Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Muhambwe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi na mimi niweze kuchangia taarifa ya Kamati iliyoko mbele yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nianze kwa kuwapongeza Mawaziri wa Wizara hizi husika kwa jinsi ambavyo wanaendelea kutekeleza majukumu lakini kipekee nimpongeze Mheshimiwa Rais wetu kwa jinsi ambavyo ameendelea kuelekeza pesa katika hizi Wizara ili kuweza kuzikwamua. Nitaendelea kuchangia pale kwenye kupanga, kupima na kumilikisha ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Gwajima ameshasema na akionyesha dhahiri kwamba nchi yetu haijapimwa, ni asilimia 30 tu ya nchi yetu ambayo imepimwa, lakini viko Vijiji 1,500 bado havijapimwa hata mipaka hii inaashiria kabisa kama Vijiji vyetu na ardhi yetu bado haijapimwa basi migogoro ya ardhi itaendele sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe mfano mdogo katika Mkoa wangu wa Kigoma. Mkoa wa Kigoma, wenye Kata 306 ni Kata 112 tu zilizopimwa ambazo ni asilimia 36, lakini yako Majimbo ya Buhigwe na Kibondo, kama Kakonko hamna hata Kijiji kimoja ambacho kilichopimwa, Muhambwe Vijiji 50 ni Vijiji tisa tu ndiyo vimepimwa! Hii ina maana gani? Ina maana kwamba ndiyo maana kule kwenye Vijiji vyetu migogoro inashindikana. Kila siku watu wanagombea ardhi, kila siku wavamizi, mkiamka asubuhi hapa ng’ombe mkiamka asubuhi hapa mbuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuna njia nyingine zaidi ya kupima ardhi ya nchi hii na njia pekee ni kuendelea kuwezesha Tume ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi, kwa kuiongezea pesa. Katika hili nimshukuru Mheshimiwa Rais, kwa kuridhia kuongeza pesa kutoka bajeti ya bilioni 1.4 mpaka bilioni nane na wote tumekuwa mashahidi mpaka Disemba wameshapokea asilimia 56 ya hii pesa bilioni nne lakini wameweza kuandaa mipango 3,000. Mipango asilimia 50 imeandaliwa kwa huu mwaka mmoja ambapo Mheshimiwa Rais ameamua kwa dhati kabisa kuweka pesa kwa kuongeza bajeti lakini na kupitia mradi wetu wa miradi ya kuboresha usalama wa umiliki ya ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo, ni dhahiri kabisa Tume yetu ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi, ikiongezewa pesa tunaweza tukaipanga nchi yetu. Tukizingatia Ilani yetu ya Uchaguzi tumesema tutaandaa mipango kina 10,000 lakini mpaka sasa tumeandaa mipango kina 3,000, kwa hiyo tuna kazi ya kufanya katika hii miezi 17, lakini kazi hii inawezekana, Tume ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi, wameshatuambia wakipata bilioni 20 kwa mwaka wanao uwezo wa kuipanga hii nchi kwa kuiandalia mipango kina na huku Halmashauri zikiendelea kupaga katika level zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wote tumeona Halmashauri zimepewa pesa lakini kama Tume ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi, haijandaa Mipango kina kwenye hizi Halmashauri zetu, basi hizi Halmashauri zetu hazitoweza kufanya hivi. Maadam Tume ya Mpango ya Matumizi Bora ya Ardhi, ndiyo tumewapa kazi ya kuanda hii mipango kina lazima tuiwezeshe kwa dhati kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiipatia bilioni 20 hii Tume itaenda kutusaidia sana ili tuendane na kasi ya kupanga hii nchi yetu kama ambavyo tumeelekeza kwenye Ilani ya Uchaguzi. Hili linawezekana kabisa, huku tukiwa tunalia na nchi yetu haijapimwa ziko Taasisi na Mashirika ya Serikali ambayo hayalipi pango la ardhi. Taarifa yetu imeeleza, taasisi zilikuwa zinadaiwa deni la bilioni 123 na Wizara kwa hapa niipongeze sana imefanikiwa kukusanya bilioni 32, sawa na asilimia 26 tunazo bilioni 91 ziko kwenye Mashirika, Mashirika yamejengwa kwenye ardhi yetu na