Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Festo Richard Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupewa nafasi niweze kuchangia kwenye Mpango wa Serikali. Kwanza ninaipongeza Serikali, kwa mapendekezo waliyonayo kwenda kwenye bajeti ijayo ya trilioni 47 na katika hizo shilingi trilioni 47 Serikali imetoka kwenye trilioni 14 za maendeleo kwa sasa imeenda kutenga trilioni 15 kwa ajili ya maendeleo. Kwa hiyo niipongeze Serikali kwamba inaenda kuongeza zaidi ya shilingi trilioni moja kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inaonesha kabisa dhamira ya Mheshimiwa Rais ipo wazi kwenye kuhakikisha kwamba miradi ya maendeleo haisimami kwenye nchi yetu na inaweza kutekelezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nijikite kwenye suala la financing ya Mpango wenyewe, kwenye Kamati wamezungumzia hata Serikali imezungumzia kwenye financing ya mpango wenyewe. Tuna Mpango mzuri sana lakini ku-finance Mpango wenyewe inatakiwa tufanye nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi najikita kwenye mambo matatu. Nitajikita kwenye kodi, mifumo lakini nitazungumzia suala la utalii kwa maana ya Sekta ya Utalii. Ukisoma kwenye Mpango, Mheshimiwa Waziri anazungumza kwamba moja kati ya changamoto ya Serikali ya ukusanyaji wa mapato ni wigo mdogo wa vyanzo vya mapato. Ukienda kwenye mifumo mingi ya Serikali na ambayo tunategemea ndiyo source ya ukusanyaji wa mapato, kumekuwa na changamoto kubwa ya mifumo kusuasua, lakini pili kumekuwa na changamoto kubwa ya mifumo kutokusomana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali yetu inakusanya mapato lakini mapato yanayokusanywa ni theluthi ndogo tu kuliko mapato mengi zaidi ambayo yangekusanywa kwa ajili ya ku-finance mipango na miradi yetu ya maendeleo. Changamoto hii naweza nikatolea mfano, kwenye mfumo mmoja tu ambao umefungwa kwenye Daraja la Kigamboni, Daraja la Kigamboni wamefunga mfumo wa ukusanyaji wa mapato, kabla ya ukusanyaji wa mapato kupitia mfumo, daraja la Kigamboni lilikuwa linaingiza Shilingi milioni 150, 200 hadi 300, baada ya kuweka mfumo Daraja la Kigamboni la Mwalimu Nyerere pale linaingiza Shilingi bilioni moja na milionii 300 kwa mwezi. Hii inamaanisha nini? Watu wengi wanakwepa mifumo Serikalini kwa sababu inawabana na wizi ambao wanaufanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakupa mfano mwingine, hospitali ya Kibaha pale Tumbi. Kabla haijafunga mfumo kwa mwezi walikuwa wanaingiza shilingi milioni 13, 12, baada ya Serikali kwenda kufunga mfumo wanaingiza shilingi milioni 350, 400 kwa mwezi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inatafsiri ya magnitude kubwa iliyopo kati ya wizi na ukwepaji wa kwenye mifumo. Ukienda kwenye Wizara ya Ardhi, hapa tukiondoka tukienda pale TAMISEMI au kwenye Wizara ya Ardhi hapo, mfumo sasa hivi utakuta upo chini. Ukienda kwenye afya hospitalini kuna wagonjwa inawezekana wanatusikiliza sasa hivi wapo kwenye foleni mfumo upo chini. Ukienda TRA mifumo ipo chini, lakini hatujawahi kuona hata siku moja mfumo wa ulipaji mishahara ukiwa chini hata siku moja kwenye Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inatupa alarm kwamba siyo kwamba mifumo ina changamoto, changamoto ipo na watu wanaoitumia hiyo mifumo, kwa sababu wanatumia mifumo hiyo kama njia ya wizi. Ndiyo maana CAG anasema wana uwezo wa kuzima POS kwa siku elfu moja na Serikali isifanye kitu! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi mapendekezo yangu kwa Serikali, tuiiombe ione dhamira ya wazi kwanza ya kufanya mifumo isomane, kilio cha Mheshimiwa Rais kwa muda mrefu ilikuwa ni hicho, hasa hasa pale bandarini na maeneo mengine. Pili, kuhakikisha mifumo hii inafanyakazi, kwa sababu tunaweza tukafunga mifumo lakini isifanye kazi. Hilo ni pendekezo langu kwenye suala la mifumo, nikiiomba Serikali, hatuna sababu ya kuruhusu watu waendelee kukutana face to face, kukutana kwa watu face to face kwenye suala la payment kunasababisha majadiliano na rushwa, Serikali inaenda kupoteza fedha nyingi kwa sababu watu wanajadiliana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tukifunga mifumo kwenye maeneo mengi kutatusaidia sana kwenye kusimamia fedha na kukusanya mapato mengi ili Mheshimiwa Mwigulu na Mheshimiwa Waziri wa uwekezaji tuweze…

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Festo Sanga, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Kingu.

