Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Muleba Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia fursa ya kuchangia Mapendekezo ya Mpango, lakini na Mwongozo wa kutengeneza Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2024/2025.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kiasi kikubwa nakubaliana na Hotuba ya Waziri mwenye dhamana ya Mipango na Uwekezaji. Nakubaliana na maelezo ya Waziri wa Fedha kwa mwongozo alioutoa, tunapotengeneza mpango na tunapotengeneza bajeti. Nina imani kwamba tukifuatilia tutaweza kutoka na mpango mzuri na bajeti nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapoanza kuzungumza, naipongeza Kamati ya Bajeti ya Bunge letu, kwa uchambuzi waliofanya katika maandiko haya mawili. Wametoka na maeneo ambayo tukijumlisha na michango yetu sisi, tutaweza kutoka na mchango mzuri. Jambo la kwanza, katika uchambuzi wa kazi ya Waziri wa Fedha lakini hata kwenye wasilisho la Waziri, nachukua fursa hii kipekee kuwapongeza wakulima wa Tanzania tena wakulima wadogo, kutokana na kwamba kazi yao imeweza kuzalisha chakula, tukawa na chakula cha kutosha uwezo wa asilimia 124, tani milioni 20. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapowapongeza wakulima, sifa zimwendee Mtumishi Mwandamizi lakini ambaye hastahili kupokea sadaka au kuungamisha watu, Msimamizi wa Sekta ya Kilimo na kiongozi wetu mkuu Mheshimiwa Rais ambaye ndiye anampa maelekezo. Mimi ni mmoja ya wakulima ambao tumefaidika na jitihada za Serikali yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na mchango wa Kamati yako unayoiongoza, nizungumze kidogo juu ya urari wa biashara ya bidhaa. Naenda kwenye nini kifanyike. Kupita kwenye historia yetu, tulikuwa na re-export, e-export ya nchi hii imepungua. Dawa nyingine ni kukimbilia re-export. Sina muda wa kulielezea, lakini Wizara ya Fedha na TRA, wapitie mjiulize, ni kwa nini re-export ilianguka? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa tunafanya re-export wakati ule ilipoanguka. Jiulize, kwa nini Kariakoo ilikufa Dar es Salaam lakini ikazaliwa Kariakoo Kampala, ikazaliwa Kariakoo Zambia? Vitenge vinanunuliwa kutoka vitokako, vinakwenda Zambia vinarudi Dar es Salaam. Re-export, re-export. Tunapokuja kuwa na bandari yenye ufanisi, kama tusipokuwa na re-export Policy, tusipoitengeneza Dar es Salaam au Pwani yenye Kariakoo mpya ambako nchi zilizotuzunguka watu watakuja kwa wingi Dar es Salaam na kufanya biashara hapa. Faida tunayoitegemea kwenye Bandari ya Dar es Salaam yenye ufanisi, itakuwa ndogo sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Waziri wa Mipango kwa kusisitiza jambo lililokuwepo ambalo lilikuwa halionekani. Kuchochea na kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii vijijini. Serikali imekuwa ikijitahidi kufanya maisha ya vijijini yawe mazuri, yaani maisha ya vijijini sasa yanapendeka na unaweza kuishi. Sasa, Waziri anakuja na jipya kwamba, tuchochee zaidi na anakwenda kwa kuelezea kwamba, tuanzishe utaratibu wa viwanda vijijini, amekuja na falsafa ya SIDO.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kuishauri Serikali, hii inawezekana na yenyewe itatusaidia kwenye urari wa biashara ya bidhaa, kwamba watu wazalishe kule. Hii itaendana na lile tatizo linalotusumbua la kuwepo kwa pesa za mikopo na watu wasiweze kukopa. Kumbe unapotaka kuipeleka SIDO kule vijijini karibu na wananchi, tofauti na taasisi zingine SIDO inafundisha. Mfuko wa Pesa wa NEDF ulioko chini ya Wizara ya Viwanda na SIDO, hawakupi pesa mpaka wakufundishe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa watu wengine wanatoa pesa hata hawamwambii mtu ni pesa ya kufanyia nini. Unampa mtu pesa atengeneze kiwanda, kumbe kiwanda anachokifikiria ni kwenda kulipa mahari. Sasa, unapokuja kukusanya huwezi kukusanya hiyo pesa. Namuunga mkono Mheshimiwa Waziri, haya mawazo yake yafanyiwe kazi kweli. Mimi ni muumini wa viwanda vidogo, ujenzi wa viwanda kwa kutoka viwanda vidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama wanavyo zungumza leo Mheshimiwa Waziri wa kilimo anajua, tunayo mafuta mengi ya alizeti lakini kitu ambacho watu hawakijui ni kwamba mafuta ya alizeti ni royal product, yanatumiwa na watu wenye uwezo wa hali ya juu, nimemweleza Mheshimiwa Waziri, nimpeleke Ulaya nimuoneshe wanaokula yale mafuta. Kwa hiyo, tupeleke mafuta hayo tuuze tupate pesa nyingi ili tuzalishe zaidi. Kwa hiyo, naunga mkono wazo hilo.