Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Madaba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UTAWALA, KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami niungane na Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati ya TAMISEMI kukushukuru wewe, Mheshimiwa Spika, Naibu Spika pamoja na Wenyeviti wa Bunge ambao wametupa ushirikiano mkubwa sana kama Kamati. Nitumie pia fursa hii kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote pamoja na Naibu Mawaziri ambao wamepata fursa yakuchangia taarifa hizi zote mbili ambazo zilikuja mbele yako. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee niwashukuru Waheshimiwa Wabunge waliyochangia hoja za Kamati ya Utawala, Katiba na Sheria ambao kwa idadi yao wanafikia sita pamoja na Naibu Mawaziri watatu, walichangia hizi hoja kwa ufasaha sana na Waheshimiwa Wabunge na Naibu Mawaziri wote waliyochangia walipata fursa ya kuunga mkono maeneo yote ambayo kamati yetu ilileta kama mapendekezo kwenye Bunge lako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo maeneo kadhaa ambayo nilitamani niwekee mkazo kwa sababu kwa sehemu kubwa michango yote ya Wabunge na Naibu Mawaziri imejielekeza kuunga mkono hoja pia kulihitajika ufafanuzi kwa baadhi ya maeneo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hoja zetu za Kamati, Kamati ilipendekeza kwa Serikali, iliitaka Serikali kupitia Wakala wa Ndege za Serikali kuongeza ndege moja kwa ajili ya matumizi ya viongozi. Ipo kasumba kwa baadhi ya Watanzania wenzetu kuamini kwamba kila aina ya usafiri ni starehe lakini wewe unajua uwekezaji kwenye vyombo vya usafiri siyo wakati wote ni starehe na vyombo vya usafiri siyo wakati wote ni liability, wakati mwingine au kwa sehemu kubwa usafiri unaohusu masuala ya utawala ni asset.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utakubaliana na mimi ndege ya Serikali F28, ilinunuliwa mwaka 1978 na ilinunuliwa na Baba wa Taifa kwa matumizi ya Serikali kwa maana ya viongozi, in aumri sasa wa zaidi ya miaka 39 bado watu wanaamini kwamba tungeweza kutumia fedha hizi tunazopendekeza kujenga vituo vya afya na zahanati, lakini ili haya yote yaweze kufanyika ni lazima kuhakikisha kwamba viongozi wetu kwanza wanakuwa salama lakini pili wanasafiri kwa haraka ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kujenga nchi kubwa kama Tanzania bila kuhakikisha kwamba wale viongozi wakubwa ambao tunawakabidhi majukumu mazito yakusimamia maslahi mapana ya Taifa letu hawawekewi mazingira salama ya usafiri lakini mazingira yatakayo wawezesha kufanya kazi hizo kwa ufanisi mkubwa zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hii ya awamu ya sita kwa haraka haraka tu imejenga hospitali za Kanda 16, imejenga hospitali za Mikoa 62, imejenga hospitali za Wilaya 351 lakini tunavyo vituo vya afya 1,126, tuna idadi ya zahanati zaidi ya 7,000, tuna shule za sekondari zaidi ya 486. Haya yote yamefanyika ndani ya Awamu hii ya Sita, mambo haya yanahitaji uwezeshwaji mkubwa wa shughuli za kiutawala, kuwawezesha viongozi wetu kuweza kuendelea kuyasimamia haya yaliyokwisha fanikiwa lakini kwenda kuwezesha mengine mengi zaidi ambayo Watanzania tunayahitaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niliombe Bunge lako liridhie Maazimio haya ya Kamati ya kuitaka Serikali iongeze ndege moja kwa ajili ya kuwezesha shughuli za utawala kwa matumizi ya viongozi ili F28 iweze kupumzishwa ili kurinda usalama na ustawi wa viongozi wetu ambao wanafanya kazi kubwa sana kwa Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya pili ambayo nilitamani niifafanue na niiseme kidogo kwa kina ni hoja hii ya madawa ya kulevya. Madawa ya kulevya ni janga kubwa sana kwa Taifa letu, hii nashukuru Waheshimiwa Wabunge waliyopata nafasi ya kuchangia wamesema hivyo akiwemo Mheshimiwa Florent Kyombo - Makamu Mwenyekiti wa Kamati hii lakini pia Mheshimiwa Naibu Waziri Patrobass Katambi, ameelezea kuhusu hoja hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha ukisikiliza takwimu. Kati ya mwaka 2017 mpaka 2020 matumizi ya madawa ya kulevya yameongezeka mara nne, yameongezeka mara nne katika muda huo mfupi lakini idadi ya watumiaji wa madawa ya kulevya kwa takwimu za mwaka 2019 duniani walifikia milioni 200. Sasa milioni 200 tafsiri yake ni nini, hii kwanza ni asilimia nne ya watu wote waliopo duniani na tafsiri yake nini, tafsiri yake katika kila watu 100 watu wanne wanatumia madawa ya kulevya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge hapa tupo karibu mia tatu na tisini na kitu, tafsiri yake ni nne mara nne kama watu 16 watakuwa wanatumia madawa ya kulevya. Naeleza tu tafsiri ya kitakwimu, hizi ni tafsiri za kitakwimu. