Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hoja ya Kuazimia Kuwahamisha Maafisa Ushirika katika Tume ya Maendeleo ya Ushirika na Maafisa Ugani chini ya Wizara ya Kilimo

Hon. Justin Lazaro Nyamoga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilolo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hoja ya Kuazimia Kuwahamisha Maafisa Ushirika katika Tume ya Maendeleo ya Ushirika na Maafisa Ugani chini ya Wizara ya Kilimo

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi ya kuwa mchangiaji wa kwanza wa hoja hii.

Mheshimiwa Spika, utaratibu wa ugatuaji wa madaraka ulipangwa kulenga kuendelea kuzipa nguvu Halmashauri kujisimamia na kusimamia shughuli zake. Kumekuwa na utaratibu wa kunyofoa vipande mbalimbali ndani ya Mamlaka za Halmashauri. Ilianza Ardhi kidogo, TARURA ikatolewa, ikaja Ardhi imetolewa, Maji imetolewa na kila moja inatolewa kwa namna yake kwa hoja mbalimbali zinazoletwa hapa ndani, ikiwa utaratibu huu utaendelea maana yake ni kwamba mwisho Halmashauri zitabaki bila Idara yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, inawezekana kukawa na mapungufu katika utekelezaji, nadhani ni vema tukaangalia namna bora ya kuimarisha Halmashauri zetu na usimamizi wake, hata hizi zilizotolewa zikaangaliwa jinsi gani Halmashauri zinaweza zikawa na udhibiti badala ya kuendelea kunyofoa kila kipande na mwisho tukaacha Halmashauri hazina kitu chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja iliyowasilishwa inaweza ikawa na mashiko, udhaifu kwenye Ushirika unaweza ukawepo, kwa hiyo siyo kwamba napinga kwamba kwenye Ushirika kuna changamoto, najua zinaweza zikawepo lakini suluhisho lake si kuendelea kunyofoa Idara katika Halmashauri na mwisho wake kuacha Halmashauri hazipo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama tuna mashaka na jinsi tulivyofanya ugatuaji wa madaraka ni bora tufute sasa hizo Halmashauri zisiwepo kuliko kila siku unatoa kipande hiki, unatoa kipande hiki, mwisho unaimaliza Halmashauri kwa hiyo itakuwa na Mkurugenzi tu.

MHE. ALOYCE A. KWEZI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mimi nilikuwa naomba…

SPIKA: Mheshimiwa Justin Nyamoga kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Kwezi.

TAARIFA

MHE. ALOYCE A. KWEZI: Mheshimiwa Spika, nilitaka nimpatie taarifa mzungumzaji kwamba hata baada ya kuwa wamechukua baadhi ya watumishi kwenye Idara hizo alizozitaja, kwa maana ya Ardhi, Maji na TARURA imetuwia vigumu sana Madiwani. Kwanza imekuwa ni kama hisani kwa hiyo utendaji wa kazi wa Madiwani ambao ndio wanatakiwa kutafsiri miradi na mambo yote yanayoendelea kwa faida ya nchi yamekuwa magumu sana.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa nataka nimpe taarifa hiyo. (Makofi)

SPIKA: Haya, ahsante sana Mheshimiwa Kwezi ulikuwa unatoa taarifa siyo unachangia. Mheshimiwa Nyamoga unapokea taarifa hiyo?

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, ninaipokea taarifa na mimi hoja yangu kwa kweli kwenye hili nafikiri tujenge mifumo mizuri ya ugatuaji wa madaraka, tuimarishe Halmashauri na hata hizi ambazo tumezitoa tutafute namna bora ya kujenga uhusiano na Halmashauri.

Mheshimiwa Spika, maji, barabara na zingine zisimamiwe vizuri lakini Halmashauri ziwe na uwezo lakini tusiendelee kunyofoa moja baada ya nyingine.

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Spika, taarifa

SPIKA: Mheshimiwa Nyamoga, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Mbunge wa Manonga.

TAARIFA

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Napenda kumpata taarifa mchangiaji, tumeona ugatuaji katika Halmashauri zetu kwa mfano TARURA toka ilipowekwa mamlaka yake, sasa hivi inafanya vizuri zaidi tofauti na ilivyokuwa mwanzo. Kwa hiyo, hawa Maafisa wetu wakati mwingine wakiwa Halmashauri hata mafuta hawana. Naomba kuwasilisha. (Makofi)

SPIKA: Haya ahsante sana. Mheshimiwa Justin Nyamoga unapokea taarifa hiyo.

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, hata sijaelewa, kwa hiyo sitapokea. (Kicheko/Makofi)

SPIKA: Sawa. Sasa ukisema hujaelewa, hujamsikia ama hoja yake huikubali? Kwa sababu sasa…

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, sijamsikia.

SPIKA: Basi wacha nikueleweshe, anasema hivi: Imetolewa mifano ya TARURA, TARURA ilivyoondolewa Halmashauri yeye kwa taarifa anayokupa ni kwamba ufanisi umeongezeka. Kwa hiyo, unaipokea taarifa hiyo? Ndiyo taarifa ya Mheshimiwa Mbunge.

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, kuhusu ufanisi kuongezeka napokea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja yangu ni kwamba kuna haja ya kuboresha Halmashauri zetu ziwe na usimamizi, ziwezeshwe, hata kwenye hilo suala la ushirika ukiangalia changamoto utaenda kukuta si kwamba kwa sababu iko kwenye Halmashauri, utakuta kuna matatizo ya kibajeti, utakuta kuna matatizo ya kiutawala na utakuta kuna matatizo mengine na siyo suala la kiutawala. (Makofi)

SPIKA: Haya, kengele ya pili imegonga Mheshimiwa.

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana.

SPIKA: Kengele ni moja, samahani kengele imegonga.

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi.

SPIKA: Shukrani.

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, kwa hili siwezi kuunga mkono hoja iliyowasilishwa. (Makofi)