Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

hon Hassan Seleman Mtenga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtwara Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikushukuru kwa kunipa nafasi hii, lakini nami niungane na wenzangu kumshukuru Rais wetu mpendwa, kwa kazi kubwa anazozifanya za kutuletea maendeleo ndani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Waziri wetu kwa bajeti nzuri ambayo ina matumaini kwa wananchi. Nadhani bajeti hii ikitekelezwa vizuri, inakwenda kutatua matatizo ya wananchi. Kabla sijaanza kuchangia, mimi ni Mwenyekiti wa Maadili wa Wabunge wa CCM hapa Bungeni. Napenda kulisema hili; Mbunge mwenzetu aliyetoka kuzungumza juu ya baadhi ya Wabunge kutokumuunga mkono Rais, hiki ni kitu kimoja kibaya sana na hapa haikuwa mahali pake kukizungumza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna moja au nyingine, Rais huyu amemgusa Mbunge kila mmoja kwenye Jimbo lake, na kwa hali ya kawaida, sidhani kama kuna Mbunge humu ndani inawezekana akatoka huko nje akamshambulia Rais. Haya nayazungumza, kesho tutasikia magazeti mengi sana yanaandika hicho kitu. Ambacho kinakwenda kufanyika sasa, ni kuwachonganisha Wabunge na Rais wao. Sasa hili siyo jambo jema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba sana Wabunge, kila mwenye shida ambayo inahusiana na suala zima la kiongozi, basi mtuone. Katika Kamati yetu tumeshaita Wabunge zaidi ya 14 humu ndani, lakini kwenye mambo tofauti, siyo masuala ambayo yanamhusu Rais. Kila tulipokaa nao hao Wabunge, hali ipo shwari na tunaendelea na Bunge letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niendelee na mchango wangu. Kwanza, nataka nizungumze kuhusu mapato. Hatuwezi tukaizungumzia bajeti, kila mwaka tunapokuja tunapandisha vitu bei, kila mwaka, lakini still tunavyo vitu vyetu ambavyo viko tayari. Kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, katika hotuba yake amezungumza, kuna baadhi ya watumishi ambao wanahusika na ukusanyaji wa kodi, wanamwangusha. Hili Mheshimiwa Waziri tunakupongeza kwa kuliona. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana nilizungumza, yuko mtu mmoja alipeleka korosho nje lakini kwenye ushuru aliotozwa ametozwa ushuru wa mbaazi. Sasa huu ni upotoshaji, lakini pia ni wizi mkubwa ambao unaendelea kufanyika. Kwa hiyo, twende tusimamie rasilimali zetu. Hatuna shida ya kufika mahali sasa tunasema tuhangaike na viwanda vya pipi, tupandishe bei kwenye ushuru wa pipi wakati bado tuna rasilimali ambazo tunashindwa kuzisimamia ili ziweze kuleta tija zaidi. (Makofi).

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kuna watu wanaagiza magari nje, unaagiza gari IST kwa gharama ya milioni tatu, linaposhuka bandarini ushuru wake TRA ni milioni sita. Tunakwenda wapi? Kama tungepunguza bei ya ushuru, wangapi wangeagiza hayo magari IST na yangekuja kwa wingi gani na sisi tungekusanya kodi ya aina gani? Sasa kuna vitu vingine inawezekana kwamba, tunasema kwamba, tunapandisha ushuru ili tupate kodi kubwa kumbe tunakwenda kujiangamiza wenyewe. Ushauri wangu kwa Serikali, katika vyanzo vyote vya kodi tuangalie population ya bidhaa ambayo inakuja kwetu, tukipunguza kodi bidhaa hizi zitakuja kwa wingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala lingine la wamachinga limezungumzwa sana. Asilimia kumi ambayo tunachangia sisi kutoka kwenye halmashauri zetu, fedha hizi ni msaada mkubwa sana kwa wananchi wetu. Leo tunapoamua kutoa asilimia tano kuipeleka kwenye huduma nyingine kwa sababu, ile asilimia kumi hata Wabunge