hayataki kulipa pango ya ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ridhaa yako leo nitawataja wale ambao wanadaiwa pesa nyingi sana. National Development Cooperation (NDC) wanadaiwa bilioni 15 kama pango la ardhi, lakini Mbeya Cement wanadaiwa bilioni nne pango la ardhi, National Bank of Commerce wanadaiwa bilioni 12 kama land rent, Msajili wa Hazina anadaiwa bilioni tano, TAMESA wanadaiwa bilioni mbili, Tanzania Airport Authority wanadaiwa bilioni 11, naweza kuendelea list hapa ni ndefu sana kuweza kuona kwamba watu gani wanadaiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mashirika yetu na Taasisi zetu zikiweza kuzilipa hizi pesa ninyi wenyewe mnaona Tume ya Mipango inahitaji bilioni 20 tu lakini kuna taasisi zimekalia bilioni 91. Tunaiomba Serikali ije na mpango mkakati wa kuzipata hizi pesa ambazo Mashirika yameshindwa kulipa ili Wizara yetu ya Ardhi na kupitia Tume ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi iweze kupanga nchi hii ili tuweze kupunguza hii migogoro. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa ni mashahidi tunaona kila siku tuongeze mabaraza. Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, tunamuona Mheshimiwa Jerry Silaa, kila siku anaenda kutatua migogoro, tumeona viongozi wakubwa wa nchi wakitembelea migogoro ya ardhi inaongoza. Hatuna sababu ya kuendelea kupoteza pesa nyingi kwenye hiyo migogoro hebu tuwekeze kwenye kupanga, kupima na kumilikisha ili nchi yetu iweze kuwa na matumizi bora ya ardhi na hii migogoro itaisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi pesa tunazopeleka kule basi ziweze kupanga na kupima. Lakini tunafahamu kabisa tukiweza kupanga nchi yetu wananchi wetu wanakuwa na uhakika. Tumetembelea miradi ya kupanga na kupima, tumeenda kule Meru, tumeenda Simiyu, wananchi wanafuraha kabisa na Serikali yao kwa sababu sasa wana hati zao, wana uhakika wa kwenda benki lakini wameondoa migogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kuwa tumewamilikisha hawa watu na kuwapatia hati basi tunaendelea kupoteza kwanza mapato lakini migogoro hatutaimaliza. Tunaomba mikakati ya dhati ya kuongezea Wizara yetu kupitia Tume, pesa ya kupanga na kupima lakini na mikakati ya kuikomboa hii hela ambayo Mashirika ya Serikali na Taasisi yameshindwa kulipa tunaitaka hii land rent iweze kutusaidia kupanga nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakwenda kuchangia kwa upande wa Maliasili. Kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwa yeye ndiye Mtalii namba moja ambaye ameonesha kwa vitendo jinsi ambavyo utalii unaweza kufanyika. Katika hili jukumu letu ni kuendelea kumuunga mkono kuendeleza kile alichokifanya. Royal Tour imeanza lakini tunapaswa kuendeleza kile ambacho Mheshimiwa Rais, amekianzisha. Tumeona jinsi gani Wizara yetu ya Maliasili, imepokea pesa kidogo kwa ajili ya miradi ya maendeleo asilimia 17, lakini tumeiona TANAPA ambavyo ina mzigo wa hifadhi hifadhi 21 kutoka 16 lakini bajeti yake bado ipo chini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii maana yake ni nini? maana yake hii nguvu kubwa tuliyoiweka kwenye Royal Tour, kama tusipoiendeleza kwa kuendeleza kuboresha miundombinu na hasa ya kwenye hifadhi zetu basi hatutaweza kufanikiwa. Niiombe Serikali iongezee bajeti TANAPA ili iweze kukabiliana na hizi hifadhi ambazo tumeiongezea, lakini ipeleke pesa kwa wakati za miradi ya maendeleo kwenye Wizara yetu ya Maliasili ili iendelee kuboresha miundombinu iliyopo katika hifadhi zetu ili watalii waendelee kuja katika hifadhi zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, liko Azimio ambalo limeshindwa kutekelezeka kama ambavyo Mwenyekiti amesoma katika taarifa yetu