Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudia Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudia Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi. Kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Rais, kwa kupeleka fedha nyingi sana kama tumetangaziwa hapa sasa hivi kupata magari ya elimu, lakini pia na afya na miradi mingine inaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo, na Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, wajukuu zangu Wanyiramba kwa kuaminiwa kupata nafasi muhimu sana. Mheshimiwa Profesa, wenzetu ni watafiti, nchi hii haina upungufu wa maandiko na makabrasha yapo mengi na Mheshimiwa Rais, sisi Wabunge na Watanzania tunataka matokeo ya Mipango ambayo inapendekezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Mpango umeletwa lakini pia kuna makisio ya fedha ambazo zitaenda kukusanywa katika vyanzo mbalimbali kuletea Watanzania maendeleo ili waendelee kukiamini Chama Cha Mapinduzi, kiendelee kushika dola katika nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitachangia kwenye eneo la software, wenzangu wamezungumza maeneo mengine. Unapozungumza utakusanya fedha ya shilingi trilioni 47.4, ni vizuri pia tukakumbushana kwamba Watumishi wa Umma wana malalamiko mengi sana kuhusu kikokotoo ambacho kinawekwa 1/540 kikaondolewa kikaja 1/580.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hili hizi fedha zote na mipango hii hawa watumishi wa umma ndiyo wataalam wetu wataenda kusimamia, lakini wana manunguniko na malalamiko. Katika Mipango ya Serikali, ni vizuri Serikali ikaonyesha matumaini kwamba maombi yao yanaendelea kufanyiwa kazi na walikutana Mheshimiwa Rais, nakumbuka Mapolisi, Walimu katika Kanda mbalimbali akawaahidi kwamba atalifanyia kazi. Jambo hili ni muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila tukifanya ziara maeneo mbalimbali wanaomba la kwanza warudishe formular ya moja chini ya 1/540 lakini umri huo wa kuishi urudishwe pale ulipokuwa 15.5 badala ya 12.5 lakini wapewe fedha zao kwa mkupuo asilimia 50 ili kupunguza mawazo, msongo wa mawazo na wengine wamepoteza maisha katika eneo hili. Hilo ni muhumu sana ili kuboresha utumishi wa umma, kusimamia miradi na ukusanyaji fedha ambazo zipo hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili tunao watumishi wa umma kwa maana ya Madiwani wetu katika Kata mbalimbali, Wenyeviti wa Vijiji pia Wenyekiti wa Serikali za Mitaa. Nimefuatilia wenzetu majirani wa Kenya hawa viongozi wanalalamika sana wamepewa posho ya shilingi 350,000 tangu mwaka 2012 mpaka leo, lakini nimeenda Kenya Machifu ambao ndiyo Wenyeviti wa Mitaa na Vijiji hapa kwetu wanajitolea, Kenya wale Manaibu Chifu wale wanalipwa 540,000, Machifu yaani Wenyeviti wenyewe wanalipwa 720,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Madiwani wa Tanzania posho ya mwezi wanalippwa 350,000, lakini Madiwani wa Kenya wanalipwa tena siyo posho ni mshahara 2,592,000. Hii maana yake ni nini? Miradi yote hii ya Mheshimiwa Mama Samia na bajeti ya makisio mnaleta hapa hawa viongozi kwenye mitaa, kwenye vijiji, Madiwani wataenda kusimamia na kusimamia vizuri ili kwenda kuangalia value for money.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa watu ambao wananung’unika, wanalalamika ni vizuri pia kupitia mpango wa Serikali na makisio 2024/2025 wakaona kwamba Serikali inaenda kuwakumbuka, kuboresha maslahi yao ili waweze kukidhi maisha katika maeneo hayo. Wanawatuma Wabunge wao hapa tuwasemee kwamba ni vizuri jambo hili likapokelewa, katika bajeti ijayo tuone projection na item ya kuonesha kwamba kuna angalau kuonesha uwezesho Wenyeviti wa Vijiji, Wenyeviti wa Vitongoji, Waheshimiwa Madiwani ili malalamiko haya yapungue au kuondoka kabisa ili wakasimamie miradi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu. Ukisoma Azimio la Arusha ukienda kitabu cha Mwl. Nyerere cha Uongozi wetu na Hatma ya Tanzania ukaenda Tujisahihishe, historia ya Mwalimu nenda kwenye ile tunaita MPH ambayo ilianzia China ikaenda mpaka Singapore, wenzangu wamezungumza habari ya Korea Kusini lakini Wachina hawa na Singapore ilikuwa ni Dunia ya Tatu katika uchumi leo ni Dunia ya Kwanza katika uchumi! Walifanya maamuzi magumu tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hapo Waheshimiwa Wabunge tukubaliane, tutapiga mark time sana kama hatuwezi kufanya maamuzi magumu. Kwanza tunapataje watu wetu sahihi katika nafasi? Profesa amem- quote huyu aliyekuwa Waziri Mkuu Singapore kupata watu sahihi wa Serikali katika maeneo sahihi. Kwamba uchukue mtu pasipo bureaucracy uchukue mtu kwa merits mwenye uwezo. Pili unafanya sera na maamuzi sahihi na tatu ni lazima tuwe na zero tolerance kwenye mambo ya corruption.

