Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Emmanuel Peter Cherehani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Awali ya yote, namshukuru sana Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema kwa kunipa nafasi ya pekee leo kunipa uhai wa kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suuhu Hassan kwa fedha nyingi ambazo anazidi kutuletea majimboni. Nampongeza ndugu yangu Daktari wa Uchumi, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba kwa Mpango wake mzuri ambao ametuwekea hapa Mezani kama Wabunge tuweze kuujadili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza ndugu yangu Mheshimiwa Profesa Kitila Alexander Mkumbo, tumepitia mipango yenu yote, ni mizuri; tumepitia mipango na maandiko haya yote yamekaa vizuri kwa manufaa ya wananchi wetu. Pia nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa wananchi wa Ushetu, kilio chao cha barabara ambazo zilikuwa hazipitiki kwa msimu mzima kupitia Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, mipango yako uliyoileta toka mwaka 2022, wananchi wa Ushetu barabara zao zote sasa zinafunguka, zinapitika, madaraja yanajengwa, hospitali ya wilaya imekamilika, jengo la utawala linaendelea vizuri na shughuli za kilimo, kwa sababu wananchi wa Jimbo wa Ushetu ni wakulima, wanafanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nampongeza sana rafiki yangu na ndugu yangu Waziri wa Kilimo, kwa kazi nzuri aliyoifanya kwa wakulima wa tumbaku hapa nchini. Uzalishaji kwa miaka hii miwili ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, imepanda kutoka uzalishaji wa kilo 60,000 lakini leo mwaka 2023 tumeweza kuzalisha kilo milioni 122 zenye thamani ya dola za Kimarekeni zaidi ya milioni 341. Ni uchumi mkubwa ambapo fedha nyingi zimesambaa kwa wakulima. Msimu huu wa 2023/2024 wanunuzi wetu wameweza kuongeza uzalishaji tani 214,000 ambazo tunatarajia kuja kupata zaidi shilingi bilioni 900. Ni fedha nyingi sana. Hongereni sana na tumpongeze sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nianze kuchangia. Nijikite kushauri kwenye upande wa maliasili na upande wa mifugo. Maeneo haya mawili yanatakiwa yaunganishwe yakae pamoja, mifumo yao isomane kwa ajili ya kuwanufaisha wananchi. Kwenye upande wa maliasili na upande wa mifugo tuna fedha pale tumeziacha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nijaribu kufafanua kidogo; ukiangalia leo tunahifadhi zetu ambazo zina vivutio na zina Wanyama, na pia tuna hifandhi ambazo hazina vivutio kabisa, hakuna Wanyama, lakini tumeweka gharama ya askari wetu kulinda yale maeneo lakini Serikali haipati chochote. Madhara yake ni kuendelea kugombana na wananchi, kufukuzana na wananchi, kutengeneza matabaka mawili kati ya askari wa wanyamapori na wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naendelea kushauri…

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, pale kuna fedha.

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Maganga.

TAARIFA

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wa ndugu yangu Mheshimiwa Cherehani ni mzuri sana. Kwa kweli tunapoishauri Serikali tufikirie tunaishaurije ili kusudi kukusanya makusanyo mazuri ili kufikia shilingi trilioni 47. Kwa mfano amewatolea mfano askari wa wanyamapori, kweli utakuta Polisi anakusanya na anatoza faini kwa wafugaji, hana POS. Anapokata faini kwa wafugaji, pesa anaweka mfukoni. Tunaiomba Serikali itengeneze mpango, ikiwezekana kila askari awe na POS ili faini hizo ziwe zinaingia kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali, ahsante sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Emmanuel Peter Cherehani, unaipokea hiyo taarifa?

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa ya Mheshimiwa Maganga, nami nilikuwa naelekea huko. Nataka nishauri, tuna hekta nyingi ambazo hakuna wanyama, misitu inaendelea kuchoka, fedha zinakusasnywa zinaingia mifukoni mwa wachache. Kwa nini maeneo haya tusiyatengeneze yawe maeneo ya malisho ya wananchi wetu ambao ni Wafugaji ili kupunguza migogoro ya wafugaji na wakulima? Leo kila ukiingia kwenye mitandao utakuta habari kuhusu migogoro ya wafugaji na wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge, mama yangu jana hapa aliongea, migogoro inazidi kuongezeka. Inazidi kuongezeka kwa sababu wafugaji hawana mahali pa kwenda kuchungia mifugo yao. Hakuna. Wafugaji hawana maji, mabwawa hakuna, Wizara ya mifugo mnaiwekea bajeti ndogo ya fedha kwa ajili ya mabwawa. Ongezeni fedha. Fedha zile hatumwombi hata Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba zile fedha, tutengewe tu sasa kwenda kutoza kwenye maliasili ambazo hazina wanyama na vivutio.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kwa sensa ya mwaka juzi 2021, tuna ng’ombe wasiopungua milioni 36 hapa nchini. Tukisema tu kila mwaka kila kichwa cha ng’ombe tuchangie shilingi 2,000 twende kuchunga kwenye mapori yetu huko ambayo hayana wanayama wala vivutio, tunaenda kukusanya zaidi ya shilingi bilioni saba kwenye upande wa ng’ombe. Pia tuna mbuzi zaidi ya milioni 24, nao tuweke shilingi 200. Tayari pale tuna shilingi bilioni 4.800. Tuna kondoo wasiopungua milioni 10 na kwenyewe tukasema tuweke shilingi 200, tayari tutakusanya shilingi bilioni mbili; tuna punda wasiopungua milioni moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zile ni fedha, lakini wale askari wetu tumeamua kuwapa bunduki wakagombane na wananchi; hakuna watalii, hakuna Wanyama, hakuna vivutio. Kwa nini tusiwape kazi ya kuwalinda wananchi wetu wachunge vizuri, badala ya kukaa na bunduki mle porini, tuwape POS tu. Wakae na POS mle wawaelimishe wakulima wetu, miti itapandwa vizuri, wafugaji watapata maeneo mazuri. Fedha hizi ambazo ukizikusanya kwa mwaka ni zaidi ya shilingi bilioni 80, zinaenda kuchimba mabwawa upande wa mifugo na uvuvi, zinaenda kuwachimbia wafugaji wetu mabwawa ya kunywesha ng’ombe na zinaenda kuwatengenezea clinic ya mifugo. Clinic ya mifugo hakuna. Ng’ombe wetu wanapata wapi clinic?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna ranchi ambazo ziko zaidi ya hekta 14 ambazo ni zaidi ya hekari 500,000. Zile ranchi ambazo tunazo ambazo zinalindwa kwa gharama kubwa na fedha nyingi ambazo zinaenda kule, Serikalini tunapata nini? Tunaomba tuzitengeneze Wizara zetu badala ya kumtegemea Waziri wa Fedha atupe fedha. Wizara zipeleke fedha Wizara ya Fedha kwa ajili ya manufaa ya wananchi na Taifa letu kwa ujumla. Tumsaidie Mheshimiwa Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ukiangalia leo hii migogoro imeongezeka, ni kwa sababu wafugaji wengi wamekimbia maeneo yao, wanaenda kutafuta maji na malisho. Wakati tungewachimbia maji kwenye maeneo yao, tukapeleka kule usukumani wakachimba mabwawa makubwa ya maji kwa fedha hizi, wala hatuendi kwa Mheshimiwa Dkt. Mwigulu. Kuna haja gani ya kuendelea kugombana na wananchi? Kuna haja gani ya kuwa na kelele nyingi, kila Mbunge analalamika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kila Mbunge anayesimama Bungeni ni kilio cha wakufugaji na wakulima. Leo…

