Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Fatma Hassan Toufiq

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. FATMA H. TOUFIQ – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA USTAWI NA MAENDELEO YA JAMII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuhitimisha hoja ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii. Hoja hii imepata jumla ya wachangiaji tisa wa kuzungumza lakini pia ninaamini kutakuwa na wachangiaji walioleta kwa njia ya maandishi ambayo bado sijaipata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya maeneo ambayo wachangiaji wamegusia ni pamoja na kuwepo na ubunifu wa usimamizi wa fedha za wamachinga, lakini pia sambamba na hilo kwenye suala zima la kuwa na data za uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine lililozungumziwa ni upatikanaji wa vitambulisho vya wajasiriamali ufanyike haraka ili kusudi wajasiriamali hawa waweze kupata fursa ambazo zipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kwamba, wachangiaji wengi wamempongeza sana Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi yake nzuri sana ya kuhakikisha kwamba makundi mbalimbali yanafikiwa na yanapata maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa lingine ambalo limesisitizwa ni kuhusiana na elimu kwa hii mifuko mbalimbali ya Serikali ili kusudi waajiri mbalimbali waweze kuijua na wafanyakazi waweze kufaidika na mifuko hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kwamba, Bajeti ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii inabidi iongezwe kwa sababu ina kazi nyingi sana. Pia, kwenye suala zima la Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, imebainika kwamba uhitaji ni mkubwa, kwa hiyo kunahitajika kuongezwe bajeti ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa dhati ya moyo wangu, ninawashukuru wachangiaji wote waliojitokeza kwani wamesaidia kufafanua na kuifanya hoja ya Kamati ieleweke vizuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nahitimisha hoja hii kwa kuweka msisitizo kwenye mapendekezo ambayo Kamati imeyatoa ili Bunge lako Tukufu liweze kuyaazimia na Serikali iyatekeleze kwa manufaa ya Taifa letu na ustawi wa wananchi kwa ujumla kama ifuatavyo:-

Kwa kuwa, Bajeti inayotengwa na Serikali kwenye Mifuko ya Maendeleo ya Vijana kila mwaka ni ndogo na vilevile bajeti hiyo haijatolewa kwa takribani miaka mitano na kupelekea kushindwa kukidhi haja ya mikopo kwa vijana;

Na kwa kuwa, uwepo wa Mifuko mingi ya uwezeshaji wananchi unasababisha ufanisi wa Mifuko hiyo kukosa tija iliyokusudiwa;

Hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba: -

(a) Serikali iongeze bajeti na kutoa fedha iliyoidhinishwa na Bunge kila mwaka kwa wakati ili kukidhi mahitaji ya mkopo;

(b) Pia Serikali ifanye tathmini itakayosaidia kuona umuhimu wa kuunganisha mifuko yote ya uwezeshaji wananchi ili kusudi kuweza kuwa na mifuko michache ambayo itaweza kufikisha lengo.

Kwa kuwa, mwenendo wa mgao wa fedha za utekelezaji wa programu hii umekuwa ukishuka kila mwaka kwa kipindi cha miaka mitano;

Na kwa kuwa, kushuka kwa mgao wa fedha hizi kumesababisha kushuka kwa idadi ya vijana wanaonufaika na programu hii;

Hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba:-

(a) Serikali itenge na kutoa fedha za programu hii kwa kufuata makubaliano ya kutoa 1/3 ya michango ya SDL.

(b) Pia Serikali itoe mafunzo ya urasimishaji ujuzi kwa wanafunzi ili kukabiliana na changamoto ya uhaba wa wakufunzi.

Kwa kuwa, ipo changamoto ya baadhi ya wastaafu kutopata stahiki zao kwa ukamilifu na kwa wakati, jambo linalosababisha usumbufu kwa wastaafu;

Na kwa kuwa, changamoto hii imesababishwa na madeni ya malimbikizo ya michango ya wanachama ambayo hawalipwi kwa wakati na baadhi ya waajiri na uwepo wa madeni ya muda mrefu hivyo kusababisha kushindwa kutelekeza majukumu kwa ufanisi;

Hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba: -

(a) Serikali iandae mpango unaotekelezeka kwa kulipa madeni ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ambayo ni mikopo ya miradi ya Serikali;

(b) Pia NSSF ichukue hatua kali za kisheria kwa waajiri wadanganyifu wanaowasilisha michango iliyo chini ya mishahara halisi ya watumishi;

(c) Pia NSSF iongeze kasi ya kuandikisha wanachama wapya ikiwa ni pamoja na kurudisha Fao la Matibabu; na

(d) Pia mifuko itoe elimu ya mara kwa mara juu ya mambo muhimu yanayohusu mifuko hiyo kwa lengo la kuongeza ufanisi.

Kwa kuwa, uhaba wa watumishi na vitendea kazi hususani maeneno ya vijijini, imeonyesha ni changamoto muda mrefu sana kwa OSHA na kushindwa kutekeleza majukumu yake, Bunge linaazimia kwamba: -

(a) Serikali itenge bajeti itakayokidhi mahitaji ya OSHA ili kuweka vitendea kazi vya kuwawezesha kufika hadi vijijini;

(b) Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora waweke mkakati wa kuajiri watumishi wa OSHA kulingana na Ikama;

(c) Hali kadhalika Serikali ikamilishe mchakato wa kuridhia mikataba ya Kimataifa ambayo ni Mkataba Na.155 wa mwaka 1981 kuhusu Usalama na Afya Mahali pa Kazi na Mkataba Na. 187 wa mwaka 2006 wa Mfumo wa Kuhamasisha Masuala ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi; na

(d) Wakala pia iongeze kazi ya usajili wa maeneo ya kazi nchini na kutoa miongozo ya namna ya kuwalida wafanyakazi wote ili kusudi wafanyakazi waweze kuwa salama.

