Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudia Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Innocent Edward Kalogeris

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Morogoro Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudia Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili nichangie hoja ambayo ipo mbele yetu. Nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa maono yake na maelekezo yake kwa wasaidizi wake katika kutaka kulipeleka Taifa hili katika nchi ya asali na maziwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kumpongeza Ndugu yangu Mheshimiwa Lameck Mwigulu Nchemba na Mheshimiwa Profesa Kitila kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya katika kumsaidia Mheshimiwa Rais. Sisi ni mashuhuda, Mpango waliouleta ni mzuri lakini mwelekeo wa bajeti ni mzuri, tunaamini kabisa ukifuatiliwa tutaweza kufanya mambo makubwa katika Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii katika mchango wangu kuishauri Serikali, niende moja kwa moja kwenye suala la kilimo. Zanzibar au Tanzania kupitia Zanzibar ni nchi ya nne duniani katika zao la karafuu, lakini Mkoa wa Morogoro umebahatika nao kuwa Mkoa ambao tunaweza kuzalisha zao la karafuu na linaweza kutuletea pesa nyingi za kigeni huko tuendako. Zanzibar inazalisha wastani wa tani 500,000 za karafuu duniani, lakini Mkoa wa Morogoro katika kipindi kifupi tu tumeweza kuzalisha tani 2,200 ambazo zimeweza kuleta uchumi kwa Wanamorogoro karibu bilioni 39 kwa mwaka huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu mkoa kama mkoa umefanya jitihada za dhati, tumekwenda mpaka Zanzibar, tumeweza kujifunza kama Halmashauri ya Morogoro Vijijini tumepeleka Madiwani na Wakulima, wameweza kufanya mambo hayo tulipofikia.

Ombi langu kwa Serikali kupitia zao hili la karafuu, naamini tunaweza tukapata uchumi mkubwa Mkoa wa Morogoro ukazalisha hadi tani 10,000, kwa sababu Mkoa wa Morogoro kuna Halmashauri ya Morogoro Vijijini, Mvomero, Kata ya Kibati, Gairo na Nongwe, kuna uwezekano mkubwa sana wa kulima zao hili na kuleta mapato kwa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uongozi wa Mkoa chini ya Mkuu wa Mkoa wetu Mheshimiwa Adam Malima, umefanya kazi kubwa katika kuhamasisha zao hili. Sasa ombi langu ni kwamba, muda muafaka kwa Serikali Kuu kupitia Wizara ya Kilimo ichukue jambo hili ambalo linaenda kuleta uchumi mkubwa kwa Taifa hili katika kusaidia kupanga zao la karafuu, tunafikaje mbele ya hapa tulipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii katika kuzungumzia suala la utalii. Mheshimiwa Rais, amefanya kazi kubwa katika Royal Tour kutangaza utalii, lakini utalii lazima tutakubaliana wote hapo tulipo uko mkubwa sana katika Nyanda za Kaskazini. Kupitia Mradi wa REGROW, ambao upo katika Uboreshaji au Uimarishaji Utalii Nyanda za Kusini ambapo kuna Mkoa wa Katavi, Morogoro na Iringa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Morogoro kupitia Hifadhi ya Mwalimu Nyerere, niombe Serikali kupitia Mradi wa REGROW, ukaboreshe Kiwanja cha Ndege cha Matambwe, kwa sababu ndiyo lango kuu la kuingilia lakini ukaboreshe madaraja na barabara ndani ya hifadhi hiyo ili kuweza kupitika katika maeneo yote na kuweza kuongeza watalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe kupitia Wizara ya Ujenzi. Barabara ya Bigwa - Kisaki tayari imeshapata Mkandarasi, bado inasubiriwa kusainiwa. Twende tukasaini Barabara ya Bigwa - Kisaki twende tukasaini barabara ya Ubena - Zomozi – Ngerengere kujengwa kwa kiwango cha lami ili kurahisisha wataliii waweze kufika katika Hifadhi ya Mwalimu Nyerere na kuweza kuendelea kuleta pesa nyingi Kitaifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nataka nizungumzie suala la umeme. Ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere, umefikia asilimia 84.35 hadi kufikia sasa hivi. Ombi langu kwa Serikali sisi mashuhuda tumeendelea kuona kukatika kwa umeme. Serikali ikaweke jitihada za dhati kuhakikisha kwamba Mkataba wa Ujenzi unakamilika kwa wakati ili umeme uweze kurudi na kuweza kusaidia Taifa lisonge mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiweza kuwa na umeme wa uhakika, maana yake tutakuwa na uhakika wa uchumi wa viwanda. Tutakuwa na uhakika wa uchumi kwa watu wetu katika viwanda vidogo vidogo, lakini katika hilo suala la Bwawa la Mwalimu Nyerere, sisi wananchi wa Morogoro, wanachi wa Mkoa wa Pwani tuna sikitiko kwa Serikali yetu, hadi tunapozungumza sasa hivi CSR ambayo ni haki ya mikoa hiyo miwili haijapatikana hata kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaambiwa tumetengewa bilioni 10 Mkoa wa Pwani na Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya miradi ya maendeleo, lakini kuna wenzetu wengine ambao hawahusiki japokuwa kwamba mradi huu ni wa kimkakati, lakini wamepelekewa bilioni 80 ambazo naamini kabisa kwamba hatujatendewa haki. Mheshimiwa Mwigulu, lakini Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, Waziri wa Nishati, watupe Wanamorogoro na Wanapwani haki yetu ya kimsingi kama vile mkataba unavyosema, ili tuweze kufikia hapo tunapokwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru na naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)