Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Rorya
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Niungane na wenzangu kwanza kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia TAMISEMI, kwa niaba ya wananchi wa Kata ya Goride Kijiji cha Nyamusi kwa kutupatia fedha. Sasa nimepigiwa simu na Injinia wa TARURA Mkoa, kuwa wametupatia fedha zaidi ya shilingi milioni 92 kwa ajili ya ujenzi wa daraja ambalo lilikuwa linaunganisha wananchi wa Kitongoji cha Mariwa na Kijiji cha Nyamusi. Nachukua nafasi hii kuwashukuru sana kwa sababu katika daraja hili wananchi wengi wamekuwa wakipoteza maisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesimama hapa kwa masikitiko makubwa sana. Kwanza, niseme tu, mimi ni miongoni mwa wale Wabunge ambao hata baada ya Bunge hili kukamilika na kurudi jimboni, sijui ni barabara ipi ambayo inaweza ikanifikisha maeneo ambayo natakiwa kuzungumza na wananchi, kwa sababu barabara zote kati ya 12, barabara nane hazipitiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Rorya maeneo mengi shughuli kubwa ya kiuchumi tunayoitegemea ni ziwa. Katika barabara 12, barabara nane zinatupeleka maeneo ambayo halmashauri ndiyo inategemea kukusanya mapato, ambayo ni maeneo ya ziwani. Katika barabara 12, barabara nane zote hazipitiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikumbushe kidogo, tarahe 31 mwezi wa Kwanza, ilikuwa ni siku ya Jumatano kilikuwa ni Kikao cha Bunge hili, alisimama Waziri wa Fedha na akaahidi ndani ya Bunge hili baada ya baadhi ya Wabunge kuuliza maswali ya nyongeza na maswali ya msingi. Akasema atahakikisha fedha ya dharura ya utengenezaji wa barabara inakwenda kwenye majimbo ambayo, kwenye maeneo yote ya halmashauri ndani ya nchi hii, ambako barabara hazipitiki. Akaendelea mwishoni akasema, atahakikisha fedha hizi zinakwenda kabla ya Bunge hili kukamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ni siku ya Jumanne, tuna siku mbili zimesalia hakuna fedha yoyote ya dharura iliyokwenda kushughulika na barabara hizi. Wananchi wanateseka, hakuna namna ambayo unaweza ukafika kutoka eneo moja kwenda maeneo mengine. Kwenye halmashauri zetu sisi tunategemea shughuli za kiuchumi magari yaende yakafanye ulanguzi kwenye maeneo ya ziwani, kwa ajili ya kuchukua samaki kwa wavuvi. Magari hayafiki. Mimi ni Mbunge ambaye nimeenda kwenye maeneo hayo, nakwama zaidi ya mara mbili, nasukumwa na wananchi. Una majibu gani ya kuwaambia hawa wananchi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana nasema, kwa kuwa hoja ya leo tunaizungumza hapa na tunachangia, Mawaziri watapata nafasi pia ya kuchangia na siyo kuhitimisha hoja, kwa sababu hoja kwa mujibu wa kanuni zinahitimishwa na Wenyeviti wa Kamati. Naomba kwa ridhaa yako, kwa hizi siku mbili zilizosalia na nitaomba Waheshimiwa Wabunge mniunge mkono, tulete Hoja ya Dharura itakayojadili barabara za dharura nchi nzima kwa umoja wake na tutoe maazimio ya moja kwa moja yatakayokwenda Serikalini kwa ajili ya utekelezaji wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiendelea hivi tunazungumza, Waheshimiwa Mawaziri watasimama hapa kujibu hoja, bado kule wananchi ni shida. Hebu niambie, leo kama kauli imetoka kwa Waziri wa Fedha mwenye dhamana kwamba atahakikisha kuwa fedha inakwenda kabla ya tarehe 31, mimi leo nakwenda Jimboni nawaambia nini wananchi? Kwa sababu wameisikia Serikali na Waziri mwenye dhamana amesema kabla ya Bunge kwisha fedha zitakuwa zimekwenda. Hakuna fedha maeneo yale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Waheshimiwa Wabunge waniunge mkono, ndani ya hizi siku mbili kama hakuna fedha ya dharura, tulete hoja ndani ya Bunge hili, tujadili kama tulivyokuwa tukifanya maeneo mengine. Tuliwahi kujadili hapa kuhusiana na issue za kilimo. Kuna maeneo ambayo wakulima walikuwa na changamoto, tukaleta hoja, tukajadili na Serikali ikapeleka fedha. Kwa maelekezo mahususi au azimio ndani ya Bunge, ninaamini hili linaweza likawa suluhisho kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni issue ya Madiwani kusimamia Miradi ya Maendeleo; utakubaliana nami kwamba, hakuna sehemu ambayo haisimamiwi kwa sasa hivi kama miradi ya maendeleo maeneo mengi ninayokwenda nchini. Kwa mfano, kwangu hakuna Diwani anayekwenda kukagua shughuli za kimaendeleo zinazofanyika ndani ya Jimbo. Kwa nini? Kwa sababu hawana fedha, hawana uwezesho wa halmashauri kuwapeleka kukagua yale maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Wizara kwa maana ya TAMISEMI, ipeleke maelekezo mahususi kwamba miradi yote ya maendeleo Madiwani wote wakague kama mnavyofanya ndani ya Bunge. Sisi tunapata nafasi ya kwenda kukagua miradi ya maendeleo, tunakuja kuchangia ndani ya Bunge. Madiwani wasipokwenda kujiridhisha fedha za miradi ya maendeleo maana yake ni nini? Watakuwa wanaletewa makabrasha ndani ya Vikao vya Madiwani bila kujua huo mradi unaendeleaje. Ndiyo maana unaona miradi haikamiliki, upotevu wa fedha unakuwa mwingi na bahati mbaya sana sisi Wabunge wakati vikao vinafanyika tunakuwa hatupo maeneo ya majimboni, wengi tunakuwa huku. Kwa hiyo, naomba Wizara ya TAMISEMI itoe mwongozo mzuri kwenye maeneo haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, natambua umenipa dakika tano, mapitio ya kanuni. Nakubaliana kabisa na Kamati yafanyike mapitio ya Kanuni ili angalau Vikao vya Baraza la Madiwani viweze kufanyika wakati ambao Wabunge tupo Majimboni tuweze kushiriki kutoa michango ya kusimamia miradi hii ya maendeleo.