Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Morogoro Kusini Mashariki
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu Azza wa Jalla, lakini pia nimshukuru Mheshimiwa Rais wetu wa Awamu ya Sita, Mama Samia Suluhu Hassan lakini vilevile niishukuru Kamati yetu, Mheshimiwa Mwenyekiti na Wanakamati wenzangu wote kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nitachangia eneo moja la michezo na nimshukuru Katibu wa Bunge, aliyepanga majina amepanga kiutaratibu. Ameanza na Profesa akaenda kwa Mama pale akaja kwangu Dkt. Taletale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninachangia kwenye suala la michezo. Watu wote humu ndani, labda tujizime data, lakini tunafahamu michezo ni uhai, tunafahamu michezo ni amana ya nchi hii. Kabla sijaenda mbali, wiki iliyopita tulikuwa tuna bonanza letu la michezo wale wenzetu, wapinzani wetu wakiongozwa na striker wao kaka yangu Mwingulu Nchemba, wakanunua mchezaji kutoka nje ni kwa sababu ya michezo tulikutana pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tukirudi kwenye hii Wizara ya Michezo. Wizara hii ni kama Wizara yatima katika Wizara zote ambazo zinaongozwa na Serikali ya Awamu ya Sita. Mimi nimechoka kuimba neno michezo, kuimba jamani Wizara ya Michezo ipewe fedha. Lakini Mheshimiwa Rais, kwa mapenzi yake ya dhati na kwa mapenzi ya kuonyesha anapenda michezo akaielekeza Wizara ya Fedha, kutoka kwenye michezo ya kubashiri wapeleke asilimia tano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini wakija kwenye Kamati ile asilimia tano kama bado wanaomba. Alhamdullilah, brother wangu Mwigulu yuko hapa; mimi leo ningeomba, na hata Mheshimiwa Mwigulu, aongee kwamba ile asilimia tano ambayo inatoka kwenye michezo ya kubashiri tungependa kujua exactly date. Kwa mfano mwezi wa nne tarehe fulani asilimia tano itatoka Wizara ya Fedha, itakwenda Wizara ya Michezo, ni aibu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunajifunza kwenye nchi zilizoendelea. Leo hii kama Sports Betting inafanya vizuri Japani, ipo ndani ya Wizara ya Michezo, inafanya vizuri Uingereza ipo ndani ya Wizara ya Michezo. Kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu, mimi nikuombe kama hautojali hili gurudumu lote hili la michezo ya kubashiri ipeleke pale Wizara ya Michezo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushahidi huu mimi ninao kutokana na Serikali ya Uingereza ambako Michezo ya Kubashiri ipo ndani ya Wizara ya Michezo, Serikali ya Japani, Michezo ya Kubashiri ipo ndani ya Wizara ya michezo. Kama mnaona ni suala la fedha hata Wizara ya Utalii, inatengeneza pia fedha mbona haipo ndani ya, mifano hiyo midogo midogo. Lakini mmeona kwa sababu huku kuna michezo, kuna fedha basi mnaona hii Wizara ya Michezo, isiwekewe fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nimeongea vitu viwili. Kitu cha kwanza naomba Wizara ya Fedha kama haitojali isimame itutajie exact date ya ile 5% ambayo ipo kisheria Mheshimiwa Rais, ameelekeza Wizara wapatiwe hii fedha hawapewi. Hata ukiwahoji hawakumbuki lini wamepata huyo hapo mtani wangu wa Kingoni na anongeza kubadilisha miwani tu ya lens kwamba haoni vizuri kwa sababu fedha hapati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina Kaka yangu, ndugu yangu Mwana FA. Unajua kuna Wizara ukiwa unaona ujiko ni hii Wizara ya Michezo, ni Wizara ujiko, lakini ujiko wenyewe ni ujiko wa kutokuwa na fedha brother. Mimi nikwambie, wiki iliyopita tumepata bahati ya kutembelea Uwanja wa Taifa na; hata hivyo tukapata bahati ya kutembelewa na mtu kutoka kwenye Gaming Board. Yule bwana anachoongea anadhani sisi hatuna mamlaka ya kuitoa Gaming Board kutoka kwenye Wizara ya Fedha, kuleta Wizara ya Michezo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu, wewe ni Mwanamichezo, unajua michezo ni striker. Kuna Mbunge wa Bunge la Kenya, alikuja kucheza Arusha alipoona Mheshimiwa Mwigulu, hayupo uwanjani akaona hapa tunafungwa. Sasa kama kweli unajua Michezo, michezo bila fedha ni uongo jamani, Wizara ya Michezo haina fedha ABMT, haina bajeti hata sisi Wajumbe tukipata nafasi ya kusafiri kwenda kwenye Kamati yoyote, tukiwa tunasafiri na Wizara ya Michezo tunaanza kupiga lamli sijui tutajilipa? Unajua of course mkisafiri cash absorber lazima mpate kwenye Wizara, lakini Wizara yetu ya Michezo inatia huruma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimuombe Mheshimiwa Mwigulu, kama hatojali tunaomba Gaming Board ihamie Wizara ya Michezo. Kuhusu wataalam ituhamishie na wataalam, yote ipo Serikali moja, yote inaongozwa na Mama mmoja. Wakati nikiongea hapa Kaka yangu Mheshimiwa Tarimba, ananiangalia kwa sababu napiga sehemu ambayo yeye ndipo anajua zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukweli ni kwamba kama hii asilimia tano imeelekezwa na Mheshimiwa Rais, na bado Wizara inapuuza wasomi mnanitia mashaka mimi tabu darasa. Wasomi mnatuharibia michezo, wasomi ambao tunawategemea mjue umuhimu wa michezo mnatuharibia michezo, mnataka kuua ndoto za Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Rais, ndoto yake kubwa ni kuona michezo inakua nchini, lakini leo hii tunawaamini wasomi, kwamba mnajua bila fedha hakuna mchezo bado mmekumbatia fedha mnasubiria muda ufike mtembeze bakuli. Hii ndiyo nchi pekee ambayo inaoongoza kwa kutembeza bakuli. Hii ndiyo nchi pekee ambayo kiukweli, ndiyo tunaanza wale wengine…
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
TAARIFA
MWENYEKITI: Mheshimiwa Hamisi, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Tarimba.
