Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudia Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Godwin Emmanuel Kunambi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlimba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudia Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais, kwa kuona umuhimu wa kuanzisha Wizara ya Mipango na Uwekezaji. Jambo hili limekuwa likisumbua Taifa letu kwa muda mrefu sana, kama tunakumbuka huko nyuma Wizara za Kisekta zilikuwa zinapanga mipango yao yenyewe bila kuratibu, lakini leo hii Mheshimiwa Rais, ametuletea Wizara hii ya Mipango na Uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, imani yangu kwamba Wizara zote za Kisekta sasa zinakwenda kuratibiwa na mipango itakoyoanzishwa na Wizara ya Mipango na Uwekezaji, nimpongeze Mheshimiwa Waziri, kwa kupata uteuzi huo. Niombe sasa kama kuna mipango ambayo tayari hapo nyuma ilikuwa imejikita kwenye sekta na haipo kwenye mipango kwa maana ya Wizara ya Mpango na Uwekezaji. Nimshauri Mheshimiwa Waziri wa Mipango, ashirikiane na Wizara hizo za Kisekta, mathalani Wizara ya Madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Madini leo hii wamekuja na mpango wanaita vision 2030. Sasa ukijiuliza vision tuliyonayo leo hii ni 2025 - 2030 imetoka wapi? Sasa wanahitaji kusaidiwa kwa sababu wanakimbia sana, wao wanakimbia sana. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Madini, all starts well ends well my brother, umeanza vizuri. Sasa naona kasi yako ni kubwa, nikuombe ushirikiane na Mheshimiwa Waziri wa Mipango, hiyo vision 2030 uje uilete kwenye Wizara ya Mipango ili sasa muwe na common understanding katika safari yako hiyo unaweza kufanikiwa. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Wizara ya Mipango kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, naomba tufanye marejeo ya huu mradi wa BBT tufanye mapitio. Hofu yangu kwamba leo hii kijana aliyemaliza Chuo Kikuu, umempa shamba la hekari tano, ameshaomba ajira benki, akafanya interview, benki wamesema tunakuajiri akabaki na hizo heka tano, aache white collar job. Nani atakaa juani? Kwa hiyo, nadhani tutafute namna bora juu ya hili jambo. Mimi nilikuwa naona nia ni njema, lakini ni namna gani tutakwenda kutekeleza mkakati wetu ili vijana wape ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kwenye eneo hili la Kilimo. Ili kilimo kiwe kilimo biashara lazima tuwe na ardhi inayofaa kwa kilimo. Lazima tuwe na mitaji, umwagiliaji na pembejeo. Taarifa na maoni ya Kamati Ukurasa wa 25, narejea Maoni ya Kamati, wanasema; “kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali ilitenga bajeti kupitia taasisi za kifedha shilingi trilioni 2.6, lakini fedha hizi asilimia tatu tu ndiyo zilizotumika kwenye uzalishaji wa Sekta ya Kilimo. Asilimia 93 zote zilikwenda kwenye mauzo ya bidhaa za Kilimo.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lipo wapi? Naomba niseme tatizo, kwa nini kwenye uzalishaji zimekwenda asilimia saba na siyo asilimia nyingi? Kwa sababu wananchi wakitanzania, wakulima wakitanzania hawakopesheki. Leo hii ukiuliza wakulima wetu wengi wale wadogo, wakati na wakubwa; wengi wao hawana hati miliki. Miongoni mwa vitu ambavyo vinafanya mkulima akopesheke ni hati miliki, kama collateral.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ndiyo maana rate ndogo ya waliokopa benki na hiyo nadhani ni muhimu sasa Wizara ya Ardhi, unasikia sababu alizosema Mheshimwa Waziri wa Mipango; kuratibu Wizara ya Ardhi, Kilimo na Biashara. Biashara ishughulike na masoko, Ardhi ishughulike na masuala ya upatikanaji wa wa ardhi inayofaa kwa kilimo na kuwapatia wananchi hati miliki. Pia, Wizara ya Kilimo yenyewe ijikite kwenye umwagiliaji na masuala ya pembejeo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili likifanyika naamini tutakwenda kukifanya kilimo sasa kiende kuwa kilimo biashara. Nakumbuka hapa miaka 20 iliyopita, kilimo ilikuwa ndiyo sekta inayochangia asilimia 20 kwa maana ya mauzo ya nje, lakini leo hii tunaona madini ndiyo inakwenda zaidi. Kwa nini kilimo kimesimama. Kuna kazi ya kufanya kwenye Sekta ya Kilimo ili tuone sasa tunaweza kuuza mazao ya kilimo nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ninalilojielekeza ni eneo la halmashauri zetu nchini. Hivi kuna dhambi gani halmashauri zisi-graduate. Kwa nini halmashauri ziendelee kutegemea fedha kutoka Serikali Kuu? Nchi zote duniani, majiji na halmashauri zinajitegemea, kwanini Tanzania ni wapi tunakwama?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila halmashauri kuna fursa za uwekezaji, mathalani mimi nitoe mfano pale Mlimba. Sisi tuna shamba la miti hekari 1,500, tunaamini miaka 10 ijayo tutaanza kuvuna, tumeona fursa ni kupanda miti. Pia, tuna shamba la mikorosho hekari 150, baada ya miaka kadhaa tutaanza kuvuna korosho tutauza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nitoe rai kupitia Wizara ya Mipango, ni muhimu sasa tufikiri tofauti, halmashauri zote zianze kuwekeza. Zianze kufukiria kujitegemea, ku-graduate ili kupunguza mzigo kwa Serikali Kuu. Sisi Mlimba tunajenga vituo vya afya vitatu kwa mapato ya ndan, Ilala, Dar es Salaam na Arusha hawawezi, kuna shida gani? Sisi Mlimba tunajenga vituo vitatu vya afya kwa mapato ya ndani na viwili tumefungua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muhimu mifano hii ikasomwa hapa na ninasema kitu ambacho kinafanyika. Kwa hiyo, hakuna sababu za kufanya halmashauri isi-graduate na zijitegemee kupitia mapato ya ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)