Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa na Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha uliuoishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishi tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezajiwa wa Mitaji ya Umma kuhusu uwekezaji wa mitaji ya umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Eng. Ezra John Chiwelesa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Biharamulo Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa na Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha uliuoishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishi tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezajiwa wa Mitaji ya Umma kuhusu uwekezaji wa mitaji ya umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti na mimi nachukua nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika taarifa ya Kamati hizi tatu PAC, LAAC na PIC. Napenda pia niungane na Wabunge wenzangu kupongeza Kamati hizi tatu kwa taarifa nzuri ambazo wameziwasilisha. Summary nzuri hata kama una usingizi unasoma utaelewa. Kwa hiyo, nawapongeza sana Wanakamati kwa kazi hii kubwa mliyoifanya kwa niaba ya sisi Wabunge wenzenu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwenda haraka, mimi naomba tu kwanza nijaribu kuongea na Wabunge wenzetu ambao wameaminiwa wakaenda Serikali, maana nimeona jana hapa mtifuano ulikuwa mkubwa sana. Napenda tu niwaambie Waheshimiwa Mawaziri, sisi ni wenzenu. Kuna wengine walikuwa huku sasa hivi wamerudi tuko nao huku, labda wengine watatoka wataenda huko. Tunawapenda zaidi kuliko hao the so called wataalam wanaojaribu kuwaambia sometimes tunasema jambo hapa, unasema wataalam waliniambia hivi na sisi kabla ya kuja humu Bungeni tulikuwa wataalam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo simaanishi kwamba tulivyoingia Bungeni humu akili zetu tulizokuwa nazo huko nje zimeisha, sasa hivi tumebaki dull kama hatujui chochote. Kuna Madaktari wengi sana humu, kuna Maprofesa wengi sana humu, kuna Mainjiania, kwa hiyo, tunaposhauri tunaomba mtupe nafasi ya kutusikiliza na ushauri wetu muupokee. Kwa sababu, ushauri huu ni wa kuisaida nchi. Tuko huko tunapambana na mambo haya yanapotokea, sisi ndiyo tunarudi Majimboni kwenda ku-defend Serikali yetu ya Chama Cha Mapinduzi, bila kujali yaliyofanyika huku, tunaenda kuwaambia wananchi nini kimefanyika. Ndiyo maana halisi ya taarifa hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hii haiji kusifia. Ukiangalia ukurasa wa tatu wa taarifa hii inasema, “Kushughulikia maeneo yenye matumizi mabaya ya fedha.” Kwa hiyo, ndugu zetu tunayoyasema haya ni matumizi mabaya ya fedha, myasikie hata kama yanaumiza, ndiyo haya! Ndiyo kazi ya taarifa hii.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema haya mwaka jana wakati nachangia taarifa hii, TANROADS walikuwa wamesababisha hasara ya riba shilingi bilioni 68 na tukasema hapa. Mwaka huu shilingi bilioni 36, in two years shilingi bilioni 104. Zaidi ya bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara. Hizo ni riba tu zinaondoka. Hatuwezi kwenda namna hii! Ifikie hatua pale tunaposhauri msikie na mkafanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa bajeti nilishauri hapa mwaka huu, nikasema haiwezekani mtu anatangaza bajeti na tender anaanza kutangaza, Wizara ya Fedha haijatoa kibali. Maana wewe unamaliza kitangaza kwenye Wizara ya Kisekta, umeshatangaza watu wamefanya kazi unanyanyuka na certificate kwa Mheshimiwa Mwigulu, Mheshimiwa Mwigulu unafika pale anakwambia, nimelipia SGR sina hela, zinaanza ku-count huku! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunayoona ni upande wa TANROADS tu, wapo watu wanafanya miradi ya maji hapa hawajalipwa zaidi ya miezi 12. Jana Waziri wa Ujenzi ameongelea Wakandarasi kulipwa kulipwa hiyo shilingi bilioni sabini, sabini, anaongea wanaofanya kazi TANROADS na Wakandarasi wengi wa Kitanzania maskini hawa, wako kwenye miradi ya maji na huko kwenye miradi mingine. Kwa hiyo, pesa wanazodai ni nyingi sana. Tujaribu kusaidia Watanzania hali kadhalika tuokoe hizi pesa. Kwa sababu, uhakika nilionao, kwenye hizi shilingi bilioni 68 na shilingi bilioni 38, hakuna mkandarasi wa Kitanzania hata mmoja anayelipwa riba! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata mimi ni Mkandarasi, sijawahi kulipwa riba, nadai hela zangu huko. Hizi pesa zinaenda kwa Wakandarasi wa kigeni! Sasa, Watanzania ambao mnaona ni wengi wanafanya kazi hizi, wako wanaumizwa lakini wageni tena wakija wanachukua hizi pesa wanaondoka nazo. Kwa hiyo, naomba hili tuliangalie sana tuweze kuwasaidia hawa watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo nataka kuongelea, nilikuwa napitia hii ripoti kidogo ukurasa wa 21. Kuna hawa watu wanaitwa TANOIL, yaani mtu anaamua tu kutoa discount, anaamua kuweka bei tofauti na EWURA, hawana uchungu na hivi vitu! Anajua hata tukipiga kelele humu na sasa hivi wanatuangalia, hii si ya mwaka 2021/2022? Bajeti tuliyopitisha mwezi wa sita, leo si ni mwezi wa 11 huu? Miezi minne imeshapita, hawa jamaa wanatuangalia tu hata huko nje. Wanajua watapiga kelele baada ya hapa ngoma imefungwa inaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, CAG akija kukagua, miaka mitatu minne ndiyo tunaelekea kwenye uchaguzi, wanatuangalia tu. Sasa, mimi naomba Bunge hili tutoke na maazimio yenye maana zaidi. Maazimio ya kusaidia nchi hii. Kazi ya CAG ni kudhibiti na kukagua lakini nafasi ya udhibiti anakuwa nayo? Kama huwezi kufanya real time auditing, leo tunajadili kitu kilichotokea mwaka 2021/2022 hawa watu walishajenga majumba, walishahamisha hizi hela ziko huko nje, wengine walishaondoka, unawatoa wapi? Mwingine kahamishwa Wizara kaenda huko, unawatoa wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba, kwa sababu ripoti hii kwa sehemu kubwa inachokisema ni kwenye Mashirika ya Umma, mimi nitakuja na proposal hapa kama utaipokea. Kwa sababu, nimeona hata huyu wa TANOIL alikuwa anakiri kabisa. Ni kweli EWURA hawakuturuhusu, ni kweli hatukufanya hivi. Kwa hiyo, unaona ni mtu yuko comfortable, yaani anafanya anavyotaka kama vile hili ni shirika lake nyumbani, hata nyumbani huko saa nyingine unakuwa na bodi kama una shirika lako, iweze kukusaidia kuendesha, lakini hapa hamna kinachofanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pendekezo jingine, nimepitia ripoti ya SGR ukurasa wa 46. Mwaka jana wakati wa bajeti nilionya hapa, maana Waziri wa Fedha alitamka kiasi ambacho kinaenda kutumika kwenye lot six, kutokea Tabora kwenda Kigoma. Waziri wa Fedha akatamka 2.1 billion dollar. Nikasema 2.1 billion-dollar ukii-convert kwenye rate ya wakati ule, ilikuwa inakua kama 4.8 trillion shillings. Nikamwambia lakini ukiingia kwenye TANePS, huyu mtu ambae anapewa kwa single source alikuwa amewasilisha pendekezo la 6.6 trillion shillings. Nikasema, ni zaidi ya shilingi trilioni 1.84, ongezeko linaloongezeka kutoka kwenye kile alichokisema Waziri na kile ambacho kinafanyika kwenye TANePS.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilijibiwa hapa kwamba, watakaa naye yule mtu apunguze zaidi ya asilimia 38 na bado abaki na faida. Mkataba ulisainiwa kwa ile ile 6.6 trillion shillings. Sasa, tunapokuwa tunashauri tusikilizwe. Tunapata muda wa kusoma na sisi tunauelewa. Hilo ndilo tunaloliomba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona hapa mabadiliko, mtu anakwambia ana justification ya kwamba ile 1.3 million dollar inayoongezeka kwa kila kilometa, ni kwa sababu kumekuwa na fluctuation ya bei na vitu vingine na miaka imeongezeka. Ndugu zangu tuko hapa, TANROADS wako hapa na Waziri wa Ujenzi yuko hapa, mimi ni Engineer naelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara kilometa moja ya double surface inajengwa kati ya shilingi bilioni 1.5 mpaka shilingi bilioni 1.8. Mbona hizo kwenye barabara haziongezeki ikawa shilingi bilioni 3? Huku kwenye reli peke yake ndiyo zinaongezeka? Kwani reli hazijengwi na madaraja? Lami haibadiliki bei? Sasa, vitu hivi mkija kufanya hapa muelewe na sisi wengine tuna akili tunasoma, msitufanye hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ambacho ninacho, mimi naomba nitoe ushauri sasa kwa kumalizia ili muda usiishe. Tangu mimi niko huko nje, kila ripoti ya CAG inaposomwa hapa, wizi, wizi, Mawaziri hawa watafukuzwa mpaka lini? Kuna Mawaziri wengine hata hawakuwepo wakati ule, walikuwa huku nyuma, wameshaenda huko mbele mambo haya yanaendelea. Hawa Watumishi wa Umma wamekuwa na comfort zone ambayo wanahangaika nayo, hamtakuja mkae muwaguse hata siku moja. Kwa sababu yeye ana uhakika Waziri ataondoka yeye atakuwepo pale! Kama Katibu Mkuu atahamishwa, yeye atakuwepo pale! Sisi tunakuja kwa kuchaguliwa. Ni kwa nini Wabunge mnakuwa committed kufanya kazi zenu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo wananchi wanatu-monitor huko nyuma. Ni kwa sababu tuna timeframe ya five years. In five years umechemsha wananchi wanakusubiri huko nje wakakupe adhabu yako. Ni kwa nini Watumishi wa Umma nchi hii tumewaacha waka-relax kiasi kwamba wao ndiyo wamiliki wa hii nchi? Tunaenda kuomba kura kwa wananchi tunawaahidi kufanya. Tunakuja hapa watumishi wanatuangusha. Ni kwa nini iwe hivyo? Chama cha Mapinduzi kinasemwa, viongozi wanasemwa, tutarudi huko nje tukahukumiwe lakini kuna watu wamekaa maofisini. Wako nyuma hawajawahi kuonekana. Wao ndiyo wanaotufanya tukaenda vibaya kwenye hii nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima ifikie hatua Watumishi wote wa Umma kuanzia ngazi ya Wakurugenzi, wapewe mikataba ya miaka mitano mitano, isizidi hapo. Kazi zitangazwe watu waombe. Sijawahi kusikia kampuni ya mtu binafsi hata siku moja kila siku inapata hasara, akawacha watu waendelee kuwepo. Wakina Bakhressa wanakua leo, kwa nini wanakua? Umepewa job descriptions, umepewa mkataba, umefeli wanakuondoa wanaleta mtu mwingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona leo akina Rostam wanakua mpaka wanafungua viwanda huko nje, hawajakua kwa sababu waliwabeba watu, There is no permanent employment ukatengeneza faida, kuwe na proper job descriptions, kazi zile zionekane, waambiwe kabisa ukikosea hapa miaka mitano unaondoka. (Makofi)

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ezra, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Nusrat Hanje.

TAARIFA

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa mzungumzaji, anachokizungumza nakubaliana naye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi mwizi ni mwizi tu, ameiba na suti, ameiba na system, ameiba na begi, kaiba na jeans, mwizi ni mwizi. Tunajua ya kwamba mwizi anatakiwa afanyiwe nini. Mimi nafikiri tuwe realistic kidogo. Tumekuwa tunazungumza sana kuhusu ripoti za CAG na anachokizungumza pia ni ushauri mzuri, lakini kwenda kusema tunyongwe na vitu vingine, nafikiri tuwe realistic. Kwanza, hawa ambao wanatajwa wametajwa wanajulikana, ripoti zimeandikwa, tuwaone angalau kuna kesi zinaendelea Mahakamani, mchakato unaendelea Mahakamani ili wengine wawe wamefungwa, tuache kwenda mbali sana, tuangalie hawa, kwa sababu tunawaweza na kweli inaumiza sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ezra muda wako ulikuwa umeisha, basi malizia tu, muda wako umeisha. Taarifa hiyo unaipokea?

MHE. ENG. EZRA J. CHILEWESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea taarifa. Kwa kumalizia naomba kitu kimoja ambacho nataka nishauri tufanye kama Bunge na tutoke na maazimio.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ezra kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais.

TAARIFA

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisimama tu niliona alignment ya anachokisema Mheshimiwa Chiwelesa na walichokisema Wabunge wengine juu ya hatua zinazochukuliwa au zinazopaswa kuchukuliwa, pia, ameongea Mheshimiwa hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa vile hatupendi kuingilia michango ya Waheshimiwa Wabunge, ninataka niwahakikishie kwamba tunavyo vyombo very competent katika nchi, vinachukua hatua na sisi sote tunaona taarifa na ripoti za vyombo hivi huwa zinaletwa humu Bungeni. Waheshimiwa Wabunge zile ripoti za vyombo vinavyofanya kazi zake hasa kwa mfano TAKUKURU, tuwe tunazisoma, tuwe tunazipitia. Tungeweza kujua hata angalau kwa hatu gani tumepiga hatua katika kushughulikia changamoto mbalimbali za uadilifu lakini za uaminifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, itafika wakati wa sisi Mawaziri tuta-respond. Tunaogopa sana kuwaingilia Waheshimiwa Wabunge, kwa hiyo, tunapoongea, ongeeni kwa kiasi kwa sababu, tusiboboe sana, siyo kwamba hatuna nchi, siyo kwamba hatuna system. Kazi zinafanyika na tutatoa ripoti hapa kesho kama zamu yetu itafika, Mawaziri tutasema kazi gani zimefanyika.

MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mulugo, hakuna taarifa juu ya taarifa. Mheshimiwa Chiwelesa malizia mchango wako. (Kicheko)

MHE. ENG. EZRA J. CHILEWESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa naipokea. Kwanza labda nimwambie tu Mheshimiwa Waziri nina 10 minutes tu ya kuongea hapa. Nikianza kuchambua tu huku ninao uwezo wa kuongea dakika ngapi na nikatoa maelezo yangu ambayo naona ni mawazo yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, Bunge linapomaliza hapa likaielekeza Serikali, Seriakali siyo kusema haichukui hatua, mkishachukua hatua TAKUKURU mmempeleka mtu Mahakamani, maana yake Bunge na Serikali mnakaa pembeni, yule mtu kapelekwa Mahakamani ni Muhimili mwingine hamtaingilia kule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wale watu ndiyo maana tukishawatoa hapa hatuwagusi kule, wanaenda kwenye haki wanapambana na wanasheria, wakishinda keshi wanakuwa huru. Ndiyo maana nasema, we have to give them three years contract, five years contract, akichemka terms zake ziko pale mnapambana naye huko, ameshatoka kwenye mfumo wa ajira ili Watanzania wengine waliosubiria huko nje wasio na kazi waje hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wana uwezo, wako huko nje, mtu anashikilia nafasi mpaka anastaafu miaka 60! Wewe leo unateua Bodi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA Mheshimiwa Mwenyekiti namalizia. Unataka tufanye biashara sawa, unateua Bodi mtu kastaafu, unaenda unamwambia aongoze Bodi, Katibu wa Bodi ndiyo Mkurugenzi pale, kuna nini hapo? (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ezra, ahsante.

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na naunga mkono hoja.