Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudia Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Sophia Hebron Mwakagenda

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudia Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi kuchangia kwenye mpango huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninashukuru hii Idara ya Mipango imerudi tena kwa sababu ilikuwepo baadae ikatoka Mheshimiwa Rais ameirudisha tena na ametupatia Waziri kamili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yoyote au hata ngazi ya familia pasipokuwa na mipango thabiti siyo rahisi kabisa kufikia malengo makubwa ambayo familia hiyo au nchi hiyo imejipangia. Tanzania tulikuwa na usemi ambao naamini bado tunaendelea nao kwamba kilimo ni uti wa mgongo. Mimi naamini kwamba bado tunaendelea nao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa asilimia zaidi ya 80 au ikishuka sana asilimia 75 bado tunaendelea na suala la kilimo na wananchi wengi ni wakulima. Bado sijaona jitihada kubwa sana ya kuhakikisha tunakuwa na kilimo chenye tija. Pamoja na kuongeza bajeti kwenye Wizara hii bado kilimo chetu hakiendani na ufasaha kamili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilizungumzia kuwa na kilimo cha kimkakati na safari hii tulizungumzia zao la alizeti, wananchi wakahamasika, wakaanza kulima alizeti, mpaka sasa alizeti imejaa kwenye maghala bado imeshuka bei wananchi wamebaki wanashangaa, kwa sababu tunafahamu kwamba mkulima anapolima lazima anakuwa na malengo yake. Leo hii kama tunakuwa na maghala alizeti imejaa na bado tunaingiza alizeti nyingine toka nje inabidi tujue mipango kama Taifa tunataka nini. Tumewaambia wakulima walime alizeti wakati huo huo tunaingiza alizetu toka nje lazima soko litayumba na anayeumia zaidi ni yule mkulima ambaye yeye kodi inambana na yule anayeleta toka nje ana unafuu wa uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zao la alizeti nimelisema lakini tunalo zao la parachichi. Tunaita parachichi ni dhahabu ya kijani, leo hii mkulima wa parachichi anahangaika na zao hili, analima lakini mwisho wa siku bado hatujapata masoko ya parachichi. Jirani zetu wa karibu wanakuja wananunua kwa bei ya kutupa kwa mkulima kule chini lakini wanavusha nje ya nchi, wakienda kwenye nchi zao wanaotuzunguka wana-brand kama yale maparachichi yametoka katika nchi zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama Taifa lazima tumtetee mkulima tuhakikishe zao hili anapolima liwe lina tija na limletee faida yeye na familia yake lakini mwisho wa siku Taifa lipate faida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiwa na kilimo kisichokuwa na masoko, tunakuwa hatujamtendea haki Mtanzania, ni lazima tutafute masoko. Leo hii Tanzania imekuwa nchi ambayo wanalima alizeti, wanalima ufuta, wanalima mazao kama hayo lakini mwisho wa siku wanakuja kununua madalali na kwenda kuuza nje wakati sisi bado tunayo nafasi. Nimesema kilimo cha tija, leo hii ukienda kwa nchi zetu jirani heka moja ina uwezo wa kutoa magunia 40, sisi tukitoa magunia mengi ni magunia 10! Lazima tubadilike katika kuhakikisha tunatetetea mazao ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tumepata wito wa kulima mbaazi, tunafahamu sote miaka mitatu iliyopita tulitangaza mbaazi kwamba ina soko Nchi ya India na wananchi wakalima, mwisho wa siku tuliambiwa tule kama mboga, haiwezekani! Ni lazima tuwe na mikakati ambayo inamsaidia mkulima wa kawaida akiambiwa anaiamini Serikali yake kwamba ninachokifanya kinaenda kutimia kweli kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo ya kuyaangalia, kwa mfano migogoro ya ardhi pia, hatuwezi kuwa na nchi yenye mipango wakati huo hatuwezi kuitumia vema ardhi yetu. Leo hii kila siku tunazungumzia migogoro. Hakuna namna bora ya kuwasaidia wananchi hasa kwenye mambo ya ardhi, mkulima ajue ana ardhi yake kiasi gani, lakini mfugaji nae aelekezwe ni sehemu gani atasimamia, tutaishia kukaa kwenye migogoro na kuweka miongozo na kulalamika kama Wabunge wakati Wizara husika ipo tunaomba muweke msisitizo katika utunzaji wa ardhi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TMA wametuambia habari ya mvua, kwamba kuanzia Oktoba mpaka Disemba tutakuwa na mvua. Mimi ninaiomba Serikali ihakikishe inanunua mazao kwa wingi. Tunafahamu mna uwezo wa kununua tani milioni tatu, lakini maghala mliyonayo yanaweka tu tani laki tano na inayobaki tani milioni mbili na laki tano ni kwa watu binafsi. Ni hatari sana kutegemea watu binafsi katika uhifadhi wa chakula wakati Serikali ipo. Tunaomba mnunue chakula kama haya majanga yataendelea na sisi tunamwomba Mungu yasitokee yashindwe, lakini mwisho wa siku lazima tujiwekee akiba na akili ya kuhifadhi chakula chetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaamini kama mvua itaendelea kusumbua mwisho wa siku tutakosa chakula hapo mbele kwa maana mazao yatakuwa hayawezi kuwa sawa sawa, lakini kwa sehemu zile ambazo mvua haijaharibu tunaomba mbolea iende kwa wakati, wananchi waweze kulima mapema labda itaenda kutuokoa kwa hiyo nafasi iliyobaki. Mheshimiwa Waziri husika wa Mipango hakikisha unamlinda mkulima na kumuwekea mipango thabiti ambayo itamsaidia katika ukulima wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado tunategemea kilimo hatujajitoa kwamba sisi ni mabepari, bado sisi ni wakulima, sisi ni wafugaji na asilimia zaidi ya 70 ni watu ambao wanaendelea kwenye kilimo. Ninaomba utuwekee mkazo uthabiti katika kulinda haya. Hili suala la mvua ambalo linaendelea na ambalo tumeambiwa na TMA tusilidharau, tuhakikishe tunaongeza idadi ya kununua chakula kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo ninaomba majibu Mheshimiwa Waziri atakapokuja tunaongeza kiasi gani cha tani cha ununuzi na kujenga miundombinu ya kuifadhi maghala ya chakula. Ahsanteni. (Makofi)