Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Asya Mwadini Mohammed

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. ASYA MWADINI MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia Bajeti Kuu ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ukisoma Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 4, katika masuala mazima ya mambo yanayohusu Muungano na pia kuna masuala ya kodi na mapato. Maana yake kodi na mapato ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano bado ni sehemu ya Muungano, maana yake Wazanzibari wamo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na changamoto kubwa sana ya ukusanyaji wa kodi kwa wawekezaji waliokuwepo Zanzibar. Zanzibar kuna mamlaka mbili za ukusanyaji wa kodi kwa wawekezaji wetu, kuna ZRB ambayo ni Mamlaka ya Mapato ya Zanzibar, lakini pia kuna TRA; Bodi ya Mapato, Mamlaka ya Mapato ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wawekezaji wetu ambao wapo Zanzibar wanalilalamikia suala hili sana na ni kwa sababu, ukiangalia halina tija na huelewi ni kwa sababu kwa nini vyombo viwili vinakusanya kodi kwa wakati mmoja kwenye nchi moja. Wawekezaji wamekuwa wanatengeneza mianya ya kutengeneza rushwa ili waweze kupona waweze kufanya biashara zao. Wawekezaji pia wamekuwa wanafunga hoteli na taasisi zao za biashara kutokana na changamoto hii. Duniani, nchi moja haiwezi kukusanywa kodi na vyombo viwili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Serikali, uchumi wa zanzibar unaporomoka kwa sababu ya changamoto hii. Ushauri wangu kwa Serikali, kuna haja sasa Mamlaka ya TRA ikasimishe madaraka kwa Mamlaka ya ZRB ili waweze kukusanya kodi, then watakutana juu kwenye level ya uongozi na kutambua asilimia ngapi ya kodi iliyokusanywa inakwenda kwenye Mfuko wa Muungano na asilimia ngapi itakwenda kwa Wazanzibari wahusika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wawekezaji wetu wanatulalamikia sana. Tuna Ushahidi, kuna kodi ambazo huwa zinatoka za misamaha, mwekezaji anakuja leo anafungua hoteli, anapewa ile miaka mitano ya msamaha wa kodi, akimaliza miaka mitano kwa sababu ya kukimbia hizi kodi mbili anarudi tena anabadilisha jina la hoteli na kampuni. Mwekezaji anaweza akawa ni huyohuyo mmoja. Hili jambo halina afya, hatuwezi kuwa na wawekezaji wakati mama kila siku anazungumza, lazima tuweke mazingira bora na rafiki kwa wawekezaji wetu na kuwe na kodi ambazo zitamfanya mwekezaji awe anamtafuta yule anayepokea kodi mwenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na vita vikubwa wawekezaji ambao wako Zanzibar wanalalamika sana. Kwa hiyo, niishauri sana Serikali waliangalie suala hili, Mamlaka ya Zanzibar ya ZRB na Mamlaka ya TRA kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lazima wakalifanyie utaratibu haraka, ili tusipoteze wawekezaji Zanzibar, tukuze uchumi wetu, tunahitaji mapato, lakini na ajira kwa watoto wetu ambao wako Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukiangalia bajeti ya mwaka 2022/2023, Mamlaka ya Mapato ya Tanzania (TRA) ilipanga kukusanya trilioni 23, lakini wamefanikiwa kukusanya trilioni 17, kwa hiyo, maana yake kuna trilioni nne zinaeleaelea hivi, hazijulikani zilikuwa wapi. Changamoto za ulipaji wa kodi kwenye Taifa hili zimekuwa sugu, lazima zirekebishwe, ili tuweze kukusanya kodi vizuri na kuweza kuleta tija katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye Sekta ya Utalii. Nimesoma hotuba ya Waziri, ukurasa 56, paragraph ya 68, amezungumza kwamba, the Royal Tour ambayo imelenga kuonesha uwezo wa fursa za huku Tanzania katika sekta ya utalii na uwekezaji, lakini pia akawataka na wana-diaspora waje Tanzania kuwekeza. Tunapozungumza uwekezaji katika sekta ya utalii hatuwezi kuiacha ardhi, mwekezaji anapokuja katika Taifa hili lazima awe na ardhi ambayo haina mgogoro. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunazungumza kelele zilizopo Ngorongoro, leo tunazungumza baadhi ya hifadhi na wananchi wanavamiana. Tume yetu ya Mipango ya Ardhi kwa mwaka huu wamehitaji bilioni 10 ili waweze kupanga na kupima na kuweka ardhi katika mazingira salama, leo wamekwenda kuwapa bilioni moja. Halafu Mheshimiwa Waziri alipokuja ku-wind up hapa aliliambia Bunge hili kuna mkopo ambao utakuja ndio utaipa hiyo bilioni tisa. Hivi kweli tunategemea mkopo ndio uende ukatupimie ardhi yetu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo ni aibu, yaani ni aibu sana. Mama anazunguka duniani, mama wa watu hapati hata muda wa kunywa juice na wajukuu zake, leo yuko Ujerumani, kesho yuko Dubai, keshokutwa sijui yuko wapi? Mama hatulii anatafuta wawekezaji, anatutafutia kula Watanzania, lakini kama yeye anaenda kuhangaika huku na wengine wanatoboa mifuko, kuna jambo ambalo tutakwenda kufanikiwa hapa? Lazima ardhi ipimwe ili Taifa hili liweze kuleta uchumi. Ardhi ikipimwa vizuri maana yake tutaweza kupata mapato, tutatengeneza ajira, wawekezaji watawekeza bila bughudha yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye sekta hiyo hiyo ya utalii nilisoma pia hotuba ya Mheshimiwa Waziri katika masuala ya tozo, nimesikitika sana. Leo tunasema tunahitaji kuwa na wageni na kuwa na utalii ulio bora, lakini tunavyozungumza utalii hatuwezi kumwacha mgeni wala muwekezaji ambaye yupo hapa. Hatuwezi kumuacha mwekezaji ambaye yuko hapa ni kwa sababu, sekta hii yani inakua kupitia private sector. Sasa leo wameweka tozo ya VAT kwenye ndege ndogondogo ambazo zinapaswa zitue kwenye viwanja vidogo vidogo kwa ajili ya utalii wa uwindaji, tutaweza kufika kweli? Kama sisi tunataka ku-compete, wenzetu Kenya wametoa…