TAARIFA

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa mchangiaji Kaka yangu Festo, Mbunge makini kabisa. Hospitali ya Taifa ya Bugando kabla ya kufungiwa mifumo ilikuwa inakusanya shilingi milioni 800 baada ya kufungiwa mfumo wanakusanya shilingi bilioni 3.5. Mifumo hii imefungwa na kampuni ya vijana wa Kitanzania wazalendo, Mheshimiwa Ummy Waziri wa Afya ni shahidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya KCMC kabla ya kufungiwa mifumo ilikuwa inakusanya only shilingi milioni 300, 400 na baada ya kufungiwa mfumo wanakusanya mpaka 1.5 billion. Hospitali ya Amana ya Serikali, haya nayasema Mheshimiwa Waziri wa Afya yupo hapa kama nasema uwongo atasimama kunikanusha. Kabla ya mifumo walikuwa wanakusanya milioni tisa, leo tunazungumza baada ya kufungiwa mifumo tena mifumo imebuniwa na vijana wazalendo wa Kitanzania, wapo hapa lakini bado kigugumizi pia cha kuwatumia vijana hawa ni kikubwa. Kwa hiyo, nakubaliana na Mheshimiwa Festo, kwamba watu wanakataa mifumo kwa sababu ya corruption na wizi wa fedha za Serikali. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Festo Sanga, taarifa hiyo unaipokea?

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipokea taarifa hii kwa sababu ninatambua anachokizungumza ni sawasawa na kile ambacho nilikuwa nakizungumza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii ukienda Morogoro kituo cha mabasi wana zaidi ya miaka mitatu wanahangaika kuvutana kwenye Baraza la Madiwani jinsi ya kufunga mfumo, kwa sababu pale junction ya mabasi mengi lakini watu hawataki, wanataka waendelee kutumia cash, fedha mbichi kuliko kutumia mifumo. Kwa hiyo ni kweli Serikali inachangamoto ya ufungaji wa mifumo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la ulipaji wa kodi. Serikali, kwanza lazima tutambue wafanya biashara nchini ni sekta binafsi, Serikali haifanyi biashara. Kama mtu anafanya sekta binafsi, kuna siku anaweza akaamua aamke aende ofisini au asiamke kwenda ofisini. Kwa hiyo, unapoenda kudai kodi lazima tuwe na lugha ya customer care, lugha nzuri, lugha yenye kumshawishi mtu alipe kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwigulu, kwenye kitabu chake cha bajeti anasema; “Mheshimiwa Spika, katika kutatua kero hizo napendekeza kuanza matumizi ya mfumo wa pamoja wa ukusanyaji wa ada, tozo na adhabu za taasisi, udhibiti, ‘single window payment system na taasisi za udhibiti kuweka utaratibu mzuri wa ukaguzi ambao hautasababisha usumbufu kwa wafanyabiashara bila kuathiri majukumu ya msingi ya taasisi hizo napendekeza hatua hizo zianze kufanyika mwaka 2023/2024”. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sisi ambao Mheshimiwa Mwigulu, tunakufahamu hili limekuwa ni moja kati ya maono yako ya muda mrefu. Leo Mheshimiwa Mwigulu, ukienda kwa mfanyabiashara, watu wa leseni asubuhi wameingia dukani, watu wa OSHA asubuhi wameingia dukani, watu wa fire asubuhi wameingia dukani, watu wa TRA asubuhi wameingia dukani, watu wa service levy asubuhi wameingia dukani! Hatuwezi kuwa na Taifa la walipa kodi wa aina hiyo ambao wanafanya kazi ya kupokea wataalam wa Serikali kila asubuhi kuliko kupokea wateja wanaokuja kununua bidhaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mipango ya Serikali lazima iwe ni jinsi gani ya kuisaidia sekta binafsi ya wafanyabiashara ifanye biashara katika mazingira mazuri. Kuliko hiki cha kuruhusu asubuhi watu wanaacha kazi maofisini wanapanga foleni kwenye maduka ya watu, kiasi kwamba kuna Watanzania wengi wamekufa mioyo