Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Singida Mashariki
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hoja iliyoko mezani, Ripoti za Kamati zetu za PAC, LAAC pamoja na PIC. Sasa naenda moja kwa moja kwenye hoja yangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipimo cha Serikali inayozingatia utawala bora kwa maana ya good governance, vipo vingi, lakini viwili ndio nguzo yake. Cha kwanza, ni kufuata demokrasia, kufuata sheria katika kuongoza, lakini ya tatu kwa maana ya haki, kutoa haki kwa wananchi wake ikiwemo huduma. Haya mambo makubwa matatu ndio yanakuwa yanaangaliwa katika vipimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ni kuzingatia matumizi bora ya fedha na rasilimali za umma. Haya mambo mawili ndio yanabeba sura ya utawala bora. Kwa hiyo, kwenye hili tumpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa dhamira yake njema ya kutoa uongozi kwa maana ya kwamba, anaonekana kwa vitendo na maneno yake kwamba, anatamani nchi iongozwe kwa utawala bora. Kwa maana ya kwamba, demokrasia anataka watu tuongozwe kwa pamoja na kufuata sheria, lakini pia wananchi wapate haki zao na tumekuwa tukimuona waziwazi kwenye hotuba zake mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utawala duniani unaongozwa na aina mbili. Utawala unaoongozwa mojawapo na viongozi wa kisiasa, lakini pia kuna watumishi wa umma ambao ni civil servants. Kwa hiyo, watu hawa wawili ndio wanasaidiana kwa pamoja kuongoza nchi au kuongoza eneo lolote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo tunaona wote, Mheshimiwa Rais anakemea, Wabunge tunasimama hapa tunakemea, lakini hata Madiwani kwenye Halmashauri zetu wanakemea kwa maana ya uongozi, viongozi wa kisisasa wanayo dhamira njema ya kuisaidia nchi hii kwa sababu, tunaonekana kila mahali. Kwa hiyo, kupitia haya tumesomewa taarifa hapa, taarifa za Kamati zetu na naomba nijikite kwenye Taarifa ya Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza kwenye taarifa hiyo ambayo inaelezea upande wa MSD ambayo ni Mamlaka ya Dawa katika nchi yetu. Kupitia Ripoti ya CAG kumeonekana kuna upotevu au kuna madeni yanayokadiriwa kuwa bilioni 375, yaani MSD hawajalipwa, yaani wanadaiwa madeni yao. Walichukua dawa kwa washitiri, wakapata dawa wakazi¬-supply, hawajalipwa kwa maana wana madeni, kwa hiyo, imeonekana CAG ameona pale jicho lake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama haitoshi hii inaathiri mtiririko wa utoaji wa dawa. Leo tunalalamika utoaji wa dawa katika vituo, kwa maana ya utoaji wa huduma katika Halmashauri zetu, hakuna dawa, ni kwa sababu, kuna mkwamo na Halmashauri zetu zimekuwa zikiomba dawa au kupeleka maombi ya kununuliwa dawa, bado haziletewi kwa sababu kuna deni kubwa liko pale wanadaiwa MSD. Hii maana yake nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii maana yake ni kwamba, tunasababisha tatizo la huduma kwa wananchi wetu kwa sababu tu, kuna baadhi ya watu hawajatimiza majukumu yao. Hili ni tatizo kubwa na CAG ametuonesha kwamba, kuna tatizo mahali. Kama tunadaiwa dawa za bilioni 300 ni wananchi wangapi wanakufa bila dawa vijijini? Ni namna gani Serikali inalaumiwa huko vijijini kwa sababu tu ya kikwazo hiki cha kudaiwa deni kubwa kiasi hiki?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, maana yake ni kwamba, leo CAG ametuonesha kwamba kuna tatizo mahali. Ndio maana leo wananchi wakienda kwenye zahanati zetu, hakuna dawa kwa sababu ya misingi hii ambayo tunaeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la MSD hapa imeelezwa kwenye ripoti zote za miaka mitatu mfululizo 2019/2020, 2020/2021 na 2021/2022. Kuna jumla ya aina 2,540 ambazo zilipokelewa zenye thamani ya bilioni 295.76, dawa hizi zilipokelewa zikiwa zimebakiza miaka miwili kwisha muda wake, lakini kama haitoshi katika hizo dawa ambazo ni thamani ya bilioni 28.4 zilikutwa muda wake umeshakwisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unajiuliza, hivi hakuna wataalam ambao wanaenda kukagua kabla dawa hizo hazijaja nchini? Wakati wanakagua walikuwa wamefumba macho? Wakati wanakagua vyeti vyao vilikuwa vimefungiwa kabatini kwamba, ni wasomi? Watu hao walikuwa hawana roho ya Mungu wakati wanakagua dawa za bilioni 28? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu hao sio wazalendo wa nchi hii? Watu hao ni wageni kutoka nchi za nje ambao wanawaletea wananchi wa Tanzania dawa zilizoisha muda wake ili waje wanywe wafe kwa sababu, dawa ikiisha muda wake inakuwa sumu. Ndio maana nilisema wenzetu baadhi ya watumishi wa umma hawana nia njema na Taifa hili, kwa sababu wasingekubali kuona mambo haya yanatokea …
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Mtaturu kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Innocent Bilakwate.