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipongeza Kamati yako, kuhusu suala la riba, mmehoji kwa nini riba hizi hazishuki. Bahati nzuri nimemuona Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya NMB. Benki zinapata faida kubwa, kupata faida kubwa siyo sifa, mimi nilikuwa nafanya kazi huko ‘Utashani’ nilitaka kufukuzwa kazi kwa sababu nilikuwa napata faida kubwa. Anakwambia no unawaonea wateja hiyo riba ipunguzwe na watu wafundishwe, wakifundishwa waweze kukopa, wakikopa waweze kuzalisha ili wachangamshe uchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, faida yake ni kwamba itaweza kutusaidia kutengeneza shughuli ambayo, shughuli zitatengeneza ajira, ajira hizo zitazalisha bidhaa na zitatuepusha katika kuagiza bidhaa ambazo hazina maana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la urali, umezungumza matumizi ya gesi asilia, matumizi ya gesi asilia kutuokoa haiwezi kuwa mchakato. Mimi nilikuwa Marketing Manager wa mambo haya mnayozungumza mwaka 2000, ni miaka zaidi ya 24 tunataka radical change, tunataka reform, tuanze leo, tunataka mpango unapokuja utamke kwamba magari mangapi ya Serikali Dar es Salaam mpaka Dodoma yanaanza kutumia gesi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeongea leo na mtaalam wa gesi, akaniambia gesi inayotakiwa kwa magari yote ya Tanzania ni kiasi kidogo wanayo. Akanihakikishia kwamba tunayo gas ya kutosha, sasa walk the talk rafiki yangu, litoke tamko magari yote yabadilike. Ukisikia mambo ya gas haya yatakuchanganya, wanakuambia gas ni nafuu, mafuta ni aghali. Sasa kama gas ni nafuu na mafuta ni ghali, kwa nini mnaagiza mafuta ambayo ni aghali mnakataa kutumia gas ambayo mnayo ninyi wenyewe, walk the talk! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka mpango ambao utakuja unatuambia kesho magari yote yawe converted na TRA mvumilie kama vifaa vya gas vyote vinaushuru samehe ushuru kwa kipindi fulani tuweke hizo petrol station za gas, tuweke converter, tu-convert magari halafu watu waende mtaani tupunguze nakisi. Mafuta hayana mbadala, mbadala wake ni kuweza kutumia gas, lakini matumizi ya gas katika usafirishaji ni kinga la tatizo la ugawaji wa mafuta kama ikitokea majanga huko mbali, kama ikitokea matatizo huko yanapotoka wewe una gas yako utatembea wakati wenzako wanatembelea magoti wewe utaendesha vifaa vyako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine nataka kukiona, nimeusoma mpango siyo kwa ndani, ningependa msitumie vilinganisho vya asilimia..
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, mtoe takwimu baadala ya vilinganisho vya asilimia.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Charles Mwijage, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Askofu Gwajima.
TAARIFA
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumpa taarifa Kaka yangu mtaalam wa biashara, maneno anayosema siyo yake lakini maneno anayosema amevuviwa na Mungu. Kule Jimbo la Kawe TPDC kampuni mojawapo yetu ya taasisi ya energy, wameanza kuweka cable kwenye nyumba za watu wakitumia gas. Tumepita sisi mguu kwa mguu, mtu aliyekuwa analipa bili ya shilingi 20,000 kwa mwezi analipa shilingi 3,000. Sasa kwa nini tusichukue maamuzi ya kutumia gas. Kwa hiyo, mtaalam wa biashara yupo sahihi kabisa. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante sana. Mheshimiwa Mwijage taarifa unaipokea?
MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Baba Askofu amesema hili nimepewa na Mwenyezi Mungu na mimi Frateri wa kudumu sistahili wala kubisha, nakubali huo upako. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kidogo. Moja; nimeomba wataalam wa Serikali msituletee ulinganisho wa asilimia kama ni tanzi sema tanzi, kama ni urefu sema kilomita. Hizi asilimia zina udanganyifu, unaweza kuwa na asilimia ndogo lakini wewe ni mkubwa. Mtuambie mpango uje unatamka, lakini tuchague maeneo mahsusi. Kwa mfano, upande wa ufugaji wa Samaki, tunayo potential ya kufuga samaki hapa, Tanzania leo tunafuga samaki tani 18,000, Uganda wanafuga 120,000, Egypt wapo milioni 1.2 na wanakwenda milioni mbili. Quantify hiki kitu Serikali muwape watu task, kama ulivyosema Mheshimiwa Waziri, unataka watu wenye weledi umkabidhi mtu kwamba wewe shughuli yako ni uvuvi na ufugaji wa samaki, tunataka bilioni kadhaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huyo mtu tumuwajibishe asubuhi au saa sita akishindwa. Haya mambo ya holela holela unatoka unakwenda huku, unasubiri Mheshimiwa Waziri apende nini, ukimuuliza mtaalam wa Serikali, anasema maelekezo. Ni mtaalam kweli lakini hawezi kukwambia chochote anasubiri maelekezo. Tafuta taasisi uwakabidhi vijana kazi washindwe waache kazi. Naunga mkono, kazi ni nzuri, mengine nitawasilisha kwa maandishi. (Makofi)