kufungua maduka kwa sababu ya mifumo hii ya ufanyaji biashara. Ndiyo maana mataifa yanayotuzunguka Zambia, wameweka mazingira mazuri, watu wanakimbilia Zambia. Mheshimiwa Waziri wa Fedha, ili upate kodi kwa Watanzania tengeneza kwanza wafanya biashara wawe marafiki wa TRA, fanya reformation kule TRA, reform TRA yote jinsi gani inavyo-operate na wafanya biashara. Tatu, kwa nini leo mfanyabiashara ukienda kununua mzigo anakwambia mimi nakukatia risiti ya shilingi milioni moja, huu mzigo wa Shilingi milioni 10 sitaki kukukatia risiti ya shilingi milioni 10, kwa nini wanakwepa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tuende far kwa wataalam wetu kufikiria kwanini wafanya biashara hawopo tayari kukatia risiti ya milioni 10, wapo tayari kudanganya watoe risiti ya milioni moja. Wafanyabiashara lazima wataalam wetu wawaze mbali ili kuweza kukusanya hizo fedha za ku-finance huu mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, dakika zangu zisije zikaisha niende kwenye Sekta ya Utalii. Mheshimiwa Rais, juzi alizungumza kuhusu utalii. Kwanza ni support kwamba utalii wetu unaongezeka, unakua kutokana na jinsi ambavyo Mheshimiwa Rais, aliondoa mguu wake ofisini na akaenda site kwenda kutengeneza The Royal Tour, ambayo leo kila mmoja na Wizara inajinasibu kwamba utalii umekua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu linabaki kwenye sekta hii, utalii kwa asilimia 90 inafanya kazi sekta binafsi. Mtalii akishuka Airport anakutana na dereva, mtalii akienda site kwa maana kwenye hifadhi atakutana na dereva na tour guides. Leo hii wizara inampango gani wa kukutana na drivers, kukutana na tour guides kukutana na hao wote ambao ni mnyororo wa thamani kwenye utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtalii anayetoka nje akija Tanzania ana uwezo wa kutumia masaa arobaini, katika masaa arobaini, masaa thelathini anakuwa kati ya yeye na dereva au na tour guides. Tour guides tumewapa level gani ya ubalozi wa kuelimisha kuhusu utalii? Kumekuwa na changamoto kubwa sana kwenye sekta hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeomba dakika mbili nimalizie. Ukija kwenye suala lingine, Mheshimiwa Rais amezungumza, Serikali inatakiwa iwe na mpango, kuna changamoto ya malazi kwenye sekta yetu ya utalii, malazi imekuwa ni changamoto ya watu kwa kulala. Ukienda Serikali ilishawahi kuwa na lodge na hoteli 23, leo hii nataka nikuambie katika mchakato ambao Serikali inaufanya, hoteli hizo zimekufa, hoteli hizo hazifanyi kazi. Nakupa tu mfano mmoja hapa nazungumza. Mfano katikati ya Jiji la Dar es Salaam, premium area kuna hoteli inaitwa Embassy Hotel, kwa muda wa miaka 14 haieleweki ni ya Serikali, haieleweki ni ya uwekezaji, lakini Taifa letu linachangamoto kubwa ya kutokuwa na hoteli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hoteli ya Ngorongoro, kuna hoteli ya Seronera Wildlife, Lobo Wildlife, TRA wanasema hawajui hizi hoteli zinamilikiwa na nani. Mheshimiwa Rais, anazungumza kwamba Taifa letu lina changamoto ya maeneo ya malazi, lakini hoteli hizi ni za Serikali zipo kwenye potential area, kuna haja ya Serikali kuwa na mpango mahsusi kuufanya utalii ukue, kuufanya utalii uonekane. Tunazungukwa na Rwanda na Mataifa mengine yanafanya vizuri, hata juzi tulijiuliza tupo kwenye kufungua michuano ya kimataifa ndani la Taifa letu ambalo tunajinasibu kutangaza utalii lakini tunatangaza visit nchi nyingine wakati sisi tulikuwa na uwezo wa kufanya matukio makubwa kwa ajili ya Taifa hili. Ahsante. (Makofi)