Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na nakushukuru kwa kunipa nafasi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetujalia afya njema, lakini pili nikushukuru sana wewe. Nimshukuru Mwenyekiti wa Kamati yetu Mheshimiwa Dennis Londo, Makamu Mwenyekiti na Wajumbe wote wa Kamati ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kwa kazi nzuri sana wanayofanya kushauri, kutoa maelekezo na mapendekezo mbalimbali ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na sisi tuwahakikishie kupitia Waziri wetu wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa tutahakikisha mapendekezo, ushauri na maelekezo yote ambayo mnayatoa tunayatekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda naomba niongee katika maeneo makubwa mawili, nitaanza nae neo la utawala; Waheshimiwa Wabunge wametoa hoja nyingi muhimu na moja ya hoja ni kuhusiana na namna ambavyo watendaji wetu na viongozi wetu katika ngazi za Mikoa na Wilaya hawajaonesha ufanisi katika kutatua kero za wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge hapa wamejaribu kulinganisha ziara ya Mwenezi wetu Comrade Makonda na namna ambavyo wananchi wanaibuka na hoja nyingi, kero nyingi, ambazo kwa kweli kero nyingi ziko ndani ya uwezo wa Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa, ziko ndani ya uwezo wa Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya, ziko ndani ya uwezo wa Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakurugenzi na watendaji wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mheshimiwa Rais aliwapa dhamana viongozi hao na sisi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa tumeendelea kusisitiza na kuchukua hatua kwa watendaji na viongozi wote ambao kimsingi hawatekelezi ipasavyo majukumu yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge kwamba na sisi tunaendelea kufanya tathmini. Maeneo yote ambayo ambayo tunaona kuna viongozi hawajatekeleza ipasavyo majukumu yao hatustahili kusubiri Mwenezi wa Taifa wa CCM afike kutatua kero za DC ambazo RC angeweza kuzitatua wakati wamepewa wajibu huo. Kwa hiyo, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba, jambo hilo tunalifanyia kazi na tutashauri mamlaka ya uteuzi kwa pale ambapo tutajiridhisha kwamba, hawajatekeleza majuku yao ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili lilikuwa ni posho; tunatambua sana kazi kubwa inayofanywa na Waheshimiwa Madiwani na Wenyeviti wa Vijij: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, utakumbuka Bunge hili mwaka wa fedha 2021/2022 lilianzisha kulipa posho kwa Waheshimiwa Madiwani katika Halmashauri 168. Huko nyuma Madiwani walikuwa wanakopwa posho zao, wanakaa miezi sita bila kulipwa posho, lakini sasa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan analipa posho kwa halmashauri 168, hakuna Diwani akakopwa posho, wote wanalipwa kwa wakati. Tunafahamu tunahitaji kuongeza kiwango cha posho, Serikali inaendelea kuongeza uwezo wa mapato yake, ili tuweze kufanyia kazi suala la posho hizi za Waheshimiwa Madiwani na Wenyeviti ziweze kuongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala la tatu ilikuwa ni susla la utoaji wa posho za watendaji wa kata; niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, Serikali ilishatoa maelekezo madhubuti kwamba, Wakurugenzi lazima walipe posho za Maafisa Watendaji wa Kata na wameendelea kulipa. Kwa miezi mitatu iliyopita ni halmashauri 80 kati ya 184 ambazo hazikulipa, na Serikali imeshachukua hatua kwa Wakurugenzi hao, kwanza kuhakikisha wanalipa posho mapema iwezekanavyo, lakini pili kuhakikisha kwamba, wanaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kulipa posho hizo.

MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Naibu Waziri, kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Janejelly Ntate.

TAARIFA

MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nina mtandao wote wa Tanzania nzima. Hakuna mahali ambako wamelipa inavyostahili na hakuna mahali ambapo hawadai chini ya miezi kumi, message zao ziko humu. Naomba nimpe Taarifa, leo, utoe tamko kwa hawa Wakurugenzi walipe hizi posho. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Naibu Waziri, taarifa hiyo unaichukua?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea Taarifa ya Mheshimiwa Mbunge, nimesema kwamba, bado kuna changamoto ya baadhi ya Halmashauri kutolipa posho hizo na tumechukua hatua na tumeelekeza Wakurugenzi kufanya hivyo. Kwa hiyo, tamko ambalo tumelitoa hapa kama Serikali kwamba ni wajibu wa Wakurugenzi kuhakikisha wanalipa posho kwa watendaji wa kata kwa wakati na kuhakikisha wanatenga bajeti za uhakika, ili Maafisa Watendaji wa Kata wapate posho hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongee kidogo sekta ya afya; sote hapa, Waheshimiwa Wabunge wamechangia, lakini wote kwa pamoja tumepongeza kazi kubwa sana iliyofanywa na Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali yetu ya Awamu ya Sita katika ujenzi wa zahanati, vituo vya afya, hpspitali za halmashauri, magari ya wagonjwa, vifaa-tiba kila sehemu. Niwahakikishie zoezi hilo ni endelevu, tutahakikisha tunaendelea kujenga vituo hivyo katika bajeti inayofuata, lakini pia kununua vifaa-tiba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)