Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Aloyce John Kamamba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buyungu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hoja ambayo iko mbele yetu lakini zaidi nawapongeza sana Wenyeviti wa Kamati kwa uwasilishaji mzuri wa taarifa pamoja na Kamati zote kwa kazi nzuri ambayo wameifanya, wametuwakilisha vema wanakamti kwenye maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Rais sisi Buyungu ametusikia, sisi Buyungu tumemwelewa, sisi Buyungu tunamshukuru sana. Mwaka kesho 2025 kazi yetu itakuwa ni moja tu kwenda kumpigia kura za ndiyo ili aweze kuendelea kutuongoza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na ujenzi wa shule za sekondari na msingi. Katika maeneo ambayo Serikali imefanya kazi vizuri sana ni kwenye upande wa elimu ya msingi na sekondari. Yamejengwa madarasa mengi, vimejengwa vyoo, zimejengwa nyumba za walimu lakini idadi ya wanafunzi vilevile imeongezeka sana. Tunapongeza sana Serikali kwa kazi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo ongezeko la wanafunzi halikwenda sambamba na ongezeko la kuajiri walimu. Nikikupa takwimu kwa upande wa elimu ya sekondari uhitaji wa walimu kwa asilimia 47, na upande wa shule za msingi uhitaji wa walimu ni asilimia 42. Nikichukua Mkoa wa Kigoma upande wa uhitaji wa walimu sekondari asilimia 33 upande wa shule za msingi asilimia 46. Nikichukua Wilaya yangu ya Kakonko uhitaji wa walimu shule za msingi asilimia 38, upande wa sekondari asilimia 52. Ukiangalia kwa ujumla bado walimu waliopo na wanaohitajika ni nusu kwa nusu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoshangaa ni kuona kwamba walimu wapo kwa asilimia 47 lakini wanafaulisha kwa asilimi 80. Maana yake ni nini? Walimu wa nchi hii wamefanya kazi ya ziada kuziba pengo la walimu ambao hawapo. Hoja yangu walimu waajiriwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwenye uhitaji wa walimu na ajira, ajira inakwenda kwamba ikishapita umri wa miaka 45 hawezi kuajiriwa; lakini tunao walimu wana miaka zaidi ya kumi wako mitaani. Tuombe sana ajira ya walimu ifanyike ili walimu waweze kuja kusaidia katika maeneo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, shule za sekondari zimejengwa kila kata nchini, lakini shule hizi zinapojengwa zilizo nyingi zimejengwa katikati ya kata. Na kutoka Kijiji kimoja kwenda kwenye shule zinapojengwa ni umbali mrefu. Kwa hiyo jua likiwaka ni la wanafunzi hao, mvua ikinyesha ni ya wanafunzi hao. Niombe sana yajengwe mabweni kwenye shule zetu za sekondari. Yakijengwa mabweni tuna uhakika moja, wanafunzi wetu wawe wa kike wawe wa kiume tuna uhakika sehemu ambayo wataishi, lingine, itakuwa ni rahisi kwa walimu hawa kuweza kuwafuatilia. Inapotokea kwamba sasa wanafunzi hawa hawana sehemu maalum ambayo wanaishi ni rahisi kuingia kwenye vishawishi, ni rahisi kuja kukutana na mimba za utotoni. Niombe sana mabweni yajengwe ili yaweze kuhudumia watoto wetu katika shule za sekondari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu elimu ya watu wazima. Ukifuata takwimu ambayo walitupatia Wizara ya Elimu wakati wanawasilisha kwenye Kamati idadi ya ambao hawajui kusoma, kuandika na kuhesabu inaongezeka kwenye nchi hii. Lakini tunao vijana wanaoanza shule ya msingi wanakosa kuendelea kutokana na sababu mbalimbali. Wapo wengine wanaanza lakiniwanakutana na vishawishi mbalimbali, wengine wanapata ujauzito, wengine wanakwenda kwenye biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mpango wa elimu ya msingi kwa walioikosa (MEMKWA) isimamiwe vizuri ili iweze kukidhi mahitaji ya vijana hao ambao wamekosa nafasi. Lakini wapo wale ambao wanakwenda sekondari, nao wanakutana na changamoto ya kushindwa kuendelea kutokana na mahitaji mbalimbali, mwingine anakwenda kwenye biashara na pia wapo wanaopata ujauzito. Tuombe sana vijana hawa wapewe nafasi ya kurudi shuleni, lakini vilevile walimu waajiriwe maalum kwa ajili ya kuhudumia vijana hawa ambao wanahitaji nao kupata elimu ya sekondari kupitia mpango wa elimu ya sekondari nje ya mfumo rasmi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Bodi ya Mikopo. Tunashukuru Serikali imeongeza fedha Bodi ya Mikopo, lakini si vijana wote ambao wanahitaji wanapata mikopo, vilevile wapo ambao wanapata lakini kwa kuchelewa. Tuombe sana Wizara ijipange vijana wetu wapte taarifa mapema wale ambao watapata; lakini iangalie zaidi wapo wanaostahili kupata hawapati, hawapati kwa nini? Tumbe sana Serikali ijipange ili kuhakikisha kwamba vijana wetu wanaohitaji mikopo wanapata na wapate kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa mitaala mipya imeanza vizuri na wameipanga vizuri, na inakuja kujibu changamoto zinazokabili wananchi na vijana wa nchi hii. Hata hivyo hapakuwa na maandalizi ya kutosha. Walimu maalum kwa ajili ya kuendesha mtaala mpya hawapo; lakini vilevile vitabu havipo. Isitoshe, wale walimu ambao tunao wanaotekeleza mradi au mtaala huu mpya hawajapewa mafunzo. Niombe vitabu viandaliwe, walimu wapewe semina na walimu wengine waongezwe kwa ajili ya kukidhi huu mtaala mpya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzangu wamezungumza sana kwenye upande wa michezo, lakini mimi kwenye upande wa michezo nitazungumzia suala uboreshaji wa michezo hadi kwenye ngazi ya jamii. Tunaipongeza Wizara, inatumia michezo kwa shule za sekondari (UMISETA) na shule za msingi (UMITASHUMTA) kupata vijana kutoka kule kuja kuwaendeleza. Lakini tunao vijana ambao hawako shule ya msingi lakini hawako shule za sekondari, hawa nao sasa tunawasaidiaje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unaweza ukamkuta haujui kusoma na kuandika lakini ukimpeleka kwenye mpira wa miguu ni mzuri sana. Uwekwe utaratibu maalumu wa kuhakikisha kwamba vijana wote walioko mitaani waandaliwe na wafuatiliwe kule ili kuhakikisha kwamba na wao wanaendelezwa kwenye upande wa michezo na katika hilo iandaliwe shule maalum ambako hawa vijana wanaotoka UMISETA, UMITASHUMTA wapelekwe katika maeneo hayo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa kwa mchango wako mzuri sana.

MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)