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa Iddi.

TAARIFA

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa mzungumzaji kwamba kwenye kata inayopatikana kwenye Jimbo la Ushetu, Mheshimiwa Diwani miaka miwili imepita alikamatiwa ng’ombe wake zaidi ya 1,500 na baada ya ng’ombe zile kukamatwa ziliuzwa na baada ya kuuzwa Mheshimiwa Diwani alienda kufungua kesi na kesi ile akashinda, lakini mpaka leo bado hawajamlipa fedha zake, ahsante.

MWENYEKITI: Mheshimiwa unaipokea taarifa hiyo?

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa kwa sababu ripoti ile tayari tulishaipeleka kwa Waziri Mkuu na aliipokea akasema ataifanyia kazi, lakini mpaka leo hatujapata majibu yoyote, ni kuongeza migogoro mikubwa kwa wananchi. Migogoro hii tunatakiwa tuiondoe kwa mapori ambayo hayana wanyama na vivutio, tuyatenge kuwa malisho, tukusanywe fedha, Serikali ipate fedha nyingi, na migogoro hii ya wakulima na wafugaji itaondoka kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nichangie upande wa Wizara yetu ya Muungano na Mazingira. Wizara ile itafutiwe fedha, hawana hela. Bajeti yao ni ndogo, haitoshi kabisa kwenda kutengeneza pesa. Kwa sababu badala ya kwenda kuzibua, kwa sababu niliona wengi tunasema kwamba wakazibue mito kwa ajili ya kuhakikisha uchafu unaondoka, lakini tugeuze uchafu kuwa pesa. Tuwafanye wananchi wetu wanapoona uchafu, wakimbilie tutengeneze viwanda ili uchafu ukatengeneze fedha. Plastics hizi sasa hivi ni hela kwenye nchi za wenzetu. Karatasi zinatua barabarani, kwenye nchi za wenzetu zinakusanywa zinakuwa pesa. Hata uchafu kwenye vyoo vyetu na majiji yetu wanaenda kutupa wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, zile zote ni pesa kwenye nchi za wenzetu. Sasa tunafanyaje? Wizara ya mazingira hawana fedha bajeti yao ni ndogo tutengenezeni, tuwape fedha za kutosha. Mheshimiwa Dkt. Mwigulu tumekubaliana kwamba fedha ziko maeneo haya. Tuna vijana wenzetu wanaochoma mkaa, kila siku tunawakamata miaka yote, miaka nenda rudi, tangu uhuru na uhuru. Magari tunatumia gharama kubwa. Tuwafanye wale wanaosimama kwenye mageti, wakae na POS ya kukusanya fedha badala ya kukaa na bunduki kukimbizana na wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuomba sana, Wizara yetu ya Mazingingira hawana fedha. Tuwape fedha wakatafute fedha ili uchafu wote unaotupwa barabarani, wananchi wakimbizane kwamba unauzwa kwenye viwanda vyetu vya hapa nchini ili tuweze kupata fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahangaika mbolea, leo Mheshimiwa Waziri wa Kilimo anaagiza mbolea kutoka nje kila mwaka. Kwa nini kupitia ng’ombe zetu, uchafu unaopatikana katika nchi yetu, mazingira haya yote tusafishe wenyewe kwa sababu tukitengeneza viwanda vyetu itasaidia sana. Nawapongeza sana ndugu zangu, Mheshimiwa Prof. Kitila Mkumbo na Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, nawaongezea hili, tumechoka kukimbiza na wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumechoka kufukuzana na wananchi kwa sababu ya ng’ombe kwamba wameenda kulisha kwa wafugaji wetu. Hili limekuwa donda ndugu kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, nami naunga mkono hoja. (Makofi)