Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Emmanuel Lekishon Shangai

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngorongoro

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia bajeti ya Serikali. Mimi nimshukuru na kumpongeza Kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu Nchemba kwa bajeti nzuri pamoja na Serikali kwa ujumla.


Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeweka mikakati mingi sana lakini mwisho wa yote tunachokusanya ndicho kitakacho-determine kile ambacho tutaenda kufanya. Tusipokusanya vizuri hatuwezi kutekeleza mikakati yote ambayo tumeweka kama Serikali. Bajeti hii itaenda kutekelezwa vizuri kama tutaweka nguvu nyingi sana kwenye ukusanyaji wa fedha pamoja na kuamua kuondoa mianya yote ya rushwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Wilaya yangu ya Ngorongoro nilishamwambia Mheshimiwa Waziri kwamba tunahitaji tujengewe kituo cha forodha mpakani mwa Kenya na Tanzania. Wananchi wale wanataabika sana kufanya biashara. Kutoka Loliondo mpaka Namanga ni zaidi ya kilomita 120. Kwa hiyo, mpaka wetu bado ni mkubwa sana, tukijenga Serikali itakusanya mapato makubwa katika lile eneo pamoja na wananchi kufanya biashara kiurahisi katika lile eneo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala lingine Mheshimiwa Waziri is not your classic kwenda kuchukua fedha za asilimia 10 ya Vijana pamoja na akina mama kwa ajili ya kuwapa machinga. Kwa hiyo, na mimi nishauri kama alivyosema Nusrat Hanje, kwamba tuache hilo, tusifikirie kabisa. Tunaweza kukusanya fedha katika maeneo mengine ambayo itaisaidia Serikali na wale akina mama pamoja na Vijana nao wanufaike na hiyo asilimia 10 katika ngazi ya halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoshauri katika halmashauri zetu kuna upotevu mkubwa wa mapato; nina uwezo wa kutoa ushuhuda. Nilipokuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro niliamua siku moja kwenda kukusanya mapato mwenyewe kwenye mnada ambao wataalamu walikuwa wanakusanya shilingi 1,000,000, nilikusanya shilingi 5,000,000. Nikasimamia mnada huo consecutively for four months; kwa sababu tarehe 15 na tarehe 02 nikakusanya shilingi milioni 40. Lakini ukiangalia data za wataalam wetu wao kwa miezi minne wanakusanya shilingi 5,000,000. Sasa kule chini kuna upotevu mkubwa. Nikawapa Madiwani kwenye minada mingine. Nikawaambia hebu tusimamie tuone kwamba ni kwamba hakuna fedha au ni wataalam hawakusanyi. Kila mnada aliyesimamia Mheshimiwa Diwani ili-double na ku-triple kwa wakati mwingine. Mnada ambao wao wanakusanya 1,000,000 sisi tukawa tunakusanya zaidi ya 4,000,000 kwa mwezi, lakini wao wanakusanya 1,000,000. Fedha nyingi za Watanzania zinaenda kwenye mifuko ya watu wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwaombe TAMISEMI msimamie ukusanyaji wa mapato, kule Wakurugenzi hawakusanyi mapato. Tulitakiwa kukusanya zaidi ya bilioni 800, tumekusanya 700 na hamsini na kitu. Kwenye Halmashauri zetu tuna uwezo wa kukusanya mpaka trioni mbili tukiamua kuwapa watu waadilifu, lakini tukiendelea hivi tutaendelea na story zilezile kila siku. Hata hii asilimia 10 wananchi wetu wangekuwa wananufaika sana kama makusanyo yangefanyika. Lakini pia TRA tunapoteza fedha nyingi sana kwenye misamaha ya kodi ambayo haina maana. Ni lazima sasa Mheshimiwa Waziri usimamie hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala lingine ni suala la kuondoa ada kidato cha tano na sita; niipongeze Serikali, lakini iendane sambamba na kuondoa michango ambayo haina maana. Kwa mfano leo mwanafunzi anaenda kuripoti shule hiyo ina zaidi ya miaka 50 unamwambia aende na kiti na meza. Ina maana kwa miaka yote kila mwanafunzi anayemaliza anaondoka na meza na kiti chake? Kila mwaka tunachanga fedha kwa ajili ya viti na meza? Haiwezekani! Kwa hiyo, niipongeze Serikali kwa kuondoa ada hiyo kwa sababu itawasaidia Watanzania wengi, lakini iendane sambamba na kuondoa michango ambayo haina maana kwa Watanzania kama kweli tunataka kuwasaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kumaliza haya niende kwenye hoja ambayo Waheshimiwa Wabunge wengi wamechangia. Wengi hawajui kinachoendelea katika eneo la Pori Tengefu la Loliondo. Mimi ni Mbunge, ni wananchi wangu ndiyo wanaoteswa kule. Naomba niwaambie kitu kimoja, watu wengi hapa wanasema, akinyanyuka mtu anasema kwamba ardhi ya Tanzania ni ya Rais. Tusimchonganishe Rais na wananchi, ardhi ya Tanzania kwa mujibu wa Sheria ni ya Umma. Rais amepewa kama mdhamini tu. Kwa hiyo kwa mtu yoyote anayesimama ukitaka soma Land Policy ya Tanzania ya mwaka 1997. Naomba kunukuu kipengele “(a) All land in Tanzania is public land, versed in the President as a trustee on behalf of all Tanzanian.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini wengine tunasimama wanaofanya kazi inayofanyika Loliondo siyo Rais ni watendaji wake ambao hawataki kujifunza kutoka kwa waliyowatangulia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo ni lazima tujue, ardhi square kilometer 1,500 katika eneo la Loliondo ni ardhi ya vijiji; kata nane, vijiji 14. Na kwa nini ardhi ile inatwaaliwa, Sera yetu ya Ardhi inatuambia nini kuhusiana na unapotaka kuchukua ardhi ya wananchi, ardhi ya vijiji? Kipengele Na. 4 inasema; “Consultation and consent of all Village council will be required whenever alienation of Village land is necessary”.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule Loliondo kinachofanyika ni unyakuaji wa ardhi, hakuna mwananchi, hakuna Serikali ya Kijiji ambayo imeridhia ardhi ile kutengwa, hakuna. Lakini watu wanasema ni ardhi, it’s not a bared land, is the land with people. Kwa hiyo, kinachofanyika pamoja na masuala mengine lakini ieleweke wananchi wa Loliondo…

