Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Mohamed Lujuo Monni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chemba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa na mimi ya kuchangia jambo hili muhimu sana lililopo mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mola ambaye ametujalia afya njema, uhai, na leo tuko hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, naomba nimshukuru kipekee kabisa Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo amekuwa akileta fedha nyingi kwenye majimbo yetu. Nawashukuru na wawasilishaji, Mheshimiwa Mwigulu na Mheshimiwa Prof. Kitila, kwa namna ambavyo wameleta wasilisho zuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kujadili huu mpango ulioko sasa hivi, naomba na mimi niseme maneno machache kama alivyosema Mheshimiwa mwenzangu aliyepita. Ni vizuri tunapoleta mpango hapa tukaangalia umefanikiwa kiasi gani, lakini pia tuangalie takwimu ambazo zinaletwa kwenye hii mipango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwenye takwimu za maji wanasema upatikanaji wa maji mijini ni asilimia 88. Jambo hili katika logic sio sahihi, sisi wote tuko hapa mjini, Dodoma hapa tulipo tunapata maji siku tatu kwa wiki, siku tatu maana yake ni 3/7 x 100 = 42%, sasa kama Dodoma ni asilimia 42, wananchi wanapata maji siku tatu kwa wiki, tunawezaji kuandika takwimu asilimia 88. Haya mambo tuyaseme vizuri ili tukapange mipango ya kuhakikisha watu wanapata maji, hawa wataalam wetu sijui wanatumia maarifa gani katika ku-calculate haya mambo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiukweli Jimboni kwangu alisema siku moja hapa Mheshimiwa Condester, kwake ni asilimia 22 kwangu ni asilimia 33. Sasa tunaweka mipango ambayo haitekelezeki lakini kwenye makaratasi inaandikwa kwamba haya mambo ukiangalia wanataja visima ambavyo tayari vinatoa maji. Mwaka 2022/2023, 2021/2022 mimi nimepewa visima, nimepewa visima 11 mpaka leo vimechimbwa viwili, nimepewa visima vitano bajeti imepita havijawahi kuchimbwa, nimepewa mabwawa ambayo hayajawahi kuchimbwa. Halafu ukiangalia kwenye takwimu wanasema kwamba maji yanapatikana vijijini kwa asilimia 78.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi taarifa zinatuchonganisha na wananchi.

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mohamed Monni, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Naibu Waziri wa Maji, Mheshimiwa Maryprisca Mahundi.

TAARIFA

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi. Naomba nimpongeze anayechangia Mheshimiwa Monni, kwenye eneo la asilimia upatikanaji wa huduma ya maji. Wataalam wanakuletea zile percentage, wanaangalia ni coverage ya miundombinu pamoja na upatikanaji wa maji bombani. Kwa hiyo, suala la visima analoliongelea, visima vyote ambavyo vinaahidiwa tumeendelea kuchimba kadri tunavyopata fedha tunawafikia na yeye mwenyewe kwenye jimbo lake atakuwa shahidi amepata upendeleo mkubwa wa gari lile ambalo Mheshimiwa, Dkt. Samia, amenunua 25, sehemu ya kwanza kuchimba visima ilikuwa ni jimboni kwake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa aongee kile kitu ambacho anakifahamu kwa dhati, kama hiki kinamchanganya ni vyema asipotoshe umma lakini kama anahitaji maelezo zaidi kama anavyokuwa anakuja ofisini pale Wizarani, basi aje tuendelee kumuelewesha lakini sio kupotosha umma, ahsante.

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Mohamed Monni, taarifa hiyo unaipokea?

MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza siipokei taarifa yake, lakini anasikitisha sana halijawahi kuja gari hilo kuchimba maji na tena naomba niseme machache kuhusu haya magari yaliyoletwa. Wabunge ni mashahidi, magari yameletwa lakini hayafanyi kazi, bora wangempa mtu binafsi wamshirikishe yangeleta maji. Kila moa, leo walete takwimu zinazoonyesha magari ya UVIKO, yamechimba visima vingapi? Walete takwimu, kama yamechimba visima, yamechimba visima viwili, vitatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Dodoma kwanza sijawahi kupata hilo gari kuja kuchimba hayo maji na huo ndiyo ukweli maana yake Mheshimiwa Waziri, anadanganya na ananitengenezea taswira mbaya kwa wapigakura wangu. Ninachojua, kuna Mkandarasi amepewa kazi ya kuchimba visima 11, tangu mwaka jana gari limekaa pale kwa Mtoro, hawajampa fedha tangu mwaka jana lina miezi 11 mpaka leo. Halafu wale watu hawana maji wanaliona gari la kuchimba maji hili hapa, halafu nauliza nini kimetokea, naambiwa hawajapewa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sitaki kusema maneno mengi zaidi. Nikisema maneno mengi zaidi nitakuwa mahali fulani naumiza. Nataka niwahakikishie Wizara ya Maji, imekuwa inaletwa kuwa inapewa fedha kwa asilimia 96, kwenye bajeti hapo ilisema hayo maneno. Hizo fedha zinapelekwa wapi, maana yake zinapelekwa sehemu nyingine, jimboni kwangu haziletwi sio sahihi, sio kweli kwa sababu Jimboni kwangu visima 11 vya 2021/2022 havijachimbwa, vimechimbwa viwili. Visima vitano vya 2022/2023 mpaka leo havijachimbwa na muda umeisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mabwawa, Kidoka kulikuwa na bwawa la bilioni tatu, tumeweka bango mpaka leo tuna mradi kule Machija, mpaka Katibu Mkuu, amekuja bado hakuna kitu kilichoendelea, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, tuna mradi wa milioni 600 Chandama, mpaka leo Katibu Mkuu, amekuja tumempeleka, miradi yote haijakamilika, haiwezekani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nisimame hapa, wakati watu wangu wanajua hawapati maji, halafu niseme kwamba mipango hii inapangwa na inaenda vizuri, haiwezekani! (Makofi)

WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Monni, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Waziri wa Fedha.

TAARIFA

WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namuunga mkono Mheshimiwa Mbunge, kwa mchango wake anaochangia. Nataka nimpe taarifa na niwaombe na Waheshimiwa Wabunge wengine, kwamba wala hatuna haja ya kugombana isipokuwa hali ya masuala ya maji imebadilika sana kutokana na mabadiliko ya tabianchi. Kwa maana hiyo fedha tumetoa, wakati tuko kwenye bajeti tulitoa bilioni 104 kwenda tu Wizara ya Maji na hizo zilikwenda lakini kwa sababu kila kijiji pana mabadiliko makubwa ya tabianchi wale watu ambao zamani walikuwa wanapata maji, kila Mbunge hapa atashuhudia waliokuwa wanapata maji tu yanatiririka sasa hivi hayapatikani maji ya aina hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, concentration ya watu wote kutakiwa wachimbiwe maji ni kubwa sana na vijiji vinaongezeka na vitongoji vinaongezeka. Ndiyo maana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameleta gari kila mkoa. Pamoja na kuwa gari liko kila Mkoa WAbunge watakubaliana nami kwamba halitaweza kuchimba kila kijiji siku moja. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge, tumepokea hoja yake hiyo na tunaichukua kama special case, tumewasikiliza na Wabunge wengine na juzi hapa Waziri wa Sekta alipokuwa anahitimisha hoja amepokea na maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepokea mchango wa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge, waendelee kuiamini Serikali, hili ni moja ya jambo la kipaumbele kwa Mheshimiwa Rais na sisi kama wasaidizi wake tunaweka uzito huo huo na sisi Wizara ya Fedha, tutaendelea kutoa fedha katika maeneo hayo.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri, ahsante. Mheshimiwa Mohamed Monni, taarifa hiyo unaipokea?

MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kiungwana kwa sababu ametoa maneno ya kunifariji na kwa sababu yeye ndiye Waziri wa Fedha, naamini sasa akirudi ofisini atatoa fedha maalum kwa ajili ya Jimbo la Chemba na Wilaya ya Chemba. Namshukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nisiseme tena kuhusu maji. Ukiangalia mpango unaeleza kwamba sasa tunaenda kuchochea maendeleo vijijini na watu hawa ni matajiri. Mimi natoka Jimbo la Vijijini ambapo kura ndiyo rahisi zaidi kuzipata kwa Chama chetu Cha Mapindizi, lakini tunawakwaza. Kwanza nishukuru kwa barabara, ile barabara ambayo tayari Mkandarasi amepewa kutoka Kibirashi – Handeni – Chemba – Singida inakata katikati mwa Jimbo langu, niwashukuru sana Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kwamba barabara ile kidogo itapunguza namna ambavyo watu wanaweza kusafiri. Hata hivyo, zipo barabara ambazo ndiyo maeneo ya uzalishaji, kuna barabara ya kutoka kwa Mtoro hadi huko maeneo ya mashambani kilometa 56, huko ndiko alizeti zote zinazalishwa, huko ndiyo ufuta wote unaouzwa Dodoma unapozalishwa, lakini gharama ya kuzileta Dodoma ni kubwa sana. Fedha zinazotengwa kwa ajili ya ukarabati wa hizo barabara milioni 30, nataka niwaombe kwenye mipango hii lazima takwimu zionyeshe uhalisia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashukuru Kamati ya Bajeti, wameeleza wazi kwamba takwimu zilizowekwa sio halisia, wanaomba watu wa mipango wakafanye upya tafiti ya takwimu zilizopo kwenye makaratasi ili sasa tuweze kusonga mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina jambo lingine la muhimu sana. Sisi ambao tunatoka majimbo ya vijijini sijui changamoto ni nini, lazima tukubali kwamba kule kama wanataka kuwarudisha watu vijijini, lazima Serikali itengeneze mazingira mazuri, huo ndiyo ukweli. Ukienda vijijini tunajenga sasa hivi madarasa, lakini hakuna mpango wowote wa namna gani sasa hata hayo madawati yanaweza kuwa yanatengenezwa baadaye. Sasa hivi tunajenga darasa tunaweka na madawati, lakini nataka niwaambie ukienda shule zote za Chemba 112, upungufu wa madawati ni asilimia 70, wazazi hawana uwezo wa ku-cover hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila mwaka tunaweza kuwa tunatengeneza asilimia 10, lakini ni makakati upi wa Serikali kwa nchi nzima sasa wa kuhakikisha wanaenda kutatua hiyo kero. Tunajenga madarasa ya aluminum, yana tiles, lakini watoto wataendelea kukaa chini, kwa sababu tumeweka vipaumbele sehemu nyingine, sehemu nyingine tumeacha. Nimwombe Waziri wa Fedha lakini pia nimwombe Mheshimiwa Profesa Kitila, rafiki yangu tunafahamiana sana tangu tukiwa Pugu Secondary, anajua na nilikuwa mshabiki wake alikuwa akigombea u-head prefect, natafuta kura zake. Nimwombe sana atafute namna ambayo tunaweza kutatua changamoto zilizoko, lakini…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme maneno mawili ya mwisho. Kuna tatizo kubwa sana.

MWENYEKITI: Mheshimiwa, malizia muda wako. Kengele ya pili imeshalia.

MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kuwapa pole sana wananchi wangu wa Kijiji cha Handa, ambao wamechomewa nyumba na mahindi kuanzia jana na juzi operation ya kuchoma nyumba na watu wa TFS, inaendelea. Amesema Mheshimiwa Deus Sangu, hapa tulitamani tuijadili ili tueleze hali halisi, jana watu kadhaa wamechomewa nyumba zao, mahindi yao yamechomwa halafu watu walioenda kuchoma pale ni watu wa TFS na magari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yawezekana kabisa wananchi wangu wamevunja Sheria. Sasa unawezaje mtu mwenye akili za kawaida unaenda unachoma nyumba ya mtu, labda kweli ipo kwenye msitu wa hifadhi, unachoma nyumba ina magunia 60 unachoma, unaenda nyumba ya pili ina magunia 30 unachoma, ndiyo nini sasa?

MWENYEKITI: Mheshimiwa, ahsante kwa mchango wako kwenye matayarisho ya mipango.

MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)