Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Salome Wycliffe Makamba

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika Wizara hii ya Nishati na Madini. Naamini nafasi hii haijaja kwangu kwa bahati mbaya kwa sababu, natokea Mkoa wa Shinyanga ambao umebarikiwa kuwa na baraka ya madini kwa sababu, nina migodi mitatu mikubwa; migodi miwili ya dhahabu, Mgodi wa Bulyanhulu na Buzwagi iliyoko Jimbo la Msalala na Jimbo la Kahama. Nimebarikiwa kuwa na Mgodi wa Williamson Diamonds ulioko Mwadui Shinyanga, lakini pia nina mgodi, medium scale mining wa El-Hilary ulioko Buganika, Kishapu, ukiacha migodi mbalimbali midogo midogo inayohusika na uchimbaji na uchenjuaji dhahabu ambayo imezunguka Mkoa mzima wa Shinyanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Shinyanga ni Mkoa ambao unachangia takribani asilimia tisa ya pato la Taifa hili na hii ni baada tu ya Mkoa wa Dar-es-Salaam na hii inatokana na uwepo wa nishati na madini katika mkoa huo. Pamoja na baraka hizi ambazo Mkoa wangu wa Shinyanga umebarikiwa kuwa nazo leo nikisema niondoke na watu wachache hapa kwenda kuangalia hali halisi ya mkoa huu, ukilinganisha na baraka hizi ambazo tunazo, mambo yanayoendelea kule ni mambo ya kusikitisha sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Mkoa wa Shinyanga hasa maeneo ya uchimbaji, walipoletewa habari hii ya uwekezaji wa sekta ya madini walifikiri kwamba, itakuwa ni faraja kubwa kwao na itawakwamua na umaskini, lakini kwa bahati mbaya watu hawa, badala ya mijadala ya kuwahamisha ili kuweza kuwapisha wawekezaji kufanyika kama inavyoelekeza Sheria ya Madini ya mwaka 2002 na 2008 badala yake watu hawa walihamishwa kwa kufukuzwa kama wakimbizi kwenye ardhi yao wenyewe. Mbali na hivyo, watu hawa walilipwa fidia ambayo intervention ya Serikali katika ulipaji wa fidia hizi, ikawa ni kinyume na matarajio ya wakazi hawa, hasa maeneo ya Kakola, ambako kuna mgodi wa Bulyanhulu na maeneo ya Kahama Mjini ambako upo mgodi wa Buzwagi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu hawa mpaka leo wamekuwa na kilio cha muda mrefu. Zaidi ya miaka 10 wanalalamika kuhusu unfair compensation iliyofanyika kwenye maeneo yale, lakini Serikali ambayo tunaamini kwamba, inaweza kushughulikia matatizo yao haioni umuhimu wa kushughulikia matatizo hayo na wale wananchi wa-feel kweli Serikali ipo kwa ajili ya kuwatumikia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Mkoa wa Shinyanga ni wapole na ni watulivu, pamoja na maumivu makali waliyoletewa kwa sababu ya unfair compensation, malipo ya fidia ambayo hawakuridhika nayo, walikubaliana kuvumilia mgodi wakiamini ipo siku Serikali itakuja kutatua matatizo yao. Pamoja na Serikali kutokutatua matatizo yao na kuwaahidi kwamba, watapata kazi kwenye migodi ile, mpaka leo wananchi wale hawapati ajira na wakifanikiwa kupata ajira basi, watapewa zile ajira ambazo mwisho wa siku zitawaacha katika hali ya umaskini mkubwa na utegemezi wa hali ya juu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wanaozunguka eneo la mgodi wakipata kazi kubwa katika migodi hii ambayo tunaamini ni ya wawekezaji watapata kazi ya kufagia, kufyeka, upishi na hakuna program zozote za msingi ambazo ni madhubuti zimewekwa na Serikali zinazoweza kuwaendeleza wananchi wale! Japokuwa tunasema wamefanya kazi kwa muda mrefu tuna-assume kwamba, wana-on job training, basi angalau i-certify ujuzi walionao ili siku moja watu wale waweze kuja kupata kazi ambazo zitawaingizia kipato na cha akiba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisikitishwa sana na matukio yaliyojitokeza kwenye Mgodi wa Bulyanhulu miaka ya 2000, 2002, 2005; wafanyakazi wale walipata ulemavu, wengi wao wakiwa ni ma-operator. Wale ambao tulipata bahati ya kwenda kutembelea migodini kuna Watanzania wenzetu