Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudia Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Mussa Ramadhani Sima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudia Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pia nichukue fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu. Vilevile nampongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa ambayo ameendelea kuifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa namshukuru Mheshimiwa Rais kwa ziara yake ya Mkoa wa Singida hususan Singida Mjini, tulimpa heshima ya kuwa Mama wa Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza kaka zangu; Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba na Mheshimiwa Prof. Kitila Mkumbo kwa kazi ambayo wanaifanya, ni kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nitajikita sana kwenye sekta ya kilimo, lakini niruhusu nifanye rejea ndogo ya nchi ya Korea ya Kusini. Korea Kusini Mwaka 1960 tulikuwa wote sawa kwenye suala la maendeleo, lakini kupitia Rais wao Park Geun Hye aliamua kwa dhati kuweka mpango wa kuwekeza kwenye utafiti na maendeleo (research and development). Utafiti na maendeleo ndiyo uliomwezesha kuwa na sera ya importation.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kawa kifupi sana, kwa sababu nimeamua eneo hili la kilimo wenzetu wa Korea Kusini walikuwa na uhaba wa natural resources.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kifupi sana kwa sababu nimeamua eneo hili la kilimo, wenzetu wa Korea Kusini, walikuwa na uhaba wa natural resources. Lakini nizungumzie eneo dogo tu la ardhi ambayo aliitumia kwenye kilimo, ni asilimia 30, asilimia 30 hii waliyoitumia kwenye kilimo ilikuwa ni substance ya agriculture kwa maana ya kilimo cha chakula. Kiliwawezesha wao kuchangia kwenye pato la Taifa (GDP) asilimia 12 lakini iliwasaidia kwenda kwenye agrarian economy. Kwa maana ya kilimo biashara na kiliweza kuchangia asilimia 30 mpaka 40 kwenye pato la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nafanya rejea hii? Nafanya rejea hii kwenye maeneo mawili. La kwanza, mpango wetu unatakiwa kujikita kwenye utafiti na maendeleo. Hili ndiyo eneo ambalo nilitarajia tujikite zaidi, tuwekeze zaidi hapa ili tuweze kukamilisha malengo mengine yanayoendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili hapa, wenzetu wakati kasi ya uchumi wao inakua na kasi ya umasikini inapungua. Sasa nirejee kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Mipango, kaka yangu Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo, alisema kasi ya uchumi inakua lakini kasi ya umasikini inaendelea kubaki palepale. Maana yake haviendani, uchumi unakua lakini umasikini ume-stack. Sasa wenzetu uchumi ulikuwa unakua lakini na umasikini pia unaondoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili limefanya niende mbali kidogo, kwa nini, sisi tunabaki kwenye umasikini wakati uchumi unakua. Inawezekana kabisa, mimi nitajielekeza sana kwenye mazao, kwenye mazao huku, watu wanauza mazao ghafi. Kwa sababu hatujawekeza, hatujajielekeza kwenye processing industry ili kuwafanya hawa watu mazao yao yawe na thamani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa kilimo, hasa kwenye zao la alizeti. Kwa mara ya kwanza Tanzania tumeweza kuzalisha alizeti tani 1,140,000 haijawahi kutokea, naipongeza sana Wizara ya Kilimo. Kutoka tani 400,000 hadi 1,140,000, hili ni jambo kubwa sana ambalo Serikali sasa ina kila sababu ya kuwekeza hapo, lakini kuna changamoto mbili zinazojitokeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ya kwanza, sasa hivi soko la alizeti limeshuka. Gunia sasa hivi ni 65,000 na kadri siku zinavyokwenda soko linashuka. Wananchi hawa ambao walihamasishwa, wakapewa mbegu bure na wakapewa ruzuku. Hawawezi kuwa na hamasa hiyo hiyo mwaka huu, wakaweza kuzalisha tena alizeti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuiomba Serikali, naiomba Wizara ya Kilimo sasa waamue kwa dhati kwenda kununua mbegu hii kwa wakulima ili kuwapa unafuu waweze kuzalisha zaidi. Kwa sababu nchi yetu leo inahitaji mafuta kama tani 600,000. Tumeweza kuzalisha tani 1,140,000, inaweza kwenda kwenye mafuta tani 400,000. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuiomba Serikali kwenye hiyo, lakini pia iwekeze kwenye viwanda vidogo vidogo kwa wakulima, ama kwa makundi ama kwa mtu mmoja mmoja. Waziri ameeleza vizuri hapa, kwamba sasa wanajielekeza kwenye rural social economic development. Kama tunaenda kwenye suala la maendeleo vijijini, kwenye uchumi wa maendeleo vijijini, hapa tunayo changamoto kubwa. Pamoja na sekta zingine alizozitaja, moja wapo ni sekta ya kilimo. Kwamba, wataendelea kutoa mbegu bora, wataendelea kutoa ruzuku, lakini miradi ya umwagiliaji itaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimwongezee tu kwamba, tunahitaji pia ambapo tayari Wizara ya Kilimo wamefanya vipimo vya afya ya udongo. Ongeza pale vipimo vya afya ya udongo, wenzetu wameshafanya hii kazi, sasa tuwape hiyo support.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ambayo ninaiona, tunatekelezaje haya wakati msimamizi mkuu ambaye ndiyo mtaalam kwenye hii Local Government, kwenye rural area ni Afisa Ugani. Afisa Ugani bosi wake ni Mkurugenzi. Mkurugenzi akiamka, jukumu lake la kwanza ni kukusanya mapato. Tumewapa maafisa ugani kuweza kuwa na pikipiki kila mmoja. Pikipiki sasa zinatumika katika kukusanya mapato. Maana yake huu mpango tunaouweka, huyu afisa ugani yuko huku TAMISEMI anafuata malengo mengine, mpango ambao umewekwa na Local Government lakini sisi huku mipango yetu tunasema itatekelezeka. Haitawezekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kushauri hapa, Mheshimiwa Waziri kaka yangu Profesa Mkumbo alikuwa Katibu Mkuu hapa wakati pia na sisi tunachangia tulishauri kwamba, Idara ya Maji kutoka Halmashauri iende kwenye mamlaka ya maji na jambo hili likafanyika. Tukashauri suala la TARURA na leo inajitegemea. Inashindikanaje maafisa ugani kuwatoa huku waliko kwa Mkurugenzi ama kwenye Local Government, tukawapeleka kwenye Tume ya Umwagiliaji. Hili linaweza kusaidia mpango ambao mmeuweka na kuboresha kilimo vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niende kwenye Tanzania Development Vision ya 2050. Hapa mwelekeo wa Tanzania 2050, nataka kujikita kwa watu waliowengi wanapojishughulisha. Asilimia 80 ya Watanzania wapo kwenye kilimo, uvuvi na ufugaji. Natamani dira hii ijikite hapo. Nataka nitoe mfano mdogo wa wenzetu wa kilimo, wanaandaa leo Tanzania Agricultural Transformation Master Plan. Kama unaandaa mpango kabambe wa mageuzi kwenye kilimo nchini, tunatarajia kuona ule mwelekeo wa Tanzania ya 2050. Kuna kuwa na chapter ambayo inaelezea mpango huu kabambe ili kuwasaidia wenzetu na kuwasaidia Watanzania kwa sababu sehemu kubwa ndiyo wamejiajiri hapo… (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana…

MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Ahsante sana.