Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote wa Mwaka 2022

Hon. Bernadeta Kasabago Mushashu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote wa Mwaka 2022

MHE. BENARDETA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia huu Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote. Kwanza kabisa nampongeza Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara kwa kazi kubwa waliyoifanya. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Afya na Masuala ya UKIMWI, vilevile nilikuwa Mjumbe wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ambao tulianza kuuchambua Muswada huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli kazi kubwa imefanyika, naipongeza Wizara, wameweza kuyachukua maoni mengi yaliyotolewa na wadau na yaliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge mbalimbali. Kwa sasa hivi Muswada ulivyo ni Muswada mzuri na sheria itakayotokana na Muswada huu inaweza kutekelezeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, maisha bora yanategemea na afya bora. Huu Muswada Watanzania wengi wameusubiri kwa muda mrefu. Walikuwa wanauleta mbele ya Kamati tunaurudisha kwa sababu tulitaka tuone kwamba kila Mtanzania sasa anaenda kushughulikiwa, anaweza akahudumiwa, ndiyo maana kila ulipokuwa unaletwa tunaleta maoni, sasa hivi tumefikia mahali tunaona maoni yamezingatiwa na huu Muswada sasa unaenda kuwajali Watanzania wote kwa hiyo naomba muupitishe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wote tunajua kwamba gharama za matibabu ni kubwa, vipimo, madawa, ukihitaji upasuaji, kwa bahati mbaya ukiugua haya magonjwa yasiyoambukiza au ya muda mrefu kama presha au kisukari, wewe unakua ni mgonjwa wa kudumu, ni mtu ambae unahitaji matibabu kila siku ni gharama kubwa ambayo Watanzania wengi hawawezi kuimudu, inabidi wafe kwa sababu wanakosa matibabu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bahati mbaya ukiugua figo ndugu zangu, unatakiwa kusafisha figo mara mbili mara tatu kwa wiki moja ambapo gharama zake ni shilingi laki mbili na nusu hadi laki tatu. Ni Watanzania wangapi wanaweza kumudu kulipa shilingi laki saba na nusu hadi laki tisa kwa wiki moja ili waweze kusafishwa figo? Utakuta ni wale wenye fedha tu wanaendelea kutibiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kupitia sheria hii ikishatungwa, ina maana kwamba hata hawa watu wanaenda kutibiwa. Kwa namna ya pekee napenda kumshukuru na kumpongeza sana Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kwamba huu mchakato wa kuleta Bima ya Afya kwa wote uanze ili kusudi hata wale Watanzania ambao walikuwa wanakufa kwa sababu ya kukosa fedha za matibabu waweze kutibiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Muswada huu nimeupenda sana kwa sababu unajali na umezingatia hali ya Mtanzania wa kawaida. Unaangalia kwamba kama kuna mwanachama wamemruhusu aweze kuwa na wategemezi wengine wanne pamoja na mwenza kwa hiyo, ni wewe na mwenzi wako ambaye anaweza akawa ni mke au mume, akapata huduma lakini unaruhusiwa vilevile na wategemezi ambao wanaweza kuwa wazazi wako wewe mwenyewe lakini kwa mara ya kwanza hata wazazi wa mke wako au wazazi wa mume wako na wenyewe watahudumiwa na huu Mfuko wa Afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile unaruhusiwa kupata huduma kwa ajili ya mtoto uliyemzaa, mtoto uliyemuasili na mtoto hata wa kambo na yenyewe inaruhusiwa ilimradi awe na chini ya umri wa mika 21. Vilevile ndugu zako wa damu ambao bima nyingi zilikuwa hazizingatii hiki kitu, anaruhisiwa sasa, ataruhusiwa kwa sheria hii ikishapita. Unaweza ukamuhudumia hata ndugu yako wa damu ilimradi awe na umri wa chini ya miaka 21.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kifungu cha 17 kinatoa wigo mpana kwamba sasa ukikatia hata Bima ya Afya Dar es Salaam, ukaikatia hata Tanga, ukaikatia hata Bukoba unaruhusiwa kwenda kuhudumiwa kwenye kituo chochote kinachotoa huduma ya afya katika Mkoa wowote ule ilimradi unazingatia yale masuala ya rufaa na masharti mengine yatakayokuwa yamewekwa na Wizara.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kifungu cha 32 cha Muswada ule uliowasilishwa kilikuwa kinaleta vikwazo kwa huduma nyingi za kijamii. Kilikuwa kinasema kwamba huwezi kupata leseni ya biashara mpaka uwe na Bima ya Afya, huwezi kupata tin au namba ya mlipa kodi mpaka uwe na Bima ya Afya. Huwezi kupata hata passport ya kusafiria, uwe na Bima ya Afya, huwezi kumuandikisha mwanafunzi wa Kidato cha Tano na cha Sita hadi awe na Bima ya Afya, kwa hiyo, ilikuwa inaleta vikwazo kwa watu kupata huduma mbalimbali za kiafya lakini sasa hivi naipongeza Serikali kwa kuwa wasikivu, hiki kipengele kimefutwa na kimeondolewa kabisa kwenye Muswada. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Ibara ya 6 inawatambua watu wasiokuwa na uwezo ili mtanzania yeyote yule aweze kupata matibabu bila kikwazo cha kutokuwa na fedha. Sensa imeshabainisha kwamba kuna watanzania wangapi au asilimia ngapi ni watu ambao ni maskini. Naomba kuweka hapa angalizo. Hapa ukishasema watu ambao hawana uwezo wanaenda kupata matibabu bure, kila mtu atajitokeza kwamba ni maskini, lazima Serikali hapa tuwe waangalifu, tuweke vigezo mahsusi vya kumtambua mtu ambaye hana uwezo ni nani ndani ya Tanzania, la sivyo kila mtu atasema hana uwezo, huu mfuko utaelemewa na Bima ya Afya ita-collapse.

Mheshimiwa Naibu Spika, napendekeza vilevile wakati wanatambuliwa watu ambao hawana uwezo, hata watu wenye ulemavu ule ulemavu mkubwa, watambuliwe kama watu ambao hawana uwezo. Nampongeza tena kwa mara nyingine Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali watu wote, hataki mtu yeyote, mtanzania yeyote afe kwa sababu ya kukosa pesa za matibabu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa kukubali kuanzisha Mfuko wa Matibabu, Mfuko wa Bima ya Afya. Mojawapo ya kitu kilichokuwa kinakwamisha Muswada usisonge mbele, tulikuwa tunajiuliza hawa watu ambao hawana uwezo wanaenda kutibiwaje? Serikali imekubali kwamba itaanzisha huo Mfuko. Vilevile wameianisha vyanzo mahsusi vya kuweza kuingiza hela kwenye huu Mfuko.

Mheshimiwa Naibu Spika, pendekezo langu ni kwamba tunaomba huu Mfuko sasa ukatungiwe sheria ili uwepo kisheria, mtu yeyote asije akaamka akaamua kuufuta. Nakuomba Mheshimiwa Mwigulu huu mfuko ukatungiwe sheria tuhakikishe kwamba hivi vyanzo viwe sustainable, tuhakikishe kwamba hizi hela zinazoingia kwenye huu Mfuko zinakuwa ring fenced kusudi ziweze kufanya kazi moja ya kutoa huduma ya Bima ya Afya kwa wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu, baada ya Muswada huu kupita, ninaomba sasa elimu itolewe kwa ukubwa, uhamasishaji ufanywe mkubwa kama tulivyofanya kwenye Sensa kusudi Watanzania waweze kuelewa maana na umuhimu wa Bima ya Afya na wakubali kuingia. Serikali iendelee kuboresha mazingira, ninajua mmejenga zahanati nyingi, vituo vya afya vimejengwa, namshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, hospitali zimejengwa, tunaomba sasa muhakikishe kwamba kwenye hizo hospitali kuna vifaatiba, vitendanishi, kuna dawa, kuna watumishi ili kusudi hata watakaoanza kuingia kwenye huo Mfuko waende kuwaambia wenzao kwamba tukienda kwenye hivyo vituo tunatibiwa, tukienda kwenye hivyo vituo tunawakuta Madaktari, tunawakuta Manesi, kwa hiyo, tuendelee kuboresha mazingira na kwa kufanya hivyo tutawahamasisha watu wengi watashawishika kuingia kwenye huo Mfuko wa Afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuwa sasa uhamasishaji umetosha ninaomba tuanze na wale ambao wana mishahara kama kawaida, wale ambao wapo kwenye private sector lakini wana vipato, kwa sababu sasa Sensa imeshatusaidia kutambua asilimia ngapi ya watu ambao hawana uwezo, tuanze kuchukua wachache wachache, tuanze kuwaingiza kwenye Bima. Kamati yetu ilienda Rwanda, Kamati yetu ilienda mpaka Ghana na wao hawajafikia 100 percent. Wameanza polepole, wanaendelea kuboresha kadri uchumi unavyokuwa na vile vyanzo vinavyozidi kuongezeka watu wanaendelea kuongezeka. Msiogope nenda muanze, ni kitu kizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, namalizia kwa kuwashawishi Waheshimiwa Wabunge wenzangu, hapa Muswada huu ulipofikia ukiulinganisha na Muswada ulioletwa hapa mwanzo, huu ni Muswada mzuri sana, wamezingatia mawazo ya Waheshimiwa Wabunge yaliyotolewa humu ndani na yaliyotolewa ndani ya Kamati kwa hiyo tukubali tuupitishe kusudi uweze kutunga sheria ya kwenda kumsaidia kila Mtanzania. Nawaomba Watanzania, sheria ikishatoka basi tuingie kwenye hii Bima ya Afya kwa sababu ndiyo mkombozi wa kutuwezesha kupata huduma bora za kiafya.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)