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa Ridhiwani.

T A A R I F A

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa taarifa msemaji anayesema sasa asipotoshe. Kinachofanyika Loliondo ni uwekaji wa mawe kuonesha mipaka baina ya ardhi ya kijiji na ardhi ambayo inatumika kwa ajili ya kupita maeneo ya mifugo. Kwa hiyo asiseme kwamba hapa kuna ardhi inayochukuliwa, hakuna ardhi inayochukuliwa kinachowekwa ni mipaka kuonesha baina ya maeneo ambayo yanatumika na wananchi na maeneo ambayo kwa shughuli nyingine. Ahsante sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Shangai, unaipokea hiyo taarifa.

MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei taarifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi ni watu wazima, unatenga ile ardhi kutoka ardhi ya nani? Unatenga kutoka kwenye ardhi ya nani.

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa Mzungumzaji, kwamba eneo la Pori Tengefu la Loliondo kwa mara ya kwanza lilitangazwa na Serikali ya Kikoloni kupitia Fauna Conservation Ordinance ya Mwaka 1959. Na tangu wakati huo hatujafuta, tumekuwa tukifuta Sheria tuna-repeal na kutengeneza nyingine. Kinachofanyika ni kuweka alama kwenye eneo la square kilometer 1,500 kati ya square kilometer 4,000 za eneo la Pori Tengefu la Loliondo. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Shangai, unaipokea hiyo taarifa.

MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba utunze muda wangu, hawa wana nia tu ya kumaliza muda wangu. Lakini ukweli ni kwamba mimi ninajua kinachoendelea. Ardhi ile ni ardhi ya vijiji kwa mujibu wa sheria zote za Tanzania.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa hajaanza hata kusema jambo jingine, msubiri aseme halafu utaomba taarifa.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, anaongopa, anavuruga, haongei ukweli.

MWENYEKITI: Hata akimaliza kusema nitakupa utoe taarifa. Mheshimiwa Shangai endelea.

MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoongelea suala la ardhi tunaongelea maisha ya wananchi na uchumi wao. Naomba ni-quote maneno kwa ruhusa yako ya Bwana William Tenga ambaye ni Mtaalam wa masuala ya ardhi, ambaye amehusisha suala la migogoro ya ardhi kwamba ni sehemu ya maisha ya wananchi.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, anasema hivi; “Nobody can live without land and most people have to share it, creating, competing right. This be about righting land the not be avoided. People relationship to land depend on many factors and have a strong cultural element”.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapozungumzia ardhi ile ya Loliondo ninazungumzia maisha ya watu wanaoishi pale na Wilaya zote za wafugani kwa sababu…

MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

Taarifa Mheshimiwa Shangai.

