Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kunipa nafasi na mimi kuchangia bajeti hii ya Seikali. Nianze kuipongeza Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi inayoongozwa na Mama yetu Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri sana anazozifanya. Nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kutuletea bajeti hii, bajeti ambayo imekonga mioyo ya Watanzania wote. Pia nimpongeze Waziri, Naibu Waziri na Watendaji wake wote wa Wizara ya Fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa mikopo ya halmashauri; mikopo hii ya halmashauri imekuwa ikiwajenga sana akina mama kiuchumi. Akina mama wengi wamechukua mikopo hii na wanalea familia zao na wanasomesha watoto Tanzania nzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi wanawake ambao tupo hapa Bungeni ni wawakilishi wanawake wenzetu, tumekuja ili tuwasaidie na wenyewe waweze kunyanyuka kiuchumi. Mikopo hii ya 4:4:2 wanawake asilimia nne, vijana asilimia nne na wenye ulemavu asilimia mbili bado imekuwa haitoshi, kwa sababu wanawake wengi wanaopata hii mikopo wanafanya biashara na wanapofanya biashara wakirudisha ile mikopo unakuta vikundi vingi vimejiunga na bado fedha haitoshelezi. Niiombe Serikali iache mikopo hii utaratibu huu wa 4:4:2 na wamachinga Serikali kuu iwatafutie fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kutoka katika mchango wangu wa kwanza nije katika sekta ya uvuvi; nitaomba kuchangia Ziwa Jipe. Ziwa Jipe lipo katika Mkoa wa Kilimanjaro katika Wilaya ya Mwanga. Naongea kwa masikitiko makubwa sana, na Wabunge wenzangu nawaomba mtusaidie katika ziwa hili. Ziwa Jipe lipo katikati ya mpaka wa Kenya na Tanzania, lakini Ziwa Jipe limekuwa na magugu kiasi kwamba shughuli zote za uvuvi pale hakuna tena.
Mheshimiwa Naibu Spika, ikumbukwe kwamba chanzo cha maji cha Ziwa Jipe kinatoka katika Mkoa wa Kilimanjaro, lakini wenzetu upande wa pili wametengeneza mazingira mazuri, wametengeneza miundombinu ya utalii wana hoteli za utalii, wanafaidika kupitia chanzo chetu cha maji ambacho kinatoka Mkoa wa Kilimanjaro. Lakini kwetu sisi magugu maji yamezidi kiasi kwamba hata wakazi wa pale hata kuvua samaki wameshindwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, walishafika viongozi wa mazingira akiwemo Mheshimiwa Waziri Makamba na Mheshimiwa Waziri Chande, wamefanya vikao na Vijiji vya Butu ambavyo vimezunguka Ziwa lile la Jipe. Lakini wamewapa wananchi matumaini, kwa sababu wananchi wanapoona viongozi wa juu wakija wanapata matumaini kwamba angalau tumesikilizwa shida yetu itatekelezwa. Hivi ninavyoongea wale Wapare hata Samaki kwa ajili ya chakula hawawezi kuvua
Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Serikali iangalie kwa kina sana na ifanye haraka iwezekanavyo kutoa yale magugu kwa kuwa Ziwa lile la Jipe ndilo linaloshisha Bwawa la Nyumba ya Mungu. Bwawa la Nyumba ya Mungu linazalisha umeme megawatt tano mpaka nane; lakini bwawa lile sasa hivi pia kutokana na yale magugu ambayo maji yanashindwa kupita vizuri maji yake yanaenda yakipungua.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni hivi karibu tu Mheshimiwa Rais alipitisha kwamba, mradi wa maji unaokwenda kuanzia Same, Mwanga, Korogwe umetengewa fedha. Sasa fedha hizo zimetengwa, mradi huo wa maji unategemea maji hayo ambayo yanatoka katika Ziwa Jipe. Niiombe Serikali itusikilize sana kilio hiki na niombe Waziri atakapokuja ku-windup atueleze ni lini lile Ziwa Jipe litatolewa magugu, Wapare wamechoka, wanashida hata Samaki kwa ajili ya chakula hawapati.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja.