Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mikumi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DENNIS L. LONDO – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu, kwa maana imempendeza yeye mjadala huu kuchangiwa na wachangiaji wengi ambao ni wawakilishi wa wananchi, kujadili mambo ambayo yanawagusa wananchi. Walatini wanasema, “Vox populi, vox Dei” (Sauti ya Wengi ni sauti ya Mungu). (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Kamati tunamshukuru na tunaungana na Wabunge wengine kumshukuru Rais wetu Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo anaifanya. Wengi wa wachangiaji wamezungumza mambo makubwa ambayo yanafanyika katika majimbo ya wachangiaji kwenye miundombinu ya elimu, afya na maeneo mengine. Natumia nafasi hii kumshukuru pia Mheshimiwa Spika wa Bunge letu ambaye pia ni Rais wa Mabunge ya IPU, Dkt. Tulia Ackson kwa namna na jinsi anavyozilea Kamati zake, Wabunge wake kutupa nafasi ya kuchangia katika ujenzi wa Taifa letu kupitia majukumu ambayo tumeaminiwa na wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru Mawaziri, Naibu Mawaziri na Makatibu Wakuu wa Wizara ambazo wanasimamia, kwa ushirikiano wao kwa Kamati. Shukrani zangu ni kwa Wabunge wote 22 ambao wamechangia na wote wameigusa Taarifa yetu ya TAMISEMI. Bila shaka ni kwa Sababu ya Ofisi hii ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa inagusa maisha ya wananchi moja kwa moja ambao ni wapigakura wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yote ambayo wamezungumza, sisi kama Kamati tuliyaeleza kwenye taarifa yetu. Kubwa kuliko yote ambalo Waheshimiwa Wabunge ambao wamechangia wamepata fursa ya kuelezea, ni kuguswa kwao na kutokuridhishwa kwa kiasi cha fedha ambacho kinaenda kwenye miradi ya kimkakati, hasa barabara na miundombinu yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge lako limepitisha bajeti, lakini kiasi cha fedha ambacho kinaenda, Kamati haikuridhishwa na Wabunge hawakuridhishwa. Ni kweli kwamba ni asilimia 12 tu ya bajeti ambayo imeidhinishwa ilienda mpaka tarehe 31 Disemba kwa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA). Kuna mkanganyiko kati ya exchequer na cash flow ambayo kama Kamati tuliweka msisitizo kwamba tuambieni ni kiasi gani cha fedha ambacho kimeenda kwa wakala kwa ajili ya kulipa wakandarasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la barabara na miundombinu yake ni suala la kufa na kupona. Ni siasa lakini pia ni uchumi kwa wananchi wetu na kwa Taifa letu. Si suala la TRAB na TRAT. Hakuna Rufaa kwa wananchi wetu ambayo wanaweza kukata zaidi ya sisi kama wawakilishi wao kuzungumzia haya ambayo tunayashuhudia kule kwenye halmashauri zetu na wilaya zetu. Sisi tukishindwa hakuna atakaye weza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni rai ya Kamati na inaungana na wachangiaji wote ambao wamezungumzia ongezeko la bajeti kwa TARURA. Tunaishukuru sana Serikali, hata kwenye bajeti iliyopita iliongeza kiasi kikubwa cha fedha kwa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini. Changamoto ni kwamba, hilo ongezeko ambalo tumeongeza halikwenda kama ilivyostahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge lako liliahidiwa shilingi bilioni 350 za ziada ambazo ilisemwa kwamba zingeweza kwenda kumaliza matatizo ya msingi kwenye barabara zetu. Kiasi hiki pia hakikwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, kuna fedha ambazo ni reinfest za tozo ambazo pia mara ya mwisho kwenda kwa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini ilikuwa ni mwezi wa tisa. Hali hii haiashirii ama haikidhi matumaini na matarajio ya wawakilishi wa wananchi ambao wako kwenye Jumba lako. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri tunahitaji Serikali kuja na mpango wa dharura ambao unatakwenda kujibu kero kubwa na changamoto kubwa ambayo imetokana na Mvua za El Nino ambazo zimeharibu barabara na miundombinu yake katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni rai ya Kamati kuitaka Serikali kutafuta vyanzo vya uhakika vya mapato ambavyo vitaisaidia Serikali kufikia lengo la trilioni 1.6 kwa miaka minne mfululizo ili tufikie lengo la asilimia 70 ya barabara zetu kuzitoa kwenye udongo kwenda kwenye changarawe, asilimia tatu kwenda lami na kumaliza changamoto ya vivuko kwenye barabara zetu na miundombinu yetu ya barabara, hasa katika maeneo ya vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili tungependa kuishauri Serikali kutafuta vyanzo vya fedha pia kuharakisha mchakato wa TARURA Samia Infrastructure Bond ili kiwe moja ya vyanzo ambavyo vinaweza vikawa raised kwa ajili ya kumaliza changamoto ya barabara na hasa kufikia lengo lile la shilingi trilioni 1.6 kumaliza changamoto ya miundombinu yetu ya barabara kwenye maeneo ya vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wachangiaji wamezungumzia kwa kirefu kuhusiana na mabadiliko makubwa ambayo yanatokea kwenye sekta ya afya na elimu. Ujenzi wa miundombinu lakini ununuzi wa vifaa vya kisasa kama mashine za mionzi na huduma za afya ya kinywa. Pamoja na manunuzi haya bado kuna changamoto ya uhaba wa wataalam pia walizungumzia suala zima la uwezeshaji mkubwa wa Serikali ambao umepelekea Halmashauri zetu kuendelea kuwa tegemezi kwa Serikali Kuu na hivyo kutoa mwanya wa kutumia mapato ya ndani ambayo ilikuwa ni lengo la Serikali kuwapa ahueni kuelekeza fedha hizo kwenye shughuli za maendeleo kama jukumu la TAMISEMI linavyoelekeza maendeleo vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hili tunaitaka Serikali kuja na mpango, kuja na mwongozo, kuja na mkakati wa kusimamia fedha za mapato ya ndani kumaliza changamoto ambazo ni umaliziaji wa maboma ya huduma za zahanati, afya na elimu katika maeneo yetu. Pia kuajiri vibarua ambao wanaweza wakajibu changamoto zetu za muda mfupi wakati Serikali inaangalia changamoto za muda mrefu. Fedha hizi za mapato ya ndani zikitumiwa vizuri zinaweza kumaliza changamoto yetu ya vyoo na madawati ambayo imekuwa ni changamoto kwenye miundombinu ya elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na Shirika la Elimu Kibaha, wakati Scandinavia na Nordic wanatujengea kituo kile, shirika lile la afya walijenga hospitali kubwa, walijenga FDC kwa maana ya Chuo cha Maendeleo ya Wananchi, walijenga Chuo cha Uunguzi, walijenga sekondari pale lakini walijenga pia chuo ambacho kilikuwa kinafundisha stadi mbalimbali kama ufugaji wa kuku, uvuvi na vitu vingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, shirika hili lilikuwa ni model ambayo ilikuwa na malengo ya kusambaza katika maeneo mengine ya nchi yetu na Afrika kwa ujumla. Shirika hili pamoja na kwamba limetoa wataalam mbalimbali wa kada mbalimbali ni masikitiko ya Kamati yangu kwamba juzi kwenye taarifa ambayo tulikuwa tumeitoa tuliiomba Serikali kupitia taarifa kama hii na Wabunge wamezungumzia hapa umuhimu wa kufuatilia Maazimio ya Bunge, kwamba shirika hili kwa umuhimu wake tuliitaka Serikali iliimarishe. Sasa tunaambiwa kwamba shirika hili ni moja ya mashirika ambayo hayajiendeshi kwa faida linaenda kuvunjwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna mahali ambapo tulitegemea kwamba shirika hili litupe cash benefits isipokuwa huduma, huduma, huduma. Shirika lile lilikuwa ni package, kitendo cha kuigawanya hospitali ya Tumbi kwenda Wizara ya Afya, kuchukua shule kupeleka Wizara ya Elimu - TAMISEMI na kugawanya vipande vipande haiendi kukidhi malengo ya msingi ya uanzishwaji wa shirika hilo. Jambo ambalo tunaitaka Serikali kufikiria upya uamuzi huo ambao hatuamini unaenda kukidhi malengo tarajiwa ama malengo halisi ya uanzishwaji wa shirika lile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa tumezungumzia suala zima la utawala bora na katika hili tulikuwa tumezungumzia dhana nzima ya D by D, na wachangiaji wengi walikuwa wamezungumzia idadi ya watu ambao wanatokea kwenye mikutano ya Mwenezi wetu wa Chama Taifa, wakielezea kero na shida mbalimbali. Kimsingi kamati tunaliona hili kama moja ya viashiria vya kufeli huo mfumo wa ugatuaji wa madaraka kwenye ngazi za chini. Ndiyo maana unaweza kuona wengi ambao wanalalamika ni waliodhulumiwa mashamba na ardhi lakini ukiuliza Maafisa Ardhi hawa wanaripoti Wizarani, hawaripoti kwa Mtendaji wa Kijiji, hawaripoti kwa Mtendaji wa Kata, hawaripoti kwa Mkurugenzi wa Wilaya ambaye kwa mujibu wa sera ya ugatuaji wa madaraka before huyu ndiyo alikuwa mwajiri, ana mamlaka ya uajiri na mamlaka ya nidhamu ya watumishi hawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni rai ya Kamati kuitaka Serikali kwenda kutekeleza kikamilifu Sera ya Ugatuaji wa Madaraka lakini pia kukemea kwa lugha ambayo itasikika na taasisi zake, kupinga jaribio lolote la kuchomoa sehemu ya madaraka ama mamlaka ya TAMISEMI kuamisha mamlaka ya TAMISEMI kwenye taasisi nyingine, badala ya kuimarisha tutaendelea kubomoa na hivyo kumuondoa mwananchi na nguvu ya mwananchi katika kuisimamia Serikali hasa katika ngazi ya chini kwenye Vijiji na Kata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulizungumzia suala la ubadhilifu na matumizi mabaya ya rasilimali katika ngazi za Halmashauri. Ni rai ya Kamati kwa Serikali tunaiomba kuwe na namna bora sasa ya kuja na muarobaini, kuja na majibu ya uhakika ni lini mambo haya ambayo yanachefua kila mtu binadamu hata na Mwenyezi Mungu yanaenda kumalizika. Vitendo ambavyo vinafanyika, uharibifu ambao unafanyika na ubadhirifu ambao unafanyika si tu kwamba ni hasara kubwa kwa Serikali ambayo inatafuta fedha za kujenga miundombinu katika maeneo mbalimbali kujibu kero na shida za wananchi, zinabomoa Imani ya wananchi kwa Serikali yetu, jambo ambalo halivumiliki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na maoni yote ambayo tumetoa na maazimio yote, naomba sasa kutoa hoja kwako ili iungwe mkono na Wabunge wote kwamba Maazimio yote ya Bunge na ushauri wa Wabunge sasa uingie kama sehemu ya Maazimio ya taarifa yetu kama Kamati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.