T A A R I F A

MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hata huyo Mheshimiwa anayezungumza sasa hivi Mbunge wa Loliondo, hata kwenye hiyo definition aliyoitoa sasa hivi inasema hakuna mwananchi anaweza akaishi bila ardhi. Hata hawa wanaohama Loliondo kwa hiyari yao wameonyeshwa maeneo mengine ya kuishi, kwa hiyo wako within hiyo definition ambayo yeye ameisoma sasa hivi.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Shangai, unaipokea hiyo taarifa.

MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei kwa sababu hajui anachozungumza. Mimi nazungumzia Loliondo hakuna mwananchi anayehama Loliondo, yeye akarejee Ngorongoro, ndicho anachotaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nirejee pia maneno ya Profesa wa Sheria Chris Maina Peter, anasema; “Land is an important resource in the world today, it is the main source of live loud and survivor. Therefore, whoever control land logically control the lives of others. This is because that person or persons control what guarantee survivor of human being. Due to the proximity of land to survivor it is frequently related to the right to live”.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia suala la ardhi ile tunazungumzia maisha ya wananchi wetu. Mimi nadhani Serikali inatakiwa kufikiria upya. Pamoja na kwamba wameweka mipaka lakini ile ardhi bado ni muhimu kwa ajili ya wananchi wale. Wananchi wale ukijaribu kuangalia katika wilaya zetu za wafugaji, ukiangalia lile eneo la Loliondo kuna vijiji. Naibu Waziri juzi alisema kwamba hakuna vijiji, wapo wananchi. Ukienda Longido kwenye lile eneo ambalo wanataka kupandisha liwe pori la akiba kuna vijiji 22.

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa Shangai.


T A A R I F A

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mchango mzuri sana wa Mbunge makini wa Ngorongoro; kumekuwepo na hoja zinazozunguka za kuzungumza habari ya maslahi ya taifa na urithi wa dunia. Tunazungumza urithi wa dunia ipi bila Ngorongoro? maslahi ya taifa lipi bila Ngorongoro? Wale ni binaadamu wenye haki sawasawa na binaadamu wengine ni sehemu ya urithi na ni sehemu ya Taifa hili. Hivyo, wana haki waachwe kwenye eneo lao kwa sababu eneo hilo ni lao ni ardhi ya wazazi wao walikowazika mababu zao. Waendelee kupata maisha yao na Sheria inawalinda na repealing clauses zote za Sheria ya Mwaka 1974 na Sheria ya mwaka 2009 Kifungu cha 120 na Kifungu cha 85 na 86 ya Wildlife Conservation Act ya 1974 zote zime repeal mambo hayo ambayo yanazungumzwa. Ni vizuri watu wakasoma Sheria kwa ukamilifu na hasa hawa waliyokuwa wanadai jana kama ni wanasheria waende kwenye repealing clause na transition clause. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Shangai, unaipokea hiyo taarifa.

MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, haya napokea. (Makofi/Vicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiuhalisia ninajua kwamba wengi wanacheka kwa sababu siyo maisha ya watu wao. Lakini mimi ni maisha ya wananchi wangu, wazazi wangu, wadogo zangu na kaka zangu; lakini watu wanafanya michezo, tunapotosha; kwa sababu yaliyofanyika Loliondo kwa wale wananchi very inhuman. Wananchi wametoroka wameenda Kenya, wananchi wanakimbia kwenda kutibiwa Kenya kwa sababu wamenyimwa PF3, kwa sababu na Hospitali zenyewe zilizopo kilomita 70 na nyingine kilometa 30…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Shangai, samahani hayo unayosema una uthibitisho nayo maana usije ukazungumza hapa Bungeni jambo ambalo huna uthibitisho nalo, halafu mwisho wa siku badala ya kusema wewe usahihi ikawa ndiyo wananchi wanapotoshwa.

MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachosema ni kwamba wananchi wameenda kutibiwa Kenya. Naomba unilinde na watu waniheshimu.

MWENYEKITI: Malizia maana muda wako kengele ilikuwa imepiga kwa hiyo kutokana na muda huu nakuongezea dakika moja tu umalizie.

MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumaliza.