Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Tunza Issa Malapo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama kuchangia jioni hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi Serikali kama kweli imedhamiria kukuza michezo nchini, ni lazima iwekeze kwenye michezo bila kuleta masihara. Yaani hatuna namna nyingine ya kuongea. Serikali itoe fedha, ipeleke kwenye Wizara yetu ya Michezo ili kusudi waweze kutekeleza majukumu ambayo wamejipangia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Wajumbe wa Kamati ambao tunaisimamia Wizara hii tunajua ni kwa namna gani Wizara ina-struggle kuhakikisha michezo inaimarika nchini. Kama alivyotoka kuongea mwenzangu, sasa hivi michezo hatuchukulii mazoea, watu wanatakiwa wacheze michezo kitaalamu. Ili ucheze michezo kitaalamu ni lazima kama nchi iwekeze. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi tumeenda kuangalia ukarabati wa uwanja wa Benjamin Mkapa, bado mambo hayafurahishi. Kuna uwanja ujenzi wa uwanja wa michezo Dodoma, Arusha na maeneo mengine lakini upelekaji wa feda katika wizara hii bado hauridhishi. Kwa hiyo, hatuna namna nyingine ya kuongea Serikali ichukulie kwa nama ya pekee kwa sababu pamoja na mambo mengine huko inawasaidia vijna wetu wengi ambao wana interest hizo kuweza konesha vipaji vyao na kusonga mbele katika michezo mbalimbali walio wengi wanafikia hapo walipofika kwa jitihada zao binafsi. Sasa tunataka tuone Serikali ina jitihada gani za makusudi za kuwezesha michezo katika nchi yetu inaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tulitembelea Chuo Kikuu cha Dodoma, nimwambie Waziri anayehusika na mambo ya maji, watu wa Chuo Kikuu cha Dodoma hawana maji. Hapo UDOM karibu tu na hapa, wafanye jitihada ya kuhakikisha maji yanapatikanawafanye jitihada ya kuhakikisha maji yanapatikana. Tumeenda siku zile ripoti yao inasema wanapata maji 30% tu. Sasa chuo kikubwa kina wanafunzi wengi tunategemea kitoe wataalam wa mambo mbalimbali maji nayo yanakosekana, kweli? Kwa hiyo, wale ambao wanahusika na mabo ya maji wakiangalie kwa jicho la tatu Chuo Kikuu cha Ddoma wahakikishe wanapata maji ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ya watu wazima, wenzangu wameizungumza kwa kasi kikubwa na pia nizungumzie kidogo kwenye eimu ya watu wazima. Hapa tunategemea wale watu ambao walikosa fursa kwa namna moja ama nyingine ya kusoma kwenye hizi shule katika mifumo hii ya kawaida waende wakasome kule lakini hali ya vile vituo vyetu vya elimu ya watu wazima ni dhoofu kweli kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wana malengo mazuri na mipango mizuri lakini wanaitekelezaje katika hali ambayo wako nayo. Nikupe mfano, katika Mkoa wa Mtwara mwaka jana 2023 kuanzia mwezi Januari mapaka mwezi Oktoba wanafunzi wa kike 6,906 walipata mimba, kwa miezi 10 wanafunzi 6,906 katika Mkoa mmoja wa Mtwara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hao ndiyo tunawatarajia waende huko na kwenye sehemu nyingine hizi zinazotoa elimu nje ya mfumo rasmi lakini wakifika kule wanaambiwa walipie ada. Ada wanaitoa wapi? Huyu mtu ambae kakatisha masomo kwa sababu mbalimbali kwa kukosa ada na huduma nyingine leo unamwambia akiingia kule alipe anatoa wapi hiyo fedha? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taarifa zilizopo sisi Wabunge wawakilishi wa wananchi tujue sasa hivi dropout ziko kwa kiasi kikubwa kwa watoto wa kiume kuliko wakike. Kwa hiyo, wakati tunawapambania watoto wa kike tukumbuke pia kuwapambania watoto wa kiume. Huo ndiyo wito wangu. Nao wanakumbwa na madhila mengi makubwa lakini kila tukisimama tukiongea nikiwepo na mimi mwenyewe tunana kama watoto wa kike wanachangamoto nyingi, sikatai wanazo lakini tusiwaache nyuma Watoto wa kiume nao wanachangamoto nyingi na Mheshimiwa Waziri wa Eimu ametuambia atatuletea takwimu anafanyia utafiti waone ni kwa kiasi gani watoto wa kiume wanaacha shule na sababu ambazo zinazosababisha kuacha shule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda naomba nimalizie jambo moja. Kila siku tumekuwa tukiongea upungufu wa walimu tunaongea general. Sasa tumeletewa takwimu naomba niwape taarifa kidogo kwa takwimu tulizoletewa yaani hapa nchini kwetu walimu wa Civics wanaotakiwa ni 16,695 lakini tunao walimu wa Civics 68. Walimu wa English wanaotakiwa 23,663 tunao 12,000 na walimu wa Physics tunatakiwa 13,000, tunao 6,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeyasema haya muone huku tunahamasisha uzalendo na utamaduni sijui vitu gani wakuwafundisha darasani watoto wetu wako 68. Huku tunazungumza ujasiramai na vitu gani walimu wa Bookkeeping wa commerce hawapo. Huku tunazungumza viwanda kuwekeza kufanyaje walimu wa physics, wa hesabu hawapo, tunaendaje namna hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri kama nchi tunatakiwa tujitafakari na tujue hasa lengo letu ni nini. Tunaenda kwenye Mfumo wa Amali kwangu nasema kila siku naunga mkono hoja hiyo ya Mfumo wa Amali lakini ni lazima Serikali iwekeze vya kutosha ili kusudi tuwapate walimu wenye ujuzi wa kuweza kufikia malengo ambayo nchi itakuwa imejipangia. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)