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Asya, Taarifa.

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na mchango mzuri sana wa Mheshimiwa Mbunge, kuna eneo moja ambalo nataka tuliweke vizuri; juu ya mamlaka mbili za makusanyo ya mapato katika nchi, aliyoiita ni nchi moja. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema Tanzania ni Nchi moja na ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini Katiba ya Zanzibar inasema Zanzibar ni Nchi na ina Serikali yake Kikatiba, ina Baraza lake la Wawakilishi linalofanya kazi ya kuisimamia na kuishauri Serikali kama sisi tunavyofanya kwenye ngazi ya Serikali ya Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Serikali hizi mbili kuwa na mamlaka za ukusanyaji wa kodi ni kutekeleza mamlaka ya Kikatiba kwa upande wa Zanzibar na mamlaka ya Kikatiba kwa upande wa Tanzania Bara, maana nao watahitaji kuwa na fedha za kuendesha Serikali ya Zanzibar na katika ngazi ya Muungano tunahitaji kuwa na chanzo cha mapato. Kwa hiyo, nataka niliweke hili bayana ili lisilete mkanganyiko kwa sababu, Katiba zetu zinasema hivyo na mimi siji hapa kuleta tafsiri ya Katiba yoyote katika hizo, nashukuru.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Asya unapokea hiyo taarifa?

MHE. ASYA MWADINI MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, sipokei.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia mchango wangu, nimezungumza utalii wa ndege ndogondogo ambao unafanywa ndani ya Tanzania kwa wawekezaji wetu na ni lazima tuondoshe kodi ili tuweze kuweka mazingira bora. Wenzetu Kenya wameitoa hii VAT kwa hiyo, wawekezaji hawataweza kuja hapa watakwenda Kenya ili waweze kuwekeza vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie kwenye suala zima ambalo mwenzangu, kaka yangu Mheshimiwa Mtenga alilizungumza, kuhusu mikopo ya wafanyabiashara wetu ambao wako nchini na watu wa benki, imekuwa ni changamoto kubwa. Watu wetu wanajaribu kujipambanua kibiashara, ukiangalia wafanyabiashara walio wengi wamepoteza maisha, wengine wame-paralyze, wengine wamepata matatizo mbalimbali wanashindwa kusomesha watoto wao ni kwa sababu ya benki hizi. Wanachukua mikopo, wanakubaliana, kabla ya kumaliza kulipa mikopo labda mtu amepata changamoto ya biashara, benki hazina simile ya kuwastahamilia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu nishauri Wizara ikae na watu wa benki wapitie tena kanuni na taratibu na sheria za benki, ili tuwanusuru wafanyabiashara wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)