tuna bilioni 4.2 tumeongezeka kwa bilioni moja na sasa kwenye makisio mapya ya mwaka fedha ujao tutakwenda kwenye bilioni 4.8. Matumizi yake yakoje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeweza kujenga vituo vya afya vitatu kwa mapato ya ndani. Kituo cha Afya cha Chita ni kwa mapato ya ndani. Kituo cha Afya cha Mofu ni kwa mapato ya ndani, Kituo cha Afya cha Igima ni kwa mapato ya ndani. Kwa nini hayafanyiki Halmashauri nyingine? Kweli tunaendelea kupeleka mzigo kubwa Serikali Kuu, nashangaa hata Majiji yanasubiri milioni 500 ya Mama Samia? Kujenga kituo cha afya kimoja kweli are we serious? Sasa nataka kusema nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefanya ubunifu Halmashauri ya Mlimba, ninavyozungumza leo tunalo shamba la miti pale Kata ya Uchindile la ekari 1,300, tunatarajia miaka 10 ijayo sisi tume-break even kwa nini wengine hawawezi kufanya? Kwa nini hawafanyi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi Dodoma. Ninatatoa takwimu ya miaka mitatu, mwaka 2016/2017 Dodoma Jiji ilikusanya bilioni 25. Mwaka 2017/2018 ikakusanya bilioni 57, mwaka 2018/2019 ikakusanya bilioni 67, Mwaka 2019/2020 ikakusanya bilioni 71 nikiwa Mkurugenzi wa Jiji. Kwa nini haya hayafanyiki? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, matumizi yake kwa mfano Dodoma Jiji wakati ule tuliona asilimia 70 ilikuwa ni mapato yanatokana na viwanja. Tukasema viwanja vikikosa soko mapato yatakuwaje? Tukaja na Miradi Mikubwa ya Kimkakati Saba na niwaambie Mheshimiwa Naibu Waziri yupo hapa. Soko siyo chanzo cha mapato ni huduma, stendi siyo chanzo cha mapato ni huduma. Tukaja na miradi saba wakati wangu tukatekeleza miradi miwili, tukajenga hoteli ya Dodoma City Hotel kwa bilioni tisa mapato ya ndani na hivi leo wanapata milioni 900 kwa kila mwaka pale mwenye macho anaona, lakini Mji wa Kiserikali tumejenga hoteli… (Makofi)

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kunambi kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere.

TAARIFA

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuliambia Bunge hili na Tanzania, Mbunge anaeongea ni hazina ya Watanzania, nilitaka kutoa taarifa hiyo. (Makofi)

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

MWENYEKITI: Mheshimiwa endelea na mchango wako.

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Getere, naipokea taarifa yako kwa asilimia 100 na Mungu akubariki kwa kutambua uwezo wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema nini? Tukajenge hoteli nyingine pale Mji wa Kiserikali, mradi wa bilioni 18 kwa mapato ya ndani na tulipanga Dodoma ndani ya miaka kumi tu-graduate ili tutoe mfano kwa Watanzania inawezekana! Mimi sizungumzi sayari nyingine nazungumzia hapa. Tukasema wapo waliosema haa Dodoma ni Mji wa Serikali Makao Makuu, mje mjifunze Mlimba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ndani Waheshimiwa Wabunge ni Halmashauri gani, Mheshimiwa Mbunge asimame hapa, mnajenga vituo vya afya vitatu kwa mapato ya ndani simama! (Kicheko)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mbunge…

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema nini?

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mbunge, Mheshimiwa Kunambi, ili Mbunge asimame anasimama kwa idhini ya Kiti siyo wewe. (Kicheko)

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Ahsante sana, nimefuata maelekezo. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema nini? Tufike mahala tuwasaidie Wakurugenzi wa Halmashauri wawe wabunifu. Msingi Mkuu wa Sera ya Ugatuaji Madaraka maana yake Halmashauri zijitegee kwa mapato ya ndani. Sasa leo nasema tunalalamika, kwa hiyo asilimia 90 unategemea mapato ya Serikali Kuu, Fedha ya Maendeleo ya Serikali Kuu! Hivi jamani, Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu nisikilize kwa makini.

MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kunambi kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Taletale.

TAARIFA

MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampa taarifa Kaka yangu wa Mlimba, naendelea kusema wewe ni hazina ya Morogoro. (Kicheko)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kunambi, taarifa unaipokea?

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nashukuru sana.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kunambi, unaipokea taarifa?

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipokea taarifa.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba unilindie muda wangu.

MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, tuelewane, taarifa ni sehemu ya muda wa uchangiaji, sasa hajapokea taarifa unampa tena taarifa!

Mheshimiwa Kunambi, endelea kuchangia.

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunilinda; nataka kusema nini? Changamoto kubwa yetu kama Watanzania, naendelea kusema ni mambo matatu fikra kwa maana ya mindset, commitment kwa maana ya utayari kufanya jambo na mwisho uzalendo. (Makofi)

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima unapokuwa Mkurugenzi wa Halmashauri au Kiongozi yeyote kwenye Taasisi yeyote ya Umma awe na fikra akiondoka anaacha alama gani? (Makofi)

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, unaacha nini kwa watu uliokuwa ukiwaongoza? (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kunambi, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Esther Matiko.

TAARIFA

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa yangu iko very positive. Naomba kutoa taarifa kwa mchangiaji kwa kile ambacho ana-narrate naungana naye na naiomba Serikali kupitia TAMISEMI, taarifa yangu ni hii sasa, vile zinavyokuja fedha kutoka Serikali Kuu wawe wanaangalia uhalisia wa kipato cha Halmashauri husika au Majiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano fedha za UVIKO zilivyogawanyishwa, Dodoma Jiji hapa imepelekewa fedha katika shule sawa sawa na fedha ambazo wamepeleka kule Tarime Mji ambako hamna mapato kabisa. Sasa ili kuweka hii creativity ya Wakurugenzi na uhalisia wa vipato katika Majiji au Halmashauri zetu, Serikali Kuu iangalie sasa upelekaji wa fedha katika Halmashauri zetu.

MWENYEKITI: Mheshemiwa Esther, ahsante sana.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naungana na wewe kabisa ili iweze kuongeza creativity kwenye halmashauri zetu kulingana na uhalisia wa vipato vya Halmashauri.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kunambi, taarifa hiyo unaipokea?

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa hiyo. Wengi wamezungumzia TARURA ni kweli, TARURA ndiyo mkombozi wa barabara zetu za vijijini, pamoja na Bunge kupitisha bajeti kwa ajili ya TARURA lakini bado fedha za mgao wa kila mwezi wanapewa ndogo.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kunambi, sawa naona muda umeisha.

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie.

MWENYEKITI: Mheshimiwa malizia.

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina ushahidi mgao wa mwezi uliopita TARURA wamepewa bilioni 11 tu na Wizara fulani wamepewa bilioni 20. Morogoro TARURA peke yake tulikuwa tunadai madeni ya wakandarasi shilingi bilioni tatu.
MWENYEKITI: Mheshimiwa ahsante sana.

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nimalizie Wananchi wa Mlimba wanaomba barabara. Itoshe kusema, ahsante. (Makofi)