Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kigoma Kusini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia kwenye Wizara hizi mbili. Nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniruzuku uhai na afya hapa ninapoenda kuzungumza mambo ya wananchi, mambo ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba kwa dhati kabisa nimpongeze Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anazofanya kwenye Wizara hizi mbili. Ni ukweli usiopingika Mheshimiwa Rais wetu ni Mwanamichezo kwelikweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwenye elimu kwenye eneo la VETA. Ni kweli Serikali imefanya mapinduzi ya kuhakikisha kwamba kila wilaya inapata chuo cha VETA. Na mimi namshukuru kwamba tayari kwenye Wilaya ya Uvinza kuna VETA tayari na imeanza mwezi huu wa kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo hili la VETA, ambapo sasa VETA hizi zinaenda kujengwa kila wilaya kwenye nchi yetu hii; ni jambo jema sana kwa sababu vijana wetu wanakwenda kupata ujuzi na maarifa moja kwa moja, na vijana wetu watakuwa na uhakika wakitoka pale wanakwenda kujiajiri kwa sababu tayari wana utaalamu. Hili ni jambo jema sana ambalo limefanywa na Serikali ya Awamu ya Sita. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina sehemu ambayo kidogo napata wasiwasi kwenye eneo la walimu, tusije tukajenga majengo na wanafunzi wakaenda pale wakakosa walimu wa kuwapa yale material ambayo yanakusudiwa kwenye kile chuo. Naomba sana kwenye eneo hili Serikali iwekeze kwenye upande wa walimu na vifaa vya kufundishia. Kwa kweli, mimi nilishangaa juzi nilikutana na kijana mmoja ambaye amesoma vizuri lakini anatamani apate mafunzo ya ufundi, kwa hiyo, yuko tayari kwenda VETA, alishamaliza elimu yake lakini anatamani aende VETA ajifunze utaalamu ili aweze kuingia kwenye ajira, maana amesubiri ajira hapati, basi anaona bora apate utaalam na maarifa, ujuzi ili aweze kuingia sokoni aanze kutafuta maisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo hili naomba Serikali iweke fedha kwa ajili ya kuwalipia hawa vijana. Kule kwenye vijiji vyetu hali ni mbaya sana, tusije tukajikuta tunajenga vyuo halafu watoto hawapo, kutokana na hiyo fedha ambayo watatakiwa kwenda kulipa pale. Mimi naishauri Serikali iweke fedha wale vijana wakopeshwe baada ya kukopeshwa, wale watakaokuwa wamehitimu vizuri wapewe mtaji mbegu, wapewe vifaa vya kwenda kufanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama amejifunza ufundi wa kushona nguo, fundi cherehani, amehitimu vizuri apewe cherehani, atakuwa anaweza kulipa ile fedha ambayo alilipiwa na Serikali wakati anaingia chuoni na mpaka kumaliza lakini pia atakuwa na uwezo wa kulipa hata hiyo cherehani. Hata wale watakao kuwa ni mafundi wa welding waweze kupewa mtaji mbegu kwa maana ya kupewa mashine ya welding ili waweze. Maana yake ukiishia pale kumpa tu maarifa halafu ukamuacha bado atazurura mtaani, bado atahitaji aende apate ajira. Sasa nadhani kwenye eneo hilo Serikali kama itafanya hivyo nina imani kwamba hapo tutakuwa tumepatia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye eneo la michezo. Ninaipongeza Serikali ya Awamu ya Sita ambayo inaongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuja na mpango wa kujenga viwanja vitatu vya michezo vyenye hadhi ya Kimataifa. Kiwanja ambacho kitajengwa Dar es Salaam, kingine hapa Dodoma, kingine Arusha hili ni jambo jema sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekaa na Uwanja wa Mkapa kwa muda mrefu sana …
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Malizia mchango Mheshimiwa, muda umeisha.
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Mwenyekiti, basi naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)