Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa na Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha uliuoishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishi tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezajiwa wa Mitaji ya Umma kuhusu uwekezaji wa mitaji ya umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Zuberi Mohamedi Kuchauka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Liwale

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa na Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha uliuoishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishi tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezajiwa wa Mitaji ya Umma kuhusu uwekezaji wa mitaji ya umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nizungumze. Namshukuru sana Mwenyezi Mungu aliyenipa kibali cha kusema haya nitakayoyazungumza.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, naomba tuwe wasikivu, naomba tusikilizane. Waheshimiwa Wabunge, naomba tusikilizane, mwenzetu anachangia.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, niseme neno moja kwa utangulizi. Neno ‘dharau,’ nitalifafanua kidogo huko mbele. Ipo dharau kubwa kwa watumishi wa Serikali ngazi za Wizara na ngazi za halmashauri kwa wanasiasa. Leo sisi tupo hapa, leo ni siku ya pili na hii hoja inakwenda siku ya tatu. Tutajadili humu, tutanyukana humu kadiri tutakavyonyukana, ukitoka nje kwenye makorido, hawa watumishi wa Serikali wanakwambia, hawa ni wanasiasa bwana, hizo ndiyo kazi zao. Ina maana kila kitu kinakwenda kama kawaida, hawabadiliki. Wanasema hizi ni kazi za wanasiasa. Kwenye kundi hili, Mawaziri hampo salama, ni kwamba na ninyi mnaonekana ni wanasiasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Serikali, lazima hatua zichukuliwe na zionekane zimechukuliwa ili dharau hii nayo iweze kuondoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuunga mkono hotuba zote za Kamati zote tatu, naunga mkono azimio la ziada lililotolewa na Mheshimiwa Waitara, Mheshimiwa Deo Sanga na jana Mheshimiwa Maganga na aliyomalizia Mheshimiwa Chiwelesa. Naunga mkono maazimio hayo yawemo kwenye maazimio ya Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kuchangia kuzungumzia mapato ya halmashauri zetu. Ni jambo lisilopingika, ndani ya miaka hii miwili hakuna halmashauri ambayo imepata chini ya shilingi bilioni 10 kutoka Serikali Kuu. Hiyo ni nje ya mapato ya ndani. Fedha hizi zinatafunwa, hakuna asiyejua. Naomba niwaulize, Accounting Officer wa fedha hizi mabilioni ni nani? Huyu Mkurugenzi amepatikanaje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu namwona Mkurugenzi anatumbukizwa kwenye bwawa lenye mamba, kwa sababu yupo Mhasibu kwenye halmashauri ana miaka sita au saba; yupo Mkaguzi wa ndani kwenye halmashauri ana miaka sita au saba; yupo Afisa Manunuzi, ana miaka sita au saba. Leo unampeleka Mkurugenzi ambaye alikuwa Mwalimu akagombea Ubunge, mkampeleka pale akawa Mkurugenzi. Salama yake pale ni nini? Kwenye mamba wale, salama yake ni nini? Ni kuungana nao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, twende mbele tuangalie, huyu Mkurugenzi ana-know how ya Uhasibu? Anajua mambo ya mipango? Anajua manunuzi? Anajua ukaguzi? Kama hajui, na wale ndio wakongwe pale, na hii inaenda mpaka mawizarani. Mheshimiwa Waziri, uliyechaguliwa leo, unaingia kwenye Wizara unakuta watu kwenye Wizara ile ndio mama wa Wizara. Mwezangu nami ili uweze kudumu kwenye ile Wizara, umefanya nini? Uungane nao. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu, narudi kwenye halmashauri. Huyu DED ambaye tumempa madaraka makubwa sana, hivi kweli Mhasibu wa Halmashauri, Mkurugenzi ni mamlaka yake ya nidhamu? Afisa Manunuzi, Mkurugenzi ni mamlaka ya nidhamu? Mamlaka ya nidhamu tumehamishia kwa Madiwani. Mkurugenzi anapeleka kesi kwa Madiwani. Madiwani wanasema hapana, huyu hana kosa, anarudi. Hivi Mkurugenzi huyu na huyu Mhasibu ambaye alimshitaki amerudishwa. Kuna kazi! Lazima eneo hilo tulifanyie mabadiliko. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwaambie, suala la uadilifu, kwamba tumpeleke mtu mwadilifu, hakuna. Huyo Malaika hatapatikana. Watu wanaishi kwa mifumo, kwa kusimamiwa. Lazima tutengeneze mifumo ya watu kuwasimamia, lakini kuwaacha kwa kusema kwamba kuna watu wenye nidhamu wenye uchungu na nchi hii, hawataiba, siyo kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo, naomba nizungumzie suala lingine kwamba Mheshimiwa Rais amepeleka fedha nyingi sana kwenye halmashauri zetu. Kwa kuona usimamizi mbovu uliopo kule, amemteua Naibu Katibu Mkuu wa miundombinu aende akasimamie hizo fedha kule. Kwenye halmashauri zetu, hiyo idara ipo. Kwenye halmashauri hiyo idara ya Naibu Katibu Mkuu wa Miundombinu ipo? Kama ipo, ina watumishi? Jibu ni hakuna. Lazima kama huku juu kuna Naibu Katibu Mkuu wa Miundombinu, nataka nimwone kule kwenye halmashauri, kuna Mkuu wa Idara ya Miundombinu na ana nyenzo za kutosha

Mheshimiwa Mwenyekiti, narudi kwenye ukaguzi wa ndani. Nashukuru Mheshimiwa Zainab, amesema kwamba tumetengeneza kifungu kwa ajili ya Mkaguzi wa Ndani, lakini bado Ofisi ya Mkaguzi wa Ndani ipo chini ya Mkurugenzi. Haiwezi kuwa sawa. Wazo langu, Ofisi ya Mkaguzi wa Ndani iwe inajitegemea. Hawezi kwenda kuomba mafuta kwa Mkurugenzi, aende akaombe gari kwa Mkurugenzi, halafu yeye mwenye anajibu kwa Mkurugenzi, na Mkurugenzi huyo ana uwezo wa kumshitaki kumpeleka kwa Madiwani akafukuzwa, halafu ndio awe Mkaguzi wa ndani! Jambo hili mimi naona siyo sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita kwenye halmashauri. Ipo miradi ya Serikali Kuu kama nilivyosema, zaidi ya shilingi bilioni 10, 15, 20 zinakwenda kwenye halmashauri zetu. Hizi fedha zinapokwenda kule kwenye halmashauri zetu, zinataka zifanyiwe nini? Usimamizi. Usimamizi huu unafanywa na nani? Kweli Madiwani, sisi Wabunge, wote sisi kwa ujumla wetu ni wasimamizi, lakini nani ni Accounting Officer? Ni Mkurugenzi. Naomba hilo jambo lijadiliwe kwa umakini sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la watumishi. Kwenye halmashauri zetu pamoja na kupelekwa fedha nyingi sana, lakini bado kuna uhaba wa watumishi, hasa wenye taaluma hizi. Kama yule niliyezungumza, mtu wa miundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu kuna tofauti moja nyingine kwenye halmashauri zetu, kuna fedha zinatoka Serikali Kuu na fedha za mapato ya ndani. Madiwani wanapanga matumizi ya mapato ya ndani, lakini Serikali Kuu inakwenda na maagizo kila siku kukicha. Halmashauri badala ya kutekeleza miradi waliyoipanga wenyewe, wanabaki kutekeleza maagizo kutoka Serikali Kuu, TAMISEMI. Huu ni mwanya mwingine wa watumishi hawa kula hizi fedha za halmashauri za mapato ya ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni Diwani gani atakataa kupitisha fedha kwenda kumalizia kituo cha afya ambacho wananchi wanakitaka? Fedha zimepelekwa TAMISEMI, shilingi milioni 500, watu wamepiga, kituo cha afya hakijaenda. Mkurugenzi analeta maombi kwenye Baraza kuongeza shilingi milioni 200 kwenda kumalizia kituo cha afya. Ni Diwani gani atakataa kupitisha hiyo kituo cha afya kisimame? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hapa napo ni dirisha lingine la halmashauri kula fedha za umma. Wametafuna zile shilingi bilioni 10 za Serikali Kuu zimeisha, sasa wanaenda kushambulia mapato ya ndani. Jambo hili kwa maoni yangu twende tuliangalie, kama lina…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Kuchauka, muda umeisha, malizia sentensi ya mwisho.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, basi kwa kumalizia, naomba niungane na Waheshimiwa Wabunge wote pamoja na hao niliyowataja, tuwajibike. Kwa Serikali tuweke mifumo. Hakuna Malaika wa kusema kwamba huyu tukimweka pale ndiyo atakuwa siyo mwizi. Mwizi analindwa.