Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Ignas Aloyce Malocha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nikushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuungana na wenzangu katika kuchangia Wizara hii. Kabla ya yote niungane na wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Nishati, ndugu yangu Profesa Muhongo, Naibu Waziri na Katibu wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi hizi siyo za unafiki, zinadhihirisha uwezo alionao, hasa kwa sisi ambao tulikuwamo katika awamu ile ya kwanza na awamu hii, tulikuwa tunamlilia arudi aokoe jahazi juu ya Wizara hii. Mwenyezi Mungu ameturudishia, ni haki yake kuwepo hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi sote tunatambua umuhimu wa nyenzo muhimu hii ya umeme kwamba, umeme ni nyenzo muhimu katika maendeleo. Umeme unaongeza uchumi, unaongeza ajira, unaboresha huduma mbalimbali, ni chanzo muhimu cha uchumi katika njia zote za uchumi; bila umeme hakuna viwanda, hakuna maendeleo, hakuna ustaarabu! Hivyo ni wajibu wa Serikali kuhakikisha umeme huo unamfikia kila Mtanzania mahali popote alipo, ili aweze kufaidika na kupata huduma zinazostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa masikitiko yangu makubwa kwa upande wa umeme wa REA. Tumekuwa na REA I, REA II na sasa hivi tunakwenda REA III, lakini ni jambo la ajabu sana Wilaya yangu ya Sumbawanga pamoja na ukubwa wote vijiji karibu 150, watu zaidi ya laki nne na nusu, hakuna hata kijiji kimoja chenye umeme! Sasa Mheshimiwa Waziri, kama wewe ndiy ungekuwa Mbunge, sijui ungejisikiaje na wananchi wako wangekuelewaje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka kwanza mwelewe kwamba, wilaya yangu ina kanda mbili, kanda ya kwanza iko Ufipa Juu, unaanzia Sumbawanga kwenda Tunduma na ukanda wa pili unaanzia Stalike, kule tunapakana na Mheshimiwa Lupembe, mpaka huku tunapakana na ndugu yangu, Mheshimiwa Silinde. Sasa nianze na ukanda wa juu. Ukanda wa juu zipo kata 13 ambazo zinatakiwa kupitisha umeme, nimeona nitaje kata maana nikitaja vijiji ni vingi mno.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Kata ya Msandamungano, Sandulula, Jangwani, Mpwapwa, Kaengesa, Kanda, Lyangalile, Mpui, Ikozi, Kalambanzite, Lusaka, Laela, Kasanzama, Myakula, Mlangalua; hizi ni kata za Ukanda wa Ufipa juu, lakini zipo Kata za Ukanda wa Ziwa Rukwa, maana kata yangu ina maeneo mawili tofauti, ndiyo maana mara nyingi nimekuwa nikilalamika jiografia ya hii Kata! Ukanda wa Ziwa Rukwa tunazo Kata 13 ambazo zina vijiji vingi; hakuna hata kata moja iliyopata umeme, ambayo ni Muze, Mto Wiza, Milepa, Ilemba, Kapenta, Kaoze, Kilya, Jamatundu, Kilangawana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya maeneo ni makubwa. Ninapotaja hizi kata, nataja kwa sababu ni kata, lakini maeneo mengine kata moja inaweza ikagawanyika kuwa kata tatu kwa ukubwa wa kata jinsi ulivyo, lakini unashangaa ni vigezo gani vinatumika kutopeleka umeme katika maeneo haya! Sijajua kwa nini Serikali, mara nyingi, imekuwa ikifanya Wilaya ya Sumbawanga Vijijini kuwa ni ya mwisho katika kupeleka huduma mbalimbali! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata suala la barabara tumekuwa karibu wa mwisho kuletewa barabara, sijui mlishatazama namna gani; kwa maana hiyo, lazima Waziri anieleze sababu za msingi za kutofikisha umeme katika maeneo hayo. Tena eneo hilo la ukanda wa chini ni eneo lenye uchumi mkubwa, jamani umeme unahitajika! Watu wa kule wana uchumi mkubwa, yapo maeneo mnapeleka umeme, nguzo zimesimama, watu hawataki kuingiza ndani ya nyumba kwa sababu hawana fedha! Sasa mnapeleka tu kama formality wakati umeme unatakiwa kujizungusha urudishe pesa! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa maeneo ninayosema haya ni maeneo ya watu wenye uchumi mzuri, ukipeleka umeme wataingiza umeme kwenye nyumba zao, wataufanyia shughuli za maendeleo, wataongeza uchumi wao, wataongeza uchumi wa Taifa; kwa nini hamtaki kufanya hivyo? Nataka unapokuja hapa unipe vigezo vinavyokufanya usipeleke umeme katika maeneo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie umeme tunaoutumia Mkoa wa Rukwa. Mkoa wa Rukwa wote tunatumia karibu megawatts tano kwa mkoa mzima na umeme huo mwingine tunaupata kutoka Zambia na mwingine unakuwa ni umeme wa generator. Ninachotaka kusema, tunavyo vyanzo vingi vya kuweza kuongeza umeme katika Mkoa wetu wa Rukwa. Kwa mfano, nikitaja umeme unaotokana na maji, Mto Nzovwe una maporomoko makubwa na ulishafanyiwa utafiti kwamba, unaweza kutoa megawatts nane ambazo zikiongezeka katika Mkoa wa Rukwa unaweza ukawa na megawatts nyingi zinazoweza kusambazwa na viwanda vikaweza kutekelezeka vizuri zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashangaa ni kwa nini hawataki kuutumia mto huo ambao ulishafanyiwa utafiti na haukauki na bahati nzuri Mkoa wetu wa Rukwa ni karibu kila mwaka una mvua. Kwa nini wasitumie maporomoko hayo ambayo yameshafanyiwa utafiti wa kutoa megawatts nane! Kwa hiyo, nataka Mheshimiwa Waziri aje anieleze, ni kwa nini hawataki kutumia njia nyingine ya kupata umeme katika Mkoa wetu wa Rukwa ambao gharama yake inakuwa ni ndogo kuliko hata umeme wa generator? Sijui wataalam wetu, nashindwa hata kuwaelewa! Tatizo hili ni kutozunguka, kutotembea! Yapo maeneo mlishayatenga, mnarudia rudia, maeneo mengine hamtaki kwenda! Mnazunguka, mnarudia maeneo yale yale! Sijui ni kwanini? Sisi sote ni Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninalotaka kuzungumzia ni juu ya utafiti. Lazima nchi yetu ijielekeze kwenye utafiti katika mambo mbalimbali kwa sababu, yapo maeneo mengi yana rasirimali, lakini nchi hii haijagundua! Ndiyo maana hata juzi nimekuja kugundua Mtwara mmegundua gesi, mmegundua mafuta, lakini rasilimali hizo zipo maeneo mengi ila hamjaweka upendeleo wa kufanya utafiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka pia kuzungumzia juu ya Ziwa Rukwa. Ziwa Rukwa halina tofauti na Ziwa Albert la Uganda, jiografia ni ile ile na bahati nzuri nimeshafika, lakini nataka anieleze ni utafiti gani umeshafanyika wa Ziwa Rukwa ili kuangalia kuna kitu gani na mkishajua maana yake mtaweza kulitunza. Ndiyo maana mmelitelekeza, hamna habari nalo, suala la mazingira hamna habari, lakini naamini upo uchumi mkubwa katika eneo lile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumzia suala lingine la utafiti, kuna shamba ambalo nimekuwa nikizungumzia mara kwa mara, Shamba la Malonje. Yule Mtaalam wa Kenya alilizungukia lile shamba akasema, lile shamba, 1/8 ya lile shamba lina madini ya kopa, lakini watafiti wetu hawajakwenda kuangalia ni kitu gani kinafanyika! Matokeo yake mwekezaji akija anang‟ang‟ania kwa sababu, anajua pale kuna faida kwa baadaye. Kwa nini, watafiti hamtaki kufanya kazi inayostahili, ili kuweza kuboresha nchi yetu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nataka tu kusisitiza kwamba, Mheshimiwa Waziri sisi sote tunafahamu uwezo wake na msukumo wake. Siwezi kuunga mkono kwa sababu, wananchi watanishangaa! Huna umeme hata kijiji kimoja, vijiji 150, halafu leo hii unasema unaunga mkono, watakushangaa! Mpaka nipate maelezo ya Mheshimiwa ndipo naweza kuunga mkono hoja, lakini kwa sasa siwezi kuunga mkono hoja wananchi watanishangaa, kwanza ni aibu kubwa, ni aibu kubwa!
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nasisitiza Mheshimiwa Waziri anieleze ni kwa namna gani atapeleka umeme katika Wilaya ya Sumbawanga Vijijini? Mkija Sumbawanga Mjini mnadhani ndio Sumbawanga Vijijini, hata Kijiji kimoja! Ni aibu kubwa sana.