Mheshimiwa Mwenyekiti, imezungumzwa stori ya maliasili hapa, Mheshimiwa Waziri wa Maliasili kwa kweli sisi ambao tunaotoka maeneo ya ukanda ule na Watanzania wengine lazima tukubaliane hiki kizungumkuti cha kufanya maamuzi ya kuuza ng’ombe za watu tofauti na mpango wa kupata fedha tuwawezeshe Watanzania wapate maisha bora. Lakini hawa ambao ng’ombe zao zimeuzwa wanapaswa kusomesha, hao wenzao ng’ombe zimeuzwa wanatakiwa wajenge nyumba bora, hawa ambao ng’ombe zimeuzwa wanatakiwa wapeleke watoto Vyuo Vikuu. Huu ndiyo uchimi wao na hawana namna.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mpango huu sijaona Mpango wa Serikali wa kupunguza migogoro kati ya wananchi na hifadhi, mpango wa kuwalipa fidia waliopo karibu na hifadhi wakatafute maeneo mengine lakini pia kupunguza migogoro ya wakulima na wafugaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Waheshimiwa Wabunge wanasimama kwenye Bunge hili wanazungumza eti wangapi wameuwawa, wangapi wamepata ulemavu wa kudumu, hii haiwezi kuwa sawa, lazima Serikali iwe na mpango wa kufanya Watanzania wote wafurahie maisha kwa kupata huduma za kimaendeleo lakini na kutendewa haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa inategemea tusipokuwa na watu sahihi katika maeneo mbalimbali unaweza ukawa na mtu yuko mahali anasimamia wenzake kumbe na yeye anatakiwa asimamiwe na wewe unasubiri matokeo. Umemuweka mtu amekaa mahali anatakiwa asimamiwe wewe unafikiri anasimamia wenzake kumbe anahitaji msaada. Kwa hiyo, tuangalie modality ya kupata viongozi katika maeneo yetu. Mimi nilifikiri kwamba kule kwangu Serengeti, Bunda, Tarime, Mbarali tumwambie Mheshimiwa Makonda afanye ziara pale halafu apige simu kwa Waziri wa Maliasili atolee maelezo kwa wananchi pale. Hii hali haiwezi kupokelewa kule vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mnapozungumza hapa na kupanga sisi kwenye maeneo yale tupo kwenye kitimoto, tupo kwenye kiota lazima tutengeneze mazingira mazuri kauli ya Serikali, kuwasikiliza tumetoka mbali tunajua, haya mambo Mheshimiwa Waziri lazima muingize kwenye mipango. Ifike mahali Wabunge humu tusipeane taarifa hawa watu wangapi wamekufa, tusipeane taarifa ng’ombe ngapi zimeuzwa. Tuseme tumeboresha huduma na Watanzania wanampenda Mheshimiwa Rais kazi ni nzuri na kazi iendelee mimi niwatakie kila la kheri viongozi wangu lakini ni muhimu tuweke haya katika mipango yetu. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana kengele ya pili imeshagonga.

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.