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, Meshimiwa Taletale anatoa hoja nzuri sana, hoja ambayo inapaswa kuungwa mkono. Hivi hawezi akashauri Serikali Mheshimiwa Taletale, katika mchango wake kwamba Serikali ilete mapendekezo ya kubadilisha baadhi ya vifungu vya sheria vinavyohusu upelekaji wa ile asilimia tano? Kwamba sasa asilimia tano ile itajwe kwenye sheria kwamba ikifika tarehe kumi ya kila mwezi fedha zile ziwe zinapelekwa Wizarani kwenye Wizara ya Michezo.
MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Taletale, taarifa unaipokea?
MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea kwa mikono miwili. Nakumbuka nimesema nina utaalam na ninachokiongea kwa hiyo hata ule mchele ambao unaingia kwenye Wizara kule anajua, ukija huku tataneemeka kiasi gani, Kaka yangu Tarimba, ahsante sana Wanakinondoni wana jembe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea kuchangia. Kwenye hili suala la hii asilimia tano ya michezo ya kubashiri ambayo sisi tumepunguza makali ni kamali. Kwa sababu sisi Waislamu tunajua kamali haramu hatuwezi kusema kamali tunasema kubashiri, sawa. Hii michezo ya kubashiri, niiombe Serikali, niombe Kiti chako kielekeze Wizara, utaratibu wa hii asilimia tano ambayo imetajwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, bado hawa Wizara hawapati hii fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nijue, kuna mtu anabisha na kauli ya Mheshimiwa Rais au? Mimi nimesema hapa Bungeni mara mbili kuna mtu anabisha na kauli yangu nikiwa Bungeni, shida ni nini? tuongee ukweli (let’s be honest). Kama tunafuata utaratibu wa kuchangia michango leo hii kuna michango mmechangia pale hotelini kuna baadhi ya watu hawajachangia vilevile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilipata bahati ya kwenda AFCON, nchi kama Ivory Coast imeendelea sana lakini imeendelea kwa sababu Serikali imeweka fedha kwenye Wizara yake ya Michezo, nchi kama Senegal imeendelea sana kuanzia timu zake zote za ndani inafanya vizuri, inafanya vizuri kwa sababu Serikali imeweka fedha kwenye michezo.
MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
TAARIFA
MWENYEKITI: Mheshimiwa Hamisi, una taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Keysha.
MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa mzungumzaji na kum-support kwamba michezo ni sehemu moja wapo kama hii nchi tutaizingatia zaidi ni sehemu moja wapo ya kutengeneza ajira nyingi kuliko sehemu nyingine yoyote. Kwa hiyo, ni eneo ambalo Serikali ikitizama kwa umakini na kwa jicho la tatu ni sehemu ambayo tutaingiza fedha nyingi sana na tutakomboa lile tatizo letu la unemployment katika nchi yetu, ahsante.
MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Hamisi, taarifa unaipokea?
MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea kwa mikono miwili. Mimi niongezee hapa maana wanasema kijiji bila wazee ni uhuni, wewe ni Mwenyekiti wa Bajeti, unajua mimi ninachokiongelea kinapita kwenye eneo lako. Sasa kama hujakaza wewe atakaza nani? Sikubani pabaya, najua nimeshambana kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu. Tumuonee huruma yule Baba wa Kingoni pale, yule Baba wa Kingoni tia maji tia maji Wizara yake haina fedha anatia huruma, Mheshimiwa Rais, hajampa Wizara ili aje kuchubuka kuongeza mvi humu ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais amempa Wizara na ameelekeza fedha ije inapita kwenye Kamati ya Bajeti na wewe unaona. Basi nikuombe kwenye hili utafute njia ya sisi wapenda michezo, sisi Watanzania tuna amani kwa sababu michezo inafanya vizuri. Lakini bado inafanya vizuri kwa namna ya tia maji tia maji. Nikuombe nafahamu unalifahamu hili twende tukaangalie hii 5% kama alivyosema kwenye taarifa yake Kaka yangu Mheshimiwa Tarimba, tuombe tupate exact date kutoka kwenye Wizara ya Fedha, tujue hii 5% aliyoelekeza Mheshimiwa Rais, inakuja vipi na tarehe ngapi… (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana, Mheshimiwa. Muda wetu umekwisha.
MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kengele ya kwanza.
MWENYEKITI: Ya pili, muda wako umekwisha Mheshimiwa, malizia.
MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)