Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbagala
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii nami niweze kutoa mchango wangu katika Bajeti kuu ya Serikali ya mwaka 2022/2023.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, kwa niaba ya wapiga kura wangu wa Jimbo la Mbagala, naomba sana nikishukuru chama changu cha Mapinduzi kwa kuandaa ilani ya uchaguzi ambayo inaenda kutatua shida za wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nachukua nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi kwa maana kwa asilimia kubwa yale yote ambayo yameahidiwa kwenye Ilani ya Uchaguzi tumeona yameletwa kwenye bajeti zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi kubwa zimefanyika katika majimbo yetu. Tumeona mambo ya elimu, afya, barabara, maji na umeme. Kila Mbunge hapa ameona vitu vilivyofanywa. Kwa hiyo, tuna kila sababu ya kuendelea kumshukuru kwa kazi hiyo aliyoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kukushukuru wewe, Mheshimiwa Spika, Naibu Spika na Wenyeviti wote mliotuongoza katika Bunge hili. Kwa maana mlitupa nafasi za kutosha katika Wizara mbalimbali tumechangia, tumeonesha mbwembwe za hali ya juu katika kudai miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nawashukuru Mawaziri wote, yale ambayo tulikuwa tukiyaomba mmeendelea kuyaweka katika ilani, na katika bajeti kuu za Serikali. Kwa maana hiyo tunatarajia mambo tuliyoyaomba yanaenda kutekelezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi iliyobaki sasa ni kwetu sisi Wabunge kuona namna ambavyo tutaisaidia Serikali namna bora ya kuweza kukusanya fedha ili fedha zile sasa ziende kutekeleza miradi ambayo tumeiomba hapa kwenye Bunge letu. Miradi mingi imeandikwa katika vitabu, lakini ili itekelezwe lazima zipatikane fedha za kwenda kuitekeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mchango wangu nataka niutoe katika Wizara ya Ardhi na namna gani Wizara ya Ardhi itaenda kuongeza pato katika Serikali. Ukisoma kitabu cha bajeti cha Waziri wa Ardhi ukurasa wa nane, kimeelezea, kulikuwa na lengo la kukusanya shilingi bilioni 221 lakini makusanyo yalikuwa shilingi bilioni 115 sawa na asilimia 52. Na ukikisoma kitabu hiki, kimesema sababu ya kutokufikia hayo malengo ni taasisi na mashirika 114 yana deni la zaidi ya shilingi bilioni 78.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wakati muafaka sasa wa kuhakikisha hizi wizara na taasisi zinalipa madeni haya, lakini vilevile wamesema wananchi wamekuwa hawalipi pango la ardhi kwa wakati. Mawaziri wetu sasa wa Ardhi na wa TAMISEMI ni wakati wa kushirikiana kwa pamoja kuona namna gani wananchi hawa wanaenda kulipa pango la ardhi. Utaona katika halmashauri karibu zote wanapitisha magari ya matangazo, wanatangaza na kuwahamasisha wananchi waende kulipa leseni za biashara zinazotozwa na halmashauri. Kuna shida gani katika gari lile linalotangaza, wakatangaza na wakahamasisha wananchi kwenda kulipa kodi ya pango la ardhi. Kwa kufanya hivyo, na hakika wananchi wataamasika na pango la ardhi litalipwa na hatimaya tutafikia malengo ya wizara yetu hii ya ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la kufanya transfer katika miliki zetu ambazo tunanunua kutoka kwa watu mbalimbali. Tulio wengi humu tuna zile sales agreement kwenye kufanya transfer tunakuwa hatufanyi na sababu kubwa aidha uhamasishaji unakuwa mdogo au mtu akishakuwa na ile sales agreements inamwezesha kufanya mambo mengine ambayo kama yangezuiliwa, tafsiri yake ingemlazimu kila mtu kwenda kufanya transfer ya ile hati aliyokuwa nayo. Hapa tunapoteza sana mapato kwa maana katika kufanya transfer kuna asilimia kumi ya thamani ya lile jengo zinakwenda TRA na tulio wengi kwa sababu hatufanyi transfer, basi mapato haya tumekuwa tukiyapoteza katika miaka yote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna suala zima la mabadiliko ya matumizi ya ardhi. Ukisoma sheria zilizokuwepo za mabadiliko ya matumizi ya ardhi, ni elfu 30 tu ambayo inatakiwa iende wizarani, lakini ukiangalia taratibu zenyewe za kubadilisha matumizi ya ardhi, ni taratibu ndefu ambazo Serikali inatumia gharama kubwa kufanya hayo mabadiliko ya matumizi ya ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu na ushauri wangu, tuangalie namna ya kubadilisha hizi sheria angalau katika mabadiliko ya ardhi yaendane na thamani ya ardhi yenyewe. Leo mtu anabadilisha ardhi kutoka matumizi ya kawaida kuwa matumizi ya ujenzi wa petrol station lakini gharama ya kisheria anatakiwa alipe Sh.30,000 ebu tuangalie uhalisia, naamini haya yote tukiyafanyia kazi, basi katika sekta ya ardhi tutapata mapato ya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala zima la viwanja vilivyopimwa na vikamilikishwa. Kwa mujibu wa sheria zetu ndani ya miezi 36 huyu mtu anatakiwa akiendeleza kile kiwanja, lakini utakuta viwanja vingi havijaendelezwa. Kwa kufanya hivyo, tunakosa zile kodi za majengo. Niombe sana mamlaka husika, zizingatie hii sheria ya kuhakikisha wale wote waliopewa ardhi wanaziendeleza ardhi zile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huo ulikuwa ndio mchango wangu katika kuhakikisha Serikali inaendelea kupata mapato ya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kengele ya kwanza hiyo?
MWENYEKITI: Ndiyo, endelea.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nizungumzie juu ya Mradi wa Uendeshaji wa Jiji la Dar es Salaam. Tumekuwa tukipata maelezo hapa ambayo yamekuwa hayana mwelekeo miaka yote. Tunaambiwa uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam awamu ya pili upo katika michakato mbalimbali, tuwaombe sana hasa Waziri wa Fedha tumalize mazungumzo haya na kama hizi fedha zikipatikana zitaenda kutatua suala zima la miundombinu ya barabara katika Jiji la Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kule kwenye Jimbo langu la Mbagala ukiangalia kata zangu zote kumi, Kata ya Chamazi Kiburugwa, Mianzini, Charambe, Kilungule, Mbagala, Mbagala Kuu, Kijichi, Tuangoma na Kata ya Kibangulile. Kata hizi zinasubiri kwa hamu Mradi huo wa Uboreshaji wa Jiji la Dar es Salaam. Kwa hiyo tumwombe sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha, mradi huu aendelee kuusimamia hili uende kutekelezwa kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Dar es Salaam tumefanyiwa mambo ya kutosha mambo ambayo bado hayajakaa sawa, sasa hivi ni suala zima la miundombinu ya barabara. Tuwaombe sana mawaziri wetu wote wanahusika watilie mkazo suala la uboreshaji wa miundombinu ya barabara katika Jiji la Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo yaliyo mengi na machache, naomba kuunga mkono Bajeti Kuu ya Serikali. Ahsante sana. (Makofi)