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hali hii siyo ya kuifanyia dhihaka, niweke tu taarifa vizuri kwamba huu ni mfano kwamba tuna Wabunge karibu 400 humu ndani na kwa tafsiri ya nne kwa 100 maana yake ni kama watu 16 siyo jambo la kulifanyia dhihaka na wote tunajua madhara ya matumizi ya madawa ya kulevya, Taifa letu linaangamia, Watanzania wanazidi kuwa useless katika sekta ya ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya ukifuatilia hata wale wanaopata huduma za urahibu wapo pia watumishi wa umma ambao wameonekana wanatumia haya madawa ya kulevya, kwa hiyo hatari yake ni kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nilitaka niliombe Bunge lako tumpongeze sana, sana Kamishina Jenerali Arestas James Lyimo ambaye ameonyesha mfano katika usimamizi wa jambo hili, lakini niipongeze sana Serikali katika ujumla wake wamefanya kazi kubwa sana kwenye usimamizi na udhibiti wa matumizi ya dawa za kulevya pamoja na biashara yenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuja na mapendekezo mahsusi au pendekezo mahsusi kwenye eneo hili na misingi ya pendekezo letu ni hii. Mnafahamu kwenye taarifa yetu mmeona yapo mashauri 1,158 ya dawa za kulevya hadi sasa, kati ya hayo ni mashauri 64 pekee ndiyo yamefanyiwa kazi hadi sasa. Kwa hiyo, mnaweza mkaelewa mzigo mkubwa ambao Mahakama zetu zinazo. Kwa hiyo, tumetoa ushauri, tumetaka iundwe division maalum ambayo itakuwa inashughulikia mashauri ya madawa ya kulevya, faida zake ni kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza itawawezesha watoa maamuzi kwa maana ya Mahakimu wetu kubobea kwenye eneo hili la madawa ya kulevya mbinu na mikakati ambayo inatumiwa na wahalifu kwenye eneo hili, pia itawezesha Serikali kutenga rasilimali mahsusi kabisa kwa kushughulikia mashauri ya aina hii ili yaishe kwa wakati ili Watanzania wawe salama zaidi. Nashukuru katika michango ya Waheshimiwa Wabunge hakuna ambaye ameonesha kutoridhika na hoja hii na ninaamini Bunge lako litaipitisha kwa maslahi mapana ya Watanzania lakini kwa usalama wa Taifa letu na watoto wetu. Hayo ni maeneo mawili muhimu ambayo nilitaka niyaseme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge pia wameongelea kuhusu Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, kwenye hili niseme tu kifupi kwa sababu muda umeisha, Serikali mnakumbuka tumelizungumza sana suala hili. Watanzania wengi wanalalamika juu ya haki zao kuvunjwa na kwa sehemu kubwa zinavunjwa na baadhi ya taasisi ambazo tumezitungia sheria ya kusimamia mambo mbalimbali. Kwa hiyo, tunaomba sana hizi sekta za taasisi za umma ambazo zimepewa wajibu wa kuwahudumia Watanzania kwa namna moja au nyingine wahakikishe wanalinda haki za binadamu na wanasimamia utawala bora. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hii Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora tumeielekeza ilete taarifa mbele ya Kamati na hapa niombe kusisitiza kwamba tupewe hii taarifa ya Tume ili Kamati ipate mwanya au fursa pana yakuishauri Serikali juu ya malalamiko mengi ambayo Watanzania wanayo juu ya uvunjifu wa haki za binadamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo maeneo mengine ambayo yamekwisha zungumzwa, masuala ya Muungano mnajua credit kubwa inaenda kwa Mheshimiwa Rais mwenyewe kuhakikisha kwamba hoja 22 kati ya hoja 25 zinafanyiwa kazi na taasisi 33 kati ya taasisi 36 za Muungano ambazo zilitakiwa ziwe na ofisi Zanzibar, tayari zinaofisi, hayo ni mafanikio makubwa na hii ni credit kubwa kwa Mheshimiwa Rais na Serikali kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua tunayo Sheria ya Maafa, tumeona namna ambavyo Serikali imeshughulikia maafa na Waheshimiwa Wabunge wamesema hapa, nami niseme tayari tunayo sheria ya kushugulikia maafa nchini, ina miaka kama mitatu hivi, lakini tumetengeneza mfuko kisheria wa kushughulikia maafa nchini. Tunao mkakati mahsusi wa kushughulikia maafa nchini. Kamati imeomba taarifa juu ya utekelezaji wa haya yote ninaamini Serikali itajipanga ilete mbele ya Kamati taarifa hizi ili pia iweze kushauri na ilete mbele ya Bunge lako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la mwisho lilikuwa msaada wa kisheria kwa kupitia hii Mama Samia Legal Aid. Tunajua namna ambavyo imekuwa na faida kubwa kwa Watanzania na hapa imetolewa mifano kivipi leo Watanzania kwa idadi kubwa ile wanakwenda kueleza matatizo yao kwa viongozi wetu wa chama. Ni jambo zuri ni kwamba watanzania wana imani na Chama Cha Mapinduzi, wana imani na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo ni taswira nzuri lakini nyuma yake kuna changamoto. Changamoto mojawapo ni kwamba hawa wananchi wetu wengi hawajapata nafasi yakusikilizwa, kwa hiyo moja ya namna nzuri ya kutatua changamoto hii ni kuiwezesha Mama Samia Legal Aid iweze kufikisha huduma kwa Watanzania walioko vijijini. Kwa hiyo Serikali inapotafakari namna yakutatua changamoto hizi pamoja na zile ambazo Waheshimiwa Wabunge wamesema, iangalie uwezekano wa kuongeza nguvu kwa Mama Samia Legal Aid iweze kuwafikia Watanzania wengi zaidi waweze kupata suluhu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemsikiliza Naibu Waziri wa masuala kwa sasa yupo ardhi lakini alikuwa Katiba na Sheria huko nyuma, ameeleza kwamba hatuwezi tukawatumia Maafisa wa Sheria wa Halmashauri kwenye eneo hili lakini sasa ndiyo hatuna watu tufanyeye, Serikali mtupe suluhisho kwenye jambo hili ili tuweze kukabiliana nalo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naomba nitoe hoja ya kwamba tunaliomba sasa Bunge lako Tukufu liridhie hoja za Kamati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja. (Makofi)