Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu aliyenipatia nafasi ya kuchangia jioni hii ya leo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na Reli ya Kati kujengwa kwa viwango vya kimataifa. Nachukua nafasi hii kumpongeza Rais kwa jinsi alivyoendeleza ujenzi huu mpaka sasa hivi umefikia hatua ambayo tayari imeshaanzishwa ambapo wananchi wa Morogoro waliona jaribio la mwendokasi lilifanyika na wananchi wa Pwani. Kwa sasa hivi kwa upande wa Morogoro mpaka Dar es Salaam ni kilomita 300, ni asilimia 98.84 na Morogoro - Makutopora ni asilimia 96. Kwa hiyo, ni jambo zuri ambalo wananchi tunajivunia.
Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu na ushauri ni kuwa, tuendelee kuhimiza wananchi, reli hii ikikamilika waweze kuitumia vyema, kwa sababu reli hii ni utalii, ni uchukuzi na inaongeza uchumi wa wananchi. Kwa mfano, kwenye vituo vyetu vya treni hii ya mwendokasi kwa mfano Morogoro tukiwa na Ngerengere, Morogoro Mjini na Kilosa, wananchi wote na vituo vingine vya Dodoma na kuendelea mpaka Mwanza na Kigoma waweze kuhamasika kujitayarisha kuwa na biashara kusudi wananchi waweze kukuza uchumi wao pamoja na ajira, hasa upande wa wanawake pamoja na watoto wakiwemo wanawake wa Mkoa wa Morogoro waweze kujitahidi kuona ni jambo muhimu sana la kujivunia reli hii ya mwendokasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikija kwenye Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere, ambalo tunajivunia sana Tanzania kuwa nalo, litafua umeme ambao unatosheleza kutumika katika Nchi yetu ya Tanzania pamoja na kuwauzia nchi jirani. Ombi langu, umeme huu ambao tayari tumeshaushuhudia na wananchi wa Morogoro na Pwani Rufiji wameshuhudia kuwa mtambo Na.1 tayari umewashwa, pamoja na vyanzo vingine vya umeme, kwa hiyo, wakati utakapozalishwa kwa wingi, kaya zote waweze kupata umeme wa kutosha kwa bei nafuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni Kiwanda cha Sukari Mkulazi. Kiwanda hiki tumekitembelea, kinaendelea vizuri katika hatua zake za ujenzi kwa asilimia 96 kama ilivyosema hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Vile vile kimetoa ajira kwa wananchi na sana sana ni vijana. Kuna vijana wengi, lakini tulipoongea nao, naona Serikali ifuatilie kuangalia maslahi yao yanakuwaje nak ama yanaendana na kazi wanayoifanya kusudi waweze kuendelea na uzalishaji wa sukari.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapo hapo naunganisha na shamba la Mkulazi Na.2 ambalo lipo Dakawa hapo hapo karibu na kiwanda cha sukari ambacho kinazalisha hiyo miwa inayochakatwa kwenye kiwanda hicho cha sukari. Ni kweli tulikuwa na tatizo la sukari kwa sababu ya mvua ya El-Nino, maji yalijaa kwenye miwa kiasi watu walishindwa kuvuna miwa, lakini sasa hivi tunategemea kuwa hicho kiwanda kitaweza kuzalisha tani 50,000 kwa mwaka ambayo itaweza kupunguza tatizo la sukari.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu ni kuwa, mashamba ya uzalishaji sukari miwa yaweze kuendelea kuangaliwa ikiwepo Kagera, Kilombero I na Kilombero II, kikiwepo Kiwanda cha Kilimanjaro na viwanda vingine mashamba yaweze kuanzishwa kusudi sukari iweze kuzalishwa kwa wingi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu mwingine ni kwenye upande wa mahindi. Huwa tunaanzisha maghala ya Serikali ambayo huhifadhi mahindi ili wakati wa njaa tuyatumie. Kwa hiyo, huu mpango unaweza ukatumika kwa upande wa sukari, tukaweza kuwa na maghala ya sukari ambayo yanaweza kutumika wakati tuna uhaba wa sukari. Hilo ni jambo muhimu ambalo naomba liangaliwe pamoja na ajira kwa watu wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo naomba kuongelea ni nishati. Nashukuru umeme umeenea kwa wastani wa vijiji vyote, umeme wa REA unaendelea, lakini nahimiza na naishauri Serikali kuwa wananchi wanaomba vitongoji vyote viweze kupata umeme. Umeme ni viwanda, umeme ukimulika na wewe mwenyewe unafurahi. Vile vile umeme ni elimu, kwa sababu wanafunzi watatumia umeme kujisomea na kujifunza. Kwa hiyo, naomba sana jambo hilo la umeme liangaliwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, natoa shukrani kwa Mheshimiwa Rais kwa kutoa nishati safi ya kupikia ambapo kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati wameweza kutoa kongamano la wanawake na kuwapatia vitendea kazi wanawake wajasiriamali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu ni kwamba, wadau wote wenye uwezo, wamuunge mkono Mheshimiwa Rais kwa kusambaza mitungi kusudi tuweze kutokana na matumizi ya kuni ambazo zina madhara ya kiafya, zinaharibu mazingira na kuongeza athari za tabia nchi. Kwa hiyo, nawaomba sana wadau wote waweze kuliangalia hilo jambo la nishati safi. Pamoja na hayo, nishati mbadala ikiwepo biogas, upepo viweze kutumika kwa sababu ni muhimu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni elimu. Elimu ni jambo muhimu sana. Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Sita amefanya kazi nzuri sana kwa upande wa elimu, ila ushauri wangu, bado kuna wanafunzi wengi ambao wamemaliza shule, wana sifa za kwenda vyuo vikuu, lakini hawana mikopo licha ya mikopo kupandishwa juu. Kwa hiyo, naomba bajeti iweze kuongezwa zaidi ili kuwasaidia wanafunzi wanaostahili kwenda vyuo vikuu ili kila mmoja aweze kutimiza ndoto zake.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukarabati wa madarasa makongwe ya sekondari pamoja na msingi ikiwepo shule zetu za huko mikoani kwenye halmashauri, naomba sana uangaliwe. Nimetembelea, kweli nimeona madarasa mengine ukiacha hii ya UVIKO ambayo tumeweza kukarabati na ambayo tumeweza kujenga ya sekondari pamoja na primary, lakini mengine pembeni unakuta bado ni machakavu. Kwa hiyo, naomba yaangaliwe kusudi yaweze kukarabatiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa afya, namshukuru sana Mheshimiwa Rais, amefanya jambo kubwa sana, lakini bado kuna matatizo ya nyumba nyingine kama nilivyosema juzi, nyumba ya akina mama na watoto bado hazijamalizika, ziweze kumalizika.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, naunga mkono hoja, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii ya kuchangia kwenye Hotuba ya Waziri Mkuu. (Makofi)