Kwa kuwa, hadi kufikia Disemba 2023 Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) ilikuwa imekamilisha mfumo wa kieletroniki katika Ofisi nne nchini. Kukosekana kwa mfumo wa kieletroniki kunaathiri ufanisi wa utekelezaji wa majukumu ya Tume katika uendeshaji wa mashauri na utunzaji kumbukumbu.

Hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba: -

(a) Serikali iongeze Bajeti ya Tume ya Usuluhishi na Uamuzi sambamba na kutoa fedha kwa wakati ili Tume iweze kusimika mfumo wa kielektroniki katika ofisi zake zote 32.

(b) Kuongeza kasi ya usimikaji wa Mfumo wa Kielektroniki ili kuongeza ufanisi wa utatuzi wa migogoro kuendane na mfumo wa kieletroniki wa Mahakama.

Kwa kuwa, ipo changamoto ya uelewa kuhusiana na masuala mbalimbali yanayohusiana na fidia kwa wafanyakazi;

Hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba: -

(a) Mfuko uandae mkakati endelevu unaotekelezeka wa kutoa elimu kwa waajiri na waajiriwa juu ya masuala mahususi kuhusiana na fidia za wafanyakazi.

(b) Sambamba na hilo, mfuko uwachukulie hatua kwa mujibu wa sheria waajiri wasiowasilisha michango ili mfuko uweze kukusanya kwa ufanisi.

(c) Mfuko uweke mkakati utakaosaidia kusajili waajiri wapya ikiwa ni pamoja na kufungua ofisi za mikoa yote nchini kusogeza huduma kwa wanachama.

Kwa kuwa, utekelezaji wa sheria hii unakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo sheria kutoweka masharti kwa waajiri wa kigeni ya kuwasilisha mpango wa kurithisha ujuzi kwa wazawa, kutoweka adhabu kwa mwajiri anayechelewa kuwasilisha maombi ya kuhuisha kibali cha kazi.

Na kwa kuwa, changamoto hizo zinapekelea kushindwa kuratibu kwa ufanisi ajira za wageni na hivyo baadhi ya wageni kufanya kazi bila kuwa na vibali vya kazi au kuhuisha vibali na kupelekea kuikosesha mapato Serikali.

Hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba: -

(a) Serikali ifanye marekebisho ya sheria hii ili kuimarisha utekelezaji wake sambamba na kuongeza mapato ya Serikali.

(b) Serikali iongeze bajeti na vitendea kazi kwa watumishi wa Idara ya Kazi ili kuwawezesha kufanya kaguzi mara kwa mara katika maeneo ya kazi.

(c) Pia Serikali iwachukulie hatua za kisheria waajiri wa kigeni watakaobanika kufanya vitendo vya unyanyasaji wazawa.

Kwa kuwa, upungufu wa rasilimali fedha na watu unaathiri kwa kiasi kikubwa ufanisi katika utekelezaji wa shughuliza uratibu wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali;

Na kwa kuwa, kukosekana kwa rasilimali fedha watu kumepelekea kushindwa kufuatilia mashirika takribani 9887 yaliyoenea maeneo mbalimbali Tanzania, basi tunaishauri Serikali ifanyie kazi jambo hili.

Hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba: -

(i) Serikali iongeze bajeti ya Wizara kwa kushirikiana na taasisi nyingine ziweze kufuatilia na kuhakikisha kuwa mashirika yanafanya kazi kwa manufaa ya jamii na maslahi ya Taifa kwa ujumla.

(ii) Serikali ichukue hatua za haraka na madhubuti kuhakikisha pamoja na kuyafutia Mashirika yeyote ambayo yanajihusisha na masuala ya mmomonyoko wa maadili.

Kwa kuwa, katika kipindi cha miaka miwili mfululizo hakuna fedha iliyotolewa kwa ajili ya mikopo yenye masharti nafuu kwa wafanyabiashara ndogondogo jambo linalokwamisha juhudi ya kuwawezesha wafanyabiashara hao kujinasua kiuchumi; basi kiasi cha riba ya asilimia saba ya mikopo kinachopendekezwa na Wizara ni kubwa inabidi iangaliwe upya.

Hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba: -

(a) Serikali itoe fedha zilizoidhinishwa na Bunge kwa ajili ya mikopo nafuu kwa wafanyabiashara ndogondogo kwa wakati ili kuwawezesha kukuza mitaji.

(b) Serikali iandae mwongozo wa uratibu na usimamizi wa fedha zilizotengwa kwa ajili ya mikopo ya Wafanyabiashara ndogondogo.

(c) Hali kadhalika Serikali iongeze kasi ya utoaji wa vitambulisho kidijitali kama alivyoelezea Mheshimiwa Waziri kwamba wameshaanza kuifanyia kazi.

Kwa kuwa, Taasisi za Vyuo vilivyopo chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii zinakabiliwa na changamoto ya ufinyu wa bajeti, basi, tunaishauri Serikali ione umuhimu wa kuiongezea Wizara hii bajeti.

Na kwa kuwa, bajeti hii, ufinyu wa bajeti unaathiri ufanisi.

Hivyo Basi, Bunge linaazimia kwamba Serikali iongeze bajeti, itoe vibali vya kuajiri watumishi na kununua vifaa pamoja na vitendea kazi. Suala zima la kulipwa mikopo limezungumziwa na lipo kwenye taarifa hii, ukurasa wa 28.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako sasa lipokee Taarifa ya Kamati na likubali Maoni na Mapendekezo yote ya Kamati kama ilivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja. (Makofi)

(Hoja ilitolewa Iaumuliwe)

MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki. (Makofi)