wengi wamesema haitoshi kwa jinsi ambavyo tumewapa mikopo wananchi wetu, haitoshi kabisa. Sasa naiomba Serikali asilimia kumi hii ibaki palepale ilipo, lakini kama kuna uwezekano wa kuitengenzea sheria tena, tuongeze fedha katika hii asilimia kumi, ni hela ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale kwangu tunaondoaondoa na leo hapa nimepigiwa simu kuna maaskari huko wanafukuza na bunduki, wanafukuza wananchi kwenye maeneo. Sisi tunalo eneo pale nyuma ya Benki Kuu, eneo lile linaota nyasi, eneo lile lina vichaka zaidi ya eka 18, liko pori mjini kwenye manispaa; nimepiga kelele hili eneo tuwajengee hawa wamachinga wakae hapa waache kazi ya kutembeatembea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapomtembeza mmachinga barabarani athari zake nini? Tunakosa kukusanya kodi. Hatukusanyi kodi kwa sababu, hakuna mmachinga anayetoa risiti, lakini mmachinga anapotembea barabarani hana insurance yoyote. Leo tunazungumza tunataka tuwape mikopo, watu wa benki ukiingia kwenye mikopo wanakwambia tunataka hati ya nyumba au ofisi yako iko wapi, mkataba wako uko wapi? Kwa hiyo, hili nalo tuliangalie sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wako wafanyabiashara wanakopa kwenye benki na hawa watu wanapokopa mikopo yao wanaweza wakalipa takribani zaidi ya asilimia 80. Anaposhindwa kulipa japo ameshalipa zaidi ya asilimia 80, watu wa benki wanaingia wananyang’anya nyumba za watu, wanauza nyumba. Hili ni hatari sana kwa wananchi wetu na hii ni kwa nchi nzima, wako watu wamekaa na pesa zao, kazi yao wao ku-coordinate na watu wa benki, nyumba gani itauzwa kesho, keshokutwa. Sasa hatuwasaidii wananchi wetu, tunakwenda kuwaharibu wananchi wetu. Hili nalo naomba nalo tufike mahali tuliangalie, lakini tuwasaidie wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nichangie pia kwenye eneo moja la ujengaji wa reli yetu. Kwanza niishukuru Serikali, kwa kweli inajenga reli, lakini nataka niseme jambo moja ambalo ni ushauri kwa Serikali. Tulikuwa tuna reli ya TAZARA, reli hii ilijengwa na Mchina. Reli ya TAZARA hatukukata kipande kipande, Mchina alijenga mwanzo mpaka mwisho, lakini tukawa na reli ya kati ilijengwa na Wajerumani. Wajerumani wale walijenga reli ile mwanzo mpaka mwisho. Ushauri wangu kwa Serikali hebu tuache kuingia kwenye kuweka wakandarasi zaidi ya watatu, wanne kwenye reli kwa usalama wa Taifa letu. Reli hii ni kitu muhimu sana hatuwezi kuweka zaidi ya watatu, wanne wanakwenda kujenga reli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali kwenye dhana ya usalama wa nchi, hebu turudi sasa tuangalie ni mkandarasi gani bora, yeye anawezekana akaingia joint venture na kampuni nyingine yoyote ikamsaidia kwenda kujenga. Kwa hili natoa mfano, tunazo barabara zetu za lami. Mimi natoka Mtwara, kule Mtwara ukiingia pale Lindi walijenga pale Kharafi, lakini kipande alichojenga Kharafi cha lami ni mkandarasi bora, mpaka leo hakijaharibika, lakini vipande vingine hivyohivyo walivyojenga kwa muda huohuo barabara hazipitiki na kila siku ziko kwenye maintenance. Sasa ombi langu kwa Serikali hebu turudi tuangalie mkandarasi mmoja anaweza akatusaidia nini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie vituo vya afya. Kwangu niishukuru Serikali tumepata kituo cha afya na kimeshaisha. Niombe katika vituo hivi ambavyo vinajengwa, kwenye suala la Madaktari na Wauguzi Serikali watoe kipaumbele tuweze sasa kupata Wauguzi na Madaktari kwa sababu, majengo ni mazuri yana kila jambo ndani mle. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante.