Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Nami nianze kwa kuwapongeza Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu na Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii, hongereni sana kwa hotuba zenu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kwanza kabisa kwa sababu nachangia kwenye elimu, niwapongeze sana sana watumishi wote ambao wameonesha hamasa kubwa ya kusoma kujiendeleza na hasa Wabunge wengi ambao safari hii wameingia katika kujiendeleza, wasikatishwe tamaa na watu ambao mara nyingi wanakwenda kubeza wasomi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakwenda kwenye suala la mikopo. Suala la mikopo niipongeze sana Serikali imejitahidi kutoa mikopo lakini hasa kwa upande wa vyuo vya kati. Safari hii vyuo vya kati vinavyoingia kwenye yale madaraja sita wanafunzi wote wa Diploma watapata mikopo, hata hivyo, inaonyesha kabisa kwamba bado kuna kundi ambalo halitapata mikopo. Kwa mfano, wale wanaochukua Diploma za Utumishi na sehemu nyingine hawako kwenye hii list.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitakuja kwa upande mwingine zaidi kwenye suala la mikopo, kama Serikali imejitahidi kutoa mikopo kwa maeneo haya sita ambayo ni afya na sayansi, elimu ya ualimu, usafiri na usafirishaji, uhandisi wa nishati, madini na sayansi ya ardhi, kilimo na mifugo ina maana Serikali hapo imejitahidi na hawa ndiyo watakaofanya kazi katika maeneo yetu ya kati, kwa kufanya hivyo tutapunguza ule upungufu wa wafanyakazi katika zahanati zetu, katika afya, maafisa wa maendeleo na watu wa manunuzi, hao wote wanaingia huko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niseme hizi fedha ingawa zimetolewa hazitoshi, kitu kingine kinachotufanya bado tukalalamika kwamba wanafunzi wetu wanahitaji mikopo hasa hawa wa kati ni kwa sababu wale waliopata mikopo hawalipi mikopo yao. Niombe sana Serikali sasa ijipange watu waliokopeshwa wamesoma, wamemaliza na wengine wapo kwenye ofisi, kwenye taasisi mbalimbali walipe ile mikopo ili hawa watoto wengine wote wapate mikopo, wakifanya hivyo hatutakuwa tena na makundi kwamba hili kundi ndiyo lipate mikopo, watoto wote watapata mikopo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wengine wako humu ndani, tumalize kulipa mikopo ili watoto wetu wote wapate mikopo. Tena kuna wengine marafiki zangu nawafahamu, sasa tukifanya hivi, mimi nawaambia tukifanya hivi hatutapata tena shida ya watoto kusema aah! Mimi sijui sina mkopo, diploma hii ipate mikopo, hii isipate mikopo kwa sababu wote watapata mikopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali na Bodi ya Mikopo ninawapongeza sana wameanza kampeni inaitwa “Fichua” hiyo kampeni inafichua wale wote wenye madeni hawataki kulipa mikopo. Kwa hiyo, usishangae utakapoona na mimi nipo kwenye hiyo Kamati ya fichua, mimi nina maeneo yangu na mimi nimepangiwa huko. Niwaombe tuwe wazalendo, tulipe madeni ili tusilalamike ili hawa watoto wetu wote wapate kusoma. Kama wewe umesomeshwa na hii mikopo kwa nini usiwalipie watoto na wengine wazazi wana uwezo walipieni vijana mikopo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hivyo basi nije kwenye hizi taasisi mbili nitazungumzia. COSTECH pamoja na Elimu ya Watu Wazima. Tulitembelea pale COSTECH mimi nilishaangaa, wale watu wanafanya utafiti na ubunifu, kuna ubunifu unaoshangaza na unaofurahisha lakini COSTECH tatizo hawajitangazi wako pale. Tulikuta vijana wamebuni utengenezaji wa mbolea kiasi kwamba wakati mwingine unaweza ukasamehe hii mbolea ya Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Bashe. Wanatengeneza mbolea ya asili inafungwa kabisa safi, haina chumvi chumvi wala nini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa COSTECH nao wana tatizo moja, niombe Serikali iwasimamie COSTECH, kwanza waorodheshe wabunifu wote katika vyuo vyote. Namba mbili, wabunifu wote waliopo kwenye jamii, wako vijana huko wanabuni vitu vya ajabu vinavyofurahisha lakini wamekaa pale ukiwauliza naomba list ya wabunifu katika vyuo, hawana! Naomba list ya wabunifu mtaani, hawana! Wabunifu wapo ili hawa wabunifu waweze kuwekwa vizuri, wapewe mipango na hao wabunifu watawezakujitegemea vizuri zaidi kiuchumi. Kwa hiyo, hii COSTECH bado haijajitangaza lakini wajipange vizuri ili tujue hawa vijana huu ubunifu tumefikia kiasi gani. Siyo wanakuja tu kwenye maonesho pale uwanjani, wanatuonyesha ubunifu tunashangaa shangaa hatuelewi kinachoendelea, tunataka wale wabunifu waje wawe matajiri, ubunifu wao uwasaidie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye elimu ya watu wazima. Hiyo elimu ya watu wazima kwenye miaka ya 1980 mpaka 1990 sisi tukiwa tunakua tulikuwa tunaisikia elimu ya watu wazima, elimu ya watu wazima leo hii ni kama haipo. Elimu ya Watu Wazima nao wana tatizo, wajitangaze hawa kama walivyosema wenzangu. Kuna watoto wale ambao wengine wanaona aibu wale ambao walitoka walishindwa kuendelea na masomo Mheshimiwa Rais akasema waingie na wao wasome. Sasa kuna wengine wanajinyanyapaa wanasikia aibu kwenda kwenye haya madarasa ya kawaida, haya ya sekondari ya kawaida lakini Elimu ya Watu Wazima ina vituo inaweza ikawachukua wao, hapa nyuma ya VETA wapo wanafunzi wanaosoma elimu hii ya sekondari kupitia elimu ya watu wazima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Elimu ya Watu Wazima ijipange kila Mkoa ikusanye, isaidiane na sekondari za kawaida, wajipange wakusanye watoto waingie wasome. Kwa kufanya hivyo tutasaidia sana kupata idadi kabisa ya wanafunzi wetu walioko nje ya mfumo wa kawaida ambao wamerudi katika madarasa. Nimesema hivyo kwa sababu gani? Elimu ya Watu Wazima wajitangaze kwa nini?
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, muda umeisha?
MWENYEKITI: Muda umeisha Dkt. Thea.
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nipe dakika moja tu nimalizie.
MWENYEKITI: Mheshimiwa malizia kwa sekunde 30.
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, haya, hawa Elimu ya Watu Wazima wenzao walikuwa wanatangaza zamani, tulikuwa na Redio Tanzania tu lakini ilisikika, leo tuna social media kibao, Elimu ya Watu Wazima wajipange wafanye kazi yao tuwasikie. Ahsante sana. (Makofi)