TAARIFA
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba nimpe Taarifa rafiki yangu Mheshimiwa Mtaturu, watu hawa hawawezi kuona kwa sababu ya rushwa. Ukiona mtu ananunua dawa ya miaka miwili ku-expire, ujue hapo kuna rushwa na rushwa hupofusha haki isiweze kutendeka. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Miraji, Taarifa unaipokea?
MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ndio maana kwenye imani mojawapo ya Chama Cha Mapinduzi inasema wazi kwamba, rushwa ni adui wa haki, sitapokea wala kutoa rushwa. Kwa hakika naomba kuiombea CCM iendelee kudumu madarakani kwa sababu inatoa miongozo mizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana ndugu yangu Bilakwate, ameniongezea maneno haya, nitakuja kuhitimisha mwishoni, hivyo kulazimika dawa hizi kuteketezwa, ziliteketezwa dawa za shilingi bilioni 28. Dawa hizi zimeteketezwa fedha za walipa kodi hawa wananchi wa Tanzania. Watu hawa ambao wengine wanatozwa kodi baadhi ya maeneno wanashurutishwa, hawalipi kwa kupenda wenyewe, leo fedha zao zimeenda kuteketezwa kwa uzembe wa watu wachache ambao wapo kama watumishi wa nchi hii na wanalipwa mshahara na masurufu makubwa kabisa. Jambo hili haliwezi kuvumiliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu inaenda kuwa dumping area. Maana yake kama watengenezaji dawa zinaendelea kuisha na kuna watu watapitisha ziletwe nchini maana yake nchi yetu inaenda kuwa dumping area, maana yake tutaletewa dawa zilizoisha na zitaletwa na zitakuja kuteketezwa na hakuna hatua itachukuliwa. Jambo hili haliwezi kupita kwenye macho ya Wabunge makini kama hawa wa Chama Cha Mapinduzi, wakaacha jambo hili liendelee. Ni hatari kwa afya lakini ni hatari kwa mazingira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye jambo la pili ni Wakala wa Manunuzi ya Umma (GPSA). Wakala huyu alipewa jukumu la kununua magari ya Serikali lakini ukiangalia kwenye ripoti ya CAG, kuna baadhi ya maeneo amesema tumekuta magari hayajanunuliwa. Wananchi waliingia taharuki kwamba kuna gari zimelipiwa hazijaja nchini, wananchi wakajua tumepigwa, kumbe ni Taasisi hii ya GPSA inachelewesha kuleta magari nchini wakati fedha zimeshalipwa na Halmashauri zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, gari za taasisi 14 zilinunuliwa zenye thamani ya fedha zaidi ya shilingi bilioni 28 zilikuwa zimenunuliwa, zimeshalipiwa gari hazijaja nchini. Maana yake ni kwamba, kumekuwa na urasimu mkubwa. Mkataba unasema utaleta gari ndani ya miezi minne au sita lakini tumeendelea kuletewa gari baada ya miaka miwili mbele. Jambo hili haliwezi kuvumiliwa kwa sababu wakala huyu amekuwa ana jambo baya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, dogo sana, dakika moja ni pamoja na kwamba, kengele nimeisikia Mheshimiwa nakuomba dakika moja nimalizie kwa pointi yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukinunua gari Japan, tunapewa offer ya kufanyiwa service kilometa 70,000 lakini gari hiyo ikinunuliwa eneo lingine hakuna hiyo offer. Kuna gari nyingi zimenunuliwa Halmashauri hazina offer ya kilometa 70,000 ambayo ni hasara kwa Serikali. Ombi langu ripoti imesema, watu waliohusika wote hawana sababu ya kuendelea kuwa ofisini. Serikali ichukue hatua ili kuisafisha Serikali ya Chama Cha Mapinduzi, kumsafisha Mheshimiwa Rais ambaye halali usiku na mchana akitafuta fedha kwa ajili ya wananchi maskini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana Serikali ichukue hatua, maazimio yote ya Kamati yazingatiwe na tuweze kuchukua hatua na kuifanya Tanzania sehemu salama. Ahsante sana. (Makofi)