Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Musoma Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia kwenye hii taarifa au Mwongozo wa Mpango kwa maana ya maandalizi lakini na kwa Taarifa ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha. Naungana na wenzangu kumpongeza sana Mama yetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu kwa kazi nzuri anazoendelea kufanya katika kulitumika Taifa hili. Sasa nimesikia kwa namna ambavyo Profesa ameweza kuwasilisha mpango, kusema kweli ni Mpango mzuri isipokuwa kuna eneo ambalo nadhani ni la muhimu sana ambalo Profesa alihitaji kulitia mkazo kuli-bold. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yoyote ile mojawapo ya kazi yake kubwa inayopaswa kufanya ni kuhakikisha kwamba watu wake wanapata ajira. Sasa kwa Tanzania kusema kweli hilo sasa ni tatizo. Kwa hiyo, ndio maana nilidhani kwamba mpango huu ungeonyesha moja kwa moja kwamba ni kwa kiasi gani Serikali imejipanga kuongeza ajira kwa watu wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitolee tu mfano pale Jimboni kwangu Musoma, yaani Musoma Mjini kwenye mambo ya social service hatuna matatizo, habari ya afya, habari ya maji, yaani habari ya elimu hatuna shida, lakini shida kubwa iliyopo ni kwamba vijana wetu hawana ajira na hili ni tatizo kubwa sana. Kulikuwa na Viwanda kama MUTEX vya nguo vimekufa, kulikuwa na Kiwanda kikubwa cha Maziwa kimekuwa, kulikuwa na Viwanda vya Samaki vimekufa. Kwa hiyo, leo usishangae kuona unatembea hata saa saba za usiku unawakuta vijana wanacheza pool, ni kwa sababu hawana ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nilidhani huu mpango ulikuwa ni lazima uoneshe kwamba ni kwa kiasi gani utaweza kuwasaidia vijana wetu waweze kupata ajira. Kusema kweli nimeona hata katika maeneo mengine hata kule kwa wenzetu kule Tarime, niliona kwa sababu ya watu kutafuta ajira mpaka wakaingia kilimo kibaya cha bangi lakini Serikali ilichofanya ni kwenda kufyeka halafu somo likaishia hapo. Kwa hiyo, lazima tuone kwamba ni kwa kiasi gani tunaweza kujipanga kuhakikisha kwamba tunawasaidia vijana wetu ili wapate ajira kwa sababu hilo ndiyo jukumu kubwa la Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Profesa Waziri wa Mipango umeweza kuzungumza hapo ukagusa kidogo kwamba katika vipaumbele vyako, Serikali ijielekeze zaidi katika kilimo. Ni kweli kwamba kilimo kitasaidia kwa sababu kinachukua, kinaweza kuajiri watu wengi zaidi, nichukue nafasi hii kumshukuru sana na kumpongeza Waziri wa Kilimo kwa kazi kubwa na nzuri anayoendelea kuifanya. Pamoja na hii kazi kubwa na nzuri ambayo anaendelea kuifanya bado tunasafari ndefu, kwa maana kwamba watu wanaoingia kwenye ajira kila siku ni wengi ukilinganisha na kiasi cha ajira kinachotolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kwenye taarifa hapo tumeona kwamba hata lile deni la Serikali sasa unajua tunaelekea kugota kwenye 100 ambapo sasa up to 25 tutakuwa kwenye kukopesheka itakuwa ni kazi kubwa. Hata ile miradi mizuri ambayo tumeianzisha return yake bado itachukua muda kuanza kupata return, kwa hiyo, bado tunayo kazi kidogo. Ushauri wangu sasa pamoja na hizi juhudi kubwa ambazo zinachukuliwa ni vizuri sasa tukaweza kuangalia na ile miradi ya quick win inayoweza kuleta matokeo ya haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa sababu lengo letu saa hizi tunaandaa mpango, tunatengeneza mapendekezo ya mpango, mimi nilitaka nilete mapendekezo ya mpango na uwe specific kwa Mkoa wa Mara, endapo huo mpango utakubalika basi tuone namna ya kuuelekeza katika mikoa mingine yote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye ule mpango wa quick win ambao nadhani unaweza ukaleta matokeo mazuri umejikita tu katika maeneo