wanaofanya kazi ya ku-operate mitambo katika migodi ile, lakini pamoja na maradhi waliyoyapata kwa sababu ya kufanya kazi ngumu na nyingine zikiwa underground, watu wale walipelekwa kutibiwa na mgodi na wakiwa wanaendelea na matibabu yale, wale watu walirudishwa kazini na kufukuzwa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kesi zao ziko Mahakamani. Mpaka leo wanahangaika wengine wanakufa kwa sababu ya magonjwa, lakini Serikali inayojiita Serikali sikivu, sijaona hatua mahususi, hatua madhubuti za kusaidia kutetea watu hawa na leo hii tunajisifu hii ni Serikali ya Hapa Kazi Tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiacha mbali suala la watu kufukuzwa kazi, kuna watu ambao leo migodi ya Tanzania, migodi ya wawekezaji imekuwa ni Serikali ndani ya Serikali ya Tanzania. Wafanyakazi wanapokosea katika migodi ile adhabu wanayopewa bila kujalisha ukubwa wa kosa alilolifanya anapewa adhabu ya kufukuzwa kazi na anafungiwa haruhusiwi kufanya kazi mahali popote pale maisha yake yote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala limewaathiri watu wengi ambao kama nilivyotoka kusema awali, wananchi wa Mkoa wa Shinyanga maisha yao yote yamekuwa ni maisha ya madini. Unapomwambia kwamba, haruhusiwi kufanya kazi tena ina maana unamzuia yule mtu kupata kipato halali na hakuna adhabu Tanzania hii, labda kama ni adhabu ya kifo, inayomfanya mtu kupewa adhabu ya milele, lakini hicho ndiyo kinachoendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo migodi inafungwa! Tumeona Mgodi wa Tulawaka umefungwa na Mgodi wa Buzwagi huenda mwakani ukaanza closure plan na migodi mingine itafungwa. Kinachotokea nyumba zinazozunguka migodi hii zimekuwa zikipata athari kubwa ya uwepo wa migodi hiyo, kama athari za milipuko na athari za kemikali inayoweza kuvuja kutoka migodini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini leo Tulawaka imeshafungwa na Buzwagi itafungwa. Vijiji vya Mwendakulima, Vitongoji vya Ikandilo, Chapulwa, Mwime, Mbulu, Kakola, kule Msalala watu wanalia, nyumba zao zimepata crack, zimepasuka kwa sababu ya athari ya milipuko! Nimewahi kushiriki kwenye Kamati kwa ajili ya kuangalia athari za milipuko na Kamati hizi zilishirikisha watendaji wa Serikali ambao ni Majiolojia na Maafisa Madini. Afisa Madini anakuja kwenye Kamati ya Uchunguzi wa Athari ya Milipuko na kalamu na karatasi; utawezaje kuchunguza athari ya mlipuko kwenye nyumba bila kuwa na vifaa ambavyo vinaweza kukupa data zinazoeleweka Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoongelea ku-improve sekta ya madini na uwekezaji, tunaongelea kuwapa vifaa Wataalam wa Serikali ili tuweze kupata ripoti ambazo zipo impartially, ambazo zinaweza kusaidia na kutetea maslahi ya wafanyakazi wetu na wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda Nyamongo kuna kesi, hata leo ukifungua kwenye google, kuna kesi inaitwa the Tigiti River; ile kesi watu waliripoti, Wabunge walipiga kelele Bungeni na mto ule ulikuwa unatiririsha maji yanayotoka mgodini ambayo yalisemekana kwamba yana sumu, yalitiririshwa kwenda kwenye vijiji na ng‟ombe wakafa na watu wakaathirika, lakini Serikali ikapuuza kelele za Wabunge, kama ambavyo mnafanya sasa! Matokeo yake ripoti ya Umoja wa Mataifa na Mataifa mbalimbali ndiyo iliyofanyiwa kazi. Hivyo, leo tutaendelea kupiga kelele humu ndani na kama kawaida Serikali itapuuza, lakini naamini sisi tukiongea msipofuatisha na mawe yataongea na ipo siku mtatekeleza matakwa ya wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nielekee kwenye suala la uchimbaji holela. Katika Wilaya ya Bukombe kuna Pori la Kigosi Moyowosi na Sheria ya Wanyamapori ya Mwaka 2009 inasema, hairuhusiwi kuchimba madini hasa ya dhahabu except for strategic minerals. Lakini leo…
MWENYEKITI: Ahsante, muda wetu ndiyo huo!