Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudia Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

hon Hassan Seleman Mtenga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtwara Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudia Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuendelea kuchangia Wizara hii ya Mipango. Vilevile, namshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuandaa au kuunda Wizara hii ya Mipango na Uwekezaji. Nachukua fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Rais, katika manispaa yangu Januari mpaka Desemba nilikuwa siwezi kujenga hata kituo kimoja au kuchimba choo cha matundu manne kwa manispaa, tumeletewa Mkurugenzi, kwa kweli huyu kijana lazima nizungumze hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeletewa kijana huyu ndani ya wiki mbili amekusanya zaidi ya milioni 160, ndani ya wiki mbili. Kwa hiyo, nampa pongezi Mkurugenzi Nyange na aendelee sasa kututengenezea Jimbo letu la Mtwara na Manispaa yetu ya Mtwara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia mipango lazima tuzungumzie kilimo. Nataka nijikite kwenye eneo hili la kilimo hasa kwanza nimpongeze Waziri wetu Bashe, kwa kazi kubwa anayoifanya. Wenzetu China waliamua kufanya mageuzi ya makusudi hasa kwenye maeneo ya vijijini, Serikali iliamua kuandaa mpango wa kuwawezesha vijana ili kwenda kutengeneza mfumo wa kilimo na kujipatia chakula cha kutosha na chakula kingine cha kuuza nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishauri kwamba sisi kama watu wa Mtwara, tuna maeneo makubwa sana ambayo ni mapori na kwa kuwa Mheshimiwa Rais, amefika mahali akaamua kwenye Sekta hii ya Kilimo kutoa fedha nyingi sana. Niombe kwenye mipango hii tuelekeze sasa tuachane na vijana kwenda kucheza pool table, twende tuwapeleke sasa kwenye maeneo ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumza mipango, tunazungumza na Pato la Taifa. Nimekuwa mara nyingi nikiishauri Serikali, kutoka Mtwara kwenda Mji wa jirani wa Mozambique, tunachukua takribani kilometa kama 60 na hilo nalizungumza Waziri wa Mipango, alisikilize vizuri sana nadhani inawezekana lina tija kwake zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mikoa nane ya Mozambique wanatumia Bandari ya Beira. Kutoka kwenye mkoa wa mwisho kwenda Beira zaidi ya kilometa 2,000 au 1,800. Kutoka kwenye Mkoa wa mwisho kuja kwenye Bandari ya Mtwara wanatumia kilometa 770. Ninachotaka kukizungumza tufungue mpaka ule ili tufanye biashara sasa kati ya nchi na nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo wenzetu wa Mozambique wanashughulika na masuala ya gesi lakini wanashindwa gesi yao kwenda nayo kwa wakati, hawana njia ya kutumia kwa sababu wale wawekezaji Bandari ya Beira kuja mpaka Palma kuja mpaka Mchimbo Naplaya, kwenye maeneo ya gesi wanashindwa kutokana na mileage. Kwa hiyo, niombe Wizara hii iliangalie hili kwa mapana na marefu, tunakwenda kufungua nchi na biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko jambo ambalo linawezekana kama Tanzania tukaenda kuungana nalo la viwanda. Bila viwanda hatuwezi ku-move hata siku moja, lakini tukiangalia maeneo mengi tunazungumzia Mbeya, Pwani, Lindi na Mtwara, yako maeneo makubwa ambayo kuna rasilimali, materials na kila kitu. Tunashindwaje kuwaleta wawekezaji waje waweke viwanda na tunapozungumza viwanda ndani ya nchi tunazungumza ajira ya watu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kila kijana anaye-graduate kwenye Chuo chochote kile mawazo yake yote anakwenda kupata ajira. Katika mfumo wetu wa elimu hatuwafundishi na hatuwajengi hawa vijana watoke kwenye Vyuo waje wajitegemee, mawazo yao yote kwamba sasa wanakwenda kutafuta elimu ni vyema tukawatengenezea vijana hawa ambao wanakwenda kumaliza elimu yao waje wafanye kazi kwenye mazingira mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili nalo naliomba kwamba Sekta hii ya Uwekezaji twendeni tukawalete Wawekezaji wa kutujengea viwanda. Tunazungumza tuna madini, lakini leo ukienda maeneo ya Lindi na Mtwara utakuta toka miaka ya 80 yuko Mwekezaji amechukua leseni ya madini zaidi ya heka 600 au 700 na hawaonekani. Hiyo leseni kila ukigusa unaambiwa hapo kuna mwenyewe, lakini madini hayachimbwi zaidi ya miaka 30, tunazungumza mipango bila fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili nalo naomba liangaliwe kwa sababu nazungumza nikiwa na ushahidi wa jambo hili. Rasilimali ni ya kwetu, mtu amekuja amechukua leseni na kwenye leseni ile sasa hivi amefika zaidi ya miaka 30 hajawahi kuchimba hata siku moja. Kama hajachimba hata siku moja faida yake ni nini na mipango ipi ambayo tunaiweka kwa sababu tunazungumza mipango kwenda kutafuta fedha ndani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Wizara ya Mipango, hili nalo waliangalie kwa mapana na marefu kwamba wale wote waliopata leseni wana zaidi ya miaka 20 au 30 na hawajachimba, watumie sheria ambazo inawezekana wanaziweza wawaondoe hawa watu, wananchi wetu waende wakachukue hayo maeneo ili wachimbe madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, sasa nimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa kweli kwenye Jimbo langu natembea kifua mbele, Rais, amefanya raha kubwa sana kunisukumia fedha kwenye Jimbo langu. Mungu ambariki sana na aendelee sasa kusogeza miradi kwenye Jimbo la Mtwara Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)