Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa na Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha uliuoishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishi tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezajiwa wa Mitaji ya Umma kuhusu uwekezaji wa mitaji ya umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Ndaisaba George Ruhoro

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngara

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa na Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha uliuoishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishi tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezajiwa wa Mitaji ya Umma kuhusu uwekezaji wa mitaji ya umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia. Tangu jana na leo asubuhi kila Mheshimiwa Mbunge, anayesimama kuchangia kuna watu wanashtuka. Naomba wale wanaoshtuka huko Wilayani, kwenye mikoa na hata humu humu Bungeni, wakae sawa sawa, kwa sababu haturudi nyuma hatuwezi kuvumilia hata siku moja, kuona pesa anayotoa Mheshimiwa, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuna watu wanaitafuna. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna watu wanafikiri kwamba Waheshimiwa Wabunge walikuwa wanapoa poa this time mambo yamebadilika. Wale wanaosikia tunazungumza wanashtuka wakashtuke kweli kweli, kwa sababu tunakwenda kuwashughulikia. Wabunge tumeamua kufanya kazi yetu ya kulinda rasilimali za Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wenzangu wamezungumza na wameelezea umuhimu wa kuanza kushughulikia wezi wote. Mimi naomba mchango wangu niuelekeze kwenye kuboresha mifumo na taratibu za kikaguzi nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na eneo la ushirikiano, maeneo mengi ambapo CAG anakwenda kufanya ukaguzi kwenye Taasisi. CAG amekuwa akifika pale anakuta kuna Wakaguzi wa Ndani wameshafanya kazi kubwa wamefanya ukaguzi wameandaa hoja, lakini kwa bahati mbaya CAG hafanyii kazi Taarifa za Wakaguzi wa Ndani. Matokeo yake unakuta CAG anatumia muda mrefu sana kufanya Ukaguzi na matokeo yake Serikali inalipa fedha nyingi. Jambo hili linaondoa ufanisi kwenye mchakato mzima wa Ukaguzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hili, naomba niishauri Serikali, Serikali itoe maelekezo mahususi kwa CAG, anapokwenda kufanya Ukaguzi kwenye Taasisi iwe ni kwenye Halmashauri au kwenye Wizara, ahakikishe CAG anaanza kufanyia kazi Taarifa za Wakaguzi wa Ndani. Jambo hili litakwenda kuleta ufanisi litaokoa muda na litaokoa fedha za Serikali ambazo vijana wale wanalipwa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo jingine ambalo ninataka kushauri na kuongelea ni kwenye uhuru wa utendaji wa Mkaguzi Mkuu wa Ndani, kwa maana ya Internal Auditor General.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nikuambia huyu Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali anapewa fedha kutoka Wizara ya Fedha na anapewa fedha na Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha. Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, katibu Mkuu - Wizara ya Fedha, ndiye anayetoa fedha kwenye halmashauri, Mamlaka zote za Serikali za Mitaa na kwenye Taasisi za Serikali. Hawa Internal Auditors waliopo kwenye Taasisi wanaripoti kwa Afisa Masuuli ambao na wenyewe wanapewa fedha kutoka kwa Katibu Mkuu Fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo yake kinachotokea hawa Wakaguzi wa Ndani wamefungwa kamba. Hakuna hata siku moja watakuja kufanya kazi nzuri wafanye Ukaguzi ambao ni independent waibue madudu yaweze kushughulikiwa, kwa sababu ya mfumo na set up tulivyoiweka, Ofisi ya Mkaguzi wa Ndani nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapendekeza tuunde, Taasisi ya Ukaguzi wa Ndani, inayojitegemea ambayo haiingiliani na Maafisa Masuuli nchini. Huu ndio mwarobani pekee utakaowezesha, Ofisi ya Wakaguzi wa Ndani nchini kuweza kufanya kazi kwa kujitegemea na kwa kutoingiliwa. Kitendo cha kutofanya hivyo, kimesababisha mpaka hawa Wakaguzi wa Ndani kushiriki kwenye dili za kuiba na wao ni wezi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani Mkaguzi wa Ndani yupo pale halmashauri anaripoti kwa Mkurugenzi watu wanacheza dili halafu yeye wakamuondoa wakamtoa mswaki, lazima na yeye apewe mgao. Lazima hii Taasisi ya Ukaguzi wa Ndani tuweze kuihuisha, tuifumue, tuitengeneze upya iwe huru na iweze kufanya kazi yake ya Ukaguzi sawa sawa, vinginevyo wizi utaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nataka kuchangia ni kwenye Kamati za Ukaguzi, zilizopo kwenye halmashauri. Kamati ya Ukaguzi iliyopo kwenye halmashauri inaundwa na Wajumbe wawili kutoka nje ya halmashauri, inaundwa na wajumbe wawili ambao ni Wakuu wa Idara zile za halmashauri. Mara nyingi wanavyowachagua wale wanawachagua wale wapigaji wanaojua kusuka dili, wale wanaojua kuchakata nyaraka, wale wanaojua kutengeneza dili pesa iweze kupigwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wajumbe wengine wa Kamati hizi za Ukaguzi wa Ndani ni Wakuu wa Idara hao wawili, Mwenyekiti mmoja Katibu mmoja. Hii Kamati inayosimamia masuala ya Ukaguzi kwenye council na maeneo mengine inakosa nguvu thabiti za kuweza kusimamia masuala la ukaguzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka ni pendekeze mambo yote haya ya Ukaguzi ikiwezekana yafanywe na Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya chini ya Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa. Ninataka nikuambie Mkuu wa Wilaya akienda kusimamia pale akiwa Mwenyekiti wa hii Kamati ninayohusika kusimamia Masuala ya Ukaguzi hakuna mtu ataiba zile pesa pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unakuta wamechaguana watu kwa dili wamepangana watu kwa dili wale wale. Kwanza, kinachofanyika pale watu wanatengeneza taarifa na nyaraka kwa ajli ya ku-justify tu. Watu wanapiga hela, ndio maana ukiangalia hizi taarifa namna ambavyo tumezipokea kwenye Taarifa ya CAG. Maeneo mengi pesa zimepigwa, kwa sababu ni systemic ni mfumo ambao umetengenezwa na bila kuubadilisha, bila kuufanyia marekebisho fedha zitaendelea kuibiwa na tutaendelea kulalamika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikiwezekana kama Kamati ya Ulinzi na Salama haiwezi kuhusika kwenye ule mchakato wakusimamia masuala ya Ukaguzi. Basi Mkuu wa Wilaya au Mkuu wa Mkoa, apewa mamlaka ya kwenda kushiriki kwenye zile Kamati. Kwanza, yeye ana authority, yeye ana nguvu na ni Mkuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama pale, anaweza akachukua hatua yoyote. Sasa matokeo yake tunasubiria pesa zinapigwa halafu tunakaa hapa Bungeni tunalalamika tunataka Serikali iagize sasa hivi vyombo vianze kushughulika na wezi walishaiba huko wameshajenga nyumba, wengine wameshahamishwa tunachelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ifike mahali tufanya maamuzi magumu kwenye nchi. Tuweke mifumo tuweke na watendaji tubadilishe, kwa sababu mambo hayaendi vizuri, ndio maana wizi unatokea. Twende kukafumue maeneo hayo tufanye mabadiliko ili tuweke watendaji watakaoweza kuisaidia, Serikali na watakaomsaidia, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mheshimiwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mama yetu ana kiu kubwa ya kuwasaidia Watanzania, mama yetu anajitahidi kutafuta fedha nje ya nchi lakini kuna watu wanazidonoa na kuna watu wanaziiba. Sasa ifike mahali waanze kushughulikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano ukiangalia kwenye performance indicators za Maafisa Masuuli nchi hakuna performance indicator ya kumfanya Afisa Masuuli nchini apimwe, ni kwa namna gani alifanyia kazi mapendekezo na hoja zote za ukaguzi. Ni kwa nini tusiongeze performance indicators kwa Maafisa Masuuli wote nchini? Ili wapimwe ni kwa namna gani walitekeleza Maagizo ya CAG kwenye Taarifa mbalimbali za Kiukaguzi zinazotokea kwenye maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi kweli kama Taifa tumeshindwa kufika mahali tukawa serious tukafanya maamuzi na mambo yakatokeea. Ifike mahali sasa iwe ni mwisho, ifike mahali pesa ya Serikali watu wakiiona waikimbie kama vile umekutana na nyoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kipindi ilitokea watu walikuwa wanaona picha ya mtu fulani nyuma kwenye Ofisi akitaka kuiba hela akiona ile picha anashtuka. Ifike mahali ndani ya nchi hii mtu akitaka kula hela ya Serikali aweze kushtuka. Ninaomba kwenye performance indicators za Maafisa Masuuli wote nchi iongezwe kipengele cha kuwapima ni namna gani walishughulikia hoja zote za kiukaguzi zinazoibuliwa na CAG. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakaa hapa CAG anaibua vitu vingi anaviweka pale ili viweze kufanyiwa kazi. Matokeo yake hakuna kitu hata kimoja kinafanyiwa kazi, tunakutana hapa tunapiga keleke, tunakutana hapa tunalia. Fedha zinaendelea kuliwa wananchi wanakosa fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo na Taifa letu linakuwa linaendelea kwa kusua sua, kwa sababu kuna watu wachache wenye matumbo makubwa kuliko watu wengine wa wanajilimbikizia fedha, wanatafuna fedha za Serikali. (Makofi)

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ndaisaba, kuna taarifa kutoka kwa Naibu Waziri, Mheshimiwa Dkt. Festo Dugange.

TAARIFA

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa mchango mzuri anaoendelea nao. Lakini tu nimpe taarifa kwamba katika Key Performance Indicators za Wakurugenzi ambazo tayari Ofisi ya Rais, TAMISEMI, ilishazifanyia kazi na kuwapa kwa maandishi. Moja wapo ni kuhakikisha kwamba wanadhibiti ubadhilifu katika fedha za umma katika halmashauri zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kuhakikisha kwamba wanakusanya mapato ya ndani kwa ufanisi unaotakiwa. Hilo Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi mara kwa mara mabadiliko ya Wakurugenzi yanapojitokeza tunaona Wakurugenzi wengi wanaachwa. Moja ya sababu ni pamoja na kutokidhi Key Performance Indicators pamoja na kutosimamia ipasavyo miradi na fedha za umma na Serikali itaendelea kufanya hivyo, ahsante. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Ndaisaba karibu, kupokea na umalizie mchango wako.

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba akafukuze Wakurugenzi wote ambao hizi hela zimeibwa na wamepewa performance indicators hawajazifanyia kazi na hela zimeendelea kuibwa. Naomba Wizara na Waziri mwenyewe mhusika, kesho fukuzeni Wakurugenzi wote mahali kote ambapo fedha zimeoneshwa kwenye Taarifa ya CAG watu wameiba hela za Mheshimiwa Rais. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahante Sana. Mheshimiwa Ndaisaba. Sawa, malizia.

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba dakika moja tafadhali, naomba nimalizie hoja yangu kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa naomba mambo yafuatayo yafanyiwe kazi. Moja wezi wote waliohusika na kutajwa kweli Ripoti ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali, wakamatwe wapelekwe Mahakamani washughulikiwe na sisi hatuna huruma na wezi wanaokula fedha za Serikali hiyo ni moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbili, ninaomba Bunge lipitishe Azimio la kuhakikisha kwamba inaenda kufanyiwa overhauling Ofisi ya Mkaguzi wa Ndani, ili iweze kuwa independent, kwa sababu kwa set up na mfumo wa namna ambavyo Ofisi hii ilivyo kwa sasa, Ofisi hii haiko huru na matokeo yake hela za Serikali za Mheshimiwa Rais, zinaendelea kuibwa. Eneo hili linatakiwa liende likafanyiwe kazi liwe na Taasisi huru.

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Ndaisamba.

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, japo sijamalizia yote. Naunga mkono hoja. Ahsante sana. Nitaonge wakati mwingine. (Makofi)