la kupandisha hadhi Wakala wa Misitu na kuwa Mamlaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakala wa Misitu ana Bodi ya Ushauri; wote tunashuhudia misitu yetu inavyoangamia katika nchi hii, tunashuhudia jinsi uchomaji wa miti ovyo ulivyo, tunashuhudia uchochoro wa kujificha kwa uvunaji endelevu, ambapo tukienda kuona kiuhalisia hakuna uvunaji endelevu, wanavuna lakini hawapandi huku Wakala wa Misitu Tanzania akiendele kuwa Wakala wa Misitu na siyo Mamlaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inasababisha haya madhara yaendelee kwa sababu huyu TFS hana bodi ya mamlaka, ana bodi ya ushauri tu. Ili kuendana na mabadiliko ya tabianchi ambayo yote tumeshuhudia nchi yetu inavyoingia kwenye majanga kutokana na ukataji wa miti hovyo, kutokana na moto kichaa, kutokana na uvunaji wa miti ambao siyo unaostahili kwenye mazingira yetu, sasa ni muda muafaka mamlaka hii kupandishwa hadhi na kuwa mamlaka kamili, kutoka kuwa Wakala wa Misitu na kuwa Mamlaka ili tuendelee kuokoa misitu yetu katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwenyekiti wa Kamati yetu amesema jinsi ambavyo tumetembelea miradi ya maliasili, kwa kweli kwa hapa tumpongeze Mheshimiwa Rais sana na maliasili kwa jinsi walivyotekeleza. Tumetembelea viwanja vya ndege kwenye hifadhi zetu, tumetembelea barabara za mawe kwenye hifadhi zetu, tumeona jinsi gani ambavyo nia ya Serikali kuboresha zile hifadhi. Kwa hiyo, jukumu letu sasa, tusimamie zile sheria ambazo tunatakiwa tubadilishe na hasa ile ya TAWA ambapo tunaona sheria ile imekuwa na changamoto, imeshindwa kutekelezeka. Tunahitaji TAWA sheria yao ipitishwe ili sasa waweze kujengewa uwezo, wawe na nguvu ya kusimamia hili jambo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwenzangu amesema, wanyama wakali na waharibifu ni tatizo katika nchi yetu. Pia tumeona ambavyo Kanuni ya kifuta jasho imechukuwa muda kuweza kubadilishwa na kutekelezeka, tumeona jinsi ambavyo kifuta jasho kinachelewa kupelekwa kwa walioathirika. Yote haya yanatakiwa TAWA kama TAWA iweze kufikishwa kwenye hadhi ya kuwa mamlaka kamili ili iwe na mamlaka ya kuweza kusimamia hizo kazi ambazo wamepewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kusisitiza kwamba ili tuweze kufanikiwa lazima tuwe na mipango madhubuti. Kwa kumalizia tu, nikumbushie lile ambalo Mwenyekiti pia amelisema kuhusu kuhamisha kukusanya mapato ya land rent kupeleka mamlaka ya Serikali za Mitaa na kuitoa Wizara ya Ardhi, imechangia ukusanyaji wa mapato ya land rent kwa kipindi cha mwaka 2023/2024 kwenda chini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu gani? Serikali imehamisha ukusanyaji wa mapato kutoka ardhi na kupeleka Serikali za Mmlaka za Mitaa bila kuwa na mifumo. Serikali za Mamlaka za Mitaa hazina mifumo na kwa bahati nzuri Serikali imeshawekeza sana kupitia Wizara ya Ardhi kutengeneza mifumo ya ukusanyaji wa mapato. Tulikuwa tumeshafikia tumesema tunataka kwenda kuonyesha sasa; tutakuwa mpaka tunaleta meseji kwenye simu zenu kuonesha kiwanja cheko kinadaiwa shilingi ngapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tumeshafikia hatua hiyo, tena system hiyo inataka ihamishwe ipelekwe mamlaka ya Serikali za Mitaa. Tunaishauri Serikali na kuiomba, kwa vile tumeshatumia fedha nyingi kuboresha mifumo ya Wizara ya Ardhi ili iweze kukusanya mapato vizuri, tunaiomba Serikali iliangalie upya hilo tena, makusanyo hayo ya pango na ardhi basi yaendelee kukusanywa na Wizara ya Ardhi ili Wizara ya Ardhi iweze kukusanya mapato na iweze kujitosheleza na kusimamia, kwa sababu tumeona umuhimu wa kupanga na kupima na kumilikisha ardhi ya nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja. (Makofi)