mawili, eneo la kilimo na eneo la ufugaji wa samaki, maana kwenye samaki hapa kwanza nilishasema katika bajeti iliyopita, nikasema hii kama hatuwezi kuunda Mamlaka wale samaki lile Ziwa litakuwa tu ni maji ya kunywa na kuogelea lakini tukiunda Mamlaka maana yake samaki watahifadhiwa watu wetu wataweza kuendelea kuvua samaki kwa utaratibu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi nimuombe Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwamba jiandae kututengea shilingi bilioni 10 kwa Mkoa wa Mara katika bajeti ijayo na katika hizo shilingi bilioni kumi sisi tutazielekeza kwenye kilimo na kwenye ufugaji wa samaki. Tukizielekeza upande huo nina uhakika kwamba kwa mpango ambao mimi nimeshaufanyia utafiti, kila mwaka tutaweza kupata ajira za moja kwa moja zisizopungua 4,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi ombi langu kwako ni moja tu kwamba Mheshimiwa Waziri utakaposimama hapa utuambie kwamba hii investment ya shilingi bilioni 10 kwenye direct ajira ya 4,000 mpaka 5,000 is that project viable or not? Kama ni viable, mimi nitakachokiomba ni kitu kimoja tu kwamba sasa nitakapotoka hapa ule mpango ambao nilishauandaa nitamshirikisha RC wangu pamoja na ma-DC. Tukishamaliza, Mheshimiwa Waziri wa Mipango uje Musoma uje pale Mara sisi tukuoneshe kwamba ni kwa kiasi gani tumeweza kujipanga kupokea hizo fedha ambazo zitaweza kuajiri vijana wetu wasiopungua 4,000 kila mwaka na kwa kufanya hivyo tunadhani kwamba tatizo la ajira tutakuwa tumelipunguza kwa Mkoa wa Mara lakini tuone ni namna gani tunaweza kulipunguza katika nchi nzima ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoweza kusema kwamba kati ya wadau ambao nategemea kuwashirikisha nimesema Mkuu wa Mkoa nikasema na ma-DC nikasema lakini pamoja na ndugu zetu wa Magereza pamoja na JKT. Tukifanya hivyo basi tunadhani kwamba tunaweza tukaajiri vijana wengi zaidi na hili tatizo litapungua. Kwa sababu leo unapozungumza habari ya kilimo, uko ule mpango wa muda mrefu kama huo wa kuchimba mabwawa, uko huo wa visima lakini kwa Mara sisi Ziwa Victoria lile, yaani ni kwamba tuna mbuga za kutosha. Ukienda pale Mto Mara tunamabonde ya kutosha, yaani pale kinachohitajika leo ukizungumza habari ya irrigation pale inahitaji power pamoja na ule mtambo unalima tayari maisha yanaendelea au ukizungumza habari ya hose irrigator yaani ni vitu ambavyo havihitaji habari ya mitaro, ni vitu ambavyo havihitaji hata hayo mambo ya feasibility study kwamba maji yatateremkaje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ndiyo maana mimi nasema nimalize tu kwa kusema kwamba utakaposimama mimi nataka tu jambo moja. Moja kwamba investment ya shilingi bilioni 10 kwa vijana 4,000 uniambie kama the project is not viable or it is viable, kama hiyo project inalipa ukubali kuja kupokea mpango na kama ukishakubali kupokea mpango, tukishajiridhisha na wewe ukaukubali basi tuuweke kwenye utaratibu na Waziri wa Fedha awe tayari kutulipa ili tuweze kupunguza tatizo la ajira kwa watu wetu. Kwa hiyo tunadhani kwamba kwa kufanya hivyo itakuwa imetusaidia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwenye hili suala nilililoomba la kuwa na Mamlaka ya Uvuvi. Leo wote ni mashahidi ukienda katika mbuga zetu zote za wanyama pamoja na changamoto zote zilizopo lakini ni kwamba hifadhi zetu zinao wanyama wa kutosha na ni kwamba zinakidhi vigezo vyote vya Kimataifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukiliangalia lile Ziwa Victoria ni Ziwa kubwa sana lakini ni kwamba kutokana na lile Ziwa kushindwa kuwa na usimamizi madhubuti ndiyo maana habari ya samaki imeisha. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Manyinyi kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Naibu Waziri.
