Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Angelina Adam Malembeka

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023


MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kunipa fursa na mimi kuchangia katika Wizara hizi. Pia, nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwenye wingi wa rehema kwa kuniwezesha kuweza kuongea katika siku hii ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais Mama yetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya hapa nchini na sisi wote tunamuunga mkono tunasema mitano tena. Niwapongeze Mawaziri wa Wizara zote mbili, Naibu Mawiziri wao, Makatibu Wakuu na watendaji kwa ujumla kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kumsaidia Mheshimiwa Rais katika kutekeleza majukumu yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa Vazi la Taifa. Vazi la Taifa limekuwa ni mjadala na swali ambalo tumelizungumza kwa kipindi kirefu tangu Bunge la Kumi na Moja tumezungumza na hili Bunge la Kumi na Mbili, nina wasiwasi tunaweza tukafika wengine mpaka Bunge la Kumi na Tatu Vazi la Taifa halijapatikana lakini ni pesa nyingi zimetumika, vikao vingi vimefanyika, posho nyingi wamelipana kwa ajili ya kutafuta Vazi la Taifa kana kwamba mpaka sasa hivi Watanzania hatujui kuvaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nafikiri Vazi la Taifa kinachotakiwa ipatikane nguo ya stara yenye ustaarabu, yenye heshima na inayoonyesha unadhifu ambayo inaweza ikavaliwa na rika lolote kwa umbo lolote na nguo ambayo inaweza iikatengenezwa na kwa malighafi yoyote ina maana kwa cotton kama tetroni kama ni ginger, kwa kitenge itapatikana na hiyo nguo iweze kuvaliwa mahali popote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nafikiria kwa mavazi anayovaa Mama yetu Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan inatosha kabisa kuwa vazi la Taifa, kwa sababu zile nguo zina stara, zina ustaarabu, zina heshima na unadhifu wa hali ya juu. Vazi la kanzu na ndani suruali hata mwanaume ameweza kuvaa tukawa tunashindana tu huku juu mbwembwe huyu akaweka vifungo, huyu akaweka zipu lakini nguo ya Taifa ikapatikana. Haiwezekani miaka kumi tunatafuta Vazi la Taifa. Naomba pafanyiwe kazi tujue nguo gani tunavaa mpaka sasa hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nilizungumzie ni juu ya mdundo wa Taifa. Tanzania hii tuna makabila zaidi ya 120 lakini nilivyouliza mdundo wa Taifa nikaambiwa mtaalamu amepatikana anataka kuchanganya midundo ya makabila yote ili upatikane mdundo, hiko kitu hakiwezani. Kuna Mikoa ya Kaskazini ngoma zao zinachezwa kuanzia mabega kwenda juu. Kuna wale wa Kusini ngoma zao zinachezwa kuanzia kwenye kiuno kwenda chini wewe unataka kuniambia ngoma ya Mngoni utaenda kumchezesha Mmasai, unataka kuniambia ngoma ya Mmakonde utaenda kumchezesha Mpare, unataka kuniambia ngoma ya Muhaya unaweza kumchezesha Mpemba? Kwa kweli hicho kitu hakiwezekani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo midundo ya Taifa ambayo ipo automatically imefika ipo. Nikitolea mfano ule mziki unaopigwa kabla ya taarifa ya habari ya Zanzibar popote ukipigwa ule wanajua sasa taarifa ya habari huo unafaa kuwa Mdundo wa Taifa. Kuna mziki unaopigwa na Redio Tanzania wa Mourice Nyunyusa ule ngoma 12 zile ukipigwa kokote tunajua hii ni taarifa ya habari inakuja. Kwa nini hiyo midundo hiyo isitafutwe ikasemwa hii ni Midundo ya Taifa badala ya kwenda kutafuta makabila 120 utuchanganyie utuambie mziki, huo mziki gani tunaenda kudundia wapi, tutachezaje kwanza? Mimi ninaomba hiyo Kamati iliyotengenezwa kwa ajili ya Mdundo wa Taifa japo imesema imemaliza kazi yake bado kuzindua mimi naona tuangalie huo mdundo tunaotengeneza una asili gani, hizo mbili tu nilizotaja mtu anajua ngoma hii asili yake mahali fulani na ilipigwa na fulani na ina historia yake badala ya kutuchanganyia vyombo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye suala la Mfuko wa Wasanii; Kwanza kwenye upande wa sanaa nimeona hata huo mfuko umeangalia zaidi kwa waimbaji siyo kwamba sitaki wapewe, kwa waimbaji, lakini tumesahau kuna waumbaji, wafinyanzi, watengeneza mikeka kama jamvi, vikapu, matenga, wasusi na wasokotaji kamba, wapaka rangi, wachoraji na wabunifu yani designers hao naona amesahauliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kusahauliwa kwao sasa hivi wazungu wanakuja, wanajifunza huko kusuka mikeka, kutengeneza makapu, kutengeneza sijui matenga halafu sisi tunaletewa ya plastiki vikapu vya plastiki, matenga manini tunapeleka mpaka kijijini. Ule utaalamu kule unakufa, hakuna watu wa kuwafundisha na wale ambao wapo hatuwawezeshi, matokeo yake baada ya miaka kadhaa watauambia hizo plastic zinaleta kansa na zinachafua mazingira, makapu ya kwetu watatuletea watatuuzia tena wakati wale wenye uwezo wa kutengeneza wameshapotea na hiyo fani haipo. Mimi napendekeza Serikali iwaone hawa wenye ufundi wa jadi wawasaidie ili ile fani iendelee na tuepukane na haya mambo mengine ya kuletewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije katika lugha yetu ya Kiswahili, sasa hivi Kiswahili kimekua na kimekua sana na kimekua kwa kasi. Nipongeze BAKITA kwa kuleta kamusi mpya kubwa na yakisasa ambayo imechanganua vitu vingi sana. Kuna wakati BAKITA walikuwa wanatoa baadhi ya maneno ya Kiswahili alafu wanatoa tafsiri yake kwamba neno hili maana yake hii tunaona kwenye mtandao sioni sijui kwanini wameacha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu na hofu yangu ni kwamba hiki Kiswahili kinachokua kuna maneno ya Kiswahili ambayo yana maana tofauti wao wanayatengeneza wanavyotaka wenyewe halafu mtu unashindwa hata kutamka mbele za watu lile neno wakati unajua ni neno la kawaida la Kiswahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zamani mtu anaweza akakwambia mimi napenda msondo, napenda sikinde, napenda taarabu; lakini siku hizi ukisema mbele za watu napenda taarabu wanakushangaa kutokana na tafsiri waliyoiweka huko mtaani. Sasa BAKITA iwe inatoa amelezo kamili kwamba lugha hii maana yake hii na lugha hii maana yake hii nah ii siyo sahihi wanavyonyamaza kimya lile neno linakua na watu wanaona la kawaida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije nizungumzie kwenye suala la michezo ya kubahatisha. Nakumbuka mwaka 2021 tulikaa hapa kufanya marekebisho ya Sheria katika Baraza la Michezo ambapo tulikubaliana 5% ya mapato yanayopatikana kwenye hii michezo ya kubahatisha ipelekwe kwenye Wizara hususani kwenye Baraza la Michezo la Taifa ili kufanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninahisi mpaka sasa hivi hizo hela haziendi na kama zinaenda zinaenda kidodo sasa basi Serikali ituambie kwanini hizo pesa haziendi wakati Sheria imeshapitishwa, Wizara kwa nini inashindwa kupokea hiyo pesa wapelekewe hizo pesa waweze kufanya kazi badala ya kuwa kila siku tunawalaumu tu kwenye michezo kumefanya hivi kumefanya hivi wakati pesa hatupeleki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na shida hiyo niwapongeze watu wa Wizara kwa kweli kwa mwaka huu wamejitahidi timu zetu nyingi zimefuzu japo huko mbele ya safari tumekosa bahati. AFCON wanaume wameenda Ivory Coast walifuzu japo kule tulipoteza lakini kuna AFCON wanawake wanaenda Morocco kuna…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa ahsante sana muda wako umeisha malizia.

MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante naomba dakika mbili za kumalizia. Kwa ufupi nizipongeze timu zote lakini mwisho kabisa nimpongeze Mama Samia Suluhu Hassan kwa hoja ya Kigoma Mjini kwa yule mtoto Ally Haji ambapo pamoja na matatizo yalivyojitokeza Mama Samia Suluhu Hassan Mheshimiwa Rais wetu aliyeamua kuonyesha Umama wake, ameamua kumtibia yule mama kujenga nyumba kwa yule mama kumpa mtaji wa biashara na kumsomesha, lile jambo ni zuri tunampongeza tunamuunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawaomba Wizara ya Maendeleo ya Jamii kwamba tunapowakuta watoto mitaani tupate fursa ya kukaa nao, tuwahoji, tujue wana matatizo gani ili tuweze kuwasaidia. Ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)