Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MUNIRA MUSTAPHA KHATIB: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuchangia taarifa hii ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii. Kwanza kabisa niunge hoja mkono Taarifa hii ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais, Mama yetu Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ambayo aliifanya kwa kuitangaza nchi kupitia filamu yake ya Royal Tour, nadhani matokeo makubwa tumeyaona. Hapo awali tulikuwa tunaingiza watalii milioni moja lakini baada ya filamu hii ya Royal Tour tumeona tumeanza kuingiza watalii 1,790,000 hii ni hatua kubwa sana kwa hiyo nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa filamu yake hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeongeza pato kubwa la Taifa, tumeweza kuingiza fedha za Kimarekani bilioni 3.3, hiki kitu hakijawahi kutokea toka Uhuru wa Tanzania upatikane. Niiombe sana Serikali iweze kuongezea fedha Wizara ya Utalii kupitia Bodi ya Utangazaji, ili waweze kutangaza zaidi kuweza kupata fedha za kigeni lakini watalii waweze kuongezeka nchini kwetu, niiombe sana Wizara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bajeti ya Ardhi, Maliasili na Utalii kupitia Wizara ya Maliasili hadi sasa imepatiwa asilimia 17 tu katika miradi yake ya maendeleo, hii fedha ni kidogo. Niiombe sana Wizara iangalie namna ya kuweza kutoa fedha kwa wakati katika Wizara ya Maliasili, kwa sababu hii fedha sasa hivi kama ukiangalia TANAPA imeongezewa hifadhi 21. Kwa hiyo, wana mzigo mkubwa wa kuweze kupambana na kutangaza hifadhi zetu za utalii, niwaombe sana Wizara waweze kuongeza fedha hzi kama zilivyopangwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la wanyama wakali na waharibifu. Waheshimiwa Wabunge, wamekuwa mashahidi kwenye Majimbo yao kila Mbunge anayeinuka hapa aliyekuwa anazungumzia suala la wanyama wakali na waharibifu, hili suala limeongelewa Bungeni kwa muda mrefu. Niiombe Serikali na Wizara itafute teknolojia ambayo inaweza kudhibiti wanyama hawa wakali na waharibifu kwa sababu hiki kimekuwa kilio cha Wabunge cha muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wamekuwa wakiathirika na mazao yao lakini wanachi wamekuwa wakiuliwa na Wanyama hawa, lakini hata nyumba zao zimekuwa zikibomolewa na wanyama hao waharibifu, tutafute teknolojia ambayo itakuja kudhibiti wanyama hao waharibifu. Hili suala limekuwa la muda mrefu na changamoto kubwa kwa wananchi wetu lakini ukiangalia kifuta machozi hebu Serikali ituambie ni lini italeta Bungeni Sheria hizi mpya kuja kuzipitia, kuangalia namna ya ulipaji fidia kwa wananchi hawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wanalipwa fidia ndogo sana, niiombe Serikali, niiombe Wizara iangalie kwa jicho la huruma namna ya kuwasaidia wananchi wetu hawa kwa ulipaji fidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Kaka yangu Mheshimiwa Jerry Silaa, tumekuwa tukimuona jinsi anavyopambana kutatua migogoro ya ardhi, amekuwa akijitahidi sana lakini bado migogoro ya ardhi imekuwa changamoto kwenye nchi yetu. Bado tuna migogoro mingi sana na migogoro hii taweza kuondoka pale tu Serikali itakapoamua kuweka wazi taarifa ya Mawaziri Nane. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuiombe sana Wizara na Serikali kwa ujumla waweze kuleta ripoti ya Mawaziri nane, kwa sababu wananchi mpaka muda huu hawajielewi nani anaondoka, nani anabakia katika vituo vyao lakini hata ukiangalia hawawezi kulima, hawawezi kufanya miradi yoyote ya maendeleo wananchi wamekuwa na taharuki kila kiongozi anayepita anazungumzia, utasema nchi yetu ina migogoro mingi wakati haina migogoro mingi ya kiasi hicho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuiombe sana Wizara, tuimbe sana Serikali iweze kuleta taarifa hii ndani ya Kamati lakini pia ndani ya Bunge lako, ije ituambie lini italeta taarifa hii ya Mawaziri nane ndani ya Bunge lako hili Tukufu. Tumeshuhudia mgogoro wa Ruaha na wananchi, niombe sana Wizara ya Maliasili, iweze kwenda kumaliza mgogoro ule wa Ruaha ili wananchi wale wajue, wananchi hawana shida lakini wanataka kujua wanaobakia wabakie, wanaoondoka waondoke. Kwa sababu haya Maazimio tumeyapitisha toka Bunge la mwezi wa saba Bunge la Bajeti, lakini mpaka muda huu hakuna kitu kilichoendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali ituambie ni lini itamaliza mgogoro wa Ruaha na Maazimio yetu ambayo tuliyaleta Bunge la mwezi wa tisa ni kauli gani Serikali inaweza kutuambia kupitia ahadi ambayo Mheshimiwa Waziri, aliahidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo niunge mkono taarifa ya Kamati na niseme ahsante sana. (Makofi)