TAARIFA
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, pamoja na mchango mzuri wa Mheshimiwa Mbunge kuhusiana na masuala ya ajira kwa vijana naomba pia apate taarifa na atambue mchango wa Serikali kwamba Serikali hii imeamua kujenga Vyuo vya VETA kwa ajili ya kuwasaidia vijana katika Wilaya zote lakini pia katika miradi mikubwa yote ya maendeleo ni kipaumbele kwa vijana ambao ni unskilled, semi-skilled na skilled wanapata ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya hapo Mheshimiwa Rais pia ametoa fedha kwa ajili ya program mbalimbali za uanagenzi pia apprenticeship lakini pia za kukuza ujuzi na recognition of prior learning ambazo hizi zote zinawa-involve vijana ambao walikuwa na changamoto ya kutambulika labda pengine kwa sababu ya sifa za kielimu. Pia ipo mikopo ambayo imeendelea kutolewa kwenye Halmashauri mbalimbali ya asilimia10. Asilimia Nne kwa ajili ya vijana pia asilimia mbili kwa watu wenye ulemavu, yote hii imeendelea na tunairatibu sasa ili ianze kutolewa katika utaratibu wa kibenki kwa wale ambao hawana ajira waweze kupata na kuendeleza biashara zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho kwa taarifa ni kwamba tunayo taarifa ya Mheshimiwa Rais kupitia TAMISEMI, hivi karibuni anaenda kutoa ajira 11,000 kwa ajili ya vijana kwenye Sekta ya Afya, ajira 11,000 kwa ajili ya Sekta ya Elimu. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mheshimiwa Mbunge anaendelea vizuri kuchagiza kwenye eneo la kuongeza kasi kwenye ajira atambue pia mchango wa Serikali.
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Naibu Waziri. Mheshimiwa Vedastus Manyinyi unaipokea hiyo taarifa?
MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, samahani sana Mheshimiwa Naibu Waziri, mdogo wangu ametumia dakika tano nzima kwa ajili ya hoja yangu lakini tuzungumze tu ule ukweli. Mimi nakubaliana kwamba Serikali imeweka mikakati mingi ambayo inayoza ku-create ajira lakini tuende kwenye hali halisi. Tukienda kwenye uhalisia ukilinganisha namba za watoto vijana ambao wanaingia kwenye ajira mfano kwa Musoma Mjini kila mwaka siyo chini ya vijana 2,000 wako tayari kuingia kwenye ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni wangapi hao ambao wanaopata ajira? Kwa sababu ukizungumza yaani pamoja na kwamba wako vijana ambao wanaingia kwenye ajira kulingana na juhudi za Serikali lakini ukija kwenye percentagewise Mheshimiwa Waziri haivuki hata asilimia tano. Kwa hiyo, ndiyo maana na sisi tunazungumza mipango ya ku-compliment kwenye hizo ajira zinazopatikana ili vijana wengi zaidi waweze kuajiriwa na maisha yao yaweze kuendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa lile la samaki kama nilivyosema kwamba ile Mamlaka ya Uvuvi itawezesha kuhakikisha kwamba inaweka utaratibu madhubuti wa kuangalia wale samaki namna ya kufanya waendelee kukua, waendelee kuwa sustainable. Pale Mjini zaidi ya viwanda vitano vimekufa kwa sababu hakuna Samaki, kwa hiyo, tusipoweka mpango wa Mamlaka inayoweza kusimamia maana yake ni kwamba ajira itaendelea kuwa tatizo.
MWENYEKITI: Ahsante sana.